Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tanzania inatafuta nini Urusi?
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameanza ziara ya siku tatu nchini Urusi kuanzia Juni 3 hadi 5, 2026, ambapo atafanya mazungumzo rasmi na Rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin, pamoja na kushiriki katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF 2026).
Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Samia nje ya Bara la Afrika, tangu vurugu za uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, lakini ni ziara ya pili kufanywa na Rais wa Tanzania nchini Urusi tangu 1969 alipozuru Baba wa Taifa, Julius Nyerere.
Na kwa mujibu wa taarifa ziara hii inalenga kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na Urusi katika sekta mbalimbali za kimkakati, zikiwamo biashara na uwekezaji, elimu, sayansi na teknolojia, nishati, madini, kilimo na miundombinu, kwa mujibu wa Ikulu ya Tanzania.
Ziara ya Rais Samia nchini Urusi ni muhimu kiasi gani katika nyakati hizi? Je, Urusi inanufaika na mkusanyiko huu wa viongozi wa mataifa mengine katika nchi hiyo iliyotumbukia katika vita vya miaka minne na nusu sasa?
SPIEF ni nini?
Lengo la mkutano wa SPIEF (St. Petersburg International Economic Forum) ni kujenga na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, biashara, na uwekezaji kati ya Urusi, nchi zinazoibukia kiuchumi, na mataifa mengine duniani.
Mkutano huu, unaofanyika kila mwaka ni jukwaa la kimkakati linalowakutanisha viongozi wa serikali, wawekezaji, na wafanyabiashara ili kujadili mazingira ya uwekezaji na kusaini mikataba mikubwa ya kibiashara.
Pia mkutano wa kuimarisha ushawishi wa Urusi kiuchumi na kisiasa.
Uhusiano wa Tanzania na Urusi ni mzuri kwa muda mrefu. Miongoni mwa biashara kubwa kutoka Urusi zinazouzwa Tanzania ni vifaa vya ulinzi na usalama, ngano na mbolea. Mataifa haya yamedumisha uhusiano mkubwa wa kidiplomasia.
Jiji la Dar es Salaam lilikuwa mwenyeji wa kongamano la uchumi la “Jukwaa la Urusi na Afrika 2016" mwezi Aprili 2016.
Mwezi Oktoba 2019 pamoja na Julai 2023 ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri Mkuu wa wakati huo Kassim Majaliwa ulishiriki katika Mkutano wa kwanza na wa pili wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Urusi na Majukwaa ya Kiuchumi na Kibinadamu.
Putin anataka washirika
Vita vya Ukraine vilivyoanza mwanzoni mwa 2022 vimeathiri uhusiano wa Urusi na nchi za Magharibi. Urusi imepata pigo kubwa kwa kukosa washirika wa kibiashara hasa kutoka mataifa hayo, sanjari na kuwekewa vikwazo vinavyolenga kudhoofisha uchumi wake na uwezo wa kugharamia vita.
Kupitia sekta ya Nishati, Marekani na nchi za Ulaya zimeweka vikwazo uuzaji wa mafuta na gesi asilia ya Urusi katika soko la kimataifa. Kwa sasa Urusi inategemea sana soko la Asia na Afrika.
Vilevile mataifa hayo yameiondoa benki kuu na benki nyingi za Urusi kwenye mfumo wa kimataifa wa miamala ya kifedha (SWIFT), pamoja na kufungiwa kwa akaunti na mali za benki hizo nje ya nchi.
Vikwazo havikuishia hapo, pia kuzuia akaunti za benki, kukamata mali (kama vile majengo na boti za kifahari), na kuweka zuio la kusafiri kwa maafisa wakuu wa serikali na wafanyabiashara wakubwa wanaomuunga mkono Rais Vladimir Putin.
Pia mataifa ya Ulaya na Marekani, yamezuia uuzaji wa teknolojia muhimu, vipuri vya ndege, na vifaa vya kijeshi kwenda nchini Urusi ili kukwamisha uwezo wao wa kijeshi.
Vikwazo hivi vinampa Putin kila sababu ya kutafuta washirika wapya nje ya bara la Ulaya na Marekani. Afrika na nchi kama Tanzania ni sehemu ya mkakati wa Urusi wa kuboresha washirika wake wa kiuchumi na kidiplomasia.
Tanzania inatafuta nini Urusi?
Baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 na tuhuma za vurugu pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu zilizofuatia, Tanzania imejikuta ikikabiliwa na shinikizo linaloongezeka kutoka kwa mataifa ya Magharibi. Umoja wa Ulaya na Marekani zimekuwa zikitoa matamko, maazimio na hatua mbalimbali zinazoonyesha kutoridhishwa na mwenendo wa kisiasa nchini.
Kwa upande wake, Serikali ya Tanzania imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuheshimiwa kwa uhuru wa taifa, kutokuingiliwa kwa mambo yake ya ndani na kuheshimiwa kwa mamlaka ya taasisi zake. Hata hivyo, hali hiyo haijazuia kuendelea kwa ukosoaji kutoka kwa baadhi ya washirika wa Magharibi. Bunge la Ulaya, kwa mfano, limelalamikia kuzuiwa kutembelea Tanzania kufuatilia hali ya haki za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria.
Wakati huo huo, Marekani nayo imeonyesha wasiwasi wake. Muswada uliowasilishwa katika Seneti ya Marekani unataka mapitio ya uhusiano kati ya Washington na Dodoma, ikiwemo biashara, misaada ya maendeleo na ushirikiano wa usalama. Aidha, hatua ya kuweka vikwazo vya usafiri kwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Faustine Mafwele, imeongeza ishara kwamba uhusiano kati ya pande hizo unapitia kipindi kisicho rahisi.
Katika mazingira hayo, ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Urusi inaweza kutazamwa kama jitihada za kuimarisha ushirikiano na mshirika mwingine muhimu wa kimataifa. Wakati mataifa ya Magharibi yakiongeza shinikizo, Moscow inaweza kuonekana kama fursa ya kupanua ushirikiano katika biashara, uwekezaji, nishati, elimu, teknolojia na diplomasia.
Kwa mtazamo wa kisiasa, Tanzania na Urusi kwa nyakati tofauti zimejikuta zikikosolewa na baadhi ya mataifa ya Magharibi. Ingawa mazingira yao ni tofauti, hali hiyo inaweza kuchochea haja ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na kutafuta maeneo mapya ya maslahi ya pamoja.
Hivyo basi, swali la "Tanzania inatafuta nini Urusi?" linaweza kujibiwa kwa namna mbili. Kwanza, ni kutafuta fursa mpya za kiuchumi na maendeleo. Pili, ni kupanua wigo wa mahusiano ya kimataifa ili taifa lisitegemee upande mmoja pekee katika dunia inayobadilika kwa kasi.
Kadri milango ya Magharibi inavyoonekana kuwa na masharti zaidi, ndivyo Tanzania inavyoendelea kutafuta na kuimarisha urafiki na washirika wengine wa Mashariki.