Kisiwa kinachoendelea kupokea wageni licha ya kuachwa na wakazi

c
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 8

Zamani kilikuwa kitovu cha biashara ya uvuvi katika eneo la Labrador. Leo, Battle Harbour ni sehemu ya mapumziko inayowavutia wageni wanaotaka kujitenga na pilikapilika za maisha ya kisasa.

Watu kadhaa wamekusanyika kwenye gati. Wakiwa wamekunja mikono ya mashati, wavuvi wanne wanaoishi katika kisiwa hiki cha mbali cha Labrador wanapara samaki aina ya chewa.

Nyuma yao, wafanyabiashara waliovalia suti na wavuvi wengine waliovaa mavazi maalumu ya kujikinga na maji wamejipanga kwa ajili ya picha ya pamoja mbele ya jengo jeupe la mbao lenye mapambo mekundu.

Lakini feri yetu inapokaribia gati, kuna kitu kinanifanya nitilie shaka ninachokiona. Watu hao wote wana rangi ya kijivu kama anga lililojaa mawingu. Na hakuna hata mmoja anayesogea.

Natikisa kichwa na kujikumbusha kuwa ninafika mahali panapojitambulisha kwa fahari kuwa umbali wa maili tisa kutoka maisha ya kawaida.

Kwa hakika, watu hao hawapo hai tena. Waliishi hapa mwanzoni mwa miaka ya 1900, wakati Battle Harbour kilikuwa kitovu kikuu duniani cha biashara ya samaki waliokaushwa kwa chumvi. Picha zao za zamani zimechukuliwa kwenye nyaraka na kutengenezwa upya katika umbo la vinyago vya ukubwa halisi wa binadamu.

"Karibu Battle Harbour," anasema Peter Bull, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Urithi wa Kihistoria ya Battle Harbour, tunaposhuka kwenye feri kupitia ubao wa mbao.

Bull anaanza kunieleza mambo muhimu kuhusu maisha kisiwani humo. Chakula cha mchana kitatolewa saa 12:30. Ziara ya kutembelea maeneo ya kihistoria itaanza saa 13:30. Familia ya mbweha wa Aktiki inaishi katika makaburi ya zamani. Minara miwili ya kihistoria ya mawasiliano ya redio inahitaji kuokolewa. Hakuna mtandao wa simu za mkononi, na kuna sehemu moja tu ya pamoja yenye huduma ya Wi-Fi.

Jua huchomoza saa 06:19. Wanda Fifield ndiye atakayenisindikiza hadi chumbani kwangu.

c

Tunapopita kwenye ushoroba karibu na chumba hicho, Fifield anasimama mbele ya kifaa cha mawasiliano ya redio.

"Huu ndio mfumo wetu wa dharura. Unawasha kwa kubonyeza kitufe hiki," anasema.

"Ukipata tatizo usiku, ukiugua au kuumia, bonyeza tu kitufe hiki cha mraba. Waeleze kilichotokea. Usisahau kuwaambia unakaa katika jengo la wafanyabiashara ili wajue ni nyumba gani ya wageni wanayopaswa kwenda."

Kwa nyumba zake za zamani za mbao zilizokarabatiwa, maeneo ya kuchakata samaki na nyumba 16 za binafsi zinazotumiwa wakati wa kiangazi, Battle Harbour kinaonekana kuhifadhiwa vizuri sana.

Lakini imepita zaidi ya miaka 50 tangu watu waishi kisiwani humo mwaka mzima. Na ni muda mrefu zaidi tangu kiwe kitovu kisicho rasmi cha Labrador.

Nina siku mbili za kujitosa katika maisha ya zamani.

Safari ya kuelekea kisiwa kilichosahaulika

f
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kufika Battle Harbour ni safari ya mbali.

Kwanza, unasafiri kwa ndege hadi Happy Valley-Goose Bay, eneo lililopo katika sehemu ya bara ya Labrador. Kisha unaendesha gari kwa takribani saa tano kupitia barabara ya Expedition 51°, inayozungukwa na misitu.

Katika safari hiyo, unakuwa na matumaini ya kuona paa, huku ukitamani kupata choo cha kutumia. Kwa sehemu kubwa ya njia hiyo, hakuna huduma yoyote.

Ukifika kwenye gati la Mary's Harbour, unapanda boti inayosafirisha wageni kisiwani humo kila siku. Wanaiita feri, lakini ni ndogo kiasi kwamba wakati mwingine mizigo ya abiria hulazimika kuwekwa ndani ya bafu.

Safari ya kilomita 14.5, sawa na maili tisa, inapita kando ya pwani yenye miamba na visiwa vidogo. Kukiwa na ukungu, mandhari huonekana ya ajabu. Lakini siku anga linapokuwa la kijivu, eneo lote huonekana lenye upweke.

Njiani, unaweza kuwaona shakwe wakiruka sambamba na boti. Wakati mwingine, bahati inaweza kukuonyesha milima ya barafu inayoelea baharini au nyangumi wakubwa, wakiwemo wale wenye nundu.

Majengo ya Battle Island yanapoanza kuonekana, ni vigumu kuamini kuwa kisiwa hiki kidogo, chenye urefu wa takribani nusu maili, kiliwahi kuwa na shughuli nyingi za wavuvi na wafanyabiashara.

f

Katika miaka ya 1770, mfanyabiashara Mwingereza John Slade alianzisha biashara katika kisiwa hicho. Hatua hiyo ilikifanya kuwa lango la kuelekea maeneo tajiri kwa uvuvi katika pwani ya Labrador.

Samaki aina ya chewa walichakatwa na kuhifadhiwa kwa chumvi kabla ya kusafirishwa kwenda Ulaya, Karibiani na maeneo mengine duniani.

Wakati wa kilele cha mafanikio yake, Battle Harbour kilikuwa na hospitali, shule, kanisa na kituo cha mawasiliano ya redio. Wakazi wa kudumu walikuwa takribani 300, huku maelfu ya wavuvi wengine wakifika kwa msimu.

Baadhi yao waliishi kwenye meli za uvuvi, huku wengine wakijenga vibanda vya muda kwenye nchi kavu.

Lakini baadaye mambo yalianza kubadilika. Moto mkubwa wa mwaka 1930, kupungua kwa samaki baharini na mpango wa serikali ya jimbo wa kuwahamisha wakazi katika miaka ya 1960 vilisababisha watu kuondoka kisiwani humo.

Kufikia miaka ya 1970, wakazi wa mwisho waliokuwa wakiishi hapo mwaka mzima walikuwa wameondoka.

Pigo kubwa zaidi lilifika Julai 2, 1992, wakati serikali ya shirikisho iliposimamisha uvuvi wa chewa. Uamuzi huo uliwaacha watu 30,000 katika maeneo ya Newfoundland na Labrador bila ajira.

Leo, Battle Harbour kinafanana na kisiwa kilichoachwa na watu. Majengo yake yaliyokarabatiwa ni ushahidi wa maisha yaliyokuwepo hapo zamani, lakini ambayo kwa kiasi kikubwa yametoweka.

Kisiwa hiki cha kihistoria, kinachosimamiwa na taasisi ya urithi, hufunguliwa kwa wageni kwa takribani miezi mitatu tu kila kiangazi. Hakuna magari, na hakuna wakazi wa kudumu. Hata hivyo, kwa watu wanaokifahamu vizuri, Battle Harbour hakijawahi kusahaulika.

Maisha katika kisiwa kisicho na pilikapilika

d

Uhusiano wa Bull na Battle Harbour unaanzia zaidi ya karne moja iliyopita, wakati babu yake alipokuwa akivua samaki katika pwani ya Labrador.

Amekuwa akifanya kazi kisiwani humo tangu mwaka 2013. Hutumia muda mwingi wa kiangazi huko, kisha hurudi nyumbani kwake St John's kila Septemba akiwa na samaki aina ya chewa, ngisi, makrill na matunda ya porini, yakiwemo bakeapple na partridgeberry, ya kumsaidia wakati wa majira ya baridi.

"Nikifa, nataka majivu yangu yatawanywe mahali ninapochuma matunda ya partridgeberry," ananiambia. "Kisha nitarejea duniani nikiwa tunda la partridgeberry."

Nelson Smith naye amekuwa na uhusiano wa karibu na kisiwa hicho maisha yake yote. Alishiriki katika kukarabati majengo ya kihistoria na amekuwa akiwaongoza wageni katika ziara za kutembelea kisiwa hicho kwa karibu miaka 30.

"Kila jengo lina harufu yake, kutegemea vitu vilivyokuwa vikihifadhiwa humo," anasema Smith kwa lafudhi nzito ya wenyeji wa Labrador.

"Ukisikia nikitumia neno usilolielewa, nisitishe. Nitajaribu kukueleza."

Katika Kiingereza kinachozungumzwa Newfoundland, majengo haya ya zamani huitwa "the rooms". Kila duka au ghala lina jina linalotokana na bidhaa zilizokuwa zikihifadhiwa humo.

Kwa mfano, duka la nyama ya nguruwe bado lina harufu hafifu ya molasi, huku ghala la chumvi likiwa na chumvi iliyotumiwa kuhifadhi samaki aina ya chewa.

Tunapoendelea na ziara, tunakutana na vinyago vingine vya ukubwa halisi wa binadamu. Kuna mfanyabiashara aliyevalia vizuri, kijana mvuvi aliyesimama ndani ya mashua ya mbao na mvuvi mzee aliyeketi karibu na mtego wa kuvulia samaki.

"Samaki wa chumvi ninaowapenda zaidi ni wale waliokaa kwa miaka miwili," anasema Smith.

Anaendelea kueleza jinsi chewa walivyosafishwa, kutiwa chumvi na kukaushwa kwenye majukwaa ya mbao yaliyoinuliwa na kuwekwa nje.

Katika sehemu ya juu ya ghala la chumvi, ninasimama mahali ambapo mvumbuzi wa maeneo ya Aktiki kutoka Marekani, Robert E Peary, alifanya mikutano miwili na waandishi wa habari mwaka 1909. Hapo alidai kuwa alikuwa amefika Ncha ya Kaskazini.

Pia alituma taarifa yake ya kwanza kuhusu msafara huo kutoka kituo cha mawasiliano cha Marconi kilichokuwa karibu, kwenda kwa gazeti la New York Times.

Kulala katika majengo ya zamani

c

Wageni wanaweza hata kulala katika baadhi ya majengo haya ya kihistoria.

Mimi ninakaa katika chumba cha Harry Smith, kilichopo ndani ya jengo la wafanyabiashara. Chumba hicho kimepewa jina la mfanyakazi wa zamani wa duka kuu la kisiwa hicho.

Pia kuna nyumba tano za wageni zilizokarabatiwa na vyumba vingine 12 vyenye bafu ndani.

Kitanda changu cha mbao kimefunikwa kwa blanketi la viraka. Kifaa cha kupasha joto kinajaribu kukabiliana na baridi inayobaki ndani ya jengo hilo la zamani, licha ya kukarabatiwa.

Hakuna televisheni. Hakuna kelele za magari wala simu. Kilichobaki ni ukimya.

Ninaketi kwenye kiti kinachoweza kuzunguka, nikitazama bahari huku nikisoma kitabu cha kumbukumbu za wageni waliowahi kufika hapa.

"Mwonekano mzuri zaidi kisiwani. Mlima wa barafu ulionekana vizuri kupitia dirishani mwetu," ameandika mmoja.

"Mambo mengine ni lazima uyajionee mwenyewe. Ni vigumu kuyaeleza kwa maneno," anasema mwingine.

Mwingine ameandika kwa kifupi: "Utulivu wa kipekee."

Wakati wa chakula cha jioni, tunakula samaki aina ya Arctic char, chewa waliokaangwa na pai ya nyama ya paa. Wageni wote wanakaa pamoja kwenye meza moja.

Mazungumzo yanahusu uwezekano wa kuona Taa za Kaskazini. Hilo linanifanya nikose usingizi usiku wangu wa kwanza. Mara kwa mara nachungulia dirishani na kutoka kwenye baraza linalozunguka jengo, nikitumaini kuona mwanga huo.

Lakini bahati yangu inakuwa nzuri zaidi wakati wa mapambazuko. Ninafuata njia ya udongo kuelekea makaburi ya zamani na kufanikiwa kuwaona mbweha wakitoka kwenye makazi yao yaliyopo kwenye kilima chenye miamba.

Kutoka hapo, ninaendelea na matembezi kwenye njia ya Battle Harbour Footpath. Njia hiyo ina urefu wa kilomita 1.9 na inapita karibu na makaburi mapya zaidi pamoja na mnara wa kumbukumbu ya wanaume watatu waliopoteza maisha katika ajali ya ndege ya majini mwaka 1976.

Wavulana wawili wa eneo hilo walikuwa wa kwanza kukutana na mabaki ya ndege hiyo. Baadhi ya mabaki hayo bado yapo kisiwani. Mmoja wa wavulana hao alikuwa Smith.

Karibu na mwisho wa njia hiyo, ninaona minara miwili ya mawasiliano ya Marconi. Hii ndiyo jozi pekee ya aina yake iliyosalia Amerika Kaskazini.

Minara hiyo ilijengwa mwaka 1906 na kujengwa upya mwaka 1931. Ilitumia mfumo wa mawasiliano bila waya uliotengenezwa na Mwitaliano Guglielmo Marconi. Zamani, minara hiyo ilisaidia kuwaongoza mabaharia na kusambaza ujumbe.

"Ni minara ya kipekee na ni sehemu muhimu ya mandhari ya kisiwa hiki," anasema Bull.

Taasisi ya urithi inajaribu kukusanya dola 200,000 za Canada, sawa na takribani pauni 106,000 za Uingereza au dola 140,000 za Marekani, ili kuikarabati.

Upepo mkali unaharibu mipango yangu ya kwenda kuvua chewa. Hata hivyo, ninafanikiwa kufanya safari fupi ya boti hadi Cape St Charles, sehemu inayotajwa kuwa eneo la mashariki zaidi katika bara la Amerika Kaskazini.

Baadaye ninavuka mkondo mwembamba wa bahari kuelekea Great Caribou Island kwa ajili ya matembezi. Huko nakutana na Tanya Russell, msimamizi wa posta wa eneo hilo ambaye pia ni mpiga picha wa kujitegemea. Namkuta akiwa katika eneo linalolimwa matunda aina ya blueberries.

Russell anasema anapenda kila kitu kuhusu Battle Harbour.

"Napenda utulivu wake, maji, hewa ya bahari yenye chumvi, ndege na mbweha. Kwa kweli, kila kitu kuhusu hapa kinakuvutia. Pia unapata nafasi ya kukutana na watu wengi wazuri," anasema.

Kisiwa ambacho hakijasahaulika

c

Kifungua kinywa changu cha mwisho kinafika, na ni wakati wa kuwaaga wageni wenzangu. Hata vinyago vya watu waliowahi kuishi kisiwani humo vinabaki nyuma.

Ninakula karibu na kinyago kilichotengenezwa kutokana na picha maarufu ya zamani ya rangi nyeusi na nyeupe, iliyopigwa Battle Harbour zaidi ya karne moja iliyopita.

Picha hiyo inaonyesha mvulana mwenye uso wa huzuni akiwa kati ya samaki wawili wakubwa wa chewa.

Mvulana huyo aliitwa Victor Croucher. Amezikwa kisiwani humo, lakini hapa kwenye ukumbi wa chakula, anaendelea kuwepo kama kumbukumbu nyingine ya maisha ya zamani.

Ni taswira inayofaa kabisa kwa Battle Harbour. Kisiwa kinachoonekana kana kwamba kiliachwa na kila mtu, lakini ambacho bado kinashikilia historia yake na kuendelea kuwakaribisha wageni.