Kwa nini Ligi Kuu ya England inakabiliwa na mgogoro baada ya uamuzi kuhusu Man City?

    • Author, Dale Johnson
    • Nafasi, Mwandishi wa Masuala ya Soka
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Ikiwa ulikuwa na dhana kwamba sakata la mashtaka 115 dhidi ya Manchester City lilikuwa karibu kumalizika, fikiria tena.

Miaka miwili na siku 10 tangu kusikilizwa kwa kesi kuanza, na siku 1,329 baada ya City kushtakiwa, sasa tunajua kuwa uamuzi umefikiwa, huku klabu hiyo ikikutwa na hatia ya ukiukwaji mwingi wa kanuni za kifedha.

Hiyo si kwa sababu Ligi Kuu ya England (Premier League) au Manchester City wametuambia - bali ni kutokana na *The Athletic* kugundua na kutoa taarifa hiyo.

Baadaye, BBC Sport ilielezwa kuwa uamuzi huo ulitumwa kwa watendaji wa klabu hiyo katikati ya wiki; ambao ilibidi watie saini makubaliano ya kutoweka wazi taarifa hizo ili waweze kufungua faili husika.

Mchakato unaweza kuonekana kuwa imara na wa siri kama ilivyotakiwa lakini kadiri mduara wa watu wanaojua siri unavyopanuka, ndivyo uwezekano wa taarifa kuvuja unavyoongezeka.

Licha ya hayo, Ligi Kuu ya England inaendelea kukaa kimya mbele ya umma.

City haikueleza wazi iwapo walikutwa na hatia katika taarifa yao ambayo ilisisitiza kuwa "mchakato unaendelea" kwa mtazamo wao, huku rufaa ikitarajiwa.

Yote haya yanaashiria kuwa uamuzi uliosubiriwa kwa muda mrefu kutoka kwa jopo huru haukuashiria mwisho wa mchakato huo, bali labda ulikuwa mwisho wa hatua ya awali tu.

Inaonekana machafuko na hali ya kutokuwa na uhakika itaongezeka zaidi sasa.

Mashabiki wa City, na wadau wengine wa soka, wamebaki wakikisia ni adhabu gani inayoweza kutolewa, na ni lini mambo haya yote yatafikia tamati rasmi.

Mashtaka hayo ni mazito kiasi kwamba kupunguziwa pointi kunaonekana kuepukika, ingawa inategemea rufaa itakayowasilishwa na City, ambao wameendelea kusisitiza kuwa hawakufanya kosa lolote.

Wakati na namna adhabu yoyote itakavyotekelezwa itakuwa muhimu sana, si kwa City pekee, bali kwa Ligi Kuu ya England kwa ujumla.

Na hayo ni kabla hata hatujazungumzia uwezekano wa klabu nyingine kuishitaki City ili kudai fidia.

Kikosi cha Enzo Maresca kitasafiri kwenda kucheza na Liverpool tarehe 11 Oktoba, wakati Ligi Kuu itakaporejea baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa.

Wanaweza kujitengenezea mwanya wa pointi sita kileleni . Lakini je, hilo sasa halitakuwa na maana yoyote?

Hebu tuangalie matukio yanayoweza kutokea, ambayo hakuna hata moja kati yake linalopendeza.

Hali ya kwanza: Hakuna kitachotangazwa msimu huu kuhusu adhabu

Kuamua adhabu kunapaswa kuwa kwa haraka zaidi kuliko kuthibitisha hatia, lakini hakuna uhakika wowote katika kesi hii.

Kwa kuwa mashtaka yamekanushwa, shauri hilo litapelekwa kwenye kikao cha kuamua adhabu kitakachoitishwa na jopo huru.

BBC Sport imefahamishwa kuwa kikao hicho kinaweza kuchukua miezi kadhaa kufanyika, na matokeo yake huenda yasitangazwe hadi mchakato wa rufaa utakapokamilika.

Katika kikao hicho, chaguzi zote zitakuwa mezani: faini, kupokonywa pointi, na hata kushushwa daraja.

Hali hii ni tofauti na kesi ya Chelsea mapema mwaka huu, ambapo klabu hiyo ya Stamford Bridge ilijiripoti yenyewe na kukiri makosa. Hilo liliwapa fursa ya kufanya mazungumzo na Ligi Kuu (Premier League) na kufikia makubaliano kuhusu adhabu.

Inawezekana City wakaamua kukiri makosa na kujaribu kufikia makubaliano - jambo ambalo lingekuwa bora kwa ligi - ingawa hilo linaonekana kutowezekana kutokana na klabu hiyo kuendelea kukanusha vikali kwa miaka mingi.

Jopo hilo litapaswa kuchunguza kwa kina mamia ya kurasa za ushahidi na kuamua adhabu inayofaa.

Ikumbukwe kuwa Everton ilipokonywa pointi sita (baada ya kupunguziwa kutoka pointi 10 kufuatia rufaa), na baadaye pointi mbili katika kesi tofauti kutokana na ukiukaji wa kanuni za faida na uendelevu (PSR). Nottingham Forest ilipokonywa pointi nne.

Hayo yalichukuliwa kuwa makosa madogo, huku City ikikabiliwa na mashtaka saba tofauti ya ukiukaji wa PSR katika Ligi Kuu pekee, pamoja na mashtaka mengine matano yanayohusiana na mashindano ya UEFA.

Hali hiyo pekee inaashiria uwezekano wa adhabu kubwa ya kupokonywa pointi.

Hayo ni kabla hata ya kuzingatia suala la mapato ya udhamini yaliyoongezwa kinyemela na kudaiwa kupitishwa kupitia akaunti za kampuni ili kukidhi kanuni za usawa wa kifedha (financial fair play), malipo kwa wachezaji na makocha, pamoja na kushindwa kushirikiana katika uchunguzi.

Ukizingatia mambo haya yote, inaweka alama ya shaka juu ya Ligi Kuu katika kipindi cha kati ya mwaka 2009 na 2018.

Chelsea na Manchester City, ambazo ni miongoni mwa klabu zilizofanikiwa zaidi katika mashindano hayo, zilihusika katika hali hiyo.

Wakati Chelsea ilikiri kufanya udanganyifu, City imepatikana na hatia. Walikwepa kanuni za kifedha ili kujiweka katika nafasi ya kusajili wachezaji wa gharama kubwa zaidi kuliko ambavyo hali yao ya kifedha ingewaruhusu.

Na ikiwa msimu huu utapita bila uamuzi wowote kuhusu adhabu, huku ikijulikana kuwa City walikuwa na hatia katika mashtaka mengi, je, hali hiyo inaashiria nini kuhusu uadilifu wa mashindano hayo?

Je, inawezekana adhabu ikaanza kutumika kuanzia msimu huu ? Ni jambo lisilowezekana.

Basi, itakuwaje ikiwa Manchester City watatwaa ubingwa wa ligi?

Kwa sasa, Coventry wanashika nafasi ya tatu kutoka mwisho. Itakuwaje wakimaliza katika nafasi hiyo na kushushwa daraja, ilhali wangeweza kubaki ligini iwapo adhabu ya City ingetolewa msimu huu?

Kuchelewa huku kwa hatua ni habari mbaya sana kwa Ligi Kuu ya Uingereza kama mashindano.

Kuna hoja yenye nguvu kwamba makubaliano kuhusu adhabu ndiyo njia mwafaka na safi zaidi ya kutatua suala hili.

Hata hivyo, huenda hilo lisiwe jambo la kuvutia kwa uongozi wa ligi, kwani watalazimika kufanya mazungumzo na City, ambao bila shaka wangependelea adhabu ndogo zaidi.

Hali ya pili: Man City wanapigwa faini msimu huu lakini wanakata rufaa

Utaratibu wa kawaida wakati adhabu yoyote ya pointi inapotolewa ni kwamba inatumika mara moja, ikiwa itakata rufaa.

Inaweza kuwa punguzo la pointi kubwa sana kiasi kwamba ni kushushwa daraja.

Vinginevyo, ikiwa uanachama wa City katika Ligi Kuu utafutwa, haijulikani jinsi hiyo inaweza kutumika katikati ya msimu.

Inaweza pia kuwa adhabu hiyo ni faini kubwa, ingawa hiyo ingeonekana kuwa haiwezekani kutokana na makato ya pointi kwa vilabu vingine.

Swali litakuwa ni lini tunasikia, na muda gani baada ya rufaa kusikilizwa.

Kwa kawaida, ligi huomba mchakato wa haraka kutoka kwa kampuni huru ya usuluhishi ambayo hushughulikia kesi za nidhamu.

Lakini, kama kawaida katika kesi hii, ugumu unaonyesha kuwa hii si rahisi.

Kuna nafasi, ingawa ni ndogo, kwamba adhabu hiyo inatumika tu kwenye jedwali la ligi baada ya rufaa.

Hilo hakika litasababisha maandamano kutoka kwa timu zilizoathiriwa msimu huu, ambazo zitadai, kama kawaida, ianze kutumika mara moja.

Hali ya tatu: Rufaa inasikilizwa kwa haraka na uamuzi unatangazwa

Kwa ajili ya kulinda heshima na uadilifu wa Ligi Kuu, na ili klabu zote zijue nini hasa zinachokipigania, hatua hii inapaswa kuchukuliwa mapema iwezekanavyo.

Msimu uliopita, uamuzi wa kuipokonya pointi klabu ya West Bromwich Albion kutokana na kukiuka kanuni za faida na uendelevu wa kifedha ulitangazwa tarehe 24 Aprili pekee.

Ingawa hatimaye walifanikiwa kubaki kwenye ligi ya Championship, hatua hiyo iliwarejesha katika mapambano ya kuepuka kushuka daraja wakati walipokuwa wakiamini kuwa wako salama; pia iliwapa matumaini timu zilizokuwa katika hatari ya kushuka daraja.

Ligi Kuu haitaki suala hili licheleweshwe hadi kufikia mwezi wa pili kabla ya mwisho wa msimu, lakini hakuna uhakika wowote katika suala hili.

Katika hali hii, tusisahau kuwa City inaweza pia kushinda rufaa yake, kama ilivyofanya ilipopinga marufuku ya miaka miwili ya kushiriki Ligi ya Mabingwa iliyowekwa na UEFA mwezi Julai 2020.

Ingawa ushindi huo ungepokelewa kwa shangwe katika Uwanja wa Etihad, kuna uwezekano mkubwa kuwa haungehitimisha mzozo unaozunguka kesi hiyo.

Hali ya nne: Hata baada ya kesi kufungwa, jambo hili halijaisha

Klabu za Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League) zinatafuta ushauri wa kisheria kuhusu fidia kutoka kwa Manchester City kuhusiana na kesi hiyo.

Chanzo kimoja, ambacho kilishikilia wadhifa wa juu wa utawala katika klabu mbili za Ligi Kuu, kilisema wanatarajia klabu kuwasilisha madai ya kibinafsi ya fidia dhidi ya Manchester City.

Wakili mwingine mashuhuri aliambia BBC kuwa mchakato huo unaweza hata kuratibiwa na ligi yenyewe.

Kanuni za Ligi Kuu zinaruhusu klabu kuchukua hatua za kisheria dhidi ya nyingine ili kudai fidia.

Mwezi Juni, Everton iliagizwa kulipa Burnley pauni milioni 35 baada ya kukiuka kanuni za Faida na Uendelevu (PSR) kwa kipindi cha miaka mitatu.

Burnley ilidai kuwa ukiukaji huo uliathiri nafasi yao ya kusalia Ligi Kuu, na kutafuta fidia kwa hasara zilizotokana na kushushwa daraja.

Everton inakata rufaa, huku vyanzo vikisema hapo awali kuwa ingepinga uamuzi huo "kwa nguvu na kwa kina," lakini jambo hilo linatoa muktadha wa kuvutia kwa kesi ya Manchester City.

Kuna kutokuwa na uhakika kuhusu sheria ya muda wa mwisho wa kufungua kesi (statute of limitations), ambayo ingeweka ukomo wa muda wa kuwasilisha madai.

Inaripotiwa kuwa Arsenal, Manchester United, Liverpool na Tottenham Hotspur zilihifadhi haki zao za kudai fidia miaka miwili iliyopita.

Hili si suala linalohusu tu Manchester United (mara mbili) na Liverpool, ambazo zilimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya City katika misimu ambayo City ilitwaa ubingwa.

Ni suala linalohusu klabu hizo ambazo zilikosa nafasi ya kuingia Ligi ya Mabingwa Ulaya (Champions League), au kushindwa kufuzu kwa mashindano ya Ulaya, au hata zile zilizoshushwa daraja.

Na inaweza hata kusababisha madai kuhusu fedha za zawadi kwa kila nafasi katika Ligi Kuu (Premier League), au mapato ya kibiashara ambayo klabu pinzani zingeweza kupata lakini zikayakosa.

Kieran Maguire, profesa wa masuala ya fedha katika soka kutoka Chuo Kikuu cha Liverpool, aliambia BBC Sport kuwa hali hiyo ingechukuliwa na walalamikaji kama "kunyimwa fursa."

Maguire alieleza kuwa "kanuni ya ukomo wa muda wa kisheria (statute of limitations)" haijatajwa katika mwongozo wa kawaida wa Ligi Kuu, ingawa hilo linaweza kupingwa kisheria na klabu ya City.

Lakini vipi kuhusu fidia? Kuangalia tu suala la kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa (Champions League) kunaweza kuibua madai makubwa ya kifedha.

"Wakati huo, thamani ya kushiriki Ligi ya Mabingwa ilikuwa angalau pauni milioni 30," alisema Maguire. "Nadhani kufikia mwaka 2018, thamani hiyo ilikuwa imefikia takriban pauni milioni 60 au 70, na hiyo ni kwa upande wa fedha za zawadi pekee.

"Zaidi ya hayo, unaweza kudai fidia kwa mapato yaliyopotea kutokana na mauzo ya tiketi na bonasi za wadhamini. Hili linaonekana kutowezekana sana, lakini bila shaka linajadiliwa.

"Wachezaji hupata bonasi kwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa. Ukizungumza na watu walio karibu na klabu hizo kubwa, bonasi hizo kwa kawaida huwa katika kiwango cha asilimia 25.

"Mshahara wa wastani wakati huo ukirejea mwaka 2012 ungekuwa takriban pauni 80,000 au 90,000 kwa wiki. Asilimia 25 ya kiasi hicho ni sawa na pauni milioni nne au tano kwa mwaka.

Hivyo ndivyo masuala haya yanavyojikusanya na kuwa mzigo mkubwa."

Kupunguzwa kwa pointi, faini, na madai ya fidia.

Hii ni hali ngumu na yenye utata mkubwa kwa Ligi Kuu, na haiwezi kutatuliwa hivi karibuni.