Moja kwa moja, Milipuko yasikika mjini Addis Ababa, mapigano yakiendelea kaskazini mwa Ethiopia

Milipuko imesikika usiku kucha katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, na katika eneo la makao makuu ya jeshi magharibi mwa mji huo.

Muhtasari

Ruka Video uendelee
  • Wicknell Chivayo
  • Kijanangoma
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Beldeen Waliaula

  1. Ethiopia yafunga ubalozi wake Eritrea, na kuwafukuza wanadiplomasia 10

    .

    Ethiopia imefunga ubalozi wake mjini Asmara, Eritrea, ikisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya vitendo vya Eritrea kuashiria wanahusika na uhasama unaondelea kaskazini mwa taifa hilo.

    Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Ethiopia, serikali hiyo pia imetangaza kuwa imewafukuza wanadiplomasia 10 wa Eritrea waliopo mjini Addis Ababa na kuwaamuru kuondoka nchini humo.

    Wanadiplomasia hao wamepewa muda wa saa 48 kuondoka Ethiopia.

    Ethiopia imesema wanadiplomasia hao wamehusika katika shughuli ambazo, zinatishia moja kwa moja usalama wa taifa hilo na kukiuka masharti ya Mkataba wa Vienna kuhusu Mahusiano ya Kidiplomasia.

    Addis Ababa imeitaka serikali ya Eritrea kusitisha vitendo vyote inavyodai vinakiuka misingi inayosimamia uhusiano kati ya mataifa huru.

    Hata hivyo, Ethiopia imesisitiza kuwa inathamini uhusiano wake wa kihistoria na kitamaduni na raia wa Eritrea.

    Serikali hiyo imesema bado imejitolea kuendelea kudumisha amani, utulivu wa kikanda na ushirikiano, pamoja na kutafuta suluhu ya amani kwa mizozo inayoendelea.

    Soma pia:

  2. Mnangagwa: Kifo cha Wicknell Chivayo ni pigo kubwa kwa Zimbabwe

    .

    Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amemuomboleza mfanyabiashara Wicknell Chivayo, akisema alikuwa na mipango mingi kwa ajili ya Zimbabwe, wananchi wake na Afrika kwa ujumla ambayo alikuwa akiitekeleza kabla ya kupoteza maisha yake katika ajali ya helikopta.

    Mnangagwa amesema Chivayo alikuwa amemshirikisha katika baadhi ya mipango yake siku moja tu kabla ya ajali hiyo, akielezea kifo chake pamoja na mkewe, Lucy Muteke, kuwa pigo kubwa kwa taifa hilo.

    "Kufariki ghafla kwa Bw. na Bi. Chivayo, pamoja na wahudumu wawili wa helikopta na msaidizi mmoja wa usalama katika ajali ya helikopta jana alasiri, kumeiacha nchi yetu, familia yangu na mimi binafsi tukiwa katika mshtuko mkubwa na majonzi," Mnangagwa amesema katika ujumbe wake wa rambirambi.

    Helikopta hiyo ilianguka hapo jana katika shamba la Kudenga, Marondera, mashariki mwa Harare, na kuua watu wote sita waliokuwa ndani mwa ndege hiyo.

    Mnangagwa amesema mfanyabiashara huyo alikuwa na maono mapana yaliyovuka mipaka ya familia yake na nchi yake.

    "Marehemu Wicknell Chivayo alikuwa na maono makubwa kwa ajili ya familia yake, nchi yetu, ukanda wa kusini mwa Afrika na bara letu la Afrika,"

    Rais huyo amesema Chivayo alikuwa na mchango katika kuimarisha uhusiano wa Zimbabwe na mataifa mengine na kuitangaza nchi hiyo kimataifa, huku akielezea shughuli zake za kutoa misaada kuwa sehemu muhimu ya urithi wake.

    "Chivayo alikuwa mtoaji mkubwa wa misaada, huku michango yake ya hisani ikifikia mamilioni ya dola na kuwafikia watu na taasisi katika siasa, dini, utumishi wa umma, utamaduni, michezo na taaluma nyingine," Mnangagwa amesema.

    Amesema binafsi alikuwa akifahamu mipango kadhaa ambayo Chivayo alikuwa akiandaa, hasa mipango iliyolenga kuwasaidia Wazimbabwe wasiojiweza na wanajeshi waliostaafu.

  3. Netanyahu: Rubani msaidizi wa flydubai alikuwa amepokea mafunzo ya itikadi kali

    Picha ya Benjamin Netanyahu
    Maelezo ya picha, Picha ya Benjamin Netanyahu

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kuwa rubani msaidizi aliyedaiwa kujaribu kuangusha ndege ya abiria YA Flydubai, iliyokuwa ikielekea Israel alikuwa amepokea mafunzi ya itikadi kali ya Kiislamu.

    "Tunajua kwamba amepokea mafunzo ya itikadi kali ya Kiislamu," Netanyahu amesema katika mahojiano na shirika la habari la Fox News.

    Bado hakuna sababu rasmi iliyothibitishwa kuhusu kilichochea tukio la kutisha la hapo jana katika ndege ya flydubai FZ1073 iliyokuwa ikisafiri kutoka Dubai kwenda Tel Aviv.

    Netanyahu ameiambia kipindi cha "Fox & Friends" kwamba ndani ya siku chache wataweza kubaini iwapo rubani msaidizi huyo alikuwa na uhusiano na Iran.

    "Nadhani bado ni mapema kusema iwapo alikuwa na uhusiano wowote na Iran au mtu mwingine yeyote."

    Netanyahu amesema ni wazi kwamba rubani msaidizi huyo alikuwa na nia ya kujiua.

    Soma pia:

  4. Omar al-Bashir apelekwa hospitalini Khartoum kwa matibabu

    Picha ya zamani ya aliyekuwa Rais wa Sudan, Omar Al-Bashir
    Maelezo ya picha, Picha ya zamani ya aliyekuwa Rais wa Sudan, Omar Al-Bashir

    Rais wa zamani wa Sudan aliyeondolewa madarakani, Omar al-Bashir, amefikishwa katika hospitali inayosimamiwa na jeshi mjini Khartoum kwa ajili ya matibabu, na inasemekana anahitaji matibabu zaidi nje ya nchi, hii ni kulingana na taarifa iliyotolewa na wakili wake.

    Bashir, mwenye umri wa miaka 82, aliondolewa madarakani na jeshi la Sudan pamoja na kikosi cha kijeshi cha Rapid Support Forces (RSF) mwezi Aprili mwaka wa 2019, kufuatia maandamano ya wananchi yaliyodumu kwa miezi kadhaa.

    Baadaye, RSF na jeshi la Sudan, walitofautiana kuhusu mpango wa kuunganisha vikosi vyao wakati wa mchakato wa kurejesha utawala wa kiraia.

    Tangu wakati huo, pande hizo mbili zimekuwa zikipigana vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimesababisha uharibifu mkubwa katika taifa hilo kwa zaidi ya miaka mitatu na nusu.

    Bashir alikuwa amehamishwa kutoka gerezani hadi hospitalini kabla ya vita kuanza, na baadaye kupelekwa katika mji wa Merowe kaskazini mwa Sudan, ambako aliwekwa chini ya ulinzi wa kijeshi.

    Bashir kwa sasa amefikishwa mjini Khartoum ili kufanyiwa vipimo vya afya baada ya hali yake kudorora.

    Katika taarifa iliyotolewa na familia ya Bashir ilisema, “hitaji lake la kupata matibabu nje ya Sudan ni la dharura na haliwezi kucheleweshwa tena”, familia hiyo bado haina kibali ya kumsafirisha nje ya nchi.

    Soma pia:

  5. Jeshi la Iran lawauwa watu sita wanaodaiwa kuwa magaidi

    .

    Jeshi la Iran IRGC, limewaua watu sita wa kundi kutoka kundi moja la kigaidi hii leo shirika la habari la serikali IRNA limeripoti.

    Tukio hilo limetokea katika eneo ambalo mara kwa mara hushuhudia mapigano kati ya vikosi vya usalama na makundi yenye silaha, yakiwemo wanamgambo wa Kisunni na makundi yanayotaka kujitenga.

    Watu hao wameuawa mjini Zahedan, mji mkuu wa jimbo maskini la Sistan-Baluchistan kusini mashariki mwa Iran, linalopakana na Pakistan na Afghanistan na ambalo ni njia inayotumiwa kusafirisha dawa za kulevya.

    Kulingana na shirika la habari la IRNA, vikosi vya usalama viligundua vifurushi vya vilipuzi vilivyokuwa vimefichwa na kundi hilo. Taarifa hiyo haikuwataja watu sita waliouawa wala kutoa maelezo zaidi kuhusu tukio hilo.

    Tehran inazituhumu baadhi ya makundi yenye silaha kuwa na uhusiano na mataifa ya kigeni na kujihusisha na biashara ya magendo mpakani.

    Shirika la kutetea haki za binadamu la Haalvsh, linalofuatilia hali katika eneo la Sistan-Baluchistan, limesema mapigano kati ya jeshi na makundi ya watu wenye silaha yalianza mapema leo asubuhi.

    Soma pia:

  6. Milipuko yasikika mjini Addis Ababa, mapigano yakiendelea kaskazini mwa Ethiopia

    Picha ya mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa
    Maelezo ya picha, Picha ya mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa

    Milipuko imesikika usiku kucha katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, na katika eneo la makao makuu ya jeshi magharibi mwa mji huo.

    Milipuko hiyo imetokea saa chache baada ya ndege zisizo na rubani kupigwa marufuku kupaa mjini Addis Ababa, na wiki moja baada ya mapigano kuzuka kaskazini mwa nchi hiyo, kati ya jeshi la taifa hilo na muungano mpya wa makundi yenye silaha, ikiwemo wapiganaji kutoka eneo la Tigray.

    Chanzo kinachohusishwa na wapiganaji wa upinzani kimeiambia shirika la habari la Reuters kwamba wao ndio waliohusika na kile walichodai kuwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani.

    "Ilikuwa sauti kubwa sana. Ilikuwa na nguvu kiasi cha kuwasha kengele za magari," mkazi mmoja wa eneo la kusini mwa jiji, ameiambia BBC Amharic.

    Chanzo hicho kimesema alisikia mlipuko huo katika eneo la Gotera karibu saa sita usiku.

    Mkazi mwingine ameiambia BBC kwamba alikuwa akicheza michezo na marafiki zake waliposikia mlipuko.

    Hakuna taarifa rasmi zakuthibitisha chanzo cha milipuko hiyo, maeneo kamili yaliyoathiriwa au iwapo kulikuwa na majeruhi au uharibifu.

    Ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Wizara ya Ulinzi, pamoja na polisi mjini Addis Ababa, hawajajibu maombi ya BBC ya kutoa maoni.

    Soma pia:

  7. Iran: Kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani Iraq ni 'ushindi wa kihistoria'

    .

    Jeshi la Iran IRGC, limesema kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani nchini Iraq ni “tukio kubwa na la kihistoria” na ni mafanikio kwao, wakitaka wanajeshi wote wa Marekani, kuondoka Mashariki ya Kati.

    Katika taarifa, jeshi hilo limesema, “Tunaipongeza taifa la Iraq, Muungano wa Kiislamu wa Upinzani na wapiganaji wa mapinduzi kwa ushindi huu wa kihistoria.”

    Taarifa hiyo ipia inasema, “Marekani lazima iondoke katika eneo hili na kuyaachia mataifa ya eneo hili jukumu la kusimamia usalama wao.”

    Jeshi hilo limesema kuwa uwepo wa wanajeshi wa Marekani kwa Zaidi ya miongo miwili eneo hilo hakujasaidia kudumisha usalama, bali kumechochea ukosefu wa usalama, utulivu na ugaidi.

    Hapo jana tarehe 30 mwezi Septemba,ilikuwa siku ya mwisho ya uwepo kwa vikosi vya Marekani nchini Iraq.

    Soma pia:

  8. Burundi yakubali kuwapokea wahamiaji kutoka Marekani

    Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye
    Maelezo ya picha, Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye

    Taifa la Burundi limejiunga na mataifa mengine ya Afrika yanayowapokea wahamiaji wanaofukuzwa kutoka Marekani chini ya sera kali ya uhamiaji ya Rais Donald Trump.

    Serikali ya Bujumbura imesema itawapokea tu wahamiaji ambao hawajashutumiwa kwa uhalifu au kuwa na uhusiano na ugaidi, hii ni kulingana na Nancy Ninette Mutoni, msemaji wa Rais wa taifa hilo Evariste Ndayishimiye.

    Washington imekuwa ikiwatuma wahamiaji wanaofukuzwa Marekani kwenda takriban mataifa sita ya Afrika kupitia mikataba isiyo wazi, ambayo maseneta wa chama cha Democratic wanasema imegharimu makumi ya mamilioni ya dola.

    Hata hivyo, mashirika ya kutetea haki za binadamu imekuwa ikipinga hatua hiyo ya Marekani.

    Mutoni amesema maandalizi yanaendelea ya kuwapatia wahamiaji hao makazi, mazingira bora ya maisha na kuwajumuisha katika jamii.

    "Kupokea kundi hili la wahamiaji kunahitaji mipango madhubuti wataishi wapi, watakula nini na wataishije pamoja na wakazi wa eneo husika," amesema msemaji huyo.

    Kuhusu uwezekano wa wahamiaji hao kupewa uraia wa Burundi, msemaji huyo alijibu kuwa "Iwapo watachagua kuungana na raia wa Burundi na kutoa mchango wenye thamani katika maendeleo ya taifa, sheria itaheshimiwa."

    Msemaji huyo ameongezea kuwa Burundi inalenga kuimarisha uhusiano wake wa kidiplomasia na Marekani, pamoja na kutoa ukarimu kwa watu wanaohitaji msaada.

    Soma pia:

  9. Israel kuimarisha ukaguzi wa marubani baada ya tukio la Flydubai

    .

    Israel imeanza kuimarisha ukaguzi wa kiusalama kwa marubani wanaoingia nchini humo kwa ndege, msemaji wa ofisi ya Waziri Mkuu wa Israell amesema.

    Hii ni baada ya kuripotiwa kuwa rubani msaidizi wa ndege ya flydubai iliyokuwa ikielekea Tel Aviv alimchoma kisu rubani mkuu na kujaribu kuangusha ndege.

    Tukio hilo la kushtua lilidhibitiwa baada ya abiria kumshinda nguvu rubani huyo msaidizi , kabla ya marubani wengine wa shirika hilo waliokuwa ndani ya ndege kuiongoza na kuitua ndege hiyo salama nchini Saudi Arabia.

    Mamlaka za Saudi Arabia zimemkamata na kumhoji rubani huyo msaidizi wa ndege ya flydubai FZ1073 iliyokuwa ikisafiri kutoka Falme za Kiarabu kwenda Israel ikiwa na watu 174, wengi wao wakiwa raia wa Israel.

    Tukio hilo limeibua maswali kuhusu namna marubani wanavyofanyiwa uchunguzi kabla ya kupewa ruhusa ya kuruka na aina ya taratibu za kiusalama wanazopitia, si Mashariki ya Kati pekee bali pia katika maeneo mengine duniani.

    "Kila rubani anayekuja Israel, tutajua utambulisho wake, tutajua yeye ni nani, na tutafanya aina fulani ya ukaguzi wa kiusalama," Doron Spielman, msemaji wa ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, ameiambia shirika la habari la Reuters.

    Amesema Netanyahu ameagiza usalama kuimarishwa katika ndege zinazoelekea Israel, iwe zinaendeshwa na mashirika ya ndege ya Israel au ya kigeni.

    "Popote ambapo Mwisraeli atakuwa akisafiri kwa ndege kuelekea Israel, jukumu letu sasa ni kufanya kila tuwezalo hata kama ndege hiyo si ya shirika la Israel kuhakikisha taratibu hizo za usalama zinaimarishwa zaidi," Spielman amesema.

    Soma pia:

  10. Ndege za kivita za Pakistan zashambulia Afghanistan

    .

    Pakistan imefanya mashambulizi mapya ya anga ndani ya Afghanistan, huku serikali ya Taliban ikisema raia tisa wameuawa na wengine 11 kujeruhiwa.

    Wizara ya Habari ya Pakistan imethibitisha mashambulizi hayo, lakini ikasema yalilenga makambi ya wapiganaji na kuwaua wapiganaji 22.

    Msemaji mkuu wa Taliban, Zabihullah Mujahid, alisema mashambulizi hayo yalipiga nyumba katika majimbo ya Kunar na Helmand, yanayopakana na Pakistan.

    Alisema wanawake na watoto ni miongoni mwa waliouawa.

    Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, Mujahid alisema:

    "Tunalaani kitendo hiki kama uvamizi na uhalifu unaokiuka kanuni zote zinazokubalika."

    Kwa upande wake, Pakistan ilisema shambulizi hilo "lilipangwa kwa makini" na lililenga "makambi ya magaidi" nchini Afghanistan, ambako kulikuwa na kiasi kikubwa cha silaha na risasi.

    Wizara ya Habari ya Pakistan ilisema tahadhari kubwa zilichukuliwa kuhakikisha hakuna madhara kwa raia au mali.

    Shahidi mmoja kutoka Garmsir, Qudratullah, aliiambia BBC kuwa mashambulizi hayo yalianza saa 9:30 alfajiri kwa saa za eneo hilo na kuendelea kwa takriban dakika 30.

    "Tulikuwa tumelala wakati ndege za kivita zilipowasili. Baada ya bomu la kwanza kulipuka, tuliamka. Baada ya shambulio la pili, tuliwachukua watoto wetu na kukimbia eneo hilo.

    "Bomu la tatu liliangukia nyumba ya jirani yetu. Kati ya watu wanne hadi watano wa familia hiyo waliuawa, huku wengine wakijeruhiwa na kupelekwa hospitalini," alisema.

    Tukio hilo linaongeza mvutano kati ya Pakistan na Afghanistan, huku kila upande ukitoa madai tofauti kuhusu waliolengwa na madhara yaliyosababishwa na mashambulizi hayo.

    Soma Zaidi:

  11. Eritrea yakataa madai ya Ethiopia huku mapigano yakiongezeka Tigray

    .

    Mapigano yaongezeka Ethiopia, Eritrea yakanusha kuhusika

    Waziri wa Habari wa Eritrea, Yemane Gebremeskel, amekanusha madai kwamba nchi yake inahusika katika mapigano mapya kaskazini mwa Ethiopia.

    Katika majibu yake nadra kwa BBC, Yemane alikishutumu chama tawala cha Ethiopia, Prosperity Party (PP), kwa kuwalaumu mataifa ya nje kwa matatizo ya nchi hiyo.

    Alisema serikali ya Ethiopia imekuwa na tabia ya kulaumu nchi jirani inapokabiliwa na migogoro ya ndani.

    "Utawala wa PP umejenga mazoea ya kuwalaumu majirani zake ili kugeuza umakini kutoka kwenye migogoro mingi ya ndani inayochochewa katika maeneo mbalimbali ya nchi," alisema.

    Mapema Septemba, makundi kadhaa yenye silaha yaliunda muungano wa wanachama saba. Muungano huo unasema unalenga kuiondoa serikali ya Addis Ababa madarakani.

    Maafisa wa Ethiopia wamezituhumu Eritrea, Sudan na Misri kwa kuunga mkono makundi ya waasi.

    Yemane amekataa madai hayo. Anasema machafuko nchini Ethiopia yanatokana na matatizo ya ndani ya kisiasa na kiusalama.

    Wiki iliyopita, mapigano yalizuka kaskazini mwa Ethiopia. Hali hiyo imeongeza hofu ya mgogoro wa kibinadamu na kuyumba kwa usalama wa eneo hilo.

    Serikali ya Ethiopia inapambana na makundi yenye silaha katika Tigray, Amhara na maeneo mengine.

    Wakati huo huo, Wakala wa Taifa wa Ujasusi na Usalama wa Ethiopia (NIA) umetangaza marufuku ya muda usiojulikana ya kurusha drone ndani ya Addis Ababa na maeneo yanayoizunguka.

    NIA ilitangaza hatua hiyo Septemba 30. Ilisema haitatoa vibali vya kurusha drone katika maeneo hayo.

    Pia ilionya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka marufuku hiyo.

    NIA imesema marufuku hiyo inalenga kuwalinda viongozi wa taifa, miundombinu muhimu na hafla kubwa za umma.

    Eritrea ilikuwa mshirika muhimu wa serikali ya Ethiopia wakati wa vita vya Tigray vilivyodumu miaka miwili. Vita hivyo vilimalizika kwa Mkataba wa Amani wa Pretoria mnamo Novemba 2022.

    Hata hivyo, uhusiano kati ya Asmara na Addis Ababa umeendelea kuzorota.

    Tangu mwishoni mwa 2023, Ethiopia imekuwa ikitaka kupata njia ya moja kwa moja ya kufikia Bahari ya Shamu.

    Ethiopia haina pwani. Serikali yake inasema hali hiyo inaleta changamoto za muda mrefu kiuchumi na kimkakati.

    Eritrea imepinga vikali mapendekezo ya Ethiopia kupata upatikanaji wa bandari kwa mamlaka ya kitaifa.

    Pia unaweza kusema:

  12. Ufilipino watuma meli na ndege kukabiliana na chombo cha China

    .

    Walinzi wa Pwani wa Ufilipino (PCG) wamesema Alhamisi wametuma meli yao kubwa zaidi pamoja na ndege kukabiliana na meli ya utafiti ya China iliyokuwa ikifanya shughuli katika bahari karibu na jimbo la kaskazini la Batanes, karibu na Taiwan.

    Msemaji wa PCG anayeshughulikia masuala ya Bahari ya Kusini mwa China, Jay Tarriela, alisema operesheni hiyo ilivuruga shughuli za utafiti wa baharini ambazo hazikuwa zimeidhinishwa na kuilazimisha meli hiyo kuondoka katika eneo ambako ilikuwa ikizunguka.

    PCG ilisema meli yake yenye urefu wa mita 97, BRP Teresa Magbanua, pamoja na ndege, zilitumwa kukabiliana na meli ya China JIA HAI KE 7, ambayo ilidaiwa kuwa imekuwa katika eneo hilo, takriban maili 37 za baharini kaskazini-magharibi mwa Kisiwa cha Itbayat, tangu Septemba 28.

    Mlinzi huyo wa pwani alisema BRP Teresa Magbanua ilisogea hadi umbali wa takriban yadi 100 kutoka kwa JIA HAI KE 7 na kutuma boti ndogo yenye uwezo wa kuhimili mawimbi makali, ambayo iliizunguka meli hiyo mara kadhaa huku maafisa wakitoa maonyo kupitia redio.

    PCG ilisema meli hiyo ya utafiti ya China ilibadili mwelekeo mara kadhaa katika jaribio la kuzikwepa boti za Ufilipino.

    Baadaye, meli ya Walinzi wa Pwani wa China iliwasili katika eneo hilo na kujaribu kuilinda meli ya utafiti, huku nayo ikitoa maonyo kupitia redio kwa meli ya Ufilipino.

    PCG ilisema kuingilia kati kwa meli ya Walinzi wa Pwani wa China ni jambo muhimu kwa sababu JIA HAI KE 7 inamilikiwa na kampuni binafsi, hali inayozua maswali kuhusu uhusiano wake na serikali ya China na madhumuni ya taarifa ilizokuwa ikikusanya karibu na njia za nyaya za mawasiliano chini ya bahari katika eneo la Batanes na Mlango wa Luzon.

    PCG ilisema operesheni hiyo bado inaendelea, lakini imefanikiwa kuilazimisha JIA HAI KE 7 kuondoka katika eneo ambako ilikuwa ikizunguka. BRP Teresa Magbanua inaendelea kufuatilia meli hiyo ili kuhakikisha inaondoka katika Ukanda wa Kiuchumi wa Kipekee (EEZ) wa Ufilipino.

    Ubalozi wa China mjini Manila haukujibu mara moja ombi la kutoa maoni kuhusu tukio hilo.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Mfungwa wa Marekani anusurika sindano mbili za kifo

    .

    Mfungwa aliyehukumiwa kifo katika jimbo la Tennessee nchini Marekani, Christa Pike, amepelekwa hospitalini baada ya moyo wake kuendelea kudunda licha ya kudungwa sindano mbili za dawa ya kutekeleza hukumu ya kifo, kwa mujibu wa wakili wake.

    Timu yake ya mawakili iliwasilisha ombi la dharura la kusitisha utekelezaji wa hukumu hiyo wakati ikiendelea, ikisema:

    “Bi Pike amepoteza fahamu lakini moyo wake bado unapiga na anatoa sauti ya kukoroma.”

    Mmoja wa mawakili wake aliiambia BBC kuwa Pike, mwenye umri wa miaka 50, alikuwa akipewa matibabu ya kuokoa maisha hospitalini baada ya kupewa dozi mbili za dawa iitwayo pentobarbital.

    Pike alihukumiwa kifo mwaka 1996 kwa kumuua Colleen Slemmer, mwenye umri wa miaka 19.

    Jaribio la kutekeleza hukumu hiyo lilifanyika katika Gereza la Riverbend Maximum Security Institution, mjini Nashville, karibu saa 20:00 Jumatano kwa saa za eneo.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, Pike alipewa dozi mbili za pentobarbital, huku pazia ya chumba cha mashahidi ikifungwa mara mbili wakati wa mchakato huo. Shirika hilo pia liliripoti kuwa waandishi wa habari waliombwa kuondoka katika eneo hilo wakati fulani.

    Timu ya mawakili wa Pike ilisema katika taarifa kwa gazeti la The Tennessean:

    “Usiku wa leo, Serikali ya Tennessee imeshindwa tena kutekeleza hukumu ya kifo kwa mujibu wa sheria.”

    Wakaongeza: “Hatufurahii kwamba tulikuwa sahihi, lakini wasiwasi ulioelezwa na Bi Pike umeonekana kuwa wa kweli: ugumu wa kupata mshipa, mishipa kuharibika, pentobarbital kuwa imeharibika, na kutokuwepo kwa huduma za dharura za matibabu wakati mambo yanapokwenda vibaya, huku yote yakifanyika chini ya utaratibu ambao bado umezungukwa na usiri.”

    Baada ya utekelezaji wa hukumu hiyo kwa kutumia sindano kuonekana kutofanyika kama ilivyotarajiwa, mawakili wa Pike waliwasilisha ombi la dharura la kusitisha utekelezaji huo na kuomba apewe huduma za matibabu.

  14. Uingereza yaishutumu Iran kuhusika na tukio la RAF Fairford

    .

    Serikali ya Uingereza inaamini kuwa Iran ilihusika kwa namna fulani katika tukio la RAF Fairford lililosababisha wanaume watano kukamatwa na baadaye kuachiliwa kwa dhamana, amesema Waziri Mkuu wa Uingereza, Andy Burnham.

    "Kuna dalili thabiti kwamba Iran ilihusika katika kile kilichotokea mwishoni mwa wiki katika RAF Fairford," Burnham aliiambia BBC.

    Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi kuhusu ushahidi ulioifanya serikali kufikia hitimisho hilo.

    Iran imejibu madai hayo, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Abbas Araghchi, akisema kiongozi huyo wa Uingereza "anapoteza mwelekeo".

    "Naweza kuthibitisha imani ya Iran kwamba kuwaachilia kwa dhamana wanaodaiwa kuwa magaidi wanaofanya kazi kwa niaba ya nchi za kigeni kunaeleza kila kitu," Araghchi aliandika kwenye mitandao ya kijamii.

    Burnham pia alijibu maswali kuhusu kwa nini watuhumiwa hao walipewa dhamana, hatua ambayo imekosolewa hadharani na Rais wa Marekani, Donald Trump.

    Akizungumza katika Ikulu ya White House Jumatatu, Trump alisema: "Nitawaambia, mimi ningesema wasipewe dhamana. Nimeshangazwa kwamba wameachiliwa. Mimi nisingefanya hivyo."

    Hata hivyo, Burnham alitetea uamuzi huo, akisisitiza kuwa watuhumiwa hao wako chini ya masharti makali sana ya dhamana.

    "Watu wanapaswa kuelewa kwamba kuachiliwa hakumaanishi kile ambacho wengi wanaweza kudhani. Kuna masharti makali zaidi ya dhamana," alisema.

    "Mamlaka zinaidhibiti hali hii kwa karibu sana, na ninaweza kuwahakikishia hilo."

    Kauli za Burnham zimekuja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kusema Jumatatu kwamba tukio la RAF Fairford "kwa wazi linahusisha mhusika wa kigeni".

    Pia unaweza kusoma:

  15. Ronaldo aondoka kambini mwa Ureno, aahidi kusema ukweli baadaye

    .

    Mshambuliaji nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo, amesema ameondoka kambini mwa timu ya taifa na kwamba atafichua sababu za uamuzi wake huo "kwa wakati muafaka".

    Hatua hiyo imekuja baada ya kocha mkuu Jorge Jesus kukanusha madai ya kuwepo kwa mgogoro kati yake na nahodha huyo wa Ureno, kufuatia ripoti zilizodai kuwa Ronaldo alikuwa amekataa kufanya mazoezi.

    Ronaldo, ambaye alisema aliwahi kufikiria kustaafu soka la kimataifa baada ya Kombe la Dunia la mwaka huu lakini akaamua kuendelea akilenga kufikisha mabao 1,000 katika kari yake, alijumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 25 cha Ureno kwa mechi za kimataifa za mwezi huu.

    Mchezaji huyo wa Al-Nassr alianza katika mchezo wa kwanza wa Ureno kwenye Ligi ya Mataifa dhidi ya Wales siku ya Jumapili, lakini hakucheza katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Norway mjini Oslo.

    Baada ya mechi hiyo, Ronaldo hakwenda kuwashukuru mashabiki pamoja na wachezaji wenzake, badala yake alielekea moja kwa moja vyumbani, hali iliyozua uvumi kuwa hakuwa na furaha na kocha wake.

    Akizungumza na wanahabari kabla ya mechi dhidi ya Denmark, Jesus alisema:

    "Hakukuwa na tukio lolote. Mchezaji yeyote akitumia dakika 20 au 30 kupasha misuli joto halafu asiingie uwanjani, hawezi kufurahia hali hiyo."

    Kocha huyo alisema alimweleza Ronaldo kabla ya mchezo kwamba hangeanza katika kikosi cha kwanza lakini angeweza kuingizwa baadaye kulingana na mazingira ya mchezo.

    "Baadaye, kama kocha, niliamua kutomuingiza. Hilo si jambo la kuleta mjadala mkubwa," alisema.

    Jesus pia alikanusha taarifa zilizodai kuwa Ronaldo aligoma kufanya mazoezi, akisema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 41 alikuwa akifanya mazoezi maalum ya kuimarisha mwili na misuli.

    Hata hivyo, Ronaldo hakuonekana uwanjani pamoja na wachezaji wenzake nchini Denmark, huku vyombo vya habari vya Ureno vikichapisha video ikimuonyesha akiondoka katika Uwanja wa Parken.

    Baadaye, Ronaldo alitangaza kupitia Instagram kuwa ameondoka kambini.

    "Baada ya mkutano wa waandishi wa habari wa timu ya taifa na baada ya mazungumzo na rais wa Shirikisho la Soka la Ureno, nimeamua kuondoka kambini."

    "Kwa wakati muafaka, nitawaambia Wareno wote ukweli kuhusu sababu zilizonifanya kuchukua uamuzi huu."

    Pia aliwatakia kila la heri wachezaji wenzake katika mechi zijazo.

    Soma Zaidi:

  16. Wicknell Chivayo: Salamu za rambirambi zaendelea kumiminika baada ya kifo chake

    .

    Salamu za rambirambi zinaendelea kutolewa kufuatia kifo cha mfanyabiashara mashuhuri wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, na mkewe Lucy Muteke, waliokuwa miongoni mwa watu sita waliofariki dunia baada ya helikopta kuanguka eneo la Marondera Rural, mashariki mwa Harare, Jumatano. Mamlaka zilisema hakuna aliyenusurika.

    Akiwa anajulikana kwa utajiri wake, misaada kwa jamii na uhusiano mpana na viongozi wa kisiasa na kidini barani Afrika, Chivayo alikuwa mmoja wa wafanyabiashara waliotambulika zaidi nchini Zimbabwe.

    William Ruto: "Rafiki yangu wa karibu"

    Rais wa Kenya, William Ruto, ameongoza salamu za rambirambi, akimtaja Chivayo kuwa "rafiki wa karibu" ambaye uchangamfu wake uliwagusa watu wengi. Ruto alisema atamkumbuka kwa urafiki wake, nguvu zake na imani yake katika uwezo wa Afrika, huku akituma pole kwa familia za waliofariki, Emmerson Mnangagwa na wananchi wa Zimbabwe.

    Ruto na Chivayo walikuwa na uhusiano uliovutia umma, huku mfanyabiashara huyo mara kwa mara akichapisha picha za mikutano yao, ikiwemo ziara zake katika State House Nairobi.

    Familia ya Chivayo: "Tumekosa maneno"

    Familia ya Wicknell Chivayo imethibitisha kuwa yeye na mkewe, Lucy Muteke, ni miongoni mwa watu waliofariki dunia katika ajali hiyo ya helikopta.

    Msemaji wa familia, Herbert Chivayo, alithibitisha vifo hivyo kwa Shirika la Utangazaji la Zimbabwe (ZBC).

    Alisema: "Tumekosa maneno kufuatia tukio hili la kusikitisha."

    Highlanders FC wamuomboleza mfadhili wao

    Klabu ya soka ya Zimbabwe, Highlanders FC, imetoa salamu za rambirambi kwa Chivayo, ambaye alikuwa mmoja wa wafadhili wake wakubwa.

    Ripoti zinasema alitoa mchango wa takriban shilingi milioni 32.4 za Kenya kwa klabu hiyo Jumatano, saa chache kabla ya ajali hiyo, jambo lililofanya msaada huo kuwa miongoni mwa matendo yake ya mwisho ya ukarimu kwa jamii.

    Viongozi wa Afrika waliokuwa na uhusiano na Chivayo

    Chivayo alikuwa akijulikana kwa kukutana na viongozi mbalimbali wa Afrika, wakiwemo Samia Suluhu Hassan, Emmerson Mnangagwa, Hakainde Hichilema, Yoweri Museveni, Bola Ahmed Tinubu na Mfalme Mswati III.

    Hata hivyo, mbali na taarifa ya Rais Ruto, hakukuwa na salamu nyingine rasmi za rambirambi kutoka kwa viongozi hao zilizokuwa zimethibitishwa kwa kujitegemea wakati makala hii ikichapishwa.

    Chapisho lake la mwisho kwenye mitandao ya kijamii

    Chapisho la mwisho la umma la Wicknell Chivayo kwenye mtandao wa X pia limezua mjadala mkubwa baada ya taarifa za kifo chake kuibuka.

    Chivayo alichapisha ujumbe huo asubuhi ya tarehe 30 Septemba, saa chache kabla ya helikopta aliyokuwa akisafiria kupata ajali.

    Ulikuwa ujumbe wa kuwapongeza mawakili wawili ambao alisema walikuwa wamemuunga mkono kwa miongo kadhaa. Alianza chapisho hilo kwa maneno haya ya Kiingereza: "APPRECIATING RELATIONSHIPS BUILT OVER DECADES... SAVED THE BEST FOR LAST."

    Chapisho hilo lilijumuisha ahadi za kutoa magari ya kifahari na zawadi kubwa za fedha kwa watu aliokuwa akiwashukuru.

    Baada ya habari za kifo chake kusambaa, ujumbe huo umevutia hisia na mjadala miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii kutokana na kuchapishwa saa chache kabla ya ajali iliyogharimu maisha yake.

    Soma Zaidi Hapa:

  17. Rubani "shujaa" azuia janga angani baada ya kudungwa kisu na mwenzake

    .

    Rubani mmoja amekamatwa baada ya kumchoma kisu rubani mwenzake kwenye ndege iliyokuwa ikisafiri kutoka Dubai kwenda Tel Aviv na "inaonekana alijaribu kuiangusha ndege hiyo", kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

    Abiria na wahudumu wa ndege walifanikiwa kumdhibiti mshambuliaji huyo na kurejesha udhibiti wa ndege ya shirika la Flydubai, ambayo baadaye ilitua salama katika uwanja wa ndege wa Tabuk, kaskazini-magharibi mwa Saudi Arabia, ikiwa na zaidi ya watu 170 ndani.

    Abiria hao, ambao wengi wao walikuwa raia wa Israel, waliwasili baadaye Jumatano mjini Tel Aviv kwa ndege maalum ya kuwarejesha nyumbani.

    Rubani aliyechomwa kisu, aliyetambulika kama raia wa India Kapteni Smit Machchhar, amelazwa hospitalini lakini hali yake inaelezwa kuwa imara.

    Netanyahu pamoja na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, wamemsifu Kapteni Machchhar na kumtaja kama "shujaa" kutokana na mchango wake katika kusaidia kuzuia tukio hilo na kuokoa maisha ya watu waliokuwa ndani ya ndege.

    "Licha ya kudungwa kisu na kujeruhiwa vibaya, alipambana, akajitetea, akafungua mlango wa chumba cha marubani na kuwawezesha abiria pamoja na wahudumu wa ndege kumdhibiti mshambuliaji huyo, na hivyo kuzuia janga kubwa ambalo lingeweza kutokea angani," Netanyahu aliandika kwenye mtandao wa X.

    "Aliokoa maisha ya watu 174, wakiwemo raia wa Israel na mataifa mengine."

    Ubalozi wa India nchini Saudi Arabia umesema Kapteni Smit Machchhar anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini na hali yake ni thabiti.

    Akitoa pongezi zake kwa rubani huyo, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, aliandika kwenye mtandao wa X: "Katika hali ya hatari kubwa sana, na licha ya kujeruhiwa vibaya, alionyesha ujasiri wa hali ya juu na azma isiyoyumba ya kulinda maisha ya wengine."

    "India inajivunia Kapteni Machchhar."

    Kauli hiyo ilikuja huku Kapteni Smit Machchhar akiendelea kupatiwa matibabu hospitalini baada ya kudungwa kisu akiwa kwenye ndege ya shirika la Flydubai iliyokuwa ikielekea Tel Aviv. Benjamin Netanyahu na Narendra Modi wamemsifu rubani huyo kwa kusaidia kuzuia kile walichosema kingegeuka janga kubwa angani

    Sababu ya tukio hilo bado haijajulikana, na rubani anayeshukiwa alikuwapo chini ya uchunguzi wa mamlaka za Saudi Arabia, kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

    Akizungumza na kituo cha habari cha Fox News usiku wa Jumatano, Netanyahu alisema rubani huyo alitarajiwa kurejeshwa katika Falme za Kiarabu (UAE), ambako ndege hiyo ilianzia safari yake, baada ya taratibu za uchunguzi kukamilika.

    Soma Zaidi Hapa:

  18. Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara. Tarehe ni 01/10/2026.