WARIDI WA BBC: Akiwa na miaka 12 alitafutiwa mume wa miaka 50, leo ameokoa mabinti 300

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Usiku ule bado naukumbuka vizuri. Nilikuwa na miaka 12 tu, nimemaliza shule ya msingi kijijini kwetu Ngorongoro. Wakati watoto wengine walikuwa wanaota ndoto za kuendelea na masomo, mimi nilikuwa nimeandaliwa kuolewa na mwanaume aliyekuwa na umri wa miaka 50.

Sikuelewa mengi kuhusu ndoa, lakini nilielewa jambo moja maisha yangu yalikuwa yanabadilishwa bila ridhaa yangu.

Kaka yangu Fredy ndiye aliyekuwa mwanga wangu. Alibahatika kupata elimu na kuona dunia tofauti na ilivyo kijijini kwetu. Aliposikia wazee wakipanga ndoa yangu kwa siri, alinifuata na kuniambia:

"Theresia, lazima uondoke hapa kama unataka kuendelea kusoma."

Maneno yake yaliniogopesha, lakini pia yalinipa tumaini.

Theresia anasema usiku uliofuata alitoroka nyumbani kwa siri.

'Nilikuwa mtoto mdogo mwenye hofu kubwa moyoni, sijui ninakoenda wala nini kitanikuta mbele. Nilitembea na kusafiri kutoka Ngorongoro hadi Arusha mjini, safari iliyoonekana ndefu lakini nilikuwa nina matumaini ya kupata msaada huko'.

Nilifika Arusha majira ya saa kumi na moja jioni nikiwa nimechoka, mwenye njaa na hofu.

Alipokelewa na sista wa kanisa Katoliki aliyemsitiri na kumpeleka katika kituo cha kuwahudumia watoto wa kike wa kimasai waliokuwa wamekimbia changamoto, alieleza Theresia

Hapo ndipo maisha yangu mapya yalianza.

Nilipewa nafasi ya kuendelea na masomo. Kadri nilivyokuwa nakua, ndivyo nilivyozidi kuelewa kuwa wasichana wengi wa kimasai walikuwa wanapitia maumivu yale yale tohara, ndoa za utotoni, kunyimwa elimu na kukosa nafasi ya kuamua maisha yao.

Safari yangu kielimu

Baada ya kuhitimu elimu ya sekondari, mwaka 2014 Theresia alijiunga na Same School of Nursing na kusomea uuguzi kwa muda wa miaka mitatu.

Mafunzo hayo yalimpatia msingi mkubwa wa kuwahudumia wagonjwa na kuelewa changamoto mbalimbali za afya zinazowakabili wanawake na watoto katika jamii.

Anaeleza kwamba kadri alivyoendelea kufanya kazi hospitalini, alizidi kuguswa na maumivu wanayopitia wanawake wakati wa kujifungua na wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji.

'Hapo ndipo nilipoamua kuongeza utaalamu zaidi katika eneo la dawa za usingizi'.

Mwaka 2019 alijiunga na chuo cha KCMC kusomea utaalamu wa dawa za usingizi na ganzi (Anaesthesia).

Mafunzo hayo yalimfanya kuwa mtaalamu wa dawa za usingizi na ganzi, taaluma inayohusika na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma salama na kupunguza maumivu wakati wa upasuaji au kujifungua.

Theresia ambaye sasa ni mwanamke anayetazamwa kama mfano kwa jamii ya kimasai anasema tangu akiwa mdogo, alivutiwa sana na wahudumu wa afya.

'Nakumbuka kila nilipokuwa nikienda hospitali na kuona wauguzi au madaktari wakifanya kazi zao kwa utulivu na huruma, nilitamani siku moja niwe kama wao'.

Nilivutiwa hata na mavazi yao ya kazi, lakini zaidi niliguswa na namna walivyowasaidia hasa wanawake wakati wa kujifungua.

Theresia anasema hakupenda kuona mwanamke anapitia maumivu makali bila msaada wakati wa kujifungua.

'Ndiyo maana nilichagua kusomea utaalamu wa dawa za usingizi ili kusaidia kupunguza maumivu wakati wa upasuaji na kujifungua'.

Lakini zaidi ya taaluma yangu, mimi ni mwanamke ninayeamini kuwa kila mtoto wa kike anastahili elimu, uhuru wa kuamua maisha yake, na nafasi ya kutimiza ndoto zake.

'Jamii inaweza kulinda mila nzuri na kuachana na zile mbaya'

'Jamii yetu ikitumia elimu vizuri tutaweza kuikomboa kwa asilimia kubwa na kuachana na mila zilizopitwa na wakati kama kukeketa watoto wa kike na kuwanyima haki ya kupata elimu', anaeleza

Shauku ya Theresia kusaidia wanawake katika jamii ya kimasai ilimsukuma kuanzisha taasisi ya Maasai Women Health akilenga kuwaelimisha na kuwawezesha wasichana na wanawake wa Kimasai kujitambua, kuelewa haki zao, na kupigania maisha bora.

'Kutokana na ukweli kwamba bado jamii yetu inapambana na tamaduni kandamizi. Tohara bado ipo.

Ndoa za utotoni bado zipo. Bado kuna wanaoamini mtoto wa kike hastahili elimu bali kuolewa mapema'.

'Niliapa kwamba nikifanikiwa, nitakuwa sehemu ya mabadiliko'

Nilivyorudi nyumbani wazazi walinipokea vizuri baada ya kuona matokeo yangu. Familia yangu ilijivunia mimi na hata jamii iliyotuzunguka ilizungumza vizuri kuhusu hatua niliyopiga.

Nilianza kuona akina mama wakiniuliza maswali na mabinti zao kunifata niwasimulie kwa vipi wanaweza kusoma na kufanikisha ndoto zao pia.

Theresia anasema kwamba alianza kufanya kazi katika Kijiji chake ambako walifanya ziara za kimatibabu ya afya na elimu kwa jamii.

Anasema amekuwa akiwafundisha kuhusu elimu ya afya ya uzazi,afya ya hedhi na kujitambua.Wasichana wameanzisha kampeni ya kujiita 'I am Teddy to be' wakimaanisha na wao ni Teddy ajaye.

Theresia amekuwa akijihusisha na kampeni za kumkomboa msichana wa kimasai katika mkoa wa Arusha akishirikiana na taasisi mbalimbali za elimu na afya katika kuwasaidia wasichana wa kimasai.

Nimekuwa nikifanya ziara kwenye vituo, shule na majumbani ambako ninakutana na wasichana wa kimasai na kuzungumza nao.

Theresia anasema msaada mdogo unaweza kufungua fursa kwa msichana mmoja kufikia ndoto zake kwa kumpatia elimu.

Anajivunia kuchangia kubadili mtazamo wa familia kadhaa za kimasai ambazo aliweza kuwapatia elimu kuhusu haki ya kupata elimu.

Lakini mimi ni ushahidi kwamba mtoto wa kike akipewa nafasi, anaweza kubadilisha maisha yake na maisha ya wengine pia.

Leo ninapotazama nyuma, namshukuru kaka yangu Fredy kwa kuniokoa. Na kila ninapomuona msichana wa Kimasai akiwa darasani, hospitalini, au akitimiza ndoto zake, ninaamini safari yangu haikuwa ya bure.

Theresia anaamini kuwa elimu ndiyo silaha kubwa ya kumkomboa mtoto wa kike dhidi ya mila na desturi kandamizi.

Anasema wasichana wanapaswa kufundishwa kutambua thamani yao, haki zao na uwezo wao wa kuamua mustakabali wa maisha yao. Kwa mtazamo wake, ndoa ni jambo jema na lenye heshima, lakini inapendeza zaidi inapofanyika kwa wakati sahihi, kwa ridhaa ya mhusika na si kwa shinikizo la familia au jamii.

Anaendelea kutumia sauti yake kuwahimiza wazazi kuwapa watoto wa kike nafasi ya kusoma na kutimiza ndoto zao kabla ya kufikiria maisha ya ndoa.

Baada ya kumaliza masomo yake na kuanza kazi kama mtaalamu wa dawa za usingizi, Theresia anasema maisha yake yalibadilika zaidi alipokutana na kijana ambaye urafiki wao ulizaa ndoa takatifu. Tofauti na simulizi ya maumivu aliyowahi kupitia akiwa mtoto, safari yake ya ndoa ilijengwa katika msingi wa upendo, heshima na maamuzi ya hiari.

Anasema jambo lililompa faraja zaidi ni kuona wazazi na familia zote mbili zikibariki ndoa yao, hatua aliyoiona kama ushindi mkubwa dhidi ya fikra zilizowahi kutaka kumkatisha ndoto zake akiwa mdogo.

Leo, Theresia ni mke, mama na mwanamke anayesimama imara kutetea haki za wasichana wa kimasai. Akisaidia zaidi ya mabinti 300 ambao walikuwa, katika hatari ya kuingia katika ndoa utotoni. Anamshukuru mume wake kwa kuwa nguzo muhimu katika maisha na harakati zake, akisema amekuwa mstari wa mbele kumuunga mkono ili afanikishe ndoto zake za kusaidia wanawake na watoto wa kike.

Theresia anabeba ujumbe mmoja mkubwa kwa jamii: mtoto wa kike akipewa elimu, nafasi na uhuru wa kuchagua maisha yake, anaweza kuwa chachu ya mabadiliko makubwa kwa familia na taifa kwa ujumla.