Nifunge ndoa na muuaji? simulizi ya mapenzi iliyofichua muuaji

Chanzo cha picha, Netflix
- Author, Yasmin Rufo
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Ungefanya nini iwapo mtu unayempenda angekiri kwamba amemuua mtu?
Ni rahisi kufikiri kwamba ungeweza kuchukua uamuzi wa haraka na wa kimaadili bila kusita, lakini filamu mpya ya uhalifu halisi ya Netflix yenye jina Should I Marry a Murderer? inaonyesha kwamba katika maisha halisi, mapenzi huchanganya kila kitu.
Mwaka 2017, Alexander McKellar, anayejulikana kama Sandy na aliyekuwa akiendesha gari akiwa amelewa, alimgonga na kumuua mwendesha baiskeli wa hisani Tony Parsons huko Argyll and Bute, Scotland. McKellar na kaka yake pacha Robert kisha wakauficha mwili wa Parsons kwa kuuzika.
Mwili huo ulibaki bila kugunduliwa kwa miaka mitatu, hadi mpenzi wake mpya, Daktari Caroline Muirhead, alipojua ukweli na kuwaongoza polisi kufikia kaburi hilo la kina kifupi.
Mkurugenzi Josh Allott anasema aliposikia dondoo hizo kwa mara ya kwanza alishindwa kuamini kama ni tukio la kweli.
"Nilidhani ni hadithi ya tamthilia, si jambo linaloweza kutokea katika maisha ya kawaida."
Mtayarishaji wa mfululizo huo Clare Beavis anasema kesi hiyo ilijulikana sana nchini Scotland, lakini sehemu muhimu iliyokosekana katika uwasilishaji wake ni ushahidi na simulizi ya Muirhead, ambaye ni mhusika mkuu katika kuibuka kwa ukweli.

Chanzo cha picha, Netflix
Mfululizo huu unaanza kwa Muirhead akiwa amevunjika moyo baada ya kuvunjika kwa uhusiano, kisha kukutana na McKellar kupitia Tinder mwaka 2020, ambapo mapenzi yao ya kasi yaliwapeleka kwenye uchumba ndani ya wiki chache.
Baada ya kuchumbiwa, alimwuliza kama kuna jambo lolote katika maisha yake ya nyuma linaloweza kuathiri mustakabali wao.
Ndipo McKellar alipokiri kwamba miaka michache iliyopita alimgonga mwendesha baiskeli alipokuwa akirudi nyumbani na kaka yake, lakini hakutoa msaada wa matibabu.
Baadaye ilibainika kuwa majeraha ya Parsons yalikuwa makubwa kiasi kwamba hangeweza kuishi kwa dakika 20 au 30 tu bila msaada wa kimatibabu.
Pacha hao waliondoka eneo la tukio na baadaye kurudi kwa gari jingine, kabla ya kuuficha mwili katika shamba la Auch Estate.
Ufunuo huo ulimweka Muirhead katika mgogoro wa hisia, akiwa amegawanyika kati ya uaminifu na kufanya kilicho sahihi.

Chanzo cha picha, Netflix
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa Allott, mgongano huo wa kimaadili ndio uliofanya hadithi kuwa nzito na ya kuvutia.
Muirhead aliwajulisha polisi kuhusu uhalifu huo, lakini kilichofuata ndicho kinachofanya hadithi hii kuwa ya kipekee.
Badala ya kuachana na McKellar, aliendelea na uhusiano huo huku akishirikiana kwa siri na polisi bila yeye kujua.
Ilichukua karibu miaka mitatu baada ya McKellar kukiri kwa mara ya kwanza kwa Muirhead kabla ya kuhukumiwa kifungo cha gerezani.
Katika kipindi hicho, Muirhead alirekodi maungamo ya siri kwa simu yake na kurudi naye katika shamba la Auch Estate ambapo kwa siri alidondosha kopo la Red Bull kama alama ya eneo hilo, kabla ya baadaye kupigia polisi kuwaambia mahali pa kutafuta mwili katika eneo hilo la mbali.
Ingawa wengine wanaweza kuhoji maamuzi hayo, Allott anasema Muirhead alifanya lililo sahihi kwa kuripoti uhalifu kwa polisi.
Ndugu hao walikamatwa mwezi Desemba 2020 na kuachiliwa kwa dhamana, na hawakushtakiwa hadi Desemba 2021.
"Alitarajia ndugu hao wangewekwa rumande, wafikishwe mahakamani na wafungwe jela milele na kutoweka katika maisha yake, lakini walirudishwa tena katika maisha yake," Allott anaeleza.
Anasema kwamba alilazimika kupitia kipindi hicho kisicho na uhakika peke yake kwani "alijihisi yuko hatarini kwa takriban mwaka mmoja na hapo ndipo maamuzi yakaanza kuingia".

Chanzo cha picha, Netflix
Ni ugumu wa tabia ya Muirhead unaomfanya kuwa mhusika wa kuvutia, kwani kwa mujibu wa Allott "alikuwa mfasaha na mwenye akili, mtaalamu mchanga wa patholojia mwenye miaka minane ya mafunzo ya tiba".
"Maisha yake yote yalikuwa sawa, lakini baada ya kukutana na Sandy na kusikia alichokifanya, kila kitu kilimuatua moyo''.
Katika kipindi hicho, Muirhead anazungumza kwa uwazi kuhusu jinsi alivyoanza kutumia pombe na dawa za kulevya ili kukabiliana na hali aliyojikuta nayo.
Allott na Beavis wanasema wazi kuwa lengo lao ni kuonyesha simulizi yenye uwiano, lakini hatimaye kuonesha "kile ambacho kuwa karibu na uhalifu bila kuhusika moja kwa moja kunaweza kutokea katika maisha ya mtu".

Chanzo cha picha, Netflix
Kesi hiyo pia imeibua mjadala kuhusu namna polisi walivyoshughulikia taarifa zake na msaada alioupata baada ya kutoa taarifa.
Allott anasema polisi "hawakujua jinsi ya kumshughulikia Caroline" na bila kutoa mengi, anasema kwamba kama angepata "uangalifu na huruma kutoka kwao, asingelazimika kufanya baadhi ya maamuzi aliyofanya".
Beavis anakubaliana na kuongeza kwamba uzoefu wa Muirhead "unaakisi uzoefu wa watu wengi ndani ya mfumo wa haki ya jinai".
"Mchakato wa haki unachukua muda mrefu sana na hilo linaathiri maisha ya watu, na hilo ndilo tulilotaka kuonyesha."
Polisi wa Scotland na Huduma ya Msaada kwa Waathiriwa wa Scotland walikataa kushiriki katika filamu hiyo.
Muirhead aliwasilisha malalamiko kadhaa dhidi ya Polisi wa Scotland.
Baada ya uchunguzi wa miaka mitano, mengi ya malalamiko hayo hayakukubaliwa, na polisi wanasema walimpa msaada unaofaa.
"Kuachwa bila msaada"
Katika maelezo yake kuhusu kipindi hicho, Muirhead alisema aliamini mfumo ungekuwa upande wake na ungemlinda alipokuwa katika hali ya hatari zaidi, lakini hilo halikuwa uzoefu wake.
"Ninatumaini kwamba kwa kuzungumza na kushiriki kilichonitokea, tunaweza kuanzisha mazungumzo ya kweli kuhusu ulinzi zaidi kwa waathiriwa na mashahidi, na kwa nini uelewa wa kina zaidi wa afya ya akili ndani ya polisi na mfumo wa mahakama unahitajika sana.
"Mara nyingi athari za mshtuko wa kisaikolojia na unyanyasaji hupuuzwa au hazizingatiwi kabisa, na hii inamaanisha watu kama mimi wanaachwa peke yao kujikusanya upya kuendelea na maisha yao."
Mwezi Julai 2023, muda mfupi kabla ya kesi ya ndugu hao kuanza katika Mahakama Kuu ya Glasgow, McKellar alikiri shtaka lililopunguzwa la mauaji ya bila kukusudia (culpable homicide).
Ndugu yake alikubaliwa kutokuwa na hatia kwa shtaka la mauaji, lakini wote wawili walikiri jaribio la kuzuia haki kutendeka kwa kuficha uhalifu huo.
Sandy McKellar alihukumiwa kifungo cha miaka 12 gerezani, huku kaka yake akihukumiwa miaka mitano na miezi mitatu.
Kesi hii pia iliwahi kuangaziwa katika makala: BBC Murder Case: The Vanishing Cyclist. Filamu ya Should I Marry a Murderer? imepakuliwa katika mtandao wa Netflix.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid









