Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maseneta waishinikiza Marekani kutathmini upya uhusiano na Tanzania
Maseneta wawili wa Marekani kutoka vyama tofauti, Jeanne Shaheen na Ted Cruz, wamewasilisha muswada mpya unaolenga kutathmini upya uhusiano wa Marekani na Tanzania kufuatia madai ya kuzorota kwa demokrasia, ukandamizaji wa kisiasa na ukiukwaji wa haki za binadamu baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Muswada huo unaoitwa 'Reassessing the United States Tanzania Bilateral Relationship Act' umewasilishwa mjini Washington na unashinikiza kufanyike tathmini ya kina ya ushirikiano wa kiusalama, kiuchumi na kidiplomasia kati ya Marekani na Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa ya maseneta hao, mamlaka za Tanzania zilidaiwa kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji, kuzima mtandao wa intaneti nchini kote, kuwazuia majeruhi kupata huduma za afya, kuwakamata baadhi ya waandamanaji hospitalini pamoja na kuondoa miili kutoka mochwari ili kuficha ukubwa wa ukandamizaji huo.
Serikali ya Tanzania hata hivyo inasisitiza kuwa matukio ya wakati na baada ya uchaguzi wa wa Oktoba 29 hayakuwa maandamano bali vurugu na kwamba maafisa wa usalama walichukua hatua kudhibiti hali ya usalama. Taifa hilo la Afrika Mashariki pia liliunda Tume ya uchunguzi ambayo iliwasilisha matokeo ya ripoti yake kwa Rais Samia Hassan Suluhu mnamo April 23, 2025.
Na wiki hii tume nyingine ya uchunguzi wa kijinai wa matukio ya Oktoba 29 imeundwa kama ilivyopendekezwa na time ya uchunguzi ya awali.
"Tanzania imekuwa mshirika muhimu wa Marekani katika Afrika Mashariki, lakini kuzorota kwa demokrasia, vurugu za kisiasa na ukandamizaji wa hivi karibuni haviwezi kupuuzwa," amesema Jeanne Shaheen.
Ameongeza kuwa muswada huo unaonyesha kuwa Marekani lazima isimame kidete kutetea misingi ya demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria, huku pia ukitaja wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa ushawishi wa China nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Ted Cruz ameishutumu serikali ya Tanzania kwa kile alichokiita "ukandamizaji wa kisiasa na mateso dhidi ya dini."
"Tanzania ilidhoofisha uhalali na uwazi wa uchaguzi wa Oktoba 2025 kwa kuzuia vyama vya upinzani kushiriki, kuwakamata na kuwateka viongozi wa dini pamoja na kuvuruga upigaji kura," amesema Cruz.
Unalenga kina nani?
Kwa mujibu wa muswada huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani atatakiwa ndani ya siku 180 baada ya sheria hiyo kupitishwa, kuwasilisha ripoti inayowataja baadhi ya viongozi wakuu wa Tanzania wanaodaiwa kuhusika na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Ripoti hiyo inaweza kuwahusisha viongozi wa serikali, CCM, polisi, jeshi na vyombo vya usalama wanaotuhumiwa kuhusika katika utekaji, kutoweka kwa watu, ukamataji wa kiholela wa wapinzani, wanahabari na wanaharakati.
Muswada huo pia unaeleza kuwa vitendo vya ukandamizaji dhidi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi vinaweza kuchunguzwa chini ya mpango huo.
Marekani inapendekeza nini?
Muswada huo unapendekeza hatua mbalimbali zichukuliwe na serikali ya Samia Suluhu ili kudumisha demokrasia na kuendana na misingi ya kuwa mshirika wa Marekani.
Hatua ambayo imepatiwa kipau mbele ni kuwawekea vikwazo dhidi ya maafisa wa Tanzania hasa wa chama tawala cha CCM watakaobainika walihusika na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ulioshuhudiwa Oktoba 29.
Pendekezo la pili ni kupiga marufuku visa, za wataokutwa hatiani na iwapo wana visa za kuingia Marekani zifutwe mara moja.
Lingine ni viongozi wa CCM watakaopatikana kuwa na mkono katika kukandamiza haki za kibinadamu kama wana mali au biashara Marekani basi zifutwe.
Na pendekezo ambalo huenda likaathiri zaidi Jamhuri ya Tanzania kwa ujumla ni Marekani kusitisha baadhi ya misaada ya kiusalama, biashara na maendeleo hadi pale mageuzi ya kidemokrasia yatakapotekelezwa.
Aidha, muswada huo unaitaka serikali ya Marekani kutathmini kiwango cha ushirikiano wa kijeshi, kisiasa na kiuchumi kati ya Tanzania na China, hasa ushirikiano unaoweza kuathiri taasisi za kidemokrasia na maslahi ya Marekani katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa muswada huo, China imekuwa na ukaribu na Tanzania na inaisaidia ilhali serikali inaminya uhuru wa raia wake.
Wabunge hao pia wameeleza mshikamano wao na wananchi wa Tanzania na kuunga mkono wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru wa kimataifa kuhusu vurugu zilizohusishwa na uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Uhuru wa kuabudu wageuka hoja mpya katika uhusiano wa Tanzania na Marekani
Huku utawala wa Samia Suluhu ukiingia mwaka wake wa pili , Marekani imeendelea kutathmni uchaguzi wa Tanzania wa mwaka 2025 ulivyothiri biashara na utulivu wa kikanda na hata baishara zao.
Muswada huo ambao una ukurasa 18 umemalizia kwa kusema kuwa bunge la Marekani lina wasiwasi na usalama wa watalii na raia wake waliokoTanzania.
Sasa wametoa tahadharii za kiusalama kwa raia wake wakiwataka wajihifadhi mahali salama
Aidha seneta Cruz amedai kuwa vyombo vya dola vya Tanzania vimedhibiti uhuru wa kuabudu, kuzuia mikusanyiko ya Wakristo na kubana shughuli za makanisa.
''Muswada huu utasaidia kukabiliana na ukandamizaji huo wa kisiasa pamoja na mateso dhidi ya Wakristo wa Tanzania, na ninajivunia kuuongoza pamoja na Seneta Shaheen," asema Cruz
Tanzania Ilifikiaje hapa
Tamko hili la Bunge la Seneti la Marekani linajiri siku kadhaa baada ya Samia Suluhu kuunda tume ya uchunguzi wa kijinai wa matukio ya Oktoba 29 ambayo ilipendekezwa na ripoti ya jaji Chande.
Upande wa upinzani, ukiongozwa na John Heche wameeleza kuwa hawajaridhishwa na kilichowasilishwa kuhusu kilichotokea katika vurugu za Oktoba 29 na kutaka uchunguzi wa kimataifa ulio huru utathmini hali ili taifa lipone.
Isitoshe, nao timu ya bunge la Ulaya iliandika wiki mbili zilizopita kuwa imesikitishwa na serikali ya Tanzania kw akutowaruhusu kuinga nchini humo kutathmini na kufanya uchunguzi wa vurugu za wakati wa uchaguzi mkuu.
Japokuwa Samia amekuwa aking'ang'ana kujisafisha na yaliyotokea Oktoba 29 kauli hizi zinaashiria kuwa bado jinamizi hili halitakuwa rahisi kwa utawala wake kulisafisha.