Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
AFCON U-17: Tanzania yafa kiume fainali, yaacha alama Afrika
Ndoto ya Tanzania kutwaa taji lake la kwanza la Afrika katika soka imeishia mikononi mwa Senegal baada ya Serengeti Boys kufungwa kwa penati 4-2 kufuatia sare ya 1-1 katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U-17) iliyochezwa mjini Rabat, Morocco.
Lakini licha ya maumivu ya kupoteza taji, vijana hao wanaondoka Morocco wakiwa wameandika ukurasa mpya katika historia ya soka la Tanzania. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Tanzania kufika fainali ya mashindano hayo na mara ya kwanza kwa timu ya taifa ya Tanzania kufika hatua hiyo katika michuano mikubwa ya CAF.
Tanzania ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la mapema dakika ya saba kupitia Hamis Chenga aliyemalizia vizuri shambulizi lililoanzia katikati ya uwanja. Bao hilo liliwapa matumaini makubwa Watanzania waliokuwa wakifuatilia mchezo huo wakiamini historia ilikuwa karibu kuandikwa.
Hata hivyo, mabingwa hao wa mwaka 2023 walionyesha kwa nini wameendelea kuwa miongoni mwa mataifa yenye mfumo bora wa ukuzaji wa vipaji barani Afrika. Senegal walitawala sehemu kubwa ya mchezo na hatimaye wakasawazisha dakika ya 64 kupitia Ibrahima Dione baada ya kipa wa Tanzania, Haji Abdallah, kushindwa kuudhibiti mpira wa adhabu uliopigwa na Souleymane Faye.
Dakika zilizobaki zilikuwa za mvutano mkubwa huku kila timu ikitafuta bao la ushindi. Tanzania ilibaki imara kama ilivyofanya katika robo fainali dhidi ya Algeria na nusu fainali dhidi ya Misri. Lakini baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1, mshindi alipaswa kupatikana kwa mikwaju ya penati.
Katika hatua hiyo ndipo safari ya Tanzania ilipofikia mwisho. Senegal walifunga penati zao zote nne huku Tanzania ikikosa mbili, jambo lililowapa Simba wadogo wa Teranga ubingwa wao wa pili wa Afrika ndani ya miaka mitatu.
Tanzania imefungwa kwa mafanikio
Hata hivyo, matokeo ya fainali hayawezi kufuta mafanikio ambayo Serengeti Boys wameyapata katika mashindano haya. Tanzania ilimaliza kinara wa Kundi C baada ya kuwashinda Msumbiji na Angola kabla ya kufungwa na Uganda. Katika hatua ya mtoano, vijana hao walionyesha uimara wa kiakili kwa kuwatoa Algeria na Misri kupitia mikwaju ya penati.
Safari hiyo imeifanya Tanzania sio tu kufika fainali kwa mara ya kwanza, bali pia kufuzu Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 17. Kwa wengi, hilo ni jambo kubwa zaidi kuliko hata matokeo ya fainali yenyewe.
Mafanikio hayo yanakuja wakati Serikali ya Tanzania ikiendelea kuwekeza katika maendeleo ya soka la vijana. Serengeti Boys wataendelewa kuwekwa kambini kwa muda mrefu kwa maandalizi maalum, huku wachezaji wakiahidiwa kupewa zawadi ya shilingi milioni 500 kwa kufika fainali.
Lakini hata bila kombe, kizazi hiki tayari kimeonyesha kuwa Tanzania inaweza kushindana na mataifa makubwa ya soka la Afrika. Kimeibua matumaini mapya kuelekea Kombe la Dunia la vijana na malengo makubwa zaidi ya muda mrefu ya kuona Tanzania ikifuzu Kombe la Dunia la wakubwa mwaka 2030.
Kwa hiyo, ingawa Senegal ndiyo waliobeba kombe mjini Rabat, Serengeti Boys wameondoka Morocco wakiwa wamejipatia kitu ambacho hakipimwi kwa medali pekee ama kombe, bali imani kwamba Tanzania inaweza kushindana na timu bora zaidi barani Afrika.