Fiona: Kiboko aliyegusa mioyo ya mamilioni duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
Kofia hiyo iliyomezwa na kiboko Fiona ilikuwa imekwama ndani ya utumbo wake mwembamba, na hivyo madaktari hawakuweza kuiondoa, kulingana na taarifa ya Bustani ya Wanyama ya Cincinnati, jimbo la Ohio nchini Marekani.
Madaktari wa mifugo walifanya juhudi za kuokoa maisha ya Fiona baada ya kumeza kofia hiyo. Hata hivyo, mahali ilipokwama pamoja na maumbile ya mwili wa mnyama huyo, aliyekuwa na uzito wa kilogramu 1,088, vilifanya isiwezekane kuiondoa.
Fiona alifariki Alhamisi wiki hii.
Uchunguzi wa mwili wake baada ya kifo umebaini kuwa kofia hiyo ilikuwa imekwama katikati ya utumbo mwembamba, umbali wa takribani mita 7.6 kutoka sehemu ya mwisho ya tumbo na mita 15 kutoka mwisho wa utumbo wake, kulingana na taarifa ya bustani hiyo iliyotolewa siku ya Ijumaa.
Mkurugenzi wa masuala ya afya ya wanyama katika bustani hiyo, Daktari Mike Wenninger, amesema juhudi za kutumia vifaa maalumu vya uchunguzi kuifikia kofia hiyo kupitia mfumo wa chakula, kutoka sehemu ya juu na ya chini, hazikufanikiwa.
Amesema pia kwamba kutokana na mahali ilipokwama na maumbile ya mwili wa Fiona, haikuwezekana kufanya upasuaji wa kuiondoa. Aidha, huduma za matibabu zilizokuwa zikitolewa kumsaidia mwili wake kuondoa kofia hiyo ndizo pekee zilizokuwa zimebaki, lakini hazikufanikiwa.
Kifo cha Fiona kimewahuzunisha wapenzi wa wanyama duniani kote, ambao walikuwa wakifuatilia kwa karibu juhudi za kumuokoa.
Siku ya Ijumaa, Baraza la Seneti la Marekani lilipitisha kwa kauli moja azimio la kumuenzi kiboko huyo na kutambua mchango wake pamoja na juhudi za wafanyakazi wa bustani hiyo waliomhudumia.
Fiona alijipatia umaarufu duniani mwaka 2017, alipozaliwa kabla ya muda wake katika Bustani ya Wanyama ya Cincinnati. Mwanzoni, alipambana na hali ngumu ya kiafya na uwezekano wake wa kuishi haukuwa wa uhakika.
Alipozaliwa, alikuwa na uzito wa kilogramu 13 pekee, uzito ambao kulingana na bustani hiyo ulikuwa takribani nusu ya uzito wa chini kabisa uliokuwa umerekodiwa kwa mtoto wa kiboko wa aina yake.
Jitihada za wafanyakazi wa bustani hiyo kumlea na kumuokoa zilivuta hisia za mamilioni ya watu duniani, na kumfanya Fiona kuwa maarufu kwenye mitandao ya kijamii.
Mkurugenzi wa bustani hiyo, Dave Jenike, amesema wameguswa na wimbi la jumbe za rambirambi na upendo kutoka kwa watu mbalimbali duniani, akisema Fiona aliwapa watu karibu miaka kumi ya furaha.
Imetafsiriwa na Phylis Mwatee































