Adenocarcinoma: Ifahamu saratani ya mapafu anayougua Papa

Papa Leo
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Papa Leo XIV amegundulika kuwa na saratani ya mapafu baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa sehemu ya chini ya pafu lake la kulia, Vatican imetangaza.

Papa huyo mwenye umri wa miaka 71 alifanyiwa upasuaji wa dakika 90 katika Hospitali ya Gemelli mjini Rome siku ya Jumanne. Madaktari walisema vipimo vilivyofanyika wakati wa upasuaji huo vilibaini kuwa ana adenocarcinoma ya mapafu, aina mojawapo ya saratani ya mapafu.

Katika taarifa yake, Vatican ilisema upasuaji huo ulifanikiwa na kwamba Papa amerejea katika makazi yake baada ya kuwa chini ya uangalizi wa madaktari kwa muda mfupi.

Hata hivyo, adenocarcinoma ya mapafu ni ugonjwa gani? Upasuaji aliofanyiwa Papa ulikuwa wa kiwango gani? Na itamchukua muda gani kurejea katika shughuli zake za kawaida?

Adenocarcinoma ni nini?

Kwa mujibu wa Vatican, madaktari waligundua uvimbe kwenye pafu la Papa Leo XIV wakati wa uchunguzi wa kawaida wa afya.

Adenocarcinoma ni aina ya saratani ya mapafu inayotokea kwenye seli zinazozalisha ute ndani ya mapafu. Ni miongoni mwa aina zinazopatikana mara nyingi zaidi za saratani ya mapafu.

Kwa Papa Leo XIV, vipimo vilivyofanyika wakati wa upasuaji vilithibitisha kuwa uvimbe huo ulikuwa adenocarcinoma ya mapafu. Ugonjwa huo uligunduliwa baada ya uchunguzi wa afya wa kawaida.

Uvimbe huo hupatikana katika eneo dogo la tishu zisizo za kawaida kwenye pafu na mara nyingi huwa si saratani. Kwa mujibu wa Shirika la Marekani la Magonjwa ya Kifua (ATS), chini ya asilimia 5 ya vinundu vidogo vya mapafu huwa vya saratani, ingawa hatari huongezeka kulingana na umri, ukubwa wa kinundu na sababu nyingine kama uvutaji sigara.

Kwa kawaida, uvimbe huo huonekana kama doa au kivuli cheupe kwenye picha za CT scan kutokana na kuwa na msongamano mkubwa kuliko tishu za kawaida za mapafu.

Hata hivyo, katika hali ya Papa Leo XIV, uchunguzi wa tishu uliofanyika wakati wa upasuaji ulithibitisha kuwa uvimbe huo ulikuwa adenocarcinoma ya mapafu, aina ya saratani inayotokana na seli zinazozalisha ute ndani ya mapafu.

Je, upasuaji huo ulikuwa mkubwa?

.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Uchunguzi wa sampuli za tishu uliofanyika wakati wa upasuaji ulithibitisha utambuzi wa saratani ya mapafu aina ya adenocarcinoma, kama ilivyokuwa imeashiriwa na vipimo vya awali vya uchunguzi kabla ya upasuaji," walisema madaktari Luigi Carbone na Stefano Margaritora katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Vatican.

Adenocarcinoma ni aina inayopatikana kwa wingi zaidi ya saratani ya mapafu na huonekana mara nyingi miongoni mwa watu ambao hawajawahi kuvuta sigara. Kwa mujibu wa Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), kati ya asilimia 50 na 60 ya visa vya saratani ya mapafu vinavyogunduliwa kwa wasiovuta sigara huwa vya aina hii.

Papa Leo XIV, aliyechaguliwa kuongoza Kanisa Katoliki mwezi Mei 2025, ni miongoni mwa mapapa vijana kwa viwango vya uongozi wa kanisa hilo. Anajulikana kwa kupenda michezo, hususan tenisi, na hakuna taarifa za umma zinazoonyesha kuwa ni mvutaji wa sigara au aliwahi kuwa na historia ya maradhi makubwa kabla ya utambuzi huu.

Je, atachukua muda gani kupona?

Vatican imesema kuwa Papa Leo XIV anahitaji takriban wiki moja ili kuendelea na hatua za awali za kupona baada ya upasuaji.

Papa huyo anatibiwa katika Hospitali ya Gemelli mjini Roma, hospitali ya chuo kikuu inayojulikana kwa muda mrefu kwa kuwahudumia viongozi wa Kanisa Katoliki. Baada ya upasuaji huo, alirejea chumbani kwake hospitalini na, kwa mujibu wa Vatican, aliweza kula chakula cha jioni na kukutana na makatibu wake pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Vatican.

Awali, Vatican ilieleza kuwa madaktari waliondoa sehemu ya chini ya pafu lake la kulia kwa kutumia mbinu ya upasuaji inayosaidiwa na kamera ya video. Madaktari Luigi Carbone na Stefano Margaritora walisema operesheni hiyo ilifanyika kwa lengo la kuhakikisha uvimbe unaondolewa kikamilifu.

Upasuaji huo ulidumu kwa takriban dakika 90, ingawa Papa alitumia karibu saa tatu katika chumba cha upasuaji. Madaktari walisema operesheni hiyo ilifanikiwa na hakukuwa na matatizo yoyote yaliyojitokeza wakati wa upasuaji.

Vatican imesema matokeo ya vipimo vya ziada yatatangazwa yatakapokamilika.

Hospitali ya Gemelli ina historia ya kuwahudumia mapapa. Marehemu Papa Fransisko alipatiwa matibabu hapo mara kadhaa kabla ya kifo chake mwaka 2025, huku Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili akiitaja hospitali hiyo kwa utani kama "Vatikani ya Tatu", akimaanisha umuhimu wake katika huduma za afya kwa viongozi wa Kanisa Katoliki.

Papa ataendelea vipi na shughuli zake?

Kabla ya kulazwa hospitalini, Papa Leo XIV alifuta shughuli zake zote za hadhara zilizokuwa zimepangwa kati ya Jumanne na Oktoba 20.

Hata hivyo, licha ya kutarajiwa kufanyiwa upasuaji, aliendelea kutekeleza ratiba yake yote ya kazi Jumatatu asubuhi. Ratiba iliyotolewa na Vatican ilionyesha kuwa alikutana na maaskofu waliokuwa wametembelea Vatican kutoka Argentina, Nicaragua, Japan, Nigeria na Marekani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Papa pia alikutana na wanachama wa shirika moja la misaada lenye makao yake mjini Roma, ambapo alizungumza kwa sauti thabiti na kuwashukuru kwa kazi yao.

Papa Leo XIV, ambaye anaongoza waumini wapatao bilioni 1.4 wa Kanisa Katoliki duniani, alikuwa amepangiwa kushiriki katika shughuli kadhaa za hadhara wiki hiyo, ikiwemo kuongoza Misa katika Uwanja wa Mtakatifu Petro siku ya Jumatano.

Hata hivyo, Vatican ilitangaza kuwa Misa hiyo itaongozwa na Kardinali Luis Tagle.

Papa huyo pia anatarajiwa kufanya ziara nchini Uruguay, Argentina na Peru kati ya Novemba 6 na 17. Bado haijafahamika iwapo upasuaji alioufanyiwa na kipindi chake cha kupona vitaathiri safari hiyo, ambayo inajumuisha safari za ndege, helikopta na matembezi katika maeneo ya miinuko mikubwa nchini Peru.

Hata hivyo, Papa alisema Jumapili kwamba bado ana nia ya kuendelea na ziara hiyo kama ilivyopangwa.

Nani hutekeleza majukumu Papa anapougua

Papa ndiye kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani na hakuna mtu anayechukua nafasi yake moja kwa moja anapokuwa mgonjwa.

Kabla ya kulazwa hospitalini, Papa Leo XIV alifuta shughuli zake zote za hadhara kati ya Jumanne na Oktoba 20. Hata hivyo, kabla ya upasuaji wake, aliendelea kutekeleza ratiba yake ya kawaida. Kwa mujibu wa Vatican, Jumatatu alikutana na maaskofu kutoka Argentina, Nicaragua, Japan, Nigeria na Marekani. Pia alizungumza na wanachama wa shirika moja la kutoa misaada mjini Roma, ambapo alisikika akizungumza kwa sauti thabiti na kuwashukuru kwa kazi yao.

Papa Leo anaongoza zaidi ya waumini bilioni 1.4 wa Kanisa Katoliki duniani. Alikuwa amepangiwa kuhudhuria shughuli kadhaa wiki hii, ikiwemo kuongoza Misa katika Uwanja wa Mtakatifu Petro siku ya Jumatano. Hata hivyo, Vatican imesema Misa hiyo itaongozwa na Kardinali Luis Tagle.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi