Somalia: Mahakama yaamua nani ni baba mzazi wa mvulana katika mzozo uliohusishwa na vifo vya watu saba

Chanzo cha picha, Getty Images
Mahakama nchini Somalia imeamua kuwa Liban Tahliil Haji Aden ndiye baba wa mvulana mwenye umri wa miaka 16, baada ya wanaume wawili kudai kuwa baba wa mtoto huyo katika mzozo wa muda mrefu uliohusishwa na vifo vya watu saba.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, watu saba wameuawa na wengine 21 kujeruhiwa katika vurugu zinazohusishwa na mzozo huo kati ya familia hizo mbili.
Uamuzi huo ulitolewa Jumanne mjini Galkayo na jopo la wanazuoni watatu wa Kiislamu walioteuliwa na mamlaka za eneo la Puntland, linalojitawala kwa kiasi fulani.
Majaji walikubali madai ya Liban na kuyakataa ya Farah Awil Ali, ambaye anasema alimlea mvulana huyo kwa miaka 13. Wanaume hao wawili wamesema wanaukubali uamuzi wa mahakama.
Kesi hiyo imevuta hisia kubwa nchini Somalia, huku ushahidi wa mama wa mvulana huyo, Halimo Yusuf Mohamed, ukiwa sehemu muhimu ya maamuzi ya mahakama.
Wakati wa usikilizaji wa kesi uliochukua siku tatu, Halimo alisema aliolewa na Liban Julai 2006, kabla ya kutalikiana naye miaka minne baadaye.
Alisema baadaye aliolewa na Farah Oktoba 2010, lakini ndoa hiyo ilivunjika mwaka 2013.
Halimo alisisitiza kuwa Liban ndiye baba wa mwanawe na kwamba hakupata mtoto na Farah. Mashahidi wawili pia waliiambia mahakama kuwa walihudhuria harusi ya Halimo na Liban mwaka 2006.
Liban aliapa na kuiambia mahakama kuwa Halimo alimweleza alikuwa mjamzito walipotalikiana Julai 2010.
Mvulana huyo naye alihojiwa kupitia video na kusema kuwa Liban ndiye baba yake.
Katika kutoa uamuzi, majaji walizingatia ushahidi wa mashahidi, maelezo ya mama na kauli ya mvulana huyo, pamoja na sheria za Kiislamu kuhusu kuthibitisha nasaba. Hata hivyo, uamuzi huo haukutaja vipimo vya vinasaba vya DNA.
Baada ya uamuzi huo, Farah alisema anauheshimu, lakini akauliza kuhusu fedha alizotumia kumlea mvulana huyo kwa miaka 13.
Aliwaomba wanazuoni wa Kiislamu na maafisa wa serikali kuzingatia gharama alizobeba katika kipindi hicho.
Mahakama haikueleza iwapo Farah atarejeshewa fedha hizo wala namna malezi ya mvulana huyo yatakavyopangwa kuanzia sasa.
Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa watu saba wameuawa na wengine 21 kujeruhiwa katika vurugu zinazohusishwa na mzozo huo. BBC haijathibitisha kwa kujitegemea idadi hiyo ya vifo na majeruhi.
Akizungumza baada ya uamuzi wa Jumanne, Liban aliomba msaada kwa walioathiriwa na vurugu hizo.
“Watu wamefariki. Watu wamejeruhiwa. Kuna watoto yatima,” alisema, akiahidi kuwasaidia familia zilizopoteza wapendwa wao na waliojeruhiwa.
Majaji wamezitaka familia zote mbili kuheshimu uamuzi huo na kuepuka vurugu zaidi.
Hata hivyo, mahakama haikutoa uamuzi kuhusu nani anawajibika kwa mauaji hayo wala madai ya Farah ya kurejeshewa fedha alizotumia kumlea mvulana huyo.





































