Nywele bandia zahusishwa na saratani

.

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Esther Kahumbi Role,Global Digital Health
    • Nafasi, BBC London
    • Akiripoti kutoka, London
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Nywele bandia zinazoongezewa kwenye nywele ambazo zinatumiwa na mamilioni ya wanawake duniani kote zinaweza kuwa na kemikali zinazohusishwa na saratani ya matiti, kuvurugika kwa mfumo wa homoni na hatari kwa mfumo wa uzazi, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa.

Wanasayansi waligundua karibu kemikali 50 hatari katika karibu kila sampuli iliyopimwa, kutoka kwa bidhaa mbalimbali za nywele za bandia na asilia, zikiwemo wigi, nywele za kusuka, vipande vya nywele na nywele za kuunganisha (kama vile zile zinazofungwa kwa klipu).

Matokeo hayo, yaliyochapishwa katika jarida la American Chemical Society, yamesababisha wito wa kuwepo kwa kanuni kali zaidi katika sekta hiyo yenye thamani ya mabilioni ya dola na uwazi zaidi kwa watumiaji.

"Tunaziamini kampuni ambazo hazina wajibu wa kutengeneza na kuzalisha bidhaa bila kemikali fulani hatari," anasema Dkt. Elissia Franklin, mwandishi mkuu wa utafiti huo.

Viongeza vya nywele huleta hatari ya kipekee kwa sababu huvaliwa kwa muda mrefu na kubaki katika mguso wa moja kwa moja na ngozi, watafiti wanasema.

Mfiduo huo wa muda mrefu unaweza kuchangia hatari za kiafya za muda mrefu.

"Viongeza vya nywele huwekwa katika hali ya kugusana kwa karibu sana na mwili," anasema Franklin.

"Hubaki kwenye ngozi ya kichwa, shingo, na mwili kwa wiki kadhaa, au hata miezi."

Kemikali hatari

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Thamani ya soko la upanuzi wa nywele duniani inakadiriwa kuzidi dola bilioni 14 ifikapo mwaka wa 2028.

Ingawa wanawake wengi huchagua kuweka nywele bandia kwa sababu za urembo au mitindo, asilimia kubwa ya watumiaji ni wanawake wenye asili ya Kiafrika, ambao huchukulia hilo kama suluhisho la kutunza nywele zao, utafiti unaonyesha.

Nywele bandia zinaweza kugharimu kiasi kidogo cha dola 20, huku nywele bandia za ubora wa juu zilizotengenezwa kwa nywele asilia zikigharimu maelfu ya dola.

Katika sampuli 43 zilizofanyiwa majaribio, wanasayansi walitambua kemikali 170, kwa kutumia njia inayowaruhusu kugundua aina mbalimbali za vitu, badala ya kuzingatia aina moja.

Kati ya hizi, kemikali 48 zinaonekana kwenye orodha kuu za kimataifa za vitu hatari, ikiwa ni pamoja na orodha zilizoandaliwa na Umoja wa Mataifa na Shirika la Kemikali la Ulaya.

"Vitu hivyo vilijumuisha kila kitu kuanzia kemikali zinazozuia moto, dawa za kuua wadudu hadi kemikali kama phthalates, ambazo huvuruga mfumo wa homoni na zinajulikana kuhusishwa na madhara kwenye mfumo wa uzazi," anasema Dkt. Franklin.

Kemikali 17 zinazohusishwa na saratani ya matiti ziligunduliwa katika sampuli 36 za nywele za bandia, zikiwemo za kutengenezwa na za nywele halisi.

Karibu asilimia 10 ya sampuli zilikuwa na kemikali hatari, ambazo hutumiwa kwa kawaida kutengeneza plastiki zinazozuia kuungua.

Watafiti wanasema washtuka kugundua kemikali zenye bati, ambazo kwa kawaida hazipatikani katika bidhaa zinazotumiwa na watu.

Kemikali hizi zimehusishwa na muwasho wa ngozi na huvuruga mfumo wa homoni, yaani huingilia homoni zinazodhibiti shughuli mbalimbali mwilini, zikiwemo uzazi na ukuaji.

Miongoni mwa kemikali zinazogunduliwa zaidi katika sampuli hizo ni fenoli, inayotumika katika kutengeneza gundi za kuunganisha mbao za tabaka na bis (2-ethylhexyl) phthalate, kemikali inayotumika kufanya plastiki kuwa laini na kunyumbulika.

Watafiti wanasema kemikali hizi husababisha mabadiliko mwilini yanayofanana na yale yanayosababishwa na kemikali zinazojulikana kuchochea saratani ya matiti, na huenda zikaongeza hatari ya mtu kupata saratani hiyo kadiri muda unavyosonga.

Je, nywele za asili ni salama zaidi?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Uchunguzi uliopita umejikita zaidi kwenye nywele za bandia, ambazo zimegundulika kuwa na metali hatari. Hata hivyo, utafiti huu pia ulipima sampuli 11 za nywele halisi ambazo hazijafanyiwa uchakataji wowote, pamoja na mchanganyiko wa nywele za binadamu na za bandia.

Nywele halisi ambazo hazijafanyiwa uchakataji wala kuwekwa kemikali kwa kawaida huuzwa kwa bei ya juu zaidi na pia hutangazwa kuwa hazijawahi kuwekwa kemikali.

Nywele za asili kwa kawaida huwa hazijafanyiwa uchakataji wowote chanzo chake huwa ni mtu aliyenyolewa moja kwa moja.

Katika baadhi ya matukio, sampuli za nywele halisi, zikiwemo zilizotajwa kuwa hazijawahi kuwekwa kemikali na ambazo hazijafanyiwa uchakataji, zilikuwa na kemikali hatari zaidi kuliko baadhi ya nywele bandia, ikiwemo kemikali nyingi zaidi zinazovuruga mfumo wa homoni.

"Kwa sababu tu bidhaa imetajwa kama nywele za binadamu au nywele za asili kutoka kwa mfadhili mmoja haimaanishi kuwa ni salama zaidi kuliko nywele za bandia," anasema Dkt. Franklin, mtafiti katika Taasisi ya Silent Spring nchini Marekani, ambaye anasoma sababu za saratani ya matiti kimazingira.

"Kumekuwa na visa ambapo katika sampuli ya nywele bandia, tulitambua dutu moja tu kwenye orodha ya vitu hatari, huku katika nywele za binadamu kukigunduliwa kuwa na dutu aina tano hadi saba hatari," anaelezea.

Watafiti wanasema kemikali hizi huenda zikaongezwa wakati wa kutengeneza au kuchakata nywele hizo, ambapo nywele huwekwa dutu ili kuboresha muonekano, uimara au urahisi wa kuzitengeneza.

Ingawa utafiti huo haukupima kiwango cha kemikali hatari zilizokuwapo, baadhi yake—kama kemikali zinazovuruga mfumo wa homoni—zinaweza kuwa na madhara hata zinapopatikana kwa kiwango kidogo, anasema Dkt. Franklin.

Moja ya mambo makuu yanayowatia wasiwasi watafiti ni ukosefu wa viwango vya wazi vya usalama ambavyo watengenezaji wanapaswa kuzingatia kuhusu kemikali zinazotumika katika nywele bandia.

"Hakuna sababu kwa nini kemikali hatari zinapaswa kuwa katika bidhaa tunazotumiwa kwa madhumuni ya urembo. Tayari tunakabiliwa na kemikali nyingi kila siku ambazo haziwezi kuepukwa," anasema Dkt. Franklin.

Viongezo vingi vya nywele huwekwa kwenye joto au maji yanayochemka wakati wa kuvitengeneza, jambo linaloweza kutoa moshi wenye sumu. Dutu hizi zinaweza kuingia mwilini kwa kuvutwa kupitia hewa.

Pia zinaweza kuingia mwilini kupitia kugusa ngozi, na kuathiri wateja pamoja na wataalamu wanaotoa huduma hizo, kulingana na watafiti.

Baadhi ya watu huripoti athari za kimwili kutokana na nywele bandia, ikiwa ni pamoja na kuwashwa na kuwa na wekundu, kuvimba kwa ngozi ya kichwa, shingo, na uso, na katika matukio machache, matatizo ya kupumua.

Unawezaje kutumia nywele za kuongezea kwa usalama?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Utafiti unaonyesha kuwa hakuna njia iliyothibitishwa ya kutumia kwa usalama nywele za kuongezea au bandia zilizowekwa kemikali, na hata hatua zinazolenga kupunguza uwezekano wa kuathiriwa na kemikali hizo huenda zisiwe na uhakika.

Kuosha nywele hizo kabla ya kuzitumia, kwa mfano kwa kutumia siki ili kupunguza muwasho, bado hakujatoa ushahidi wa kutosha kuthibitisha usalama wa matumizi yake.

Katika utafiti huo, sampuli mbili pekee kati ya 43 zilizopimwa hazikuwa na kemikali hatari zilizotambuliwa na wanasayansi. Zote mbili zilikuwa na vitambulisho vinavyosema "hazina sumu" . Hata hivyo, Dkt. Franklin anasema madai kama hayo yanaweza kutoa hisia potofu ya usalama.

"Maneno haya hayadhibitiwi na taasisi yoyote, hivyo kampuni zinaweza kuyatumia kwenye bidhaa zao bila kuchukuliwa kuzingatiwa."

Nchini Uingereza, kanuni mpya na kali zaidi kuhusu kemikali hatari zinazosababisha saratani zitaanza kutekelezwa mwezi Agosti 2026, lakini wataalamu wa sekta ya nywele wanasema mapungufu katika udhibiti wa nywele bandia yanamaanisha kuwa watumiaji hawajalindwa kikamilifu.

Vipodozi hudhibitiwa na kufanyiwa tathmini ya usalama kwa masharti makali, lakini nywele bandia huainishwa kwa namna tofauti na hivyo hazifanyiwi tathmini hiyo.

Rangi za nywele na kemikali za kunyoosha nywele pia zimehusishwa na ongezeko la hatari ya saratani ya matiti katika tafiti za awali. Hata hivyo, tofauti na nywele bandia, bidhaa hizo hudhibitiwa kama vipodozi na hufanyiwa majaribio ya usalama.

"Udhibiti hufanya kazi tu ikiwa bidhaa zimeainishwa kwa usahihi na kama sheria inatekelezwa wakati wa uingizaji na uuzaji wa bidhaa hizo," anasema Caroline Larissey, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Kitaifa la Nywele na Urembo, nchini Uingereza.

"Hili ni pengo kubwa, na utafiti huu unaonyesha wazi kuwa suala hili linahitaji kushughulikiwa."

Mwaka 2016, BBC ilibaini kuwa taarifa za kupotosha kuhusu aina ya nywele ilikuwa kawaida wakati wa uchakataji, huku jukumu la kutaja kwa usahihi aina ya nywele likiwa kwa kiasi kikubwa mikononi mwa uaminifu wa wafanyabiashara.

Tovuti za baadhi ya watengenezaji zinapendekeza njia ambazo watumiaji wanaweza kutumia kutathmini ubora wa nywele kabla ya kuzinunua. Hata hivyo, wanasayansi wanasema jukumu hili halipaswi kuwa la mnunuzi.

"Kama bidhaa hizi hazingekuwepo sokoni, tusingelazimika kufanya chaguo lolote," anasema Dkt. Franklin.

"Mtu yeyote anayetumia nywele bandia anapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu matokeo haya ya utafiti."