Israel: Netanyahu au upinzani? Uchaguzi waacha taifa njia panda

Chanzo cha picha, EPA/Reuters
- Author, David Gritten
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Matokeo ya awali ya kura za maoni baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura nchini Israel yanaashiria kuwa hakuna mshindi wa wazi katika uchaguzi mkuu muhimu, huku Waziri Mkuu wa muda mrefu Benjamin Netanyahu na aliyekuwa mkuu wa jeshi Gadi Eisenkot wakikosa kuonekana kuwa na uwezekano wa kupata viti vya kutosha kuunda serikali.
Vituo viwili vya televisheni nchini humo vilikadiria kuwa chama cha Yashar cha Eisenkot na vyama vingine vitatu vya upinzani vyenye wafuasi wengi wa Kiyahudi, vinavyounda muungano wake wa kisiasa unaoitwa Change Bloc, vingepata viti 51 kati ya 120 katika bunge la Israel, Knesset. Muungano wa Netanyahu, unaojumuisha chama chake cha Likud pamoja na washirika wake wa mrengo mkali wa kulia na vyama vya kidini vya Kiyahudi vya Kiorthodoksi, nao ulikadiriwa kupata viti 51.
Hata hivyo, makadirio ya kituo cha tatu cha utangazaji yalionyesha kuwa muungano wa Netanyahu ulikuwa mbele kwa viti vitatu.
Mengi yatategemea nafasi ya vyama viwili vya Waarabu, ambavyo vilikadiriwa kupata jumla ya viti 18 au 19, idadi ambayo ingekuwa rekodi.
Idadi ya wapiga kura waliojitokeza Jumanne ilikuwa kubwa zaidi katika kipindi cha miongo kadhaa.
Tume ya Uchaguzi ya Israel ilisema kuwa kufikia saa nne usiku kwa saa za huko (22:00), vituo vilipofungwa, asilimia 77.7 ya wapiga kura walikuwa wamepiga kura. Hii ilikuwa idadi kubwa zaidi kufikia muda huo tangu mwaka 1999.
Matokeo rasmi yataanza kutangazwa usiku kucha, lakini inakadiriwa kuwa kura 600,000 zilizopigwa nje ya vituo vya kawaida vya wapiga kura, nyingi zikiwa za wanajeshi, hazitakuwa zimehesabiwa zote hadi Alhamisi. Kura hizo zinakadiriwa kuwa karibu asilimia 10 ya kura zote zilizopigwa.
Baada ya matokeo ya mwisho kuthibitishwa na kufuatia mashauriano na vyama vyote vya kisiasa, rais wa Israel atamwalika kiongozi wa chama anayeamini kuwa ana nafasi nzuri zaidi ya kufanikiwa kuunda muungano wa serikali.
Mchakato huo unaweza kuchukua wiki kadhaa. Iwapo kiongozi huyo atashindwa, hatimaye uchaguzi mwingine utalazimika kufanyika.
Wafuasi wa upinzani washangilia, Netanyahu akataa kushindwa

Chanzo cha picha, BBC/Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika makao makuu ya chama cha Yashar cha Eisenkot mjini Tel Aviv, wafuasi wake walishangilia na kupiga kelele za, "Bibi, rudi nyumbani!", baada ya matokeo ya awali ya kura za maoni kutangazwa na shirika la utangazaji la umma Kan pamoja na vituo vya Channel 12 na Channel 13.
Makadirio hayo yalionyesha kuwa muungano wa Eisenkot ungeibuka na idadi kubwa zaidi ya viti bungeni, ukiwa na kati ya viti 52 na 53, ikilinganishwa na viti 50 vya muungano wa serikali ya Netanyahu.
Eisenkot alisema walikuwa "wameandika historia" na akaahidi kuhakikisha kuwa "uamuzi wa wananchi unatafsiriwa kuwa serikali ya Kizayuni, thabiti na nzuri kwa raia wote wa Israel".
Mshirika wake katika chama cha Beyachad, aliyekuwa waziri mkuu Yair Lapid, alisema muungano wa Netanyahu ulikuwa umepata "kipigo kikubwa".
Hata hivyo, hakukuwa na dalili za Netanyahu na washirika wake kukubali kushindwa katika makao makuu ya chama cha Likud mjini Jerusalem. Makadirio yalionyesha kuwa Likud kingekuwa chama chenye viti vingi zaidi bungeni.
Wafuasi wa chama hicho waliiambia BBC kuwa walikuwa na wasiwasi kuhusu matokeo.
"Itikadi ni moja, lakini bado haijaisha hadi itakapokwisha. Hata hivyo, natokwa na jasho," alisema Itzik, mmoja wa wafuasi wa Netanyahu.
Mshirika wa Netanyahu ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje, Gideon Saar, alisema sherehe za upande wa kushoto zilikuwa za mapema mno.
Naye Waziri wa Usalama wa Taifa, Itamar Ben-Gvir, aliwataka wafuasi wa chama chake cha mrengo mkali wa kulia, Jewish Power, kusali ili matokeo ya mwisho yawezeshe kuundwa kwa "serikali ya mrengo wa kulia pekee".
Mapema Jumatano, vituo vya utangazaji vilisasisha makadirio yao ya kura za maoni. Makadirio ya Kan na Channel 13 yalionyesha kuwa miungano hiyo miwili ilikuwa imelingana kwa viti 51 kila mmoja, huku Channel 12 ikiipa miungano ya Netanyahu viti 52 na muungano wa Eisenkot viti 49.
Baadaye, Netanyahu alijitokeza katika makao makuu ya Likud na kutangaza katika hotuba yake kuwa muungano wake wa mrengo wa kulia ulikuwa na "wengi mkubwa". Pia alitoa wito wa kuundwa kwa "serikali ya kitaifa yenye nguvu inayoongozwa na mrengo wa kulia".
Vyama vya Waarabu vyaweza kuwa na sauti ya mwisho
Vyama viwili vya Waarabu, United Arab List na Joint List, vilikadiriwa kupata viti kadhaa zaidi bungeni kufuatia taarifa za idadi kubwa ya Waarabu wa Israel kujitokeza kupiga kura.
Waarabu hao wanaunda takriban sehemu ya tano ya wakazi wa Israel na wengi wao hujitambulisha kama Wapalestina wenye uraia wa Israel.
Vyama hivyo vinazidi kuonekana kuwa na nafasi muhimu ya kuamua ni muungano gani utakaoanzisha serikali, ingawa ni chama kimoja tu kilichotangaza wazi kuwa kiko tayari kushirikiana navyo katika serikali.
"Natumai kuwa idadi ya viti itaruhusu sisi, muungano wa Change Bloc na UAL, kupata viti 61 vya bunge," alisema kiongozi wa United Arab List, Mansour Abbas.
Katika uchaguzi wa mwaka 2021, chama cha Abbas kilikuwa sehemu ya muungano wa serikali ulioongozwa na Naftali Bennett na Yair Lapid. Serikali hiyo ilidumu kwa mwaka mmoja kabla ya kusambaratika.
Mwenyekiti wa Joint List, Yousef Jabareen, alionya kuwa muungano huo wa vyama vya Waarabu "hauwezi kupuuzwa katika hali yoyote ya kisiasa".
Uchaguzi muhimu baada ya vita vya kikanda

Chanzo cha picha, Reuters
Uchaguzi wa Jumanne ulikuwa wa kwanza kufanyika nchini Israel tangu mashambulizi mabaya yaliyoongozwa na Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023, na vita vilivyofuata katika Ukanda wa Gaza, Lebanon na Iran.
Pia ulionekana na Waisraeli wengi kuwa miongoni mwa chaguzi zenye athari kubwa zaidi katika historia ya nchi hiyo, kwa kuwa ungeweza kuamua si tu nani atakayeongoza serikali, bali pia iwapo Israel itaendelea na mwelekeo wake wa sasa wa kisiasa unaosisitiza misimamo mikali ya mrengo wa kulia na utaifa unaochochewa na dini.
Masuala muhimu yaliyojadiliwa wakati wa kampeni yalijumuisha uwajibikaji kuhusu mapungufu ya kiusalama yaliyoruhusu mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba, namna vita vya kikanda vilivyoendeshwa, jinsi ya kugawana mzigo unaoongezeka wa utumishi wa kijeshi, mageuzi ya mfumo wa mahakama na nafasi ya Israel katika jumuiya ya kimataifa.
Nje ya kituo cha kupigia kura katika eneo la kaskazini mwa Tel Aviv linalounga mkono upinzani, wanaharakati wa kampeni, vijana kwa wazee, walikuwa wamejitokeza kwa wingi wakijaribu kuwashawishi wapiga kura katika dakika za mwisho.
Zivit Abramson, mwenye umri wa miaka 88, aliiambia BBC kuwa alikuwa amempigia kura Eisenkot kwa sababu, kwa maoni yake, Netanyahu alikuwa "anaiharibu nchi hii".
"Anajali maslahi yake mwenyewe tu, yeye mwenyewe tu," alisema.
Katika eneo jingine, Claire Tugendhaft alisema alikuwa amempigia kura Netanyahu kwa sababu aliamini kuwa "ndiye mtu bora zaidi nchini kuiongoza nchi katika mahusiano yake na mataifa mengine".
Waziri mkuu na washirika wake serikalini waliwahimiza wafuasi wao kujitokeza kupiga kura, huku wakionya kuhusu ongezeko la wapiga kura wa mrengo wa kushoto na Waarabu.
"Ikiwa hamtapiga kura, tutaamka kesho na kukuta kuna serikali ya mrengo wa kushoto, vyama vya Waarabu, Uislamu wenye misimamo mikali, na tutakuwa tumepoteza nchi," Netanyahu alinukuliwa akisema katika video iliyorekodiwa wakati wa kampeni.
Likud na vyama vingine kadhaa vya mrengo wa kulia viliomba muda wa kupiga kura uongezwe zaidi ya saa nne usiku kwa saa za Israel, hatua ambayo wapinzani wao wengi waliitafsiri kuwa ishara ya kuongezeka kwa wasiwasi.
Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi ya Israel ilikataa ombi hilo, ikisema kuwa "hali zilizopo hazihalalishi kuongeza muda wa kupiga kura" na kwamba idadi kubwa ya waliojitokeza kupiga kura "inaonyesha ushiriki mkubwa wa wananchi katika mchakato wa kidemokrasia".



































