Kwa nini baadhi ya wanafunzi wa vyuo hugeuza mahusiano kuwa biashara?

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wanaweza kujikuta wakitumia mahusiano kama njia ya kujipatia fedha, hali ambayo mwanaharakati wa vijana Luciana Massawe anasema inaweza kuwaweka katika mazingira yenye changamoto za kiafya, kiakili na kijamii.
Luciana, ambaye ni mwanzilishi wa jukwaa la Uni Girls Power na taasisi ya Journey of Nurture and Care (JNC), anasema aliona changamoto hiyo alipokuwa chuoni na kuamua kuhamasisha mabinti kuhusu kujitambua na kutumia fursa wanazopata wakiwa vyuoni.
"Jambo kubwa ambalo nilikuwa naliona chuoni, la tofauti ni suala zima la mahusiano," anasema.
Kwa mujibu wa Luciana, tatizo linatokea pale mahusiano yanapoanza kutazamwa kama njia ya kujipatia kipato.
"Watu wanafanya mahusiano kuwa chanzo cha kipato, yani wanawekeza kwenye mahusiano kama ndio uchumi wao sasa," anasema.
Anasema baadhi ya wanafunzi hujikuta wakiishi maisha yenye mahitaji makubwa kuliko uwezo wao wa kifedha, hali inayoweza kuwafanya kutafuta njia nyingine za kupata fedha.
"Mtu sasa anakuwa ana ratiba mbili, ana ratiba ya masomo na ana ratiba ya kuutumia mwili wake kwaajili ya kupata kipato," anasema.
Uhuru wa maisha ya chuo

Chanzo cha picha, JNCTANZANIA
Luciana anaamini kuwa uhuru wanaoupata vijana wanapoingia chuo kikuu unaweza kuwa na faida ikiwa utatumika kujijenga, lakini pia unaweza kuwa chanzo cha matatizo iwapo utatumika bila mipaka.
"Kwanza kila mtu anakuja chuoni akiwa na mitazamo yake, kuna mwingine anakuja akiamini kwamba ile ndio sehemu pekee ya yeye kupata uhuru, wa kufanya kile kitu ambacho anajisikia," anasema.
Anaongeza kuwa wanafunzi wanapofika chuoni wanaweza kutafuta makundi ya watu wanaoendana nao na kuanza kufanya mambo ambayo huenda hawakuyafanya kabla.
"Kwahiyo kitu pale ni uhuru, uhuru ndio unaomfanya binti au kijana aone hii ndio nafasi pekee ya kuitumia, wakati ule uhuru pia anaweza kuutumia vizuri ukamjenga," anasema.
Kwa mtazamo wake, mahusiano yanapogeuzwa kuwa biashara yanaweza pia kuwa na madhara mengine iwapo hayatafanikiwa.
"Mwisho wa siku yale mahusiano hayafanyi kazi, unakuta sasa mambo mengine yanatokea yani kama mambo ya afya ya akili, mwanaume anaamua kukufanyia makusudi, anakudhalilisha, au mwanamke hivyo hivyo," anasema.
Kujitegemea badala ya kutegemea mahusiano

Chanzo cha picha, JNCTANZANIA
Luciana anawataka wanafunzi kutafuta njia nyingine za kujijengea uwezo wa kifedha badala ya kutegemea mahusiano.
"Kwa nini asiangalie namna ya pili ya kutafuta namna bora na sahihi ambapo atakuwa na uhuru wake wa kifedha," anasema.
Anashauri wanafunzi kutumia muda wanaopata nje ya masomo kujaribu shughuli za ujasiriamali, kujitolea au kujifunza ujuzi ambao unaweza kuwasaidia baada ya kumaliza masomo.
Kwa wanafunzi wanaopokea fedha za matumizi kutoka serikalini, maarufu kama 'boom', Luciana anaona fedha hizo zinaweza pia kutumika kama sehemu ya kujenga biashara ndogo.
"Unaweza ukawa unanunua vitu vya urembo watu wanapenda unawauzia, unaweza ukaja na mbinu nyingine tofauti," anasema.
Anaongeza kuwa wanafunzi wanaweza pia kutumia mitandao ya kijamii kutengeneza maudhui au kujenga mtandao wa watu ambao unaweza kuwasaidia kupata uzoefu na fursa baada ya chuo.
"Kubali uhalisia wa maisha yako"
Kwa vijana wanaohisi wanahitaji kuishi maisha ambayo hawawezi kuyamudu kwa kipato walichonacho, Luciana anasema suluhisho linaanza kwa kukubali hali yao halisi.
"Kwanza mtu akubali uhalisia wa maisha yake," anasema.
Anaamini kwamba kukubali uwezo wa kifedha alionao mtu kunaweza kumsaidia kuweka mipaka na kuepuka kufanya maamuzi kwasababu tu anataka kumudu maisha fulani.
"Utakapo kubali kwanza ulipotoka kukoje, ukakubali uhalisia wa maisha yako, kuna vitu ambavyo sio vya lazima kuvifanya utaviepuka," anasema.
Kwa Luciana, maisha ya chuo si tu kuhusu kupata shahada, bali pia ni nafasi ya kujenga uzoefu, mitandao na uwezo wa kujitegemea.
"Unatakiwa kujijenga na kujipatia wewe mwenyewe kipato," anasema.
Kutoka Uni Girls Power hadi mazingira

Chanzo cha picha, JNCTANZANIA
Mbali na masuala ya uwezeshaji wa vijana, Luciana pia anajihusisha na masuala ya mazingira kupitia JNC.
Anasema alipoanza kujifunza kuhusu taka aligundua kuwa taka zinazotupwa zinaweza kuwa fursa ya kiuchumi.
"Kwenye taka kuna fursa nyingi sana, na kuna pesa pia," anasema.
Kwa mfano, anasema chupa za plastiki zinazotupwa zinaweza kukusanywa na kuuzwa kwa kilo, huku taka nyingine zikibadilishwa kuwa bidhaa zenye thamani.
Kwa Luciana, kutumia fursa zilizopo katika mazingira yanayowazunguka vijana ni sehemu ya kuwasaidia kujenga maisha yao badala ya kutegemea vyanzo vya kipato vinavyoweza kuwaweka kwenye mazingira hatarishi.
Ujumbe wake kwa vijana ni kuanza na kile walicho nacho na kujenga hatua kwa hatua.
"Lakini zaidi ya yote aanze hata na kidogo alicho nacho. Akishainuka na kuanza na kidogo alicho nacho, basi naamini Mungu atamfungulia njia ataendelea kufanya vizuri zaidi."
Wazazi na walezi nao wana nafasi
Luciana pia anasema wazazi na walezi hawapaswi kuacha kuwafuatilia watoto wao wanapofika chuo kikuu wakidhani kuwa sasa wamekuwa watu wazima na hawahitaji tena malezi.
"Mzazi asikifikirie kuwa mtoto ameshafika chuo basi ameshakuwa mtu mzima ameshajitambua, hapana. Mzazi ataendelea kuwa mzazi," anasema.
Anasema wazazi wanapaswa kuendelea kuwa karibu na watoto wao na kuwa tayari kuwasaidia wanapokutana na changamoto, badala ya kuwahukumu.
"Wajibu wake na jukumu lake ni kuhakikisha pia anamuwekea mtoto mazingira mazuri, mtoto anapokuwa na tatizo alichukulie kama ni tatizo aweze kumsaidia."
Kwa Luciana, mawasiliano na ushirikiano kati ya wazazi na watoto ni muhimu hata baada ya mtoto kuanza maisha ya chuo.
"Kwahiyo wazazi waendelee kuonyesha ushirikiano nao na watoto wao, hata kama wameshafika vyuoni kwasababu mambo ni mengi watoto bado wanahitaji kukumbushwa na malezi bado ni msingi."















