Rio Ferdinand, nyota wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya England, amesema ziara yake nchini Tanzania haina uhusiano wowote na siasa, akisisitiza kuwa hajihusishi na masuala ya kisiasa popote duniani, ikiwemo nchini kwake.
''Mimi sio mwanasiasa, sikuja hapa kufanya siasa, hakuna wa kuniambia nini nifanye/nisifanye-Rio
Ferdinand amesema hakuna mtu mwenye mamlaka ya kumwelekeza nini afanye au asifanye, huku akieleza kufurahishwa kwake kwa kupewa heshima ya kuwa balozi wa utalii wa Tanzania.
"Nashukuru kwa heshima hii na ninaiona kama fursa ya kuitangaza Tanzania kwa ulimwengu," amesema Ferdinand.
Haya yanajiri baada ya kukosolewa kwa kile kinachoitwa “sportswashing” yaani kutumia michezo kusafisha taswira ya nchi, baada ya kuonekana akiunga mkono serikali ya Tanzania ambayo imekuwa na utata.
Ferdinand, 47, aliripotiwa kupokelewa katika ziara yake nchini Tanzania na Waziri wa Utamaduni na Michezo, Paul Makonda, ambaye aliwekewa vikwazo na serikali ya Marekani mwaka 2020 kutokana na kile kilichoelezwa kama “ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu”.
Makonda anasemekana kuhusishwa na kampeni dhidi ya watu wa jinsi moja.
Mke wake pia aliripotiwa kuwekewa vikwazo na Marekani.
Serikali ya Marekani ilisema: "Amehusishwa katika ukandamizaji wa upinzani wa kisiasa, kukandamiza uhuru wa kujieleza na kujumuika, na kulenga watu waliotengwa."
Katika hafla ya mapokezi baada ya Ferdinand kuwasili nchini, ambapo alivishwa bendera ya Tanzania, alinukuliwa akimwita Makonda: "Rafiki yangu Paul".
Mkurugenzi wa kampeni ya Amnesty International UK, Felix Jakens, aliambia The Times: "Amnesty International imekuwa ikifuatilia kwa karibu hali ya haki za binadamu inayotatiza sana nchini Tanzania, ambapo vikosi vya usalama vilitumia nguvu zisizo halali dhidi ya waandamanaji mwishoni mwa 2025, na kuua na kujeruhi mamia."
"Kutokana na hali hiyo, Rio Ferdinand anapaswa kuzungumza dhidi ya ukiukwaji wa haki unaofanyika huko, sio kutoa wasifu wake kuunga mkono serikali."
"Ziara ya watu mashuhuri hayafanyiki kwa urahisi - hutuma ujumbe - na hii ina alama zote za kusafisha taswira ya Tanzania kupitia michezo."
Shirika hilo limemtaka Ferdinand kutumia jukwaa lake kuzungumzia madai ya ukiukwa wa haki za binadamu badala ya kuonekana kuihalalisha serikali kupitia umaarufu wake.