Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Putin aapa kulipiza kisasi baada ya kuishutumu Ukraine kushambulia bweni la wanafunzi

Putin amesema shambulio la Ukraine lilifanywa kwa mfululizo mara tatu kwa kutumia ndege zisizo na rubani 16.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Shirika la ndege la Uganda lasitisha safari za Kinshasa kwa hofu ya Ebola

    Shirika la ndege la Uganda Airlines limetangaza kusitisha kwa muda safari za ndege kwenda na kutoka Kinshasa kufuatia hofu ya mlipuko wa Ebola hivi karibuni katika eneo hilo.

    Katika taarifa kwa umma iliyotolewa na usimamizi wa shirika hilo la ndege, kampuni hiyo ilisema uamuzi huo utaanza kutekelezwa kuanzia Mei 23, 2026, hadi watakapotoa taarifa nyingine

    Shrika hilo aidha limesema kuwa uamuzi huo umechukuliwa “kama hatua ya tahadhari kwa maslahi ya afya, usalama, na ustawi wa abiria wetu, wahudumu wa ndege, na abiria kwa ujumla.”

    Shirika hilo la ndege lilisema kuwa abiria walioathiriwa na kusitishwa kwa safari wanapaswa kuwasiliana na kampuni kupitia njia zake za huduma kwa wateja ili kupata msaada.

    “Tunasikitika kwa usumbufu wowote utakaosababishwa na hali hii na tutashkuru kwa uelewa na ushirikiano wa wateja wetu tunaowathamini katika kipindi hiki,” taarifa hiyo ilisema.

    Uganda Airlines iliongeza kuwa itaendelea kufuatilia hali hiyo “kwa karibu kwa kushirikiana na mamlaka husika za afya na usafiri wa anga,” na kusema kuwa taarifa zaidi zitatolewa zitakapopatikana.

    Mnamo Mei 21, Uganda ilithibitisha visa viwili vya kuambukizwa kutoka nje vya aina ya Bundibugyo ya Ebola vinavyohusishwa na mlipuko unaoendelea katika Jamhuri ya Demokrasi ya Congo (DRC), jambo lililosababisha kuimarishwa kwa ufuatiliaji na hatua za dharura za kukabiliana na ugonjwa huo nchini kote.

    Katibu wa kudumu katika Wizara ya Afya ya Uganda, Diana Atwine, alisema kuwa mmoja wa wagonjwa hao amefariki dunia huku mgonjwa wa pili akiendelea kupata nafuu baada ya kupatikana hana maambukizi ya Ebola katika vipimo vilivyofanywa Mei 18 na Mei 20

    Atwine alisema mamlaka tayari zimewatambua na kuwaweka watu 127 waliokaribiana na wagonjwa hao chini ya karantini ya taasisi kama sehemu ya juhudi za kudhibiti ugonjwa huo.

    Soma zaidi:

  2. Uganda yathibitisha visa vitatu vipya vya Ebola

    Uganda imethibitisha visa vitatu vipya vya Ebola, huku mamlaka zikiimarisha ufuatiliaji wa waliogusana na waliotambuliwa kuwa na virusi hivyo ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

    Shirika la Afya Duniani limetangaza kuzuka kwa aina adimu ya virusi vya Ebola Bundibugyo kuwa dharura ya afya ya umma inayotia wasiwasi kimataifa, na kusema hatari ya janga la kitaifa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ni "juu sana".

    Takriban maambukizi 750 yanayoshukiwa kuwa ya ugonjwa huo na vifo 177 vimerekodiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo ni kitovu cha mlipuko huo.

    WHO imesema ugunduzi wa kuchelewa, kutokuwepo kwa chanjo au tiba maalum kwa virusi, vurugu zilizoenea za kutumia silaha na uhamaji mkubwa miongoni mwa wakazi hufanya Congo kuwa katika hatari zaidi.

    Visa vipya nchini Uganda vinajumuisha dereva aliyemsafirisha mgonjwa wa kwanza aliyethibitishwa nchini humo na mfanyakazi wa afya aliyevipata wakati akimtunza mgonjwa huyo.

    Wote wawili wanapokea matibabu na walitambuliwa miongoni mwa watu wanaojulikana kuwasiliana nao mwathiriwa, wizara ilisema katika taarifa.

    Kisa cha tatu ni mwanamke kutoka Congo ambaye aliingia Uganda akiwa na dalili ndogo za tumbo na baadaye akasafiri kutoka Arua, karibu na mpaka, hadi Entebbe kabla ya kutafuta huduma katika hospitali ya kibinafsi katika mji mkuu wa Kampala.

    Soma zaidi:

  3. Rais wa Senegal amfuta kazi Waziri Mkuu Sonko

    Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye amemfuta kazi Waziri Mkuu Ousmane Sonko, kwa kutumia amri ya rais siku ya Ijumaa.

    Uamuzi huo uliotangazwa kwenye runinga ya serikali unamaliza miezi kadhaa ya kile kinachoonekana kuwa mzozo wa madaraka na mvutano kati ya Rais Faye na Waziri Mkuu Sonko.

    Waziri Mkuu Sonko, ambaye ni maarufu miongoni mwa vijana alimchagua Faye kama mbadala wake kwa uchaguzi wa urais wa 2024 baada ya kuzuiwa kugombea.

    Kufutwa kazi huku kunafuatia msururu wa maswali na majibu katika Bunge la Kitaifa ambapo alimkosoa waziwazi Rais Faye.

    Mamia ya wanafunzi kutoka UCAD (Chuo Kikuu cha Cheikh Anta Diop) waliingia kwenye mitaa ya Dakar kuonyesha kumuunga mkono Ousmane Sonko.

    Sonko alitangaza kwenye mtandao wa X kwamba anaweza kulala kwa amani usiku wa jana.

    "Alhamdulillah. Usiku wa leo nitalala nikiwa na amani katika mtaa wa Keur Gorgui."

    Hivi majuzi, Ousmane Sonko mwenyewe alikuwa amedokeza uwezekano wa kurejea kwa upinzani.

    Ousmane Sonko na chama chake walishinda viti 130 kati ya 165 katika Bunge la Kitaifa.

    Mnamo Jumanne, Aprili 28, Wabunge wa Senegal walipitisha marekebisho ya vifungu viwili vya kanuni za uchaguzi, kuruhusu watu waliopatikana na hatia ya makosa madogo kushiriki katika chaguzi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Ousmane Sonko, kwa uchaguzi ujao wa urais mwaka wa 2029.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Takriban watu 90 wafariki katika mlipuko wa mgodi wa makaa ya mawe China

    Takriban watu 90 wameuawa katika mlipuko wa mgodi wa makaa ya mawe kaskazini mwa China, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya nchi hiyo.

    Mlipuko wa gesi ulitokea katika Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Liushenyu, unaoendeshwa na Kundi la Tongzhou, katika Mkoa wa Shanxi.

    Mamia ya waokoaji wametumwa kwenye eneo hilo. Picha kutoka kwa vyombo vya habari vya serikali zilionyesha wahudumu wa afya wakiwa wamebeba machela kwenye eneo hilo, huku magari ya wagonjwa yakiwa nyuma. Inasemekana zaidi ya watu 100 wamepelekwa hospitalini, huku kazi ya uokoaji kwenye eneo hilo ikiendelea.

    Mlipuko huo ulitokea saa 19:29 kwa saa za huko siku ya Ijumaa (11:29 GMT) katika mgodi wa makaa ya mawe huko Shanxi, huku wafanyakazi 247 wakiripotiwa kuwa kazini wakati wa tukio hilo.

    Kufuatia tukio hilo, Rais wa China Xi Jinping alitoa wito wa juhudi zozote zisifanyike kuwatibu waliojeruhiwa na kuwatafuta manusura.

    Pia aliiomba serikali kuchunguza chanzo cha ajali hiyo na kuwawajibisha waliohusika.

    Maafisa wanaoendesha mgodi wa makaa ya mawe wamekamatwa, kulingana na vyombo vya habari vya serikali. Chanzo cha mlipuko wa gesi bado hakijafichuliwa, lakini vyombo vya habari vya serikali viliripoti kwamba viwango vya kaboni monoksaidi - gesi yenye sumu kali na isiyo na harufu - katika mgodi vilipatikana kuwa "vimezidi kiwango" kinachokubalika.

  5. Putin aapa kulipiza kisasi baada ya kuishutumu Ukraine kushambulia bweni la wanafunzi

    Rais wa Urusi Vladimir Putin ameahidi kulipiza kisasi baada ya kuishutumu Ukraine kwa kufanya shambulio baya kwenye bweni la wanafunzi katika sehemu inayokaliwa mashariki mwa Ukraine.

    Watu sita waliuawa na 39 kujeruhiwa katika shambulizi la usiku kucha katika mji wa Starobilsk, mkoa wa Luhansk, Putin alisema. Watu wengine 15 hawajulikani walipo.

    Jeshi la Ukraine lilisema limeshambulia makao makuu ya kitengo cha kijeshi cha kifahari cha Rubicon huko Starobilsk. Halikusema kama lilikuwa jengo lile lile na lile lililotambuliwa na Urusi.

    "Hakuna vituo vya kijeshi, vituo vya huduma za ujasusi, au huduma zinazohusiana katika eneo hilo," Putin alisema huko Urusi.

    "Kwa hivyo, hakuna msingi wowote wa madai kwamba silaha zilishambulia jengo hilo kutokana na mifumo yetu ya ulinzi wa anga," alisema katika mapokezi katika makazi yake Kremlin siku ya Ijumaa.

    Aliamuru jeshi la Urusi kuandaa "mapendekezo" yake kuhusu jinsi ya kulipiza kisasi.

    Kiongozi huyo wa Urusi alisema shambulio la Ukraine lilifanywa kwa mfululizo mara tatu kwa kutumia ndege zisizo na rubani 16.

    Televisheni ya serikali ya Urusi ilionyesha kile ilichosema ni mmoja wa wanafunzi waliojeruhiwa, ikimtambulisha kama Diana Shovkun, mwenye umri wa miaka 19.

    Soma zaidi:

  6. Hatari ya Ebola yaongezeka hadi 'juu zaidi' nchini DR Congo - WHO

    Kiwango cha hatari ya afya ya umma kutokana na mlipuko wa sasa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imeongezwa kutoka "juu" hadi "juu zaidi" na Shirika la Afya Duniani (WHO).

    Katika taarifa mpya Ijumaa, mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus pia alisema hatari katika eneo pana barani Afrika ilikuwa "juu", lakini imesalia "chini" duniani kote.

    Aina adimu ya Ebola, inayojulikana kama Bundibugyo, haina chanjo iliyothibitishwa na inaua takriban theluthi moja ya walioambukizwa. Hadi sasa, mlipuko huo unaojikita katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo umesababisha vifo takriban 177 na maambukizi yanayoshukiwa kuwa 750.

    Hii inakuja huku wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza wakitengeneza chanjo mpya ambayo inaweza kuwa tayari kwa majaribio ya kimatibabu ndani ya miezi miwili hadi mitatu.

    Kulingana na teknolojia ile ile waliyotengeneza kwa ajili ya chanjo ya Covid ya AstraZeneca, hakuna uhakika kwamba itafanya kazi na itahitaji utafiti wa wanyama na majaribio kwa watu ili kujua kama itafanya kazi.

    BBC inaelewa kuwa majaribio ya wanyama tayari yanaendelea huko Oxford.

    Taasisi ya Serum ya India imepangwa kutoa chanjo ya Ebola kwa wingi mara tu Oxford itakapoweza kutoa vifaa vya kiwango cha matibabu.

    Chanjo tofauti ya majaribio ya Bundibugyo pia inatengenezwa, lakini inatarajiwa kuchukua miezi sita hadi tisa kwa kipimo chochote kuwa tayari kwa majaribio.

    Soma zaidi:

  7. Rubio ajaribu kutuliza washirika wa Nato juu ya mabadililo ya wanajeshi wake kupelekwa Ulaya

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amejaribu kuwahakikishia washirika wake kuhusu maamuzi ya Marekani juu ya kupelekwa kwa wanajeshi barani Ulaya.

    Kuingilia kati kwa Rubio mwishoni mwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Nato nchini Sweden kulikuja baada ya Rais Donald Trump kusema kwamba Marekani itatuma wanajeshi 5,000 zaidi nchini Poland.

    Uamuzi huo ulikuwa wiki moja baada ya mpango wa kupeleka wanajeshi 4,000 nchini humo kufutwa na siku chache baada ya tangazo kwamba wanajeshi wa Marekani wangeondolewa kutoka Ujerumani.

    Matangazo hayo yamesababisha mkanganyiko miongoni mwa washirika wa shirika la ulinzi la trans-Atlantic. Hata hivyo, katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mkutano wa Nato siku ya Ijumaa, Rubio alisema Marekani ilikuwa ikitathmini upya uwepo wake wa wanajeshi kila mara kwa kuzingatia ahadi zake za kimataifa.

    Baadhi ya wanajeshi wa Marekani kwa sasa wako Mashariki ya Kati, kufuatia mzozo wa Marekani na Israel na Iran.

    Trump alitoa tangazo kuhusu kupelekwa kwa wanajeshi wapya Poland huku mawaziri wa Nato wakiwa Sweden kwa mazungumzo.

    Akiandika kwenye jukwaa lake la Truth Social siku ya Alhamisi, Trump alisema uamuzi huo ulitokana na uhusiano wa Marekani na Rais wa Poland Karol Nawrocki, ambaye alimuunga mkono wakati wa uchaguzi wa rais mwaka jana na ambaye ni mfuasi wake wa muda mrefu.

    Kiongozi huyo wa Marekani hakufafanua zaidi kama wanajeshi hao wa ziada walikuwa sehemu ya mpango wa awali wa kupelekwa au operesheni tofauti.

    Soma Zaidi:

  8. Hujambo msomaji wetu. Karibu katika matangazo ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 23/05/2026