Hizi ndizo nchi 10 zenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika kwa mwaka 2026

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Kila mwaka, Shirika la Fedha la Duniani (IMF) huchapisha ripoti yake ya World Economic Outlook, na kila mwaka viwango vya Pato la Taifa kwa bei ya sasa (nominal GDP) vya uchumi wa nchi za Afrika huzua mjadala mkubwa kuliko ufafanuzi wa kina.

Takwimu hizo hutumiwa mara nyingi ama kama ushahidi wa maendeleo ya bara au kama ukumbusho kuwa Afrika bado ina safari ndefu kiuchumi.

Kile ambacho mara chache hupatikana ni uchambuzi makini unaostahili: tathmini ya wazi ya vichocheo vya kila uchumi, misingi ya kimuundo inayofafanua viwango hivyo, pamoja na mwelekeo wa muda mrefu unaoonekana kupitia takwimu hizo.

Makadirio ya IMF ya Aprili 2026 yanatoa fursa ya kuondoka kwenye vichwa vya habari vya kawaida vinavyoangazia mataifa machache makubwa kiuchumi na badala yake kuangalia kwa mapana orodha nzima ya uchumi wa Afrika katika muktadha wake kamili.

Zifuatazo ni ndizo nchi 10 zenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika kwa mwaka 2026.

1. Afrika Kusini

Afrika Kusini inaendelea kushikilia nafasi yake kama uchumi mkubwa zaidi barani Afrika, huku uchumi wake ukiongezeka kwa takribani asilimia 11 kutoka dola bilioni 427.1 mwaka uliopita, kwa mujibu wa Business Day ya Nigeria.

Uongozi wake unatokana na uwepo wa sekta ya kifedha iliyoendelea kwa kiwango kikubwa, masoko ya mitaji yenye kina, pamoja na viwanda vya kisasa vinavyoanzia uchimbaji wa madini hadi uzalishaji wa viwandani.

Licha ya changamoto zinazoendelea kama upungufu wa nishati ya umeme, matatizo ya miundombinu ya usafirishaji na usambazaji, pamoja na kasi ndogo ya utekelezaji wa mageuzi ya kiuchumi, kiwango cha utata na maendeleo ya muundo wa uchumi wake bado kinaitofautisha Afrika Kusini na mataifa mengine mengi ya bara hilo.

Ni nafasi ambayo imeidumisha kwa miongo kadhaa, na inayodhihirisha kina cha kimuundo cha uchumi ambao hakuna taifa jingine la Afrika limeweza kuujenga kwa kiwango sawa hadi sasa. Soko la Hisa la Johannesburg bado ndilo lenye maendeleo makubwa zaidi barani humo katika masuala ya mitaji na fedha.

Sekta za viwanda, madini, huduma za kifedha, kilimo, pamoja na sekta pana ya huduma zinaifanya Afrika Kusini kuwa na msingi wa uzalishaji uliotofautishwa kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na mataifa mengi ya Afrika.

2. Misri

Misri inaendelea kushikilia nafasi ya pili kwa uthabiti, huku uchumi wake ukikua kwa asilimia 17.84 kutoka dola bilioni 314.6.

Ukuaji huo umechochewa na utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu, upanuzi wa eneo la kiuchumi la Mfereji wa Suez, pamoja na msingi mpana wa uchumi unaojumuisha sekta za utalii, ujenzi, na nishati.

Mageuzi ya kiuchumi yanayoungwa mkono na wakopeshaji wa kimataifa pia yamechangia kuimarisha mazingira ya uchumi na kuvutia uwekezaji.

Hata hivyo, Misri bado inakabiliwa na hatari muhimu zinazotokana na mfumuko wa bei pamoja na shinikizo la thamani ya sarafu, mambo ambayo yanaendelea kuathiri uthabiti wa uchumi wake kwa muda mrefu.

3. Nigeria

Nigeria, ikiwa na GDP ya dola bilioni 334.34, inashikilia nafasi ya tatu barani Afrika. Ikiwa na idadi ya watu zaidi ya milioni 200 pamoja na akiba kubwa ya mafuta inayozalisha sehemu kubwa ya mapato ya serikali na fedha za kigeni, ukubwa wa uchumi wa Nigeria unaakisi zaidi rasilimali zake za asili na ukubwa wa idadi ya watu kuliko mageuzi mapana ya uzalishaji wa kiuchumi.

IMF inakadiria ukuaji wa uchumi wa Nigeria kufikia asilimia 4.0 mwaka 2025 na asilimia 4.1 mwaka 2026, ukuaji unaochochewa na kuongezeka kwa uzalishaji wa mafuta pamoja na upanuzi wa sekta ya huduma.

Mpango wa mageuzi ya kiuchumi ulioanzishwa mwaka 2023, ukiwemo kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta na kuachiliwa kwa soko la ubadilishaji wa fedha za kigeni, umeanza kuonesha matokeo ya awali.

Hata hivyo, deni la serikali linafikia asilimia 35.5 ya GDP mwaka 2025, huku malipo ya riba yakitumia sehemu kubwa isiyo ya kawaida ya mapato ya serikali.

Kwa hiyo, nafasi ya Nigeria katika viwango vya uchumi wa Afrika inaonesha zaidi ukubwa wake wa kiasili na kidemografia, wakati mwelekeo wa ukuaji wake unaonesha mchakato wa marekebisho ya kiuchumi ambao bado haujaonesha matokeo kamili ya muda mrefu.

4. Algeria

Uchumi wa Algeria ulikua kwa asilimia 11 kutoka dola bilioni 285.7, na hivyo kuifanya nchi hiyo kushika nafasi ya nne barani Afrika.

Mauzo ya nje ya mafuta na gesi yanaendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wake, yakinufaika na mahitaji ya kimataifa ya nishati.

Katika miaka ya hivi karibuni, Algeria imeanza juhudi za kupanua msingi wa uchumi wake kwa kuwekeza katika sekta za viwanda na nishati jadidifu.

Hata hivyo, maendeleo ya mageuzi hayo yamekuwa ya taratibu, huku uchumi ukiendelea kutegemea kwa kiasi kikubwa mapato yatokanayo na sekta ya hydrocarbons.

5. Morocco

Morocco inashika nafasi ya tano, huku GDP yake ikiongezeka kwa asilimia 6.4 kutoka dola bilioni 182.6.

Nguvu ya uchumi wake inatokana na sekta za utalii, kilimo, pamoja na msingi wa viwanda unaoendelea kupanuka, hasa katika utengenezaji wa magari na vifaa vya anga.

Uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu pamoja na uhusiano wa kibiashara na Ulaya umeongeza zaidi uimara wa uchumi wa Morocco, na kuifanya kuwa moja ya mataifa yenye uchumi uliotofautishwa zaidi katika Afrika Kaskazini.

Uwezo wa bandari ya Tanger Med umeifanya Morocco kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji na biashara katika Bahari ya Atlantiki na Mediterania.

Mwelekeo wa ukuaji wa uchumi wa Morocco pia umekuwa wa uthabiti zaidi kuliko baadhi ya mataifa yaliyo juu yake katika viwango vya uchumi wa Afrika.

6.Angola

Angola, mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa mafuta barani Afrika, ilirekodi ukuaji wa asilimia 7.53 kutoka GDP ya dola bilioni 141.73. Mapato ya juu yatokanayo na mafuta yamechangia kuimarika kwa uchumi wake, huku mageuzi yanayolenga kuleta uthabiti wa fedha za umma na kuvutia uwekezaji wa nje yakianza kutoa matokeo chanya.

Hata hivyo, juhudi za kupanua uchumi zaidi ya sekta ya mafuta bado zinakabiliwa na changamoto kubwa, na utofautishaji wa vyanzo vya mapato unabaki kuwa suala kuu la kimkakati kwa maendeleo ya muda mrefu ya Angola.

7. Kenya

Kenya inaendelea kushikilia nafasi yake kama uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki, huku uchumi wake ukikua kwa asilimia 7.9 kutoka dola bilioni 136.46.

Kwa mujibu wa jarida la Business Day, nguvu ya uchumi huu inatokana na sekta ya huduma yenye uhai mkubwa, ikijumuisha huduma za kifedha, teknolojia, na usafirishaji, pamoja na msingi imara wa kilimo.

Nairobi inaendelea kutumika kama kitovu muhimu cha biashara cha kikanda, jambo linalochochea zaidi ukuaji wa uchumi na kuimarisha nafasi ya Kenya kama mhimili wa shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

Bandari ya Mombasa na Reli ya Standard Gauge inayoiunganisha na Nairobi na kuendelea hadi Uganda na Rwanda huzalisha shughuli za kiuchumi zinazovuka mipaka ya Kenya yenyewe, na kuifanya kuwa kitovu cha kikanda cha biashara na usafirishaji.

8.Ghana

Uchumi wa Ghana ulikua kwa kiwango cha wastani cha asilimia 3.2 na kufikia dola bilioni 114.71. Licha ya changamoto za hivi karibuni za kifedha na deni la umma, nchi hiyo bado inaendelea kuwa mhusika muhimu katika uchumi wa Afrika kutokana na mauzo yake ya nje ya dhahabu, mafuta, na kakao.

Mageuzi ya kiuchumi yanayoendelea pamoja na programu zinazoungwa mkono na IMF yanatarajiwa kusaidia kuleta uthabiti wa ukuaji wa uchumi katika muda wa kati.

9. DRC

DRC inajitokeza kwa ukuaji mkubwa wa asilimia 32.9 kutoka GDP ya dola bilioni 98.83. Utajiri wake mkubwa wa madini, hasa cobalt na shaba,

Hata hivyo, ukosefu wa utulivu wa kisiasa na migogoro ya mara kwa mara bado vinaendelea kuleta hatari kubwa kwa maendeleo ya muda mrefu ya nchi hiyo, na kupunguza uwezo wa ukuaji huo kugeuka kuwa maendeleo endelevu ya kiuchumi.

10. Ethiopia

Ethiopia inakamilisha orodha ya mataifa kumi bora, huku GDP yake ikikua kwa asilimia 11.4 na kufikia dola bilioni 109.1. Nchi hiyo, ambayo hapo awali ilikuwa miongoni mwa uchumi unaokua kwa kasi zaidi barani Afrika, inaendelea kuimarika taratibu baada ya athari za migogoro ya ndani.

Uwekezaji unaoongozwa na serikali katika miundombinu na sekta ya viwanda, pamoja na uwepo wa soko kubwa la ndani, unaendelea kusaidia mwelekeo wa ukuaji wa uchumi wa Ethiopia na kuimarisha msingi wake wa muda mrefu wa maendeleo ya kiuchumi.