WARIDI WA BBC: 'Nina uke mara mbili na sijawahi kupata hedhi'

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Hebu fikiria, ukigundua kuwa mwili wako una hali ambayo ni nadra sana hivi kwamba hata madaktari wanatatizika kuielezea - na kwamba figo moja ulionayo, inaweza kuwa muamuzi wa hatma ya maisha yako.

Ndivyo ilivyo kwa msichana Abigael Kendi, binti mwenye umri wa miaka 19, kutoka Kenya aliyezaliwa na mlango wa kizazi mara mbili, tumbo la uzazi mara mbili, uke mara mbili na figo moja.

Asha Juma alipata fursa ya kuzungumza naye na kuangazia changamoto anazokumbana nazo.

Abigael amekukuwa akipitia changamoto ya maradhi kutokana na hali yake aliyozaliwa nayo kutoka mwaka 2020 hadi sasa.

Safari ya ugonjwa ya Abigael

Abigael aliinukia kama watoto wengine wa kisichana lakini hali yake ya kiafya ilianza kubadilika wakati alipoingia kwenye kipindi cha kuvunja ungo.

"Nilianza kupata maumivu makali wakati wa hedhi, na kila nilipomwambia mama, aliniambia hiyo ni hali ya wasichana. Nikawa navumilia tu. Nikaanza kutoenda chooni, kutokojoa kawaida na pia nikawa ninatapika. Nilimueleza mama ingawa aliona ni mzaha," Abigael anasema.

Hali hii ilimfanya binti huyo kukosa furaha na siku iliyofuatia mwili wake ulianza kubadilika na akapelekwa hospitalini.

"Walianza kunifanyia vipimo vya mimba kwa sababu tumbo langu lilionekana kufura huku wengine wakisema mimi ni mjamzito," anasema Abigael.

Ila vipimo vilipoonyesha kuwa yuko sawa. Ililazimu madaktari kuagiza vipimo vingine kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi.

Ni wakati gani wazazi wa Abigael waligundua binti yao ana tatizo hili?

"Wakati nilipolazwa hospitalini ili niwekewe dawa ya kupitisha choo kwa sababu tumbo lolikuwa limefura. Nilifanyiwa vipimo vya CT scan ndio wakaona kwamba kando na figo moja, nina mlango wa kizazi mara mbili, mifuko ya uzazi mara mbili pamoja na uke mara mbili," Abigael anasema.

"Mimi nilijua kuwa na figo moja sio shida kwa sababu watu wanaweza kutoa kiungo hiki na kusaidia wengine lakini yangu ilikuwa na maji kila wakati, nilikuwa naambiwa nitumie dawa isiwe na vijiwe vya figo. Nilikua na uwoga sana kuwa maisha yangu yako hatarini na kipindi hicho niliona ni kheri niwachane nayo tu," Abigael anakumbuka.

Hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kabisa kwa wazazi kujua kuwa mtoto wao ana matatizo la kiafya.

Abigael anakumbuka kumuona mama yake akibubujikwa na machozi baada ya kupewa taarifa hizo.

'Sijawahi kupata hedhi'

Abigael, anasema hali hii imemfanya apitie changamoto nyingi.

""Mimi hupata maumivu lakini siwezi kupata hedhi kama wanawake wengine. Sijawahi kupata hedhi hata siku moja. Pengine, wakati nimetoka CT scan ndio niliona kitu kama damu damu na nikasema pengine nimeanza kupata siku zangu za hedhi.

"Napata maumivu kabisa, mfano, mwezi huu kuanzia tarehe 10 hadi 15 na tarehe 20 hadi 25 lakini siwezi kupata hedhi. Sijawahi kupata hedhi wala kuvaa sodo kama msichana wa kawaida akiwa kwenye siku zake," Abigael anasema.

Hali hii ilimfanya Abigael ajihisi kuwa hayuko sawa. "Nikaanza kujitoa makosa, nililaumu mwili wangu, hata nimeandika kitabu, nikizungumzia sehemu hii".

'Sio rahisi kwenda haja'

"Wakati mwingine nilihisi mwili wangu unatoa harufu nyingine ambayo hata sikuwa naelewa," Abigael anasema.

Binti huyo pia anaongeza kuwa wakati anapitia maumivu makali kuashiria kuwa ndio yuko kwenye hedhi, akitembea, watu walikuwa wakimwambia anaonekana akiwa ameegemea upande mmoja. Hii inatokana na uzito anaohisi kipindi hiki ambao umelalia utumbo mpana.

Na pia akiwa katika hali hii, kuna vitu ambavyo anatamani kupata lakini hawezi.

"Siwezi kwenda haja kubwa. Wakati mwingi huwa ninatumia dawa. Pia huwa ninatumia mpira wa kupitisha mkojo. Nawekwa wa kukaa kama wiki mbili. Lakini walipoona ninapata maambukizi mengi, wakaanza kunifunza namna ya kujiweka mpira mwenyewe. Ikawa wakati wa kujisaidia, naingia, natoa mkojo kisha nautupa.

Ugonjwa anaopitia, Abigael umemfanya kuwa na matatizo ya kupata ama haja kubwa au haja ndogo.

"Sio rahisi. Labda iwe ni wakati ambao nimefanyiwa mchakato wa kusafisha utumbo mpana ili kuondoa uchafu wa tumboni. Na pia hata kama nimefanyiwa mchakato huo, sitahisi kwenda haja. Nitaenda tu kwa sababu nimekula na niseme acha niende chooni nijaribu kujisaidia. Kwa namna hii naweza kupata choo, vinginevyo, huwa natumia mipira tu," Abigaeli anasema.

Wakati hedhi nyingi zimeingia kwenye sehemu ya viungo vya uzazi, ndio anakwenda kusafishwa utumbo.

'Madhila niliyopitia shuleni'

Mpira wa kupitisha mkojo ni kifaa alichokitumia hata alipokuwa shuleni.

"Bado hata saa hivi huwa nautumia nikienda kujisaidia haja ndogo kwa sababu waliona kibofu changu cha mkojo kimetanuka," Abigael anasema.

Kama haitoshi, Abigael alikuwa amepewa ruhusa ya kutumia choo chake peke yake akiwa shuleni, ila kibaya zaidi wanafunzi wenzake walitaka kujua kwanini yeye apewe hadhi kama hiyo.

"Wanafunzi wengi walikuwa wananiuliza kwani mimi ni wa kipekee namna gani hadi napewa choo changu. Pia kuna walimu ambao hawakunielewa na pengine ikiwa ni zamu mmoja wao. Atazungumza vibaya akidai kuwa mimi sio wa kwanza kufanyiwa upasuaji ila nilivumilia hadi wiki yake iishe," Abigaeli anasema.

Usichokijua ni kwamba Abigaeli amekuwa kwenye maumivu kwa kipindi kirefu cha maisha yake.

"Nimekuwa nikiumwa na kichwa kila wakati. CT scan nyingine nilifanyiwa na wakagundua kwamba nina maji kwenye kichwa. Lakini walisema hawawezi kuniweka marija kwa sababu kibofu cha mkojo bado kina matatizo. Na figo ni moja ambayo itakuwa na wakati mgumu wa kufanyakazi vizuri ikiwa nitafanyiwa upasuaji huo," anasema Abigael.

Nimefanyiwa upasuaji mara saba

Abigael anasema safari yake ya kutafuta tiba, haijakuwa rahisi.

"Nimefanyiwa upasuaji mara saba kurekebisha uzazi ili niweze kuona hedhi zangu kama wanawake wengine lakini sijafaulu," Abigael anasema.

Kama mwanadamu, binti huyo amewahi kufika wakati akahisi kuwa amechoka na matibabu.

"Upasuaji nimefanyiwa. Kuna wakati naona nawachosha wazazi wangu kwa sababu wametumia pesa zao, wameuza vitu vingi kwa ajili yangu na hata wakiuza hakuna kitu kinafaulu. Huwa ninahisi kukata tamaa. Kuna wakati nilikuwa nimewaambia afadhali nife," Abigael anakumbuka, "lakini kwa sababu ya maneno yao ya kunitia moyo. Ninaona wananijali na kunihitaji, najipa moyo na kusema kesho itakuwa siku nzuri zaidi."

Dhana potofu

Katika jamii ni jambo la kawaida wengine kukosa kukuelewa hasa wakati unapitia changamoto zako za maisha. Abigael anasema kila mtu amekuwa na mtazamo wake juu ya hali anayopitia.

"Hatukuwa tumefunguka moyo kuwaelezea kuwa nina viungo vya uzazi mara mbili mbili. Hawakuwa wanatuelewa. Walifikiri labda nasema tu mimi ni mgonjwa lakini hawajui hasa naumwa na nini.

"Wengine wanasema pengine ni uchawi au labda kuna kitu bibi yetu aliacha na hakusema, kuna wanaosema tunafaa kwenda kwa muhubiri kwa ajili ya uponyaji. Wengine wanasema nimerongwa," Abigael anakumbuka.

Binti huyo anasema kuwa amelazimika kufungua moyo wake wakati huu na kuzungumzia hali anayokabiliana nayo kwa kuwa wazazi wake wamefanya kila wanaloweza ili apate matibabu lakini bado hajafanikiwa kupata tiba ambayo imetatua shida aliyonayo.

"Nimefungua moyo wangu kwa matumaini kuwa huenda nitakutana na msamaria mwema anayeweza kusikia shida yangu na anisaidie kwa njia moja au nyingine. Pengine pia wengine ambao wamejifungia, wenye tabu kama zangu watafunguka.

Abigael anatoa wito kwa wale ambao wamekuwa wakikabiliana na matatizo ya kiafya kimya kimya kuacha uwoga na wajitokeze ili waweze kupata usaidizi.

Kufikia sasa, Abigael amepata fursa ya kupata matibabu katika hospitali kuu ya kitaifa ya Kenyatta nchini kenya na hili limeendelea kumtia matumaini kuwa ipo siku, ndoto yake ya kuwa daktari itatimia.