Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Xi Jinping: Alivyopoteza kila kitu hadi Kutawala China
Rais wa China, Xi Jinping, anatarajiwa kufanya ziara yake ya kwanza ya kiserikali katika mji mkuu wa Marekani, Washington DC, tarehe 23, Septemba 2026.
Kwa kuangalia historia yake, Xi amekuwa na uhusiano na Marekani tangu zamani kabla ya kuwa kiongozi mwenye nguvu zaidi nchini China katika kizazi cha sasa.
Miaka 40 iliyopita, Xi alikuwa afisa wa mkoa uliopo kaskazini mwa China, aliposafiri kwenda maeneo ya Midwest nchini Marekani kwa ziara ya mafunzo.
Xi alitumia siku kadhaa katika jimbo la Iowa akijifunza kuhusu kilimo, kutembelea mashamba na kukaa katika nyumba ya familia moja katika eneo hilo.
Vyombo vya habari vya serikali ya China vimetangaza kwa kina ziara hiyo, vikisisitiza urafiki wa Xi na Terry Branstad, ambaye wakati huo alikuwa gavana wa Iowa.
Baadaye, Branstad aliteuliwa kuwa balozi wa Marekani nchini China wakati wa utawala wa Donald Trump, hatua iliyobainisha uhusiano wa muda mrefu wa kibinafsi kati yake na Xi.
Leo, uhusiano kati ya Marekani na China ni tofauti kabisa, ukiwa na mivutano inayohusisha ushuru wa bidhaa unaotozwa na kila nchi, udhibiti wa teknolojia na ushindani wa kijeshi.
Xi mwenye umri wa miaka 73 si tena afisa wa ngazi ya chini. Miaka 14 akiwa kiongozi wa China, amefanya mabadiliko makubwa ndani ya Chama cha Kikomunisti cha China na duniani.
'Mwanamfalme' aliyepoteza kila kitu
Hadithi ya Xi inaanza na maisha yake ya kifahari.
Alizaliwa mjini Beijing mwaka 1953, akiwa mtoto wa sita wa Xi Zhongxun, mwanamapinduzi wa Kikomunisti aliyeshiriki katika kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China.
Baba yake Xi hatimaye alifikia nafasi ya juu katika uongozi wa chama na kuwa makamu wa waziri mkuu.
Akiwa mtoto, Xi alisoma katika shule kadhaa za kifahari, akifurahia fursa na marupurupu ambayo familia nyingi hazikuwa nazo.
Lakini baadaye mambo yaligeuka.
Mwanzoni mwa miaka ya 1960, baba yake Xi alishtakiwa kwa kuwa sehemu ya kundi lililotajwa kuwa la "wapinga chama" na kupelekwa uhamishoni huko vijijini, ambako alilazimishwa kufanya kazi katika kiwanda.
Baba yake pia aliondolewa katika Chama cha Kikomunisti.
Akiwa mtoto wa mtu aliyetajwa kuwa "mpinga mapinduzi", Xi ambaye wakati huo alikuwa kijana alilazimishwa kupelekwa katika vituo vya serikali vya "kuelimishwa upya".
Kufuatia wito wa Mao Zedong kwa vijana kwenda vijijini na kujifunza kutoka kwa wakulima, Xi mwenye umri wa miaka 15 alielekea mashambani pamoja na mamilioni ya wanafunzi wengine kutoka mijini.
Akielezea safari hiyo katika mahojiano ya mwaka 2004, Xi alisema: "Kila mtu kwenye treni alikuwa akilia. Mimi ndiye nilikuwa nikitabasamu.
Xi alifika katika kijiji cha mbali cha Liangjiahe, katika Mkoa wa Shaanxi. Huko aliishi kwa miaka saba katika yaodong, nyumba ya pango iliyochongwa kwenye mteremko wa mlima. Xi alifanya kazi za kilimo, kubeba samadi na kuchimba mifereji.
"Mboga zilizotiwa chumvi ndizo zilikuwa chakula nilichokipenda zaidi," alisema akielezea maisha yake huko. "Hadi leo, bado ninazikumbuka kwa furaha."
Xi alisema alishtushwa na uzito wa kazi na mwanzoni alitatizika kukabiliana na njaa pamoja na chawa. Hata hivyo, alisema alipata nafuu kwa kutumia muda wa mapumziko kabla ya chakula cha mchana kuvuta sigara.
Kupanda madaraka
Xi aliondoka kijijini akiwa na umri wa miaka 22 na kwenda kusomea uhandisi wa kemikali katika Chuo Kikuu cha Tsinghua, mojawapo ya taasisi maarufu zaidi za elimu ya juu nchini China.
Baada ya kuhitimu, alifanya kazi kama afisa wa serikali katika mikoa ya Fujian na Zhejiang. Mikoa hiyo ya pwani baadaye ikawa miongoni mwa maeneo tajiri zaidi nchini China baada ya uchumi kufunguliwa katika miaka ya 1980.
Kurejeshwa kwa hadhi ya baba yake baada ya kifo cha Mao kulimsaidia Xi kupata nafasi katika serikali kuu na jeshi. Pia kulimpa fursa ya kujenga uhusiano na viongozi wengine ndani ya chama.
Baadhi ya maafisa hao baadaye wakawa sehemu ya mduara wa viongozi ambao Xi anawaamini hadi leo.
Xi alimuoa mke wake wa kwanza, Ke Lingling, binti wa aliyekuwa balozi wa China nchini Uingereza, mwaka 1979. Waliachana miaka mitatu baadaye.
Rafiki mmoja ndiye aliyemtambulisha Xi kwa mke wake wa pili na wa sasa, Peng Liyuan, ambaye wakati huo alikuwa mwimbaji katika jeshi.
Peng Liyuan huonekana mara kwa mara katika vipindi vya televisheni vinavyoandaliwa wakati wa sherehe za Mwaka Mpya wa China, ambavyo hutazamwa na mamia ya mamilioni ya watu.
Kwa Wachina wengi katika miaka ya 1980 na 1990, Peng alikuwa maarufu zaidi kuliko Xi.
Baadaye, Peng alianza kumsindikiza Xi mara kwa mara katika safari zake za nje ya nchi, jambo lililobadilisha taswira ya jadi ya mke wa rais wa China, ambaye kwa kawaida alikuwa mtu wa kujisitiri na kutotafuta umaarufu.
Binti yao na mtoto wao pekee, Xi Mingze, alizaliwa mwaka 1992. Taarifa chache zinajulikana kumhusu, isipokuwa kwamba alisoma katika Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani.
Mwaka 2007, baada ya kuhudumu kwa muda mfupi kama kiongozi mkuu wa Shanghai, Xi alijiunga na Kamati ya Kudumu ya Politburo, chombo cha juu zaidi cha kufanya maamuzi nchini China.
Miaka mitano baadaye, Xi alichukua nafasi ya Hu Jintao kama kiongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China.
Akiwa kiongozi wa China, Xi amekuwa akibadilisha mfumo wa uchumi na siasa nchini humo kwa njia ambazo watu wachache walitarajia.
China ambayo Xi ameijenga
Katika miaka 14 ya utawala wa Xi, China imezidi kujiamini katika nafasi yake duniani.
Kimataifa, Xi amekuwa akipanua ushawishi wa China kupitia miradi kama Mpango wa Ukanda Mmoja, Njia Moja (Belt and Road Initiative), huku Beijing ikijiweka kama mtetezi wa nchi za Kusini mwa Dunia.
Wakati huohuo, uhusiano wa China na mataifa mengi makubwa ya kidemokrasia umezidi kuwa na mikwaruzano, ikiwemo kuhusu mizozo ya mamlaka katika Bahari ya China Kusini, kuongezeka kwa mvutano kuhusu Taiwan na ushindani unaozidi kati ya China na Marekani.
Hata hivyo, utawala wa Xi pia umeongeza udhibiti wa kisiasa ndani ya China.
China imeweka mkazo mkubwa zaidi kwenye usalama na utulivu wa kisiasa. Serikali yake imetekeleza sera zenye utata katika Xinjiang, Tibet na Hong Kong.
Wafuasi wake wanamsifu Xi kwa kurejesha utulivu, huku wakosoaji wakisema amepunguza kwa kiasi kikubwa uhuru wa kiraia.
Xi anakuza itikadi iliyopewa jina lake, inayojulikana kama "Mawazo ya Xi Jinping kuhusu Ujamaa wenye Sifa za Kichina kwa Enzi Mpya".
Itikadi hiyo imepewa nafasi katika mfumo wa kisiasa kwa kiwango ambacho watangulizi wake wawili hawakuweza kufanya.
Xi pia aliondoa ukomo wa mihula ya urais katika katiba, hatua iliyomruhusu kuhudumu kwa zaidi ya mihula miwili.
Vyombo vya habari vya serikali ya China humwonyesha Xi kama kiongozi mwenye uzito, lakini wakati mwingine huonyesha upande wake wa kirafiki zaidi.
Xi amezungumzia mara kadhaa mapenzi yake kwa soka, na hata aliwahi kufanya mzaha kuhusu kukerwa kwake na timu ya taifa ya wanaume ya China alipokuwa akizungumza na waziri mkuu wa Thailand.
Pia aliwahi kunywa bia na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na kumtania rais wa Korea Kusini kuhusu kukagua simu.
Tangu alipoingia madarakani, Xi amekutana na Putin zaidi ya mara 40. Xi hata amemtaja Putin kuwa mtu wake wa karibu zaidi na wa kuaminika.
Uhusiano wa Xi na Trump ni wa aina tofauti na wenye changamoto zaidi. Licha ya Trump kuendesha vita vya kibiashara dhidi ya China, mara nyingi huzungumza kwa mtazamo chanya kuhusu Xi. Trump humwita Xi rafiki yake na kumsifu kwa umahiri wake wa kisiasa.
Mwanzoni, Xi aliwekeza kwa kiasi kikubwa katika diplomasia ya kibinafsi na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi. Viongozi hao walifanya mazungumzo yasiyo rasmi kwa lengo la kusisitiza ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili makubwa ya Asia.
Hata hivyo, mapigano mabaya ya mpakani mwaka 2020 yalifanya uhusiano kati ya China na India kuzorota.
Tofauti na viongozi wanaojulikana kwa haiba yao binafsi au kufanya maamuzi kwa kusukumwa na hisia za wakati huo, Xi mara chache huweka uhusiano wa kibinafsi mbele ya maslahi ya taifa.
Xi anaporejea Washington DC, hatawasili kama afisa wa mkoa aliyekuwa ameenda kujifunza kuhusu kilimo huko Iowa, bali kama mmoja wa viongozi mwenye ushawishi mkubwa wa kisiasa katika karne ya 21.