Kombe la Dunia 2026: Wachezaji 10 wa kutazamwa zaidi

Chanzo cha picha, Getty
Wachezaji wawili mashuhuri wa soka duniani huenda wakaingia kwenye mashindano makubwa zaidi ya soka duniani yaani Kombe la Dunia la 2026, kwa mara yao ya mwisho.
Ni Lionel Messi, raia wa Argentina ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 38 akiwa katika klabu ya Inter Miami ya Marekani na Cristiano Ronaldo raia wa Ureno mwenye miaka 41 na mchezaji wa klabu ya Al-Nassr ya Saudi Arabia.
Vijana chipukizi kama Lamine Yamal wa Uhispania na Kylian Mbappé wa Ufaransa huenda wakachukua mikoba ya wakongwe hao. Lakini pia kuna wachezaji wengine wanaolenga kujipatia umaarufu nchini Marekani, Canada na Mexico wakati wa kombe la dunia mwaka huu.
Makala hii inakutajia wachezaji 10 wa kutazama kwenye Kombe la Dunia la mwaka huu, litakalochezwa katika katika nchi tatu, katika miji 16 na timu 48 zinazoshiriki.
Lionel Messi

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika historia ya kombe la dunia, Messi alifanikiwa nchini Qatar miaka minne iliyopita kuiongoza Argentina kushinda Kombe la Dunia na kufuatia nyayo za nyota wa taifa hilo Diego Maradona.
Messi amepata mafanikio makubwa katika soka, akishinda mataji makubwa ya klabu hasa alipokuwa Barcelona, kwa nchi yake na mataji yake binafsi kama mchezaji.
Tangu kumaliza kombe la dunia Qatar, amehamia Marekani na kuifanya Inter Miami kuwa timu inayoongoza katika Ligi Kuu ya Marekani (MLS), akishinda Kombe la MLS mwaka jana.
Cristiano Ronaldo

Chanzo cha picha, Getty Images
Nyota huyo wa Ureno anaelekea kwenye Kombe la Dunia baada ya kuiongoza klabu ya Saudi Arabia, Al Nassr kutwaa ubingwa wa ligi ya ndani msimu huu. Alijiunga rasmi na klabu hiyo tangu mwezi Disemba 2023.
Kombe hilo linaongeza orodha ya makombe ya ligi akiwa na Manchester United nchini Uingereza, Real Madrid nchini Uhispania na Juventus nchini Italia, pamoja na mataji matano ya Ligi ya Mabingwa (manne akiwa na Madrid, moja akiwa na United).
Pia ameshinda Mashindano ya Ulaya akiwa na Ureno na mataji mawili ya Ligi ya Mataifa ya UEFA. Huku akiwa na umri wa miaka 41, njaa yake ya mataji na kuweka rekodi haionyeshi dalili yoyote ya kupoa.
Kylian Mbappé

Chanzo cha picha, AP
Mbappé kwa muda mrefu amekuwa akichukuliwa kuwa mchezaji bora duniani baada ya Messi na Ronaldo.
Wengine watasema mshambuliaji huyo wa Real Madrid tayari amefanya makubwa baada ya kushinda Kombe la Dunia 2018 na kushinda mataji mengi, lakini bado hajashinda Ligi ya Mabingwa Ulaya wala Ballon d'Or.
Ana nafasi nzuri ya kutwaa tuzo ya Ballon d'Or ya mwaka huu, ni tuzo inayotolewa kila mwaka kwa mchezaji bora duniani - ikiwa anaweza kuiongoza Ufaransa kutwaa taji lingine la Kombe la Dunia huku akiwa anaongoza chati za mabao nchini Uhispania na kuongoza kwa mabao katika Ligi ya Mabingwa.
Ousmane Dembélé

Chanzo cha picha, Si
Kwa sasa ndio anashikilia tuzo ya Ballon d'Or na ndiye mshindi wa Ligi ya Mabingwa kabla ya kuanza Kombe la Dunia. Timu yake PSG imeichapa Arsenal katika mikwaju ya penalti na kutwaa ubingwa.
Mshambuliaji huyo wa Ufaransa amepanda kiwango chake tangu ajiunge na Paris Saint-Germain miaka mitatu iliyopita, akiisaidia kupata taji lake la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita na msimu huu.
Barcelona ilimnunua Dembélé kwa dola milioni 173 mwaka 2017. Ingawa hakufanya vizuri katika timu hiyo, na makali yake yalionekana alipohamia PSG.
Erling Haaland

Chanzo cha picha, Goal
Mshambuliaji wa Manchester City anacheza katika mashindano yake ya kwanza makubwa ya kimataifa baada ya kuvunja rekodi katika ngazi ya klabu.
Haaland, mwenye umri wa miaka 25, anajuulikana kwa kuvunja rekodi za mabao katika Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu ya England na tayari amevuka rikodi ilivyowekwa na Messi katika suala la kasi anayotumia kufunga mabao.
Norway haionekani kuwa katika nafasi nzuri katika Kombe la Dunia la mwaka huu, lakini ina Haaland ndiye mshambuliaji hatari zaidi katika mashindano hayo.
Lamine Yamal

Chanzo cha picha, Getty Images
Kijana wa Uhispania alikuwa nyota katika Mashindano ya Ulaya mwaka 2024 licha ya kuwa na miaka 17 tu hadi usiku wa fainali. Kwa kasi ya kupita wachezaji na uhodari wa miguu yake, alikua mfungaji mdogo zaidi kuwahi kutokea katika mashindano ya Euro ya wanaume.
Yamal analinganishwa na Messi, na aliwahi kupigwa picha na nyota huyo wa Argentina alipokuwa mtoto.
Yamal huenda akashindana na Mbappé kama wachezaji wanaoweza kujaza pengo la Messi na Ronaldo watakapostaafu. Na uchezaji wao katika Kombe la Dunia huenda ukaongeza mjadala huo.
Jude Bellingham

Chanzo cha picha, Reuters
Ndiye kiungo wa kati ambaye karibu kila timu kubwa ilimtaka wakati Real Madrid iliposaini mkataba wake mwaka 2023, akitokea katika klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani.
Aliiongoza klabu hiyo kutwaa taji la 15 la Ligi ya Mabingwa na taji la Ligi ya Uhispania katika msimu wake wa kwanza klabuni hapo kabla ya kuifikisha England fainali ya Euro.
Bellingham ni mchezaji mzuri licha ya msimu mgumu akiwa Madrid. Atakuwa ni mmoja wa wachezaji tegemezi wa Uingereza, huku nchi hiyo ikilenga kushinda taji hilo kubwa kwa mara ya kwanza tangu 1966.
Neymar

Chanzo cha picha, wallpaper
Ni mfungaji aliyeweka rekodi ya muda wote kwa Brazil. Ameshinda tuzo kubwa kama mchezaji, na amefunga magoli 79 kwa taifa lake na kuipiku rekodi ya Pele.
Lakini bado hajaiongoza Brazil kutwaa taji la sita la Kombe la Dunia.
Neymar, sasa ana umri wa miaka 34, ameitwa na kocha wa Brazil, Carlo Ancelotti kwa ajili ya Kombe la Dunia kwa mara ya nne.
Kwa sasa yuko katika klabu ya nyumbani kwao ya Santos FC, ambako alijiunga 2025 na kuongeza mkataba wake hadi mwisho mwa 2025, baada ya mkataba wake na Al Hilal ya Saudi Arabia kuvunjwa.
Mohamed Salah

Chanzo cha picha, caf
Nyota huyo wa Misri ataondoka Liverpool baada ya msimu mbaya kwa timu hiyo, lakini bado ni nyota hatari kwa nchi yake.
Misri ina matumaini mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 33 atafanya vyema kwenye Kombe la Dunia.
Salah alifunga mabao 257 katika michezo 442 na kushinda mataji mengi akiwa na Liverpool, ikiwa ni pamoja na Ligi ya Mabingwa na mataji mawili ya Ligi Kuu.
Akiwa na Misri, ameishifika timu hiyo katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika mara mbili, bila kuchukua kombe.
Christian Pulisic

Chanzo cha picha, fifa
Akiwa na umri mdogo Pulisic alionekana kuwa na uwezo wa kuwa nyota mkubwa wa soka.
Amechezea katika baadhi ya vilabu vikubwa barani Ulaya nchini Ujerumani, Uingereza na Italia, akishinda tuzo kubwa na hakuna tuzo kubwa zaidi kuliko Ligi ya Mabingwa akiwa na Chelsea.
Sasa akiwa AC Milan, mshambuliaji huyo amepanda kiwango na atakuwa sehemu muhimu ya matumaini ya kocha wa Marekani, Mauricio Pochettino kufika mbali na Timu ya Taifa ya Wanaume katika Kombe la Dunia la nyumbani.















