"Falcon Strike Force" ni nini, na kwa nini Marekani 'inahaha' kukiimarisha?

Chanzo cha picha, U.S. Army photo by Spc. Kayla Mc Guire
Wakati ripoti zikionyesha kupungua kwa akiba ya Marekani ya makombora ya masafa marefu na makombora ya kuzuia mashambulizi katika vita dhidi ya Iran, pamoja na kusainiwa kwa mikataba mipya ya kuongeza uzalishaji wake, Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) imetangaza mpango wa kuunda "kikosi cha kwanza cha kimataifa cha droni za mashambulizi."
Kwa mujibu wa tangazo rasmi la CENTCOM, kikosi hicho kitajumuisha droni na mifumo isiyo na rubani inayofanya kazi angani, majini na chini ya maji, na kitaundwa kwa ushirikiano kati ya vikosi vya Marekani na washirika wake wa kikanda.
Mnamo Agosti 13, CENTCOM ilitangaza kuwa imeanza mchakato wa kuunda "Falcon Strike Force", na kwamba mialiko kwa nchi za ukanda huo kujiunga ilikuwa ikiendelea, ingawa haikutaja nchi au washirika watarajiwa.
Kwa mujibu wa mpango huo, kikosi kitatumia mifumo ya mashambulizi isiyo na rubani inayoweza kutumika mara moja, angani, juu ya maji na chini ya maji. Kikosi hicho kitaendeshwa na wanajeshi kutoka Marekani na nchi za eneo hilo, huku muundo wa uongozi na uratibu wa shughuli ukisimamiwa na Kamandi Kuu ya Operesheni Maalum ya CENTCOM.
Tathmini kutoka kwa taasisi za utafiti wa kijeshi na ripoti mbalimbali za vyombo vya habari zinaonyesha kuwa vita dhidi ya Iran vimepunguza kwa kiasi kikubwa akiba ya Marekani ya baadhi ya silaha za masafa marefu na makombora ya ulinzi wa anga. Hata hivyo, Pentagon na Ikulu ya Marekani zimesisitiza kuwa nchi hiyo bado ina risasi na silaha za kutosha kuendelea na operesheni.
Wakati huohuo, mashambulizi ya Iran yameonyesha pia udhaifu wa vituo vya kijeshi na miundombinu isiyohamishika katika eneo hilo.
Stacey Pettyjohn, mkurugenzi wa programu ya ulinzi katika Center for a New American Security, aliambia BBC Persian kwamba droni zimefanya mashambulizi ya masafa marefu kuwa rahisi zaidi. Kwa sababu hiyo, vituo vya kijeshi, miundombinu ya kiraia na vituo vya kiuchumi vimekuwa katika hatari zaidi ya kushambuliwa.
Kwa mujibu wa Pettyjohn, mifumo ya bei nafuu na inayopatikana kwa wingi imebadilisha uwiano wa nguvu kwa manufaa ya mshambuliaji, kwa sababu mifumo mingi ya ulinzi inayotumika Mashariki ya Kati ni ghali na ni haba.
Mpango mpya wa CENTCOM unaweza kuonekana kama sehemu ya juhudi za Marekani kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuongeza mifumo mingi ya bei nafuu ya mashambulizi katika ghala lake la silaha, sambamba na makombora, ndege na meli za kisasa na za gharama kubwa.
Kutoka Scorpio hadi Falcon

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Falcon Strike si jaribio la kwanza la CENTCOM kutumia mifumo isiyo na rubani kwa kushirikiana na vikosi vya eneo hilo. Jeshi la Wanamaji la Marekani lilianzisha Task Force 59 nchini Bahrain mnamo Septemba 2021. Lengo lake la awali lilikuwa kutumia droni na akili mnemba kufuatilia maji ya eneo hilo, kuanzia Mlango-Bahari wa Hormuz hadi Bab al-Mandeb na Mfereji wa Suez.
Kwa mujibu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, kufikia mwanzoni mwa 2024 kikosi hicho kilikuwa kimefanyia majaribio au kutumia zaidi ya aina 23 za mifumo isiyo na rubani. Shughuli zake zilifanya zaidi ya upelelezi na, katika zoezi la mwaka 2023, kilijaribu kurusha risasi za moto kutoka kwenye mfumo usio na rubani.
Mnamo Agosti mwaka huo, Pentagon ilianzisha mpango wa "Replicator" kwa lengo la kuingiza maelfu ya mifumo ya kiotomatiki, ya gharama nafuu na inayoweza kubadilishwa kwa urahisi katika vikosi vya kijeshi ndani ya miezi 18 hadi 24.
Sera hiyo iliendelea mwaka 2025 kupitia mpango wa "Drone Supremacy". Desemba iliyopita, Idara ya Vita ya Marekani ilitangaza mipango ya kutenga dola bilioni moja kuzalisha takribani mifumo 340,000 midogo ya anga isiyo na rubani ndani ya miaka miwili.
Wakati huohuo, CENTCOM iliunda Scorpion Strike Force, iliyotajwa kuwa kikosi cha kwanza maalum cha Marekani cha droni za mashambulizi katika Mashariki ya Kati.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, alisema nchi hiyo haiwezi kumudu kutumia makombora yenye thamani ya dola milioni mbili kukabiliana na droni za bei nafuu.

Chanzo cha picha, U.S. Central Command Public Affairs via DVIDS
Mfumo wa Lucas kwa muhtasari
- Mfumo wa mashambulizi wa kijeshi usio na rubani, wa gharama nafuu
- Bei kwa kila ndege: takribani dola 35,000
- Unaweza kurushwa kutoka ardhini, kwenye gari au kwenye sitaha ya meli
- Ulitumika katika Scorpion Strike Force
- CENTCOM inasema ulitumika katika vita dhidi ya Iran
- Inadaiwa muundo wake umeathiriwa na droni ya Iran aina ya Shahed.
"Lucas" $35,000

Chanzo cha picha, U.S. Army photo by Spc. Kayla Mc Guire
Mpango wa kuunda Kikosi cha Falcon Strike Force unaweza pia kuonekana katika muktadha huu: kupanua matumizi ya mifumo ya mashambulizi ya bei nafuu na yenye idadi kubwa, sambamba na silaha za kisasa na za gharama kubwa za Marekani.
Mfumo wa Lucas, au Low-Cost Unmanned Combat Attack System, ni miongoni mwa mifumo inayojulikana zaidi katika mpango wa Marekani wa droni za mashambulizi katika eneo hilo. Reuters iliripoti mapema Machi 2026 kuwa muundo wa droni hiyo, ambayo CENTCOM imesema inagharimu takribani dola 35,000 kwa kila moja, uliathiriwa na droni ya Iran aina ya Shahed.
Lucas inaweza kurushwa kutoka ardhini, kwenye gari au kwenye sitaha ya meli. CENTCOM inasema mfumo huo ulitumika katika Operesheni Epic Fury dhidi ya Iran.
Mnamo Juni 2026, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani, helikopta aina ya Corsair ilitumika kuwaokoa wanajeshi wawili wa kikosi cha helikopta aina ya Apache iliyokuwa imeanguka katika pwani ya Oman. "Helikopta hiyo iliwachukua na kuwapeleka eneo jingine baharini, ambako walipandishwa kwenye helikopta nyingine ili kuendelea na safari," alisema wakati huo msemaji wa CENTCOM, Tim Hawkins.
Mwezi mmoja baadaye, CENTCOM ilitangaza kuwa helikopta tatu za Corsair zilishambulia vituo vya ukarabati wa meli na nyambizi katika kituo cha kijeshi cha majini cha Bandar Abbas, operesheni ambayo CENTCOM iliitaja kuwa matumizi ya kwanza ya droni za mashambulizi za Marekani katika mapigano.

Chanzo cha picha, U.S. Central Command Public Affairs via DVIDS
Kambi Kubwa, Malengo Makubwa
Uwepo wa kijeshi wa Marekani katika Ghuba ya Uajemi umejikita kwa kiasi kikubwa katika kambi chache kubwa. Kambi ya Udeid nchini Qatar ni kitovu kikuu cha operesheni za anga za Marekani katika eneo hilo; Meli ya Tano ya Marekani iko Bahrain; na Camp Arifjan nchini Kuwait ni mojawapo ya vituo vikuu vya msaada kwa vikosi vya ardhini vya Marekani.
Kambi ya Arifjan nchini Kuwait iko takribani kilomita 100 kutoka Iran, makao makuu ya Meli ya Tano ya Marekani nchini Bahrain yako takribani kilomita 205, huku kambi ya Al-Udeid nchini Qatar ikiwa takribani kilomita 275 kutoka Iran. Kwa mujibu wa Council on Foreign Relations, mpangilio huu wa kambi ulikuwa na faida wakati wa vita vya Iraq na Afghanistan. Hata hivyo, kadiri masafa na usahihi wa makombora na droni za Iran vilivyoongezeka, kambi kubwa na zisizohamishika za Marekani katika Ghuba ya Uajemi zimekuwa katika hatari zaidi.
Stacey Pettyjohn aliiambia BBC Persian kuwa vita dhidi ya Iran vimeonyesha kwamba "kambi zisizohamishika pamoja na ndege na meli kubwa ziko katika hatari." Vikosi vidogo vilivyosambazwa katika maeneo mbalimbali — kuanzia droni zinazozinduliwa ardhini hadi boti na mifumo isiyo na rubani chini ya maji — ni vigumu zaidi kugundua na kulenga. Na vikiharibiwa, gharama yake ndogo hufanya hasara hiyo kuwa rahisi kuvumilia.
Alisema huenda Marekani ikawa inafanya mapitio ya "mpangilio wake wa wakati wa amani" katika eneo hilo: "Kwa kuzingatia ukaribu wa kambi za Marekani katika Ghuba ya Uajemi na Iran, sidhani kama uwekaji wa ndege zenye marubani na meli katika kambi hizi utaendelea kama ilivyokuwa hapo awali."
Kwa kuzingatia hilo, moja ya faida zinazoweza kupatikana kutokana na mpango wa Falcon Strike Force ni kupunguza utegemezi wa uwezo wa mashambulizi wa Marekani kwenye kambi na majukwaa machache makubwa na yasiyohamishika. Droni na vyombo vya majini visivyo na rubani vinaweza kupelekwa kutoka maeneo na majukwaa mbalimbali.
Hata hivyo, Bi Pettyjohn anasisitiza kuwa hakuna suluhisho kamili. Anasema mifumo ya bei nafuu zaidi ya kukabiliana na droni, kuimarisha vituo na kutumia vifaa vya kuigiza au kupotosha mashambulizi vinaweza kupunguza hatari, lakini baadhi ya hatari bado zitaendelea kuwepo.

Chanzo cha picha, U.S. Central Command Public Affairs via DVIDS
"Kimataifa" kwenye karatasi, mtihani upo kwenye utekelezaji
Huenda sehemu ngumu zaidi ya kutekeleza mpango wa Falcon Strike Force isiwe kupata droni, bali kushawishi nchi za eneo hilo kushiriki waziwazi katika kikosi cha pamoja cha mashambulizi.
Stacey Pettyjohn anasema operesheni zinazohusisha maeneo mbalimbali ni ngumu zaidi kutokana na ushiriki wa vikosi na ujuzi tofauti. Kuifanya kuwa kikosi cha kimataifa kunaweza kuongeza uhalali wa kisiasa na uwezo wa kijeshi, lakini pia kunaweza kupunguza kasi ya maamuzi na kuleta changamoto katika kushirikishana taarifa, kujenga mwafaka na kuhakikisha vifaa vinaendana.
Anaamini motisha kuu ya Marekani kuifanya nguvu hiyo kuwa ya kimataifa huenda ikawa "ya kisiasa na inayohusiana na upatikanaji wa vituo." Vikosi vya Marekani vinahitaji viwanja vya ndege, bandari na mitandao ya mawasiliano ya nchi mwenyeji ili kupeleka vifaa vya kurushia mashambulizi, kufanya matengenezo na kuendesha operesheni.
Nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi zimekuwa zikitegemea Marekani kwa ulinzi wa anga na usalama wa kikanda, lakini wakati wa vita vya hivi karibuni zimejaribu kujitenga na ushiriki wa moja kwa moja katika mashambulizi dhidi ya Iran — rasmi na hadharani.
Maafisa wa Iran pia wameonya kuwa kutakuwa na madhara kwa nchi zitakazoshiriki katika mashambulizi dhidi ya Iran, ikiwa ni pamoja na kutoa vituo na kambi. Kwa hiyo, baadhi ya nchi zinaweza kushiriki tu katika mafunzo, ufuatiliaji wa baharini au ulinzi wa miundombinu, huku zikiwa waangalifu zaidi kuhusu kushiriki katika operesheni za mashambulizi. Nyingine zinaweza kupendelea kushirikiana kwa siri katika masuala ya kijasusi badala ya kuwa wanachama rasmi.
Kilichotangazwa hadi sasa, badala ya kuonyesha kuundwa kwa jeshi tayari la droni, kinaonyesha mwelekeo ambao Marekani inataka kuchukua: kupunguza utegemezi wa silaha chache na ghali, kusambaza vikosi katika maeneo mbalimbali na kushirikisha nchi za eneo hilo.
Kubadilisha mpango huo kuwa kikosi chenye ufanisi kutahitaji uzalishaji wa viwandani, makubaliano ya kisiasa na mfumo wa kuzuia vita visivyotarajiwa kuenea.















