Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Marekani na Iran zaanzisha mashambulizi mapya huku mazungumzo yakikwama

Mashambulizi ya hivi karibuni yanatokea baada ya mazungumzo kuhusu makubaliano ya kukomesha vita vyao vya miezi kadhaa kushindwa kuendelea mwishoni mwa juma.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Upinzani wataka raia kususia kutoka nje ishara ya kupinga jaribio la kurekebisha Katiba DRC

    Viongozi wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wamewataka wananchi kushiriki katika mgomo wa kutotoka mijini leo Jumatano, ili kupinga kile wanachokieleza kuwa ni vitisho dhidi ya Katiba ya nchi hiyo.

    Hatua hiyo inakuja wakati bunge likijadili mswada wa kura ya maoni, ambao wachambuzi wanasema unaweza kufungua njia ya uwezekano wa kuongeza muda wa utawala wa Rais Félix Tshisekedi.

    Viongozi mashuhuri wa upinzani kama vile Moïse Katumbi na Martin Fayulu walioshika nafasi ya pili na ya tatu mtawalia katika uchaguzi wa rais wa 2023, wanasema wanapinga jaribio lolote la kubadilisha katiba ya sasa, ambayo inaruhusu mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja.

    Katika matamko tofauti, waliwataka raia kukaa nyumbani Jumatano, na kuongeza kwamba shule, majengo ya biashara na huduma za umma zinapaswa kufungwa kama kielelezo cha wao kupinga.

    "Mtu yeyote asitoke nje, ili kuonesha kwamba tunapinga ukoloni wa nchi yetu, mabadiliko ya Katiba, na kukataa kuruhusu mtu kubaki madarakani milele," Fayulu alisema katika ujumbe wa video kwa wafuasi wake.

    Mamlaka za DRC ziliwataka watu - hasa watumishi wa umma - kutotii wito kama huo wa kususia.

    "Wasimamizi na wafanyakazi ambao, katika kipindi husika...hawapo wenyewe kwenye vituo vyao vya kazi bila uhalali watakabiliwa na sheria kwa mujibu wa kanuni zinazotumika," Jean-Pierre Lihau Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Utumisi wa Umma alisema katika taarifa kwa umma.

    Pia alisisitizia uhitaji wa watumishi wa umma kutoegemea upande wowote kisiasa na kutopendelea.

    Mwezi uliopita, Rais Felix Tshisekedi alisema yuko tayari kugombea muhula wa tatu iwapo "wananchi wanataka" abaki. Alisema ili hilo lifanyike, kutahitajika marekebisho ya katiba baada ya kura ya maoni. Rais pia alipendekeza kwamba mzozo wa mashariki mwa nchi unaweza kusababisha kucheleweshwa kwa uchaguzi wa 2028, na kuzua hasira miongoni mwa upinzani.

    Wengi wanasema anapanga mkakati wa kusalia madarakani, huku wabunge wa upinzani wakiondoka kwenye kikao cha bunge cha Mei 27, kilichokusudiwa kujadili muswada wa kura ya maoni.

    Kilichosalia ni kusubiri kuona iwapo watu wataitikia miito ya upinzani.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Muswada wa kuongeza muda wa rais wa Zimbabwe wapita hatua ya kwanza ya usomaji bungeni

    Muswada tata ambao unaweza kuongeza muda wa urais nchini Zimbabwe umepita hatua yake ya kwanza ya usomaji bungeni.

    Sheria hiyo inayopendekezwa inalenga kurekebisha katiba ili kuongeza muda wa muhula wa rais na wabunge kutoka miaka mitano hadi saba.

    Pia unalenga kubadilisha mfumo wa uchaguzi wa rais, ambapo badala ya kura ya moja kwa moja ya wananchi, bunge litakuwa na mamlaka ya kumchagua kiongozi wa nchi.

    Utasomwa mara ya pili Jumatano wakati wabunge watakapojadili uhalali wa marekebisho zaidi ya kumi.

    Ibara zenye utata zaidi zinapendekeza kuruhusu Rais Mnangagwa na wabunge kusalia ofisini hadi 2030 na kubadilisha kura ya urais kutoka kwa mchakato wa umma hadi wa bunge.

    Marekebisho yaliyopendekezwa yamesababisha ghadhabu kwa wananchi na yanakabiliwa na changamoto kadhaa za kisheria.

    Wakosoaji wakiwemo Chama cha Wanasheria nchini humo wanasema mapendekezo hayo yanadhoofisha taasisi za kidemokrasia na kulimbikiza madaraka kwa rais.

    Makanisa makubwa na mashirika ya haki za binadamu wanasema mabadiliko hayo ni kinyume na katiba na yanahitaji kura ya maoni.

    Mswada huo utahitaji angalau theluthi mbili ya kura katika Mabunge yote mawili ili kupitishwa.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Marekani yawawekea vikwazo waasi wanaohusishwa na serikali ya DRC na Rwanda

    Marekani imewawekea vikwazo makamanda wawili wa makundi yenye silaha wanaotuhumiwa kuchochea ghasia na ukosefu wa utulivu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumanne, Ofisi ya Idara ya Hazina ya Marekani ya Udhibiti wa Mali za Kigeni (OFAC) iilimwekea vikwazo Gustave Kubwayo, iliyemtambua kama kamanda wa kitengo cha kijasusi na operesheni maalum cha Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR).

    Wakati huo huo, John Imani Nzenze, aliyesemekana kuwa kamanda na mkuu wa upelelezi wa kundi la waasi la M23 pia aliwekewa vikwazo.

    "FDLR na M23 wameteka maeneo kwa kutumia nguvu na kuua raia mashariki mwa DRC," taarifa kutoka Idara hiyo ilisema.

    Iliongeza kuwa: "Kutokana na hatua ya leo, mali na maslahi yote katika mali ya watu waliotambuliwa au waliozuiwa walioelezwa hapo juu ambazo ziko Marekani au katika milki au udhibiti wa watu wa Marekani zimezuiwa."

    Rwanda inaishutumu serikali ya DRC kwa kuunga mkono FDLR, kundi lenye silaha lililoundwa na wanajeshi wa zamani wa Rwanda na watu wenye itikadi kali ambao walikimbilia mashariki mwa Congo wakati wa mauaji ya kimbari ya 1994. Kigali inawachukulia waasi hao kuwa tishio.

    Kwa upande mwingine, mamlaka ya Congo na waangalizi wengine wa kimataifa wameishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la M23, kundi lenye silaha ambalo limeteka maeneo mengi kutoka kwa serikali ya DRC katika kipindi cha mwaka uliopita.

    "Ghasia zinazoendelea kufanywa na makundi yenye silaha zinazidisha mzozo mbaya wa kibinadamu na ni tishio kwa maslahi ya Marekani katika eneo hilo," Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent alisema.

    "Vikwazo vya leo vinaunga mkono azimio la amani na kukomesha umwagaji damu," aliongeza, akizitaka DRC na Rwanda kusitisha uungaji mkono wao kwa makundi yenye silaha yaliyoidhinishwa kama ilivyoainishwa na mikataba ya amani inayoongozwa na Marekani iliyotiwa saini mwezi Desemba mwaka jana.

    Hii si mara ya kwanza kwa wanachama wa makundi yenye silaha nchini DRC kuwekewa vikwazo. Lakini hatua hizo zimeshindwa kukomesha mapigano katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo lenye machafuko.

    Soma zaidi:

  4. Tetesi za Soka Ulaya: Aston Villa haina mpango wa kumuuza Rogers

    Aston Villa haina mpango wa kumuuza Morgan Rogers huku klabu kadhaa zikiwa na nia ya kumsajili kiungo huyo mshambuliaji, Barcelona bado wana hamu ya kumsajili Marcus Rashford kutoka Manchester United na Real Madrid wanafanya mazungumzo na beki wa kulia wa Inter Milan Denzel Dumfries.

    Aston Villa wanajua kuwa kuna nia ya kumsajili kiungo mshambuliaji Morgan Rogers kutoka klabu kadhaa, ikiwemo Arsenal, lakini hawana mpango wa kumuuza mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 23. (Telegraph - subscription required)

    Beki wa pembeni wa Eintracht Frankfurt, Nathaniel Brown, mwenye umri wa miaka 22, ndiye anayewindwa na Bayern Munich na Arsenal. (The Athletic - subscription required)

    Manchester City na Chelsea wanamtaka beki wa pembeni wa Juventus Andrea Cambiaso, 26, huku Barcelona pia ikifuatilia hali ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Italia. (Gazzetta dello Sport - in Italian)

    Liverpool na Paris St-Germain huenda zote zikamtaka winga wa RB Leipzig Yan Diomande lakini klabu hiyo ya Ujerumani haitikiswi na hali hiyo kwani inaamini mchezaji huyo wa miaka 19 hataendelea kuwa nao kwa mwaka mwingine tu bali pia atasaini mkataba mpya ulioboreshwa. (Sky Sports Germany)

    Kocha wa Barcelona Hansi Flick, mkurugenzi wa michezo Deco na rais Joan Laporta bado wana hamu ya kumsajili mshambuliaji wa Manchester United Marcus Rashford kwa mkataba wa kudumu huku Bayern Munich, Newcastle, Tottenham na Aston Villa wakimtaka mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 28. (The I)

    Juventus wanaangalia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Bournemouth na Uholanzi Justin Kluivert mwenye umri wa miaka 27 kama mbadala wa mchezaji wa Real Madrid mwenye umri wa miaka 26 wa Morocco Brahim Diaz. (Gazzetta dello Sport - in Italian)

    Manchester United wamemfuatilia mlinzi wa Juventus na Ufaransa Pierre Kalulu na klabu ya Turin huenda ikalazimika kumuuza mchezaji huyo wa miaka 25 ili kusawazisha masuala ya miamala baada ya kushindwa kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa. (Corriere dello Sport - in Italian)

    Kiungo wa kati wa Ureno Mateus Fernandes, 21, ameruhusiwa kuondoka West Ham baada ya mawasiliano kutoka Manchester United na Arsenal, huku Liverpool na Paris St-Germain pia zikimfuatilia. (Teamtalk)

    Aston Villa, Atletico Madrid na Borussia Dortmund zinamtaka mshambuliaji wa Club Brugge, Mjerumani Nicolo Tresoldi, 21, baada ya msimu mzuri Ubelgiji. (The Athletic - subscription required)

    Real Madrid wamefanya mazungumzo na mlinzi wa Inter Milan Denzel Dumfries, ambaye kima chake cha kuuza ni pauni milioni 21.6, huku wakimwona mchezaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 30 kama shabaha yao kuu ya kuimarisha safu yao ya beki wa kulia. (Athletic)

    Pia unaweza kusoma:

  5. Israel yashambulia kusini mwa Lebanon

    Israeli imeendelea na mashambulizi yake kusini mwa Lebanon siku ya Jumanne, lakini haikushambulia Beirut kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano kwa kiasi fulani na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.

    Lebanon ilisema kwamba, chini ya makubaliano yaliyotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump usiku wa Jumatatu, vikosi vya Israeli havitashambulia mji mkuu kwa mabomu nayo Hezbollah haitashambulia Israeli.

    Hii ilitokea baada ya Iran kusema kwamba hatua ya Israeli nchini Lebanon inahatarisha mazungumzo kuhusu makubaliano ya kukomesha vita vyake na Marekani.

    Kufuatia tangazo la kusitisha mapigano, jeshi la Israeli lilisema limezuia makombora mawili yaliyorushwa kaskazini mwa Israeli.

    Hezbollah ilisema imeshambulia vikosi vya Israeli kusini mwa Lebanon, ambapo maafisa waliripoti mashambulizi mabaya ya Israeli.

    Soma zaidi:

  6. Marekani na Iran zaanzisha mashambulizi mapya huku mazungumzo ya kusitisha mapigano yakikwama

    Jeshi la Marekani linasema limeanzisha mashambulizi ya "kujilinda" dhidi ya Iran na kudungua makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani kwenye meli na nchi za Ghuba.

    Mashambulizi hayo kwenye Kisiwa cha Qeshm, katika Mlango-Bahari wa Hormuz, yalikuwa "kujibu majaribio ya mashambulizi ya Iran kote Mashariki ya Kati", Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) ilisema.

    Iran ilisema imeshambulia kambi na helikopta za Marekani katika "nchi ya kikanda" kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani kama kulipiza kisasi.

    Centcom ilisema Tehran imerusha makombora mawili dhidi ya Kuwait na matatu dhidi ya Bahrain, ambayo yote yalivunjika vipande vipande au kuzuiliwa.

    Mashambulizi ya hivi karibuni yanatokea huku mazungumzo ya kusitisha mapigano yakikwama, baada ya mazungumzo kuhusu makubaliano ya kukomesha vita vyao vya miezi kadhaa kushindwa kuendelea mwishoni mwa juma.

    Centcom iliongeza kuwa shambulio hilo katika Kisiwa cha Qeshm lilikuwa limelenga kituo cha udhibiti wa ardhini cha jeshi la Iran, na kwamba jeshi la Marekani pia lilidungua ndege tatu zisizo na rubani ambazo zilikuwa zimerushwa na Iran kuelekea kwa "mabaharia raia waliokuwa wakipitia maji ya kikanda kihalali".

    IRGC ilisema "kuvuruga usalama wa Mlango-Bahari wa Hormuz kutakuwa na gharama kubwa kwa jeshi la Marekani lenye uchokozi".

    Iran imekuwa ikishambulia mara kwa mara maeneo ya Bahrain na Kuwait, ambapo kambi za kijeshi za Marekani zipo.

    Hapo awali, Centcom ilisema imeishambulia na kuiharibu meli ya mafuta isiyo na mizigo iliyokuwa ikielekea Iran, kama sehemu ya kizuizi cha majini cha Washington kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz.

    Soma zaidi:

  7. Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara tarehe ni 03/06/2026.