Moja kwa moja , Maandamano Ujerumani: Gharama ya maisha yachochea ghasia na uporaji

Ghasia pia ziliripotiwa katika miji ya Berlin, Cologne na Hamburg, huku polisi wakitumia maji kuwatawanya waandamanaji.

Muhtasari

Moja kwa moja

Ambia Hirsi

  1. Iran: Marekani haitaamua namna au wakati vita vitakapomalizika

    Tehran imeonya kuwa mzozo wowote mpya kati yake na Marekani unaweza kuwa wa muda mrefu zaidi na huenda ikavuka mipaka ya Iran, kufuatia tishio la Rais wa Marekani Donald Trump la kushambulia maeneo mengine nchini humo.

    Msemaji wa jeshi la Iran, Mohammad Akrami Nia, alisema kuwa vita vyovyote vijavyo havitaamuliwa na Washington, akisisitiza kuwa Marekani haitakuwa na uwezo wa kuamua lini au kwa namna gani vita hivyo vitamalizika.

    Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Iran, Mehrdad Akhlaghi, amesema nchi yake itatoa jibu "la uwiano, thabiti na lenye ufanisi" endapo itakabiliwa na shambulio lolote. Kauli hiyo ilitangazwa kupitia televisheni ya taifa ya Iran.

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Iran ina nia ya kufikia makubaliano na Washington, akieleza: "Iran inaonyesha utayari wa kufanya makubaliano, na tutasubiri kuona iwapo hilo litatimia."

    Akizungumzia uwezekano wa kurejea kwa mzozo wa kijeshi, Trump alisita kutoa msimamo wazi ikiwa Marekani itaanzisha tena operesheni za kijeshi dhidi ya Iran, akisema: "Sitawaambia."

    Trump aidha, alidai kuwa Marekani imeharibu sehemu kubwa ya uwezo wa kijeshi wa Iran, lakini akadokeza kuwa bado kuna "eneo moja au mawili" ambayo Washington inahisi inahitaji kushughulikiwa.

  2. Trump: Flávio Bolsonaro anaweza kukaa Marekani 'kwa muda anaotaka'

    Donald Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema Seneta wa Brazil, Flávio Bolsonaro, anaweza kuendelea kuishi nchini Marekani "kwa muda wowote anaotaka."

    Akizungumza na waandishi wa habari Jumamosi katika makaazi yake ya Mar-a-Lago huko Palm Beach wakati wa sherehe za Halloween, Trump alisema hana mpango wa kumfurusha mwanasiasa huyo wa zamani wa Brazil, kwa mujibu wa Reuters.

    Flávio Bolsonaro alikimbilia Marekani baada ya kushindwa katika uchaguzi wa urais wa Brazil dhidi ya kiongozi wa mrengo wa kushoto, Luiz Inácio Lula da Silva.

    .

    Mapema Jumamosi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema Marekani haikutoa msaada wowote kwa Bolsonaro kuondoka Brazil.

    Mwanasiasa huyo aliwasili Miami kwa ndege binafsi asubuhi ya Jumatano, Oktoba 28.

    Kwa mujibu wa Rubio, Rais Trump aliamua kumpa Bolsonaro kibali cha kuingia nchini kwa muda (parole), ambacho humruhusu mtu kuingia na kuishi Marekani kwa muda maalum nje ya taratibu za kawaida za uhamiaji.

    "Serikali ya Marekani haikuhusika kwa namna yoyote katika hatua alizochukua kuondoka Brazil," alisema Rubio. "Hatukumwezesha kwa njia yoyote."

    Maelezo zaidi:

  3. Meli ya gesi ya Qatar yagongwa na kifaa kisichojulikana

    .

    Shirika rasmi la habari la Qatar limesema meli iliyokuwa imesheheni gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) imegongwa na "kifaa kisichojulikana kilichorushwa kutoka angani" wakati ikiwa safarini katika maji ya Ghuba ya Uajemi.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tukio hilo lilitokea Ijumaa jioni na kuhusisha meli ya Al-Muaidah, inayomilikiwa na kampuni ya Qatar inayojishughulisha na usafirishaji wa gesi.

    Hakuna mfanyakazi aliyeripotiwa kujeruhiwa, huku mamlaka zikisema tukio hilo halikusababisha athari yoyote kwa mazingira.

    Kampuni inayomiliki meli hiyo imesema kuwa chombo hicho kiko salama na kinaendelea na shughuli zake kama kawaida.

    Tangu kuzuka kwa vita katika Mashariki ya Kati, Iran imekuwa ikitangaza hatua za udhibiti katika Mlango wa Hormuz dhidi ya meli inazodai zinakiuka sheria, huku Marekani ikiendelea na operesheni zake za kijeshi za majini dhidi ya bandari za Iran.

    Qatar, ambayo imekuwa ikitekeleza jukumu la upatanishi katika mgogoro huo, imeongeza juhudi zake za kidiplomasia katika siku za karibuni kwa lengo la kufufua mazungumzo kati ya Marekani na Iran.

    Pia unaweza kusoma

  4. Iran yaorodhesha jeshi la Uingereza kama shirika la 'kigaidi'

    Bendera za Uingereza na Iran

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetangaza kuwa kuyajumuisha Jeshi la Wanamaji la Uingereza na Jeshi la Anga la Uingereza (RAF) katika orodha yake ya mashirika ya ''kigaidi''.

    Katika taarifa, wizara hiyo pia imesema kuwa Shirika la Ujasusi la Uingereza (MI6) limeorodheshwa miongoni mwa taasisi zinazotajwa kuwa na "uadui" dhidi ya Iran.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi huo umefanywa kwa kuzingatia azimio la Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran na ni sehemu ya hatua za kulipiza kisasi kufuatia maamuzi yaliyowahi kuchukuliwa dhidi ya Iran.

    Iran imeeleza kuwa kuiorodhesha taasisi hizo za Uingereza kunafanyika chini ya kile ilichokiita "Sheria ya Kulipiza Kisasi" na imehusisha hatua hiyo na ushirikiano wa kijeshi wa Uingereza na Marekani pamoja na Israel katika vita hivyo.

    Wizara hiyo ilisema maamuzi hayo yamefanywa kwa kuzingatia kanuni ya usawa wa hatua za kidiplomasia na kwa lengo la kulinda usalama na maslahi ya taifa la Iran.

    Soma Pia:

  5. Kaka yake Tundu Lissu afariki dunia Tanzania

    Wakili Alute Mughwai Lissu, kaka wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, amefariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 1, 2026.

    Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na dada yake, Rose Masesa, katika mazungumzo na Jambo TV.

    Alipoombwa kueleza chanzo cha kifo hicho, Rose alisema kwa sasa hawezi kutoa maelezo zaidi, akibainisha kuwa msiba upo jijini Arusha.

    "Ni taarifa za kweli. Msiba upo Arusha na mimi ninaelekea huko," alisema Rose kwa ufupi.

    Maelezo zaidi kuhusu chanzo cha kifo hicho bado hayajatolewa.

    Kwa mujibu wa Rubio, Rais Trump aliamua kumpa Bolsonaro kibali cha kuingia nchini kwa muda (parole), ambacho humruhusu mtu kuingia na kuishi Marekani kwa muda maalum nje ya taratibu za kawaida za uhamiaji.

    "Serikali ya Marekani haikuhusika kwa namna yoyote katika hatua alizochukua kuondoka Brazil," alisema Rubio. "Hatukumwezesha kwa njia yoyote."

  6. Trump aidhinisha viza kwa mama wa kijana Mghana aliyeuawa Marekani

    .

    Rais wa Marekani Donald Trump amekubali kutoa viza kwa mama wa kijana Mghana, Javits Frimpong, aliyeuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Bronx, New York, ili aweze kusafiri kwenda Marekani kumuaga mwanawe.

    Hatua hiyo imekuja baada ya mazungumzo ya simu kati ya Meya wa New York, Zohran Mamdani, na Trump.

    Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, Mamdani alisema mama huyo anastahili kupata fursa ya kumuomboleza mwanawe ana kwa ana.

    Doris Adu Gyamfi, mama wa kijana huyo, anayeishi Kumasi nchini Ghana, anatarajiwa kuwasili Accra kwa ajili ya kuanza mchakato wa kupata viza.

    Frimpong, mwenye umri wa miaka 15, alipigwa risasi na kuuawa Alhamisi asubuhi alipokuwa njiani kuelekea shuleni.

    Polisi wanasema bado wanawatafuta washukiwa watatu waliotoroka baada ya tukio hilo, huku picha za kamera za usalama zikionyesha kijana huyo akijaribu kukimbia kuokoa maisha yake.

    Serikali ya Ghana imelaani mauaji hayo na kuitaka Marekani kufanya uchunguzi wa kina ili kuhakikisha wahusika wanawajibishwa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa, amesema serikali itaendelea kulinda na kutetea maslahi ya raia wake popote walipo.

    Mauaji hayo yamezua maombolezo makubwa katika jamii ya Waghana wanaoishi Bronx. Hadi sasa, hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

  7. Mawaziri wa Ethiopia wapewa mafunzo ya kijeshi

    Abiy Ahmed na viongozi wa serikali yake

    Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, amewaweka mawaziri wake na maafisa wengine waandamizi wa serikali kwenye mafunzo ya kijeshi, akisema kuwa nidhamu ya kijeshi inaweza kusaidia kujenga viongozi imara zaidi na kuharakisha maendeleo ya taifa.

    Picha alizochapisha kwenye mitandao ya kijamii zinamwonyesha akishiriki mazoezi hayo pamoja na mawaziri, manaibu mawaziri na wakuu wa taasisi za serikali katika Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Hurso.

    Hatua hiyo ni ya kipekee nchini Ethiopia, ambako maafisa waandamizi wa serikali kutoka sekta ya kiraia mara chache huonekana wakipitia mafunzo ya kijeshi.

    Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo ni Spika wa Baraza la Shirikisho, Muferiat Kamil, Waziri wa Fedha Fitsum Assefa na Waziri wa Afya Mekdes Daba.

    Bado haijafahamika mafunzo hayo yalianza lini au yatadumu kwa muda gani.

    Katika chapisho lake, Abiy alisema kuwa azma ya Ethiopia ya kufikia ustawi wa wote inahitaji viongozi wenye afya njema, maadili thabiti na uwezo mkubwa wa kiakili.

    Alieleza kuwa taasisi za kijeshi hutoa mafunzo muhimu katika nyanja za nidhamu, uzalendo, ushirikiano, uwajibikaji na uongozi.

    "Wanajeshi wana shabaha, huku raia wakiwa na malengo. Dhamira ya pande zote mbili ni ushindi," alisema, akiongeza kuwa kuunganisha taaluma za kijeshi na za kiraia kunaweza kusaidia kujenga kizazi chenye uwezo wa kufanikisha yote mawili.

  8. Gharama ya maisha yachochea ghasia na uporaji Ujerumani

    ..

    Maandamano dhidi ya gharama ya maisha nchini Ujerumani yaligeuka kuwa ya vurugu Jumamosi jioni, baada ya waandamanaji kupora maduka katikati ya jiji la Frankfurt.

    Ghasia pia ziliripotiwa katika miji ya Berlin, Cologne na Hamburg, huku polisi wakitumia maji kuwatawanya waandamanaji waliowarushia fataki, mawe na chupa maafisa wa usalama na wahudumu wa dharura.

    Awali, maelfu ya watu walikuwa wamejitokeza kushiriki maandamano yaliyoandaliwa na kundi la kampeni la Gen Z regelt ("Gen Z wanachukua jukumu"), kupinga ongezeko la gharama ya maisha, ufadhili mdogo wa shule, kupunguzwa kwa matumizi ya umma na sera za huduma ya kijeshi.

    Machafuko hayo yanajiri wakati maandamano makubwa yanayoongozwa na vijana pia yakishuhudiwa nchini Ufaransa, ambako zaidi ya watu 320,000 waliripotiwa kuandamana Jumamosi.

    Shirika la habari la AFP liliripoti kuwa polisi walifunga sehemu kubwa ya barabara kuu ya kibiashara ya Frankfurt, huku watu kadhaa wakikamatwa.

    Mamlaka katika Frankfurt, Munich na Berlin zilikadiria idadi ya waandamanaji kuwa karibu 18,000, ingawa waandaaji walikuwa wamekadiria idadi kubwa zaidi.

    Vyombo vya habari vya Ujerumani viliripoti kuwa maelfu ya watu walishiriki maandamano katika miji mbalimbali nchini humo.

    Msemaji wa Gen Z regelt, Lina Friedrich, alisema maandamano hayo yalikuwa ya kutetea amani na uhuru..

    "Tunachotilia mkazo zaidi ni kuboreshwa kwa mifumo ya afya na elimu. Tunapinga utumishi wa kijeshi wa lazima na tunaunga mkono mgawanyo wa majukumu kwa usawa," alisema.

  9. Natumai hujambo.