Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Marekani yamuwekea vikwazo Mafwele kwa madai ya 'kuwatesa' wanaharakati wa haki za binadamu
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imemuwekea vikwazo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Faustine Jackson Mafwele kuingia nchini Marekani.
Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio imesema kwa kuzingatia taarifa zinazoaminika, Mafwele alihusika katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
"Mwaka jana, jeshi la polisi liliwakamata, kuwatesa na kuwafanyia ukatili wa kingono raia wa Uganda Agather Atuhaire na raia wa Kenya Boniface Mwangi, waliokuwa jijini Dar es Salaam kufuatilia kesi mahakamani dhidi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu," imeeleza sehemu ya taarifa ya Rubio.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Mahmoud Thabit Kombo aliiambia BBC kwamba serikali bado haijapokea rasmi taarifa ya hatua hiyo, ambayo inamzuia Mafwele kuingia nchini Marekani.
Vikwazo hivyo vinakuja wakati ambapo uchunguzi kuhusu rekodi ya haki za binadamu ya Tanzania unaongezeka, huku wabunge wa Marekani wakitaka hatua kali zaidi zichukuliwe.
Mwezi Februari mwaka huu kitengo cha uchunguzi cha BBC Africa Eye kilitoa filamu iliyoitwa 'Hali ya hofu Tanzania' na kuchunguza juu ya wimbi la matukio ya utekaji Tanzania. Katika filamu hiyo manusura wa matukio hayo wakiwemo Atuhaire na Mwangi walimtaja Mafwele kama mhusika mkuu wa kadhia zilizowafika.
Jeshi la Polisi na Mafwele hawakuwapa ushirikiano BBC licha ya kutafutwa. Hata hivyo serikali ya Tanzania iliiambia BBC Africa Eye kuwa wawili hao waliingia Tanzania kwa madhumuni ya utalii lakini uchunguzi wa idara ya uhamiaji ukagundua kuwa walikusudia kuhudhuria kesi kinyume na tamko lao la kuingia nchini.
"Kukamatwa kwao kulifanyika kisheria. Idara ya uhamiaji inakanusha madai yoyote ya makosa," serikali ya Tanzania iliiambia BBC Africa Eye.
Wanaharakati hao wawili walikuwa wamesafiri kwenda Tanzania kufuatilia kesi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu mwezi Mei mwaka jana walipokamatwa na baadaye kuachiliwa, huku Mkenya Boniface Mwangi akisema alizuiliwa kwa siku kadhaa pamoja na Agather Atuhaire kutoka Uganda.
Mwangi alidai kuwa alivuliwa nguo, alining'inizwa kichwa chini, alipigwa kwenye nyayo za miguu na kufanyiwa ukatili wa kingono akiwa mahabusu, huku Atuhaire pia akisema alibakwa wakati wa kuzuiliwa kwake nchini Tanzania.
Polisi wakati huo ilikanusha madai hayo ya mateso, ikieleza simulizi za wanaharakati hao kuwa ni "maoni" na "tetesi".
Taarifa ya Rubio haikueleza moja kwa moja jukumu analotuhumiwa kuwa nalo Faustine Jackson Mafwele, lakini Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia Demokrasia, Haki za Binadamu na Kazi Riley Barnes alisema Marekani ilikuwa "ikichukua hatua kuhimiza uwajibikaji kwa kitendo hiki cha kinyama".
Mafwele, ambaye anahudumu kama Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi nchini Tanzania, ndiye afisa wa kwanza mwandamizi wa serikali chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan kukumbwa na vikwazo kutoka nje ya nchi.
BBC imeliomba jeshi la polisi la Tanzania kutoa maoni kuhusu suala hilo.
Amnesty International hapo awali ilikuwa imetaka uchunguzi wa haraka kuhusu kile ilichokiita kukamata kiholela, mateso, kuzuiliwa bila mawasiliano na kufukuzwa kwa nguvu kwa wanaharakati hao wawili.
Human Rights Watch pia ilitaja kesi hiyo katika ripoti yake ya mwaka huu kuhusu Tanzania, ikielekeza kwenye kile ilichosema kuwa ni ukandamizaji mkubwa dhidi ya viongozi wa upinzani, wanaharakati na uhuru wa kujieleza.
Vikwazo hivyo vinakuja wakati Tanzania ikiendelea kuchunguza taarifa za ukandamizaji wa kisiasa na ukiukwaji wa haki zinazohusishwa na uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana.
Jumla ya watu 518 walifariki dunia, wakiwemo 197 waliopigwa risasi hadi kufa, katika maandamano makubwa yaliyofuatia uchaguzi uliozozaniwa, tume ya uchunguzi iliyoundwa kuchunguza vurugu hizo ilitangaza mwezi uliopita.
Haikusema ni nani aliyewajibika kwa mauaji hayo lakini ilishutumu makundi yanayofadhiliwa na mataifa ya kigeni kwa kusababisha vurugu hizo. Hata hivyo, upinzani na makundi ya haki za binadamu yanasema idadi ya waliokufa ilikuwa kubwa zaidi na kushutumu vikosi vya usalama kwa kuwapiga risasi waandamanaji wasio na silaha.
Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo kwa kupata asilimia 98 ya kura, jambo ambalo upinzani ulilitaja kuwa ni "dhihaka" kwa demokrasia baada ya wapinzani wake wakuu kuzuiwa kushiriki.
Wakati huo, rais alisema uchaguzi ulikuwa wa haki na wa uwazi na akawalaumu wageni kwa vurugu hizo, akisema zilikuwa sehemu ya njama ya kumuondoa madarakani.
Mamlaka zimekiri kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji, zikidai kuwa baadhi ya makundi yalikuwa yakijaribu kubadilisha utawala kwa nguvu.
Jumanne, wabunge wa Marekani walitaka hatua kali zaidi zichukuliwe dhidi ya taifa hilo la Afrika Mashariki ili kurejesha kile wanachokiita kudorora kwa demokrasia.
Desemba mwaka jana, Washington iliishutumu serikali ya Tanzania kwa kukandamiza uhuru wa dini na uhuru wa kujieleza, kuzuia uwekezaji wa Marekani na kushindwa kuzuia vurugu kabla na baada ya uchaguzi wa mwaka jana.
Ilisema hatua hizo zimewaweka raia wa Marekani, watalii na maslahi ya Marekani katika hatari na kuhatarisha miongo kadhaa ya ushirikiano wa usalama na maendeleo.
Mamlaka za Tanzania hazikujibu.