Ghasia za Uchaguzi Tanzania: Mwaka mmoja baadaye, familia bado zinatafuta haki

Neema Munuo
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 9

Mwaka mmoja baada ya ghasia zilizohusiana na uchaguzi nchini Tanzania, familia zilizopoteza wapendwa wao bado zinadai majibu kuhusu hatima ya ndugu zao waliouawa au kutoweka, huku manusura wakikabiliwa na majeraha ya kudumu na gharama kubwa za matibabu.

Familia hizo zinasema bado hazijapata haki wala ufafanuzi wa kutosha kuhusu yaliyotokea wakati wa ghasia hizo, na zinataka waliohusika wawajibishwe. Pia zinataka msaada utolewe kwa waathirika waliobaki na ulemavu au majeraha makubwa kutokana na vurugu hizo.

Miongoni mwa wanaotafuta majibu ni Neema Munuo (40), aliyempoteza binti yake wa miaka 18, Maria Chami, aliyepigwa risasi na kufariki siku ya uchaguzi, tarehe 29 Oktoba 2025.

Kwa familia nyingi na manusura, kumbukumbu za ghasia hizo bado ni sehemu ya maisha yao ya kila siku. Wanasema maswali kuhusu haki, uwajibikaji na msaada kwa waathirika bado hayajapata majibu, mwaka mmoja tangu kutokea kwa matukio hayo.

Safari ya mama kutafuta haki

Neema Munuo

Kwa Neema Munuo, kumbukumbu za siku aliyompoteza binti yake Maria bado ni chungu. Anamkumbuka Maria Chami, mwenye umri wa miaka 18, si tu kama binti yake, bali pia kama rafiki yake wa karibu.

Asubuhi ya siku hiyo, Neema na Maria walikuwa pamoja nyumbani kwao jijini Arusha. Muda mfupi baadaye, Maria alijitolea kwenda kumnunulia mama yake vocha ya kuongeza salio la simu.

Kwa mujibu wa Neema, Maria alipigwa risasi tumboni alipokuwa akitoka dukani.

Familia ilijaribu kumkimbiza hospitalini kwa matibabu. Neema anasema Maria alipatiwa huduma ya kwanza katika zahanati ya karibu kabla ya kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru jijini Arusha. Hata hivyo, barabara zilizokuwa zimefungwa zilichelewesha safari hiyo.

Neema anasema walipofika hospitalini, Maria alikuwa tayari amefariki.

Baada ya hapo, familia ilikumbana na changamoto ya kuupata mwili wake kwa ajili ya mazishi. Kwa mujibu wa Neema, waliambiwa walihitaji kibali rasmi, na kwa muda hawakuruhusiwa kuuchukua mwili huo. BBC haikuweza kuthibitisha kwa njia huru mazingira ya vizuizi hivyo.

Hatimaye, mwili wa Maria ulikabidhiwa familia tarehe 5 Novemba na kusafirishwa kwenda kijiji cha Kibosho, mkoani Kilimanjaro, ambako alizikwa.

Neema Munuo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwaka mmoja baadaye, Neema anasema maumivu ya kumpoteza binti yake bado yanamuathiri. Anasema majonzi hayo yameathiri afya yake na uwezo wake wa kufanya kazi. Ameutumia muda mwingi wa mwaka uliopita akiwa nyumbani, huku watoto wake wawili waliobaki wakijaribu kukabiliana na msiba huo.

"Ni siku ambayo sitawahi kuisahau maishani mwangu. Kila ninapoikumbuka, nahisi maumivu makubwa ndani ya moyo wangu. Moyo wangu umekuwa ukilia kila siku. Ni siku ambayo nilimpoteza binti yangu wa pekee," anasema.

Neema anasema alitarajia mamlaka zingetambua mateso ya familia zilizopoteza wapendwa wao na kuwapa faraja. Anaamini kuwa maumivu na hasara waliyoipata bado havijatambuliwa ipasavyo.

Anataka mamlaka zisikilize sauti za familia zilizoathiriwa, zitambue mateso yao na kutoa majibu kuhusu haki na uwajibikaji.

Kwa Neema, kupata haki ni njia ya kuhakikisha kuwa vifo vya wapendwa wao havisahauliki, na kwamba familia zilizoathirika haziachwi kubeba maumivu hayo peke yao.

Manusura wanahangaika kugharamia matibabu

Meshack

Kwa Meshack Sane (33), athari za ghasia hizo zimekuwa za kimwili na kifedha pia.

Baba huyo wa watoto watatu anasema alipigwa risasi mguuni na hadi sasa amefanyiwa zaidi ya upasuaji mkubwa tano. Hata hivyo, bado anahitaji upasuaji zaidi, lakini hana uwezo wa kumudu gharama za matibabu hayo.

Meshack anasema baadhi ya hospitali hapo awali zilikataa kuwahudumia watu waliojeruhiwa wakati wa ghasia hizo na badala yake kuwapeleka katika hospitali za serikali. Pia anadai kwamba katika baadhi ya hospitali hizo, alilazimika kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kupata matibabu.

Anasema ndugu zake walitafuta msaada kutoka kwa viongozi wa eneo lao na Mkuu wa Wilaya. Kwa mujibu wa Meshack, waliambiwa kuwa serikali haikuwa imetenga fedha za kusaidia watu walioathiriwa na matukio ya Oktoba. BBC haikuweza kuthibitisha kwa njia huru maelezo ya mazungumzo hayo.

Meshack anasema alikaa hospitalini kwa miezi saba kabla ya familia yake kushindwa kuendelea kugharamia matibabu yake.

"Tumefanya kila tulichoweza, lakini tumefikia mwisho wa uwezo wetu," anasema.

"Serikali inapaswa kuangalia hali ya sisi tuliopatwa na madhila haya ili tupate matibabu, kwa kuwa baadhi yetu bado tunaumwa sana. Hatuwezi tena kumudu gharama ya matibabu."

Anasema bado anahitaji kufanyiwa upasuaji mwingine mara mbili.

Kwa Meshack, jambo la muhimu zaidi kwa sasa ni kupata huduma za matibabu, kwake na kwa wengine ambao majeraha yao bado yanaendelea kuathiri maisha yao.

Simulizi ya Meshack inaonyesha athari za muda mrefu za majeraha makubwa, ambazo huendelea kuzibebesha familia gharama na changamoto za kifedha hata baada ya hali ya dharura kuisha.

Mzigo wa kulea familia peke yake

Kwa Mwajuma Hamisi (32), kifo cha mume wake kimemuachia jukumu la kulea watoto wao watano peke yake, bila msaada wa mtu ambaye familia hiyo ilikuwa ikimtegemea.

Anasema mume wake, George Kisivani, alipigwa risasi tarehe 29 Oktoba 2025 na kufariki dunia siku mbili baadaye.

Wanandoa hao walikuwa wamepanga kufunga ndoa rasmi Desemba mwaka huo na walikuwa na ndoto ya kujenga nyumba yao. Hata hivyo, mipango hiyo haikutimia.

Kwa sasa, Mwajuma huuza mboga katika soko la karibu ili kuikimu familia yake.

"Nilimpoteza mume wangu ambaye alikuwa tegemeo la familia yetu yenye watoto watano. Sasa hatuna chanzo kingine cha kututegemeza. Nimebaki kupambana peke yangu kuihudumia familia. Hatuna msaada mwingine wowote," anasema.

Anasema watoto wao pia wamekuwa na wakati mgumu kuelewa kilichotokea kwa baba yao. Wale wadogo bado hawaelewi kikamilifu kifo chake, huku wakubwa wakimuuliza maswali kuhusu jinsi alivyopigwa risasi.

Mwajuma anasema familia yake haijapata msaada wowote tangu tukio hilo litokee.

Simulizi yake inaonyesha athari za muda mrefu za kumpoteza mtegemezi mkuu wa familia, ambapo mzazi aliyebaki analazimika kubeba jukumu la kulea na kuhudumia watoto huku akiendelea kukabiliana na maumivu ya msiba.

Mpwa aliyetoweka bila kuacha alama

.

Kaskazini-magharibi mwa Tanzania, Juma Nasibu bado anaishi na maumivu ya kutojua hatima ya mpwa wake wa miaka 25, Juma Shabani.

Shabani alikuwa akifanya kazi katika shamba la mjomba wake, ambako alikuwa akijifunza mbinu za kilimo kwa matumaini ya kuanzisha shamba lake mwenyewe siku zijazo. Jioni, mara kwa mara alikuwa akitembelea kibanda umiza cha eneo hilo, mahali ambapo wakazi walikusanyika kutazama mechi za mpira wa miguu na taarifa za habari.

Mjomba wake anasema baadaye alipata taarifa kuwa Shabani alikuwa miongoni mwa watu waliouawa katika kibanda hicho wakati wa ghasia.

Kwa mujibu wa familia, rafiki aliyekuwa pamoja na Shabani siku hiyo alisimulia kuwa watu walitolewa nje, wakaamriwa kuinua mikono yao juu, kisha wakapigwa risasi. BBC haikuweza kuthibitisha madai hayo wala kubaini waliohusika na tukio hilo.

Siku chache baadaye, Juma anasema alienda Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Sekou Toure mjini Mwanza kutambua miili ya waliouawa, lakini hakufanikiwa kuupata mwili wa mpwa wake.

Familia iliendelea kumtafuta katika maeneo mbalimbali, yakiwemo vituo vya polisi na gereza la karibu, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda.

Mwaka mmoja baadaye, mwili wa Shabani bado haujapatikana.

"Kitu kinachoniumiza zaidi hadi wa leo ni kwamba hatukuwahi kuupata mwili wake," anasema Juma.

Kutopatikana kwa mwili huo kumeendelea kuiacha familia katika hali ya sintofahamu. Juma anasema wakati mwingine hujiuliza iwapo baadhi ya ndugu zake wanaamini hakufanya juhudi za kutosha kumtafuta mpwa wake.

"Hunifanya nijiulize, inawezekanaje mtu kufa halafu apotee bila kuacha alama yoyote?" anasema.

Kwa Juma, kuupata mwili wa mpwa wake kungesaidia familia kufahamu kilichomkuta na kuwapa mahali pa kwenda kumkumbuka na kumuomboleza.

Simulizi yake pia inaangazia changamoto ya kuwatafuta watu ambao miili yao haikupatikana baada ya ghasia hizo, na maumivu ya muda mrefu ambayo familia zao zinaendelea kuyabeba kwa kutojua hatima ya wapendwa wao.

Ni nini kinachojulikana kuhusiana na vifo hivyo?

.

Simulizi za familia zilizoathiriwa zinakuja wakati ambapo bado kuna maswali mengi kuhusu ukubwa wa ghasia hizo, waliohusika na vifo vilivyotokea, na hatua ambazo mamlaka zitachukua kushughulikia athari zake.

Ghasia hizo zilizuka baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 uliogubikwa na utata, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi kwa karibu asilimia 98 ya kura.

Kiongozi wa upinzani, Tundu Lissu, alikuwa amekamatwa mwezi Aprili 2025 na kushtakiwa kwa uhaini baada ya kuendesha kampeni chini ya kauli mbiu ya "No reforms No Election". Amekuwa akikanusha shitaka hilo.

Serikali ilikanusha madai ya kuwalenga raia wasio na hatia na badala yake ikawalaumu watu wa ndani na nje ya Tanzania kwa kuchochea ghasia hizo. Rais Samia pia alisema maandamano hayo yalikuwa sehemu ya njama za kuiangusha serikali yake na kudai kuwa yalifadhiliwa na wadau kutoka nje ya nchi.

Mwezi Aprili 2026, tume ya uchunguzi iliyoteuliwa na serikali iliripoti kuwa watu 518 walifariki kutokana na vifo visivyo vya kawaida, wakiwemo 197 waliouawa kwa kupigwa risasi. Tume hiyo pia ilieleza kuwa zaidi ya watu 2,000 walijeruhiwa.

Hata hivyo, mwenyekiti wa tume hiyo, Mohamed Chande Othman, hakubainisha ni nani aliyewajibika kwa vifo hivyo na badala yake alipendekeza uchunguzi zaidi ufanyike.

Vyama vya upinzani na makundi ya kutetea haki za binadamu vimetoa takwimu za juu zaidi za waliofariki na vimezituhumu vyombo vya usalama kwa kuwaua waandamanaji. BBC pia imethibitisha video kadhaa zinazoonyesha polisi wakifyatua risasi kuelekea makundi ya waandamanaji wakati wa ghasia hizo.

Katika ripoti iliyochapishwa kwenye kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kuanza kwa ukandamizaji huo, Amnesty International imesema mamlaka za Tanzania zimeshindwa kuwawajibisha waliohusika na matukio ya vurugu. Shirika hilo linasema hakuna afisa aliyefunguliwa mashtaka, kuchunguzwa au kuadhibiwa kutokana na matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.

Amnesty pia inadai kuwa katika mwaka uliopita imekusanya ushahidi wa ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu, ukiwemo ukamataji wa kiholela, utekaji, kupotezwa kwa watu kwa lazima, pamoja na vitendo vinavyoweza kufasiriwa kama mateso au ukatili mwingine.

Kwa mujibu wa shirika hilo, ripoti ya tume ya kwanza iliyoteuliwa na serikali ilikabidhiwa kwa Rais Samia mwezi Aprili 2026, lakini haikuwa imewekwa wazi kwa umma hadi tarehe 28 Oktoba 2026.

Ingawa serikali imetangaza kuundwa kwa tume ya pili ya uchunguzi, maswali kuhusu uwajibikaji, haki kwa waathirika, na hatima ya wale ambao bado hawajapatikana yanaendelea kubaki bila majibu.

Kwa familia kama za Neema na Juma, maswali hayo ni ya binafsi zaidi. Wanataka kufahamu kilichowapata wapendwa wao, waliohusika na vifo au kutoweka kwao, na iwapo uchunguzi unaoendelea utasababisha haki kutendeka.

Kwa manusura kama Meshack, swali kubwa ni kama watapata msaada wa kugharamia matibabu yao yanayoendelea. Kwa Mwajuma, kifo cha mume wake kimemuacha na jukumu la kulea watoto watano bila kipato ambacho familia yao ilikuwa ikiitegemea.

Ni nini kitakachofuata?

Mwanasheria na mtetezi wa haki za binadamu, Dkt. Anna Henga
Maelezo ya picha, Mwanasheria na mtetezi wa haki za binadamu, Dkt. Anna Henga

Mwanasheria na mtetezi wa haki za binadamu, Dkt. Anna Henga, anasema serikali inapaswa kutambua kwamba makosa yalifanyika wakati wa ghasia hizo na kuchukua hatua za kuwajibikia madhara yaliyotokana nayo.

Anaamini hatua hiyo inapaswa kufuatiwa na fidia pamoja na msaada wa muda mrefu kwa manusura na familia zilizopoteza wapendwa wao.

"Ushauri wangu kwa serikali ni kwanza kukubali kwamba makosa yalifanyika. Baada ya hapo, iwafidie waathirika, kwa mfano kwa kuanzisha mfuko au mfumo wa bima utakaowasaidia," anasema.

Dkt. Henga anasema mfuko maalum unaweza kusaidia watu waliojeruhiwa vibaya, kama wale waliovunjika au kupata majeraha yanayohitaji matibabu ya muda mrefu.

Pia anatoa wito juhudi zaidi zifanyike kuwatafuta watu ambao bado hawajulikani walipo, kubaini maeneo walikozikwa baadhi ya waliopoteza maisha, na kusaidia familia kupata majibu kuhusu mahali walipozikwa wapendwa wao.

Serikali tayari imechukua hatua ya kuunda tume ya pili ya uchunguzi kuhusu ghasia hizo.

Mwezi Agosti 2026, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua tume hiyo na kuipa miezi mitano kuchunguza waliohusika kupanga, kufadhili, kuratibu au kutekeleza ghasia hizo. Tume hiyo pia imepewa jukumu la kuchunguza madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi na kutafuta taarifa kuhusu watu ambao bado hawajapatikana.

"Tume hii itafanya uchunguzi zaidi ili kubaini nani alichochea ghasia hizo, nani alihusika na nani aliyefadhili matukio hayo katika nchi yetu," alisema Rais Samia.

Uchunguzi huo unaweza kutoa majibu zaidi kuhusu nani anayewajibika kwa ghasia hizo. Matokeo yake, pamoja na hatua zitakazofuata, yatakuwa muhimu katika kubaini kama maswali yanayoibuliwa na familia za waathirika na watetezi wa haki za binadamu yatapatiwa majibu.

Mbali na vifo na majeruhi, ghasia hizo pia zilivuruga maisha ya wananchi na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya umma. Ingawa baadhi ya miundombinu hiyo imejengwa upya, hali hiyo haijafuta maswali yanayozisumbua familia zilizopoteza ndugu zao wala changamoto zinazowakabili manusura wenye majeraha makubwa.

BBC iliiomba serikali kufanya mahojiano kuhusu suala hilo, lakini haikupata majibu. Polisi pia hawakujibu maswali kuhusu miili ambayo haijapatikana, wanaodaiwa kuhusika na mauaji, pamoja na madai kwamba baadhi ya watu wanaogopa kuzungumzia yaliyotokea.

Mwaka mmoja baadaye, kilio cha familia nyingi bado ni kilekile: kujua kilichowakuta wapendwa wao, kuwatafuta waliopotea, kuwapa msaada manusura, na kufahamu kama waliohusika na vifo hivyo watawajibishwa.