Mchungaji mmoja katika jimbo la Ohio, Marekani, amezua
mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii na miongoni mwa waumini baada ya
kumtambulisha mke wake wa pili kwa waumini wa kanisa lake, huku mke wake wa
kwanza akiunga mkono hatua hiyo.
Israel T. Ford, mwanzilishi na mchungaji mkuu wa kanisa la
LifeWorks Church lililoko Wickliffe, karibu na mji wa Cleveland, alimtambulisha
mke wake wa pili, Shakayla Ford, wakati wa ibada ya Jumapili hivi karibuni.
Katika video iliyorekodiwa wakati wa tukio hilo na kusambaa
sana mtandaoni, mke wake wa kwanza ambaye pia ni mchungaji mwenza, Lydia Ford,
alisimama madhabahuni kumkaribisha Shakayla, akimtaja kama “dada yangu katika
ndoa.”
Baadaye, Shakayla alilihutubia kanisa na kufichua kuwa yeye
na Mchungaji Ford walikuwa wameoana kwa siri kwa karibu miaka mitatu.
Utetezi wa kibiblia na ukosoaji
Baada ya tangazo hilo, Mchungaji Ford alitumia mitandao ya
kijamii kutetea ndoa hiyo, akidai kuwa msimamo wa mwanamume kuwa na mke mmoja
pekee ni mtazamo uliobuniwa na binadamu, wala si sharti la Biblia.
Akinukuu vifungu vya Agano la Kale, ikiwemo Kutoka 21:10,
alisema kuwa mwanamume kuwa na wake wengi kunaruhusiwa kwa mujibu wa maandiko.
“Tumezoeshwa kama jamii kuamini kuwa mwanamume anaweza kuwa
na mke mmoja tu. Hilo halipatani na mafundisho ya Biblia,” alisema Ford katika
video aliyochapisha mtandaoni akijibu utata ulioibuka. Naelewa kuwa ukweli huu
hauwapendezi watu wengi na kwamba viongozi wengi huepuka kuuzungumzia. Lakini
jukumu langu si kuwapendeza watu, bali kufuata yale ambayo yamefunuliwa.”
Ford alikiri kuwa msimamo wake unaweza kuwafanya baadhi ya
waumini kuondoka kanisani, akisema yuko tayari kupoteza waumini kutokana na
uamuzi huo.
Mwitikio
wa umma na masuala ya kisheria
Tangazo
hilo limeibua hisia tofauti kwenye mitandao ya kijamii. Wasomi wa Kikristo na
wakosoaji wamepinga tafsiri ya Ford ya maandiko, wakirejelea mafundisho ya
Agano Jipya, hususan 1 Timotheo 3:2, ambayo inasema kuwa kiongozi wa kanisa
anapaswa kuwa “mume wa mke mmoja.”
Pia,
maswali yameibuka kuhusu uhalali wa mpango huo kisheria. Sheria za jimbo la
Ohio zinakataza mtu kufunga ndoa na mtu mwingine wakati bado yuko kwenye ndoa
halali na mtu mwingine.
Hata hivyo,
haijabainika iwapo ndoa ya pili ya Ford ilisajiliwa rasmi kwa kupata leseni ya
ndoa kutoka kwa mamlaka za serikali au ni makubaliano ya kidini pekee ndani ya
kanisa lake.
Kwenye
mitandao ya kijamii, baadhi ya watu walionyesha mshangao kuhusu tukio hilo,
hasa kutokana na namna mke wa kwanza alivyomkaribisha mke wa pili madhabahuni.
Wengine walimshutumu Ford kwa kutafsiri maandiko ya Biblia kwa namna
inayolingana na maisha yake binafsi.