Wafahamu wafanyabiashara wenye utata kama Wicknell Chivayo

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Mipango ya mazishi ya aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, inaendelea nyumbani kwao kijijini Gandami katika wilaya ya Chikomba.

Wakati wengi wakimkumbuka kama mfanyabiashara aliyependa kuonyesha utajiri wake kupitia magari ya kifahari, ndege, majumba makubwa na zawadi kwa watu mashuhuri pamoja na wenye uhitaji, wengine wanakumbuka tuhuma za ufisadi na zabuni za serikali zilizomkabili mara kadhaa. Wakosoaji wake walidai kuwa fedha zilizohusishwa na zabuni hizo zingeweza kutumika kuendeleza zaidi Zimbabwe.

Kutokana na mjadala huo, tunawaangazia baadhi ya watu mashuhuri barani Afrika ambao, kama Chivayo, wamejenga utajiri mkubwa huku wakikumbwa na maswali, utata au kesi za kisheria kuhusu namna walivyoupata.

Kilichowaunganisha wengi wao ni simulizi ya kuanzia maisha ya kawaida au ya umaskini na baadaye kufikia utajiri mkubwa na ushawishi wa kisiasa au kijamii.

Wengi wao walitokea katika mazingira magumu, walijijenga kibiashara kwa kasi kubwa na wakati huohuo wakakabiliwa na tuhuma za ufisadi, utapeli, zabuni tata za serikali au biashara zilizozua maswali mengi kuhusu chimbuko la utajiri wao.

1. Kenny Kunene (Afrika Kusini)

g

Kenny Kunene, aliyezaliwa Oktoba 21, 1970, ni mfanyabiashara, mwanasiasa, mzungumzaji wa motisha, mwanaharakati na mwalimu wa zamani wa Afrika Kusini.

Kabla ya kuingia siasani, alifanya kazi kama mwalimu wa Kiingereza katika shule ya sekondari. Baadaye alifungua biashara ya pombe na kuanza kujihusisha na shughuli za uhalifu, zikiwemo wizi na ulaghai.

Mwaka 1997 alihukumiwa kwa kuendesha mpango wa kitapeli wa Ponzi na kutumikia miaka sita gerezani.

Baada ya kutoka gerezani, alijijenga upya kupitia biashara, hotuba za motisha na siasa. Umaarufu wake uliongezeka kutokana na maisha ya anasa na sherehe za kifahari alizokuwa akiandaa.

Mwaka 2011 aliibua mjadala mkubwa baada ya kuandaa kile kilichojulikana kama "sherehe za sushi", ambapo wageni walikula sushi iliyowekwa kwenye miili ya wanawake waliovalia mavazi madogo.

Kwa sasa amewahi kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama cha Patriotic Alliance na ameendelea kuwa mmoja wa watu wenye ushawishi katika siasa za Afrika Kusini.

2. Nana Kwame Bediako (Cheddar) – Ghana

d

Nana Kwame Bediako, anayejulikana pia kama Freedom Jacob Caesar au Cheddar, ni mjasiriamali wa Ghana anayejihusisha na sekta ya majengo.

Alizaliwa Februari 13, 1980, na amejijengea jina kupitia kampuni yake ya Kwarleyz Group, pamoja na miradi mikubwa kama Wonda World na Petronia City.

Pia alianzisha New Africa Foundation, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi barani Afrika.

Mwaka 2024 alijitosa rasmi katika siasa kupitia vuguvugu la New Force Movement na kugombea urais nchini Ghana.

Licha ya kujitambulisha kama mfano wa mafanikio ya kizazi kipya cha wafanyabiashara wa Afrika, kumekuwa na maswali ya muda mrefu kuhusu ukubwa wa utajiri wake, kasi ya mafanikio yake na vyanzo vya baadhi ya miradi yake, jambo ambalo limeendelea kuwa mjadala katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

3. Gayton McKenzie (Afrika Kusini)

Gayton McKenzie ni mwanasiasa na mfanyabiashara wa Afrika Kusini ambaye kwa sasa ni Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni.

Alizaliwa Machi 10, 1974 na alihukumiwa kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha akiwa kijana na kutumikia miaka minane gerezani.

Umaarufu wake uliongezeka baada ya kuachiwa huru, alipokuwa akiandika kuhusu maisha ya gerezani na kuzungumza hadharani kuhusu makosa aliyoyafanya.

Baadaye aliingia katika biashara, uandishi wa vitabu na mazungumzo ya motisha kabla ya kuingia kikamilifu katika siasa.

Mwaka 2013 alikuwa mmoja wa waanzilishi wa chama cha Patriotic Alliance, ambacho amekiongoza kwa miaka kadhaa.

Kwa wafuasi wake, McKenzie ni mfano wa mtu aliyebadilisha maisha yake baada ya uhalifu. Kwa wakosoaji wake, historia yake ya uhalifu inaendelea kuwa sehemu ya mjadala kuhusu uongozi wake.

4. Ramon Olorunwa Abbas (Hushpuppi) – Nigeria

y
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ramon Olorunwa Abbas, maarufu kama Hushpuppi, ni mmoja wa watu maarufu zaidi kuwahi kuonyesha maisha ya kifahari kupitia mitandao ya kijamii.

Akiwa anaishi Dubai, alifahamika kwa kuposti magari ya kifahari, saa za bei ghali, ndege binafsi, mavazi ya chapa maarufu na picha akiwa pamoja na watu mashuhuri.

Kwa muda mrefu alijitambulisha kama mfanyabiashara wa sekta ya majengo.

Hata hivyo, mwaka 2020 alikamatwa Dubai katika operesheni iliyohusisha mamlaka za Umoja wa Falme za Kiarabu na FBI ya Marekani.

Baadaye alikabidhiwa Marekani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 11 gerezani baada ya kukiri kuhusika katika njama za utakatishaji wa fedha na ulaghai wa kimtandao.

Waendesha mashtaka wa Marekani walimtaja kama mmoja wa wahusika wakuu katika mtandao mkubwa wa kimataifa wa uhalifu wa mtandaoni uliohusisha mamilioni ya dola.

Wakati wa kukamatwa kwake, maafisa walikamata kiasi kikubwa cha fedha taslimu, magari ya kifahari, simu, kompyuta na vifaa vingine vya mawasiliano.

Nini kinawaunganisha?

Licha ya tofauti zao, watu hawa pamoja na Wicknell Chivayo wana sifa kadhaa zinazofanana:

1. Kuonyesha utajiri hadharani

Kwa wengi wao, utajiri haukuwa tu mali ya binafsi bali sehemu ya utambulisho wao wa umma.

Magari ya kifahari, ndege binafsi, majumba makubwa, mavazi ya gharama kubwa na zawadi za thamani vilitumika kuonyesha mafanikio yao na kujenga taswira ya nguvu na ushawishi.

2. Mchanganyiko wa biashara na siasa

Baadhi yao waliingia moja kwa moja katika siasa, huku wengine wakijenga uhusiano mkubwa na viongozi wa kisiasa au mikataba ya serikali.

Uhusiano huu uliwasaidia kuongeza ushawishi wao wa kijamii na kisiasa.

3. Wafuasi na wakosoaji kwa wakati mmoja

Karibu wote wamegawanya maoni ya umma.

Kwa wafuasi wao, ni mifano ya watu waliojitengeneza wenyewe kutoka mazingira magumu hadi mafanikio makubwa.

Kwa wakosoaji wao, ni mfano wa utajiri wenye maswali mengi, matumizi ya anasa kupita kiasi na wakati mwingine tuhuma za ufisadi au biashara zenye utata.

4. Utajiri uliozua maswali

Ingawa baadhi yao walijenga biashara halali na kufanikiwa kibiashara, safari zao zimeambatana na tuhuma, kesi au maswali yaliyowafanya kuwa miongoni mwa wafanyabiashara wanaozungumziwa zaidi barani Afrika.

Kwa sababu hiyo, majina yao yanaendelea kutajwa kila mara kunapokuwa na mjadala kuhusu utajiri mkubwa, ushawishi wa kisiasa na uwazi wa vyanzo vya mali barani Afrika.