Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Araqchi: Iran iko tayari kwa amani, lakini pia kwa vita vya maangamizi

Kauli hiyo imekuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuripotiwa kukataa pendekezo la Iran la kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Sifuna apewa tiketi ya urais 2027 na Linda Mwananchi

    Muungano wa kisiasa wa Linda Mwananchi umemtangaza rasmi Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, hatua inayolenga kuondoa uvumi kuhusu migawanyiko ndani ya vuguvugu hilo la upinzani.

    Katika taarifa iliyotolewa baada ya kikao maalum cha viongozi wa muungano huo mwishoni mwa wiki, viongozi walisema wamekubaliana kusonga mbele kwa umoja wakiongozwa na lengo la kushughulikia changamoto za uongozi na utawala nchini Kenya.

    Viongozi hao walitangaza kuwa Sifuna ndiye atakayepeperusha bendera ya muungano huo katika kinyang'anyiro cha urais, huku akitarajiwa kutangaza rasmi chama atakachotumia kugombea mwanzoni mwa mwezi Oktoba.

    Muungano huo pia ulisema unakusudia kujenga ushirikiano na vyama vingine vya kisiasa vinavyoshiriki maono yake ya kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini Kenya.

    Tangazo hilo linajiri wakati kumekuwa na maswali kuhusu mshikamano wa viongozi wa Linda Mwananchi, hasa kufuatia mijadala ya umma kuhusu matarajio ya kisiasa ya baadhi ya viongozi wake.

    Akizungumza baada ya mkutano huo, Sifuna alieleza matumaini kuhusu mustakabali wa muungano huo na kusisitiza kuwa viongozi wake wako pamoja katika safari ya kuelekea 2027.

    Kwa upande wake, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alisema viongozi wa muungano huo wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wao na kujenga msingi imara wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

    Msimamo huo wa pamoja unakuja siku chache baada ya Babu Owino kuthibitisha hadharani kumuunga mkono Sifuna katika azma yake ya kuwania urais.

    Sifuna amekuwa akitafuta jukwaa jipya la kisiasa baada ya kutofautiana na chama cha ODM, na tangazo la sasa linaweka wazi nafasi yake kama sura kuu ya mkakati wa Linda Mwananchi kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027.

  2. Yemen yadai kuwaua wataalamu wanne wa Iran

    Msemaji wa jeshi la serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa, Kanali Majid Abdullah Al-Nuzaili, amesema vikosi vya serikali vilitekeleza operesheni 756 za kijeshi ndani ya saa 72 zilizopita, na kusababisha kuuawa au kujeruhiwa kwa wapiganaji 2,316 wa Wahouthi pamoja na wataalamu wanne wa Iran.

    Al-Nuzaili alisema operesheni hizo zilitumia ndege za kivita, ndege zisizo na rubani, makombora, mizinga na vikosi vya ardhini kulenga ngome, wapiganaji na vifaa vya kijeshi vya Wahouthi katika maeneo kadhaa yakiwemo Taiz, Marib, Al-Jawf, Al-Bayda na Lahj.

    Kwa mujibu wa jeshi la Yemen, mashambulizi hayo yaliharibu magari ya kijeshi, majukwaa ya kurushia makombora pamoja na maghala ya silaha na risasi.

    Al-Nuzaili alidai kuwa wataalamu wanne wa Iran waliouawa walikuwa wakihusika na uendeshaji wa ndege zisizo na rubani na makombora katika mkoa wa Taiz, jambo alilosema linaonyesha kuendelea kwa uungwaji mkono wa Tehran kwa Wahouthi.

    Wakati huo huo, msemaji wa Wahouthi Yahya Saree alisema Saudi Arabia ilifanya mashambulizi 27 ya anga katika mikoa kadhaa ikiwemo Taiz, Marib, Saada, Amran, Ibb na Hajjah. Saudi Arabia nayo ilitangaza kuwa ilidungua ndege mbili zisizo na rubani zilizorushwa kuelekea mji mkuu, Riyadh.

    Mapigano kati ya Wahouthi na serikali ya Yemen yameongezeka tangu Julai baada ya kipindi cha utulivu wa miaka kadhaa. Mkoa wa Taiz umekuwa miongoni mwa maeneo makuu ya mapambano katika miezi ya hivi karibuni.

    Mfalme Mohammed VI wa Morocco amelaani mashambulizi ya Wahouthi dhidi ya Saudi Arabia na kusema usalama wa Saudi Arabia ni sehemu ya usalama wa Morocco, huku akitoa wito wa kuongezwa kwa shinikizo la kimataifa dhidi ya kundi hilo.

    Vita vya Yemen vilianza mwaka 2014 baada ya Wahouthi kuteka mji mkuu Sana'a, hatua iliyosababisha muungano unaoongozwa na Saudi Arabia kuingilia kati kijeshi mwaka uliofuata kuunga mkono serikali inayotambuliwa kimataifa.

    Soma Zaidi:

  3. Tetesi za Soka Ulaya Jumatatu: Nyota wa Chelsea Estevao kwenye rada za Barcelona

    Winga wa Brazil Estevao Willian anazidi kukerwa na ukosefu wa muda wa kucheza Chelsea, huku Barcelona ikifuatilia kwa karibu hali ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 19. (Sport - in Spanish)

    Mshambuliaji wa Ureno Joao Felix, anayekipiga kwa sasa Al-Nassr, amesema angependa kurejea kucheza soka barani Ulaya, ingawa hajataja klabu anayotamani kujiunga nayo. (AS - in Spanish)

    Nyota wa Norway Erling Haaland, 26, ameanza kuvutia macho ya Arsenal na Real Madrid kutokana na hali ya sintofahamu inayoikabili Manchester City. (Football Insider)

    Newcastle United inamfuatilia beki wa Morocco Abdelhamid Ait Boudlal, 20, wa Rennes, lakini itakumbana na ushindani kutoka Everton, Brentford na Hull City. (Teamtalk)

    Arsenal na Tottenham Hotspur zinatajwa kufuatilia kiungo wa Algeria Ibrahim Maza, 20, wa Bayer Leverkusen. (Teamtalk)

    Chelsea inamuwania beki wa kushoto wa England Tyrick Mitchell, 27, wa Crystal Palace, lakini pia inakabiliwa na ushindani kutoka Manchester United na Liverpool. (Caught Offside)

    Leeds United haina mpango wa kumuuza beki wa Wales Ethan Ampadu, 26, licha ya taarifa zinazomhusisha na kurejea katika klabu yake ya zamani ya Chelsea. (Football Insider)

    Soma Zaidi:

  4. Wachezaji wa Ireland wakataa kusalimiana na timu ya Israel

    Kocha wa Jamhuri ya Ireland, Heimir Hallgrímsson, amesema wachezaji wake walivutia hisia duniani baada ya kukataa kutekeleza baadhi ya taratibu za kawaida kabla ya mechi yao dhidi ya Israel.

    Kabla ya mchezo huo uliochezwa Hungary na kumalizika kwa ushindi wa mabao 3-0 kwa Ireland, wachezaji wa Jamhuri ya Ireland na Israel hawakusalimiana kwa kupeana mikono. Aidha, wachezaji wa Ireland waliinamisha vichwa vyao wakati wimbo wa taifa wa Israel ukipigwa.

    Nahodha wa Ireland, Dara O'Shea, na mwenzake wa Israel, Manor Solomon, pia hawakusalimiana kabla ya mechi, huku timu hizo mbili zikikosa kubadilishana bendera za kumbukumbu kama ilivyo kawaida.

    Tangu droo ya Kundi B3 ilipofanyika mwezi Februari, mechi kati ya timu hizo zimezua mjadala kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Israel na Gaza.

    Awali, baadhi ya wachezaji wa Ireland walikabiliwa na wito wa kujiondoa kwenye mashindano hayo, huku kampeni ya "Stop the Game", iliyoandaliwa na kundi la Irish Sport for Palestine, ikipata uungwaji mkono mkubwa katika wiki za hivi karibuni.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Ruto afichua mpango wa kuifikisha SGR Tanzania

    Rais William Ruto amesema serikali yake inapanga kuipanua reli ya Standard Gauge Railway (SGR) hadi Tanzania ili kuimarisha biashara na shughuli za kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

    Akizungumza katika ibada ya kanisa eneo la Mwatate, kaunti ya Taita Taveta, Ruto alisema serikali imetenga takriban shilingi bilioni 5 za Kenya kwa ajili ya mradi huo.

    "Tunaendelea kuipanua SGR kutoka Naivasha hadi Kisumu na mpaka wa Malaba. Wakati huo huo, ni muhimu kuunganisha Voi na Tanzania. Tayari tumetenga takriban shilingi bilioni 5 kwa mradi huo," alisema.

    Kenya na Tanzania zinatazamia kuunganisha mitandao yao ya reli ya SGR, hatua itakayorahisisha usafiri na biashara katika eneo la Afrika Mashariki, ikiwemo Uganda, Rwanda na Burundi.

    Kenya tayari ina mpango wa kuipanua SGR kutoka Naivasha kupitia Kisumu hadi mpakani Malaba.

    Wakati wa tangazo hilo, Ruto pia aliahidi kutoa hati miliki za ardhi kwa wakazi wa Taita Taveta wiki ijayo pamoja na kuanzisha miradi mingine ya maendeleo katika eneo hilo.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Araqchi: Iran iko tayari kwa amani, lakini pia kwa vita vya maangamizi

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, ambaye alisafiri kwenda Marekani pamoja na Rais Masoud Pezeshkian kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema ujumbe wa ngazi ya juu wa Iran ulifika New York ukiwa na lengo la "kuandaa mazingira ya amani."

    Hata hivyo, Araqchi alisema Iran itaendelea kusimama imara dhidi ya aina yoyote ya uchokozi, hata kama hali hiyo itasababisha kile alichokiita "vita vya maangamizi."

    "Tulikuja New York kutafuta njia ya amani, lakini iwapo italazimu, tuko tayari pia kwa vita vya apokalipsi. Wakati huohuo, tuko tayari kwa diplomasia ya kweli," amesema Araqchi katika mahojiano na vyombo vya habari vya Marekani.

    Kauli hiyo imekuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuripotiwa kukataa pendekezo la Iran la kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz, huku baadaye akisema kuwa mazungumzo zaidi kati ya Marekani na Iran yatafanyika katika siku zijazo.

    Wiki iliyopita, Araqchi alisema kuwa iwapo Marekani itakubali mpango uliopendekezwa na Iran, Mlango Bahari wa Hormuz unaweza kufunguliwa ndani ya siku saba.

    Soma Zaidi Hapa:

  7. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 28/09/2026.