Kwa nini mpenzi wa kwanza hawezi kusahaulika?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa watu wengi, kupendwa kwa mara ya kwanza ni jambo wanalokumbuka kwamuda mrefu maishani. Lakini kwa nini mahusiano ya kwanza husalia akilini hata baada ya miongo kadhaa kupita? Ni nini hufanya kumbukumbu za wakati hio kusalia kwa muda mrefu, na kuwa zisizoweza kusahaulika?
Ubongo hutengeneza kumbukumbu za kudumu, hasa wakati wa ujana.
Kwa watu wengi, uzoefu wao wa kwanza wa kimapenzi hutokea wakati wa ujana, kipindi ambacho ubongo huwa katika kilele cha uwezo wake wa kurekodi na kuhifadhi kumbukumbu. "Katika umri huu, tuna uwezo mkubwa wa kurekodi na kuhifadhi kumbukumbu kwa usahihi," anasema Catherine Lovey, profesa wa saikolojia ya neva katika Chuo Kikuu cha Westminster.
Anaeleza pia kuwa ubongo huhifadhi taarifa zinazohusiana na hisia na mihemko vizuri zaidi na kwa njia ya kudumu zaidi. Tukio linapotokea kwa mara ya kwanza, likawa na athari kubwa maishani, au hata kusababisha mateso makali na usumbufu, kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kurekodiwa kwenye kumbukumbu na kusalia kwa muda mrefu, anasema.
Aidha, kadiri kumbukumbu inavyokumbukwa mara kwa mara, ndivyo inavyodumu zaidi. Ndiyo maana matukio yanayoambatana na hisia kali huwa yanaunda baadhi ya kumbukumbu zinazodumu zaidi katika akili ya mwanadamu. "Kila tunapokumbuka matukio na kumbukumbu hizo, tunaimarisha miunganisho ya neva inayohusiana nayo ndani ya ubongo wetu," anasema Lovey.
Kwa nini homoni za ujana huwa na athari kubwa sana katika mapenzi ya kwanza?
Iwe ni furaha na bashasha tele au maumivu makali ya kuvunjika moyo, hisia zinazohusiana na mapenzi ya kwanza huwa na nguvu na kina cha ajabu. Catherine Loveday anasema kuwa, hasa wakati wa kubalehe, mchanganyiko wa kemikali mbalimbali huanza kufanya kazi mwilini na kwenye ubongo, na hivyo kuchochea hisia kali.
Awali, ongezeko la homoni za ngono kama vile estrojeni na testosteroni husababisha mvuto wa kihisia. Kisha, uhusiano unapoanza, homoni nyingine na kemikali zinazopitisha ujumbe katika mfumo wa neva hutolewa ubongoni, zikiwemo serotonini, dopamini, na oksitosini,kemikali zinazohusishwa na hisia za kuridhika, ukaribu, furaha, na kushikamana kihisia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mapenzi ya kwanza ni hatua muhimu katika kuanzishwa kwa mahusiano ya kihisia.
Katika hatua ya msingi kabisa, mahusiano ya kibinadamu yanahusiana na uhai wetu na kuendelea kwa maisha yetu. Kwa kijana anayebalehe, uhusiano wa kwanza wa kimapenzi ni hatua muhimu sana, kwani anapata uzoefu wa aina mpya ya muunganisho wa kihisia na mtu aliye nje ya familia yake ya karibu na mzunguko wake wa kawaida wa watu wa karibu.
Catherine Loveday anaelezea mapenzi ya kwanza kuwa"huenda mojawapo ya matukio muhimu zaidi katika maisha ya mtu yeyote kuhusiana na mahusiano ya kibinadamu." "Tunapaswa kujifunza kumwamini mtu aliye nje ya mzunguko wetu wa karibu na tuliozoea," anasema. "Tunapaswa kupiga hatua kuelekea upande mpya."
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mujibu wake, mapenzi ya kwanza si tukio la hisia pekee, bali ni sehemu ya mchakato wa kujifunza jinsi ya kujenga uhusiano; ni uzoefu unaowafundisha watu jinsi ya kuaminiana, kupata uzoefu wa ukaribu wa kihisia na kimwili, na kuunda aina mpya ya uhusiano wa kibinadamu.
Mnamo mwaka wa 1993, mwanasaikolojia wa Marekani Dkt. Nancy Kalish alifanya utafiti kwa mamia ya watu duniani kote ambao walikuwa wamerudiana na wapenzi wao wa zamani baada ya miaka mingi kupita.
Muhimu zaidi, hali ya maisha ya watu hawa ilichukua nafasi kubwa katika matokeo ya mahusiano hayo. Wengi wa wale walioungana tena na wapenzi wao wa zamani walikuwa hawana wapenzi wakati huo au walikuwa wamefiwa na wenzi wao.
Miongoni mwa watu hawa, wanandoa wengi walianzisha upya uhusiano wao ndani ya wiki chache tu, na jambo la kushangaza zaidi, asilimia 72 yao hatimaye walioana.
Kuenea kwa mtandao kumerahisisha sana na kupunguza maumivu katika kutafuta na kuungana tena na wapenzi wa zamani. Mahusiano haya ya awali hayakuhitaji ahadi kubwa za kudumu, lakini pia yalileta matokeo tofauti.
Dkt. Nancy Kalish alipofanya utafiti mwingine mwaka wa 2004, asilimia 62 ya watu waliorudiana na wapenzi wao wa zamani walisema kuwa walianzisha uhusiano wa kimapenzi nao. Hata hivyo, ni asilimia 5 tu ya mahusiano hayo ndiyo hatimaye yaliishia kwenye ndoa.
Kwa nini mapenzi ya kwanza husalia akilini mwetu kwa miaka mingi?
Utafiti wa Catherine Lovey haukomei kwenye mapenzi ya mwanzoni tu. Anachunguza kumbukumbu za watu katika hatua mbalimbali za maisha yao, lakini anasema kuwa kumbukumbu za mahusiano ya kwanza ya kimapenzi mara nyingi huwa na nafasi ya pekee.
"Nimewahi kuzungumza na watu wenye umri wa miaka 70 na 80 ambao bado wanazo baadhi ya kumbukumbu muhimu na zilizo wazi kabisa kuhusu mahusiano yao ya kwanza ya kimapenzi," anasema.
Kulingana na Lovey, kwa watu wengi, mapenzi ya kwanza si kumbukumbu ya wakati uliopita tu, bali ni tukio muhimu linaloacha alama na kubaki akilini na katika hisia zao kwa miaka na hata miongo mingi ijayo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, hisia za kuthamini na kukumbuka mapenzi ya zamani zinaweza kusaidiaje mahusiano yetu ya sasa?
Kukumbuka mapenzi ya zamani hakumaanishi lazima kutamani mahusiano yaliyoisha, inaweza hata kusaidia kuimarisha mahusiano ya sasa. Adam Fetterman, profesa katika Chuo Kikuu cha Houston huko Texas, anachunguza jambo linaloitwa "romantic nostalgia" hali ya kuthamini na kukumbuka kwa hisia mapenzi ya zamani, ambayo anaifafanua kama "hisia ya kutamani na upendo kwa wakati uliopita, ikihusishwa na mwenzi wa sasa wa kimapenzi."
Fetterman anasema kuwa kukumbuka kwa makusudi matukio muhimu waliyoshiriki katika uhusiano, kama vile kutazama tena filamu waliyoiona katika siku walioiona mara ya kwanza, kunaweza kuwasaidia watu kuhisi tena baadhi ya hisia za kipekee na za kufurahisha walizopata wakati wa uhusiano huo, hata kama hawawezi kuelezea hisia hizo waziwazi kwa maneno.
Pia alibaini kuwa hali hiyo ya kukumbuka mapenzi ya zamani haileti tu hisia za furaha, bali wale wanaorejelea mara kwa mara kumbukumbu hizo za pamoja huhisi kujitolea zaidi kihisia kwa wenzi wao, na hata kiwango chao cha upendo na mapenzi huongezeka.
Baadhi ya mapenzi ya kwanza hayasahauliki kamwe.
Kate na Gunther walikutana mwaka 1989 walipokuwa likizoni huko Devon. Walipendana mara walipoonana kwa mara ya kwanza. Gunther ilibidi arudi Ujerumani, lakini waliendelea kutembeleana na kuwasiliana kwa barua, ingawa hawakuweza kupata njia ya kuwa pamoja.
Kate anasema kuwa kumwambia Gunther kwamba hangeweza kuhamia kwake ilikuwa "uamuzi mgumu zaidi katika maisha yangu." Hivyo, walivunja uhusiano wao huku wakiwa na huzuni kubwa, baada ya kuwa pamoja kwa miaka miwili.
Miongo mitatu baadaye, Kate alikuta tena barua za Gunther kabatini, na kumbukumbu zote zilimjia tena kwa nguvu. "Nililia na kulia tu," anakumbuka, "nikajiambia, 'Nimemvunja moyo mwanaume mwema sana hivi bila yeye kujua sababu hasa.'" Alipata anwani ya biashara ya familia ya Gunther na kumwandikia barua, bila kutarajia majibu yoyote.
Na Gunther alijibu. "Simu iliita saa 12:36 mchana kamili tarehe 22 Novemba," Kate anakumbuka, "na moyo wangu uliruka kwa mshangao nilipoona simu hiyo inatoka Ujerumani." Walizungumza kwa saa nyingi, na majuma machache baadaye Gunther alisafiri kwa ndege hadi Manchester kukutana na Kate. "Nilipomwona, ilikuwa kana kwamba hatukuwahi kutengana," anasema.
Walifunga ndoa baada ya Gunther kumvisha pete ya uchumba kwenye mlima waliokuwa wameupanda pamoja miaka 30 iliyopita. "Mara nyingi huwa hupati nafasi ya pili," anasema Kate, "lakini sasa, kila siku ninapomwona, sijutii chochote." Gunther anakubaliana naye kwa kusema "Sitampoteza tena."















