Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchambuzi: Mwanga wa amani Ukraine bado hafifu licha ya msukumo wa Marekani
- Author, Steve Rosenberg
- Nafasi, Mhariri Urusi
- Akiripoti kutoka, Moscow
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Baada ya siku mbili za juhudi za kidiplomasia zilizofanyika Oslo, Norway, na St Petersburg nchini Urusi, swali linalobaki ni kama vita vya Ukraine vimekaribia zaidi kuelekea mwisho wake.
Waziri Mkuu wa Norway alieleza mazungumzo ya Jumanne yaliyowakutanisha Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, mjumbe maalum wa Rais wa Marekani Donald Trump, Steve Witkoff, pamoja na viongozi wa Ulaya, kuwa yalikuwa "mazuri na yenye tija".
Mjini Oslo, pendekezo la kufanyika kwa mazungumzo ya pande tatu katika ngazi ya viongozi lilijadiliwa. Matumaini yalikuwa kwamba ziara ya Witkoff nchini Urusi ingeweza kufungua njia kwa mkutano wa pamoja kati ya Vladimir Putin, Zelensky na Trump, kwa lengo la kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.
Hata hivyo, Putin ameonyesha nia ndogo ya kukutana uso kwa uso na Zelensky, isipokuwa kama mazungumzo hayo yangefanyika mjini Moscow.
Kremlin imesema huenda ikawa tayari kurejea kwenye mazungumzo ya pande tatu mwezi ujao mjini Abu Dhabi, lakini katika ngazi ya wataalamu wa kiufundi pekee.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Witkoff alikiri kwamba "bado kuna kazi muhimu ya kufanya," ingawa alisisitiza kuwa Trump anaendelea kujitolea kutafuta suluhisho la kumaliza vita vya Ukraine.
Kauli hiyo inaashiria kwamba, licha ya kuimarika kwa juhudi za kidiplomasia, amani ya haraka nchini Ukraine bado inaonekana kuwa mbali kufikiwa.
Kauli iliyoibua hisia zaidi siku hiyo ilitolewa na mshauri wa sera za kigeni wa Vladimir Putin, Yuri Ushakov, ambaye alishiriki katika mazungumzo yaliyofanyika mjini St Petersburg.
Ushakov alisema kuwa Steve Witkoff alimweleza Putin kuhusu mazungumzo ya Oslo na kile alichokitaja kuwa "mbinu mpya" kutoka kwa mataifa ya Ulaya na Ukraine.
Hata hivyo, kauli zake zilionyesha wazi kuwa Kremlin haikuvutiwa sana na mawazo hayo.
"Kuhusu kutafuta suluhisho la mgogoro wa Ukraine, hakukuwa na mambo mengi ya manufaa," alisema Ushakov.
Baadaye, alipoulizwa na televisheni ya serikali ya Urusi kuhusu uwezekano wa kufikiwa kwa amani, alitoa jibu lililoacha tafsiri mbalimbali.
"Sijui tumekaribia kwa kiwango gani, lakini mambo yanaendelea kusonga katika mwelekeo huo," alisema.
Kauli hiyo ilikuwa ya jumla na isiyoonyesha kwa uwazi hatua iliyofikiwa katika juhudi za kutafuta amani.
Kwa sasa, Putin haonekani kuwa chini ya shinikizo la haraka la kumaliza vita. Anafahamu kuwa uwezo wa ulinzi wa anga wa Ukraine unaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa. Vilevile, anajua kuwa majira ya baridi yanakaribia, hali ambayo huenda anaiona kama fursa ya kuongeza shinikizo dhidi ya Kyiv.
Aidha, Putin anatambua kuwa Ikulu ya White House inaongozwa na rais wa Marekani ambaye ameonyesha nia ya kujenga uhusiano mpana zaidi, wenye manufaa ya kiuchumi na kisiasa, kati ya Washington na Moscow.
Kutokana na hali hiyo, kuna ishara chache zinazoonyesha kuwa Kremlin inaona sababu ya kubadili msimamo wake au kuharakisha mchakato wa kumaliza vita kwa sasa.
Katika siku za karibuni, Donald Trump amesitisha baadhi ya vikwazo dhidi ya Moscow, kuidhinisha ununuzi wa dizeli ya Urusi na kutoa ukosoaji mkali dhidi ya Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky.
Hatua hizo zinaonekana kuipa Urusi nafuu ya kisiasa, kwa kuwa zinapunguza shinikizo lililokuwa likimkabili Rais Vladimir Putin.
"Kwa sasa, Trump ndiye kiongozi pekee wa ulimwengu wa Magharibi anayechukua hatua za kuleta amani," anasema mbunge wa Urusi na mtangazaji wa televisheni, Evgeny Popov.
Nilipomuuliza kama anamaanisha amani kwa masharti ya Urusi, alijibu bila kusita:
"Bila shaka."
Kwa sasa, mkutano wa pande tatu unaoweza kuwakutanisha Putin, Zelensky na Trump hauonekani kuwa karibu kutimia.
Hata hivyo, mwezi ujao nchini China, huenda Putin, Trump na Rais wa China Xi Jinping wakakutana kandokando ya mkutano wa APEC.
Baadhi ya wachambuzi nchini Urusi tayari wameanza kuuita mkutano huo unaowezekana "Yalta Mpya", wakirejelea Mkutano wa Yalta wa mwaka 1945 uliowakutanisha Joseph Stalin, Winston Churchill na Franklin Roosevelt kujadili mustakabali wa Ulaya baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
"Urusi, China na Marekani ndizo nguvu kuu za dunia kwa sasa," anasema Popov. "Bila shaka itakuwa jambo jema kwa dunia nzima ikiwa viongozi wetu watakutana nchini China."
Baada ya karibu miaka mitano ya vita, mkutano wa aina hiyo ungeweza kumrudisha Putin katika nafasi anayoitaka zaidi, ya kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa zaidi katika siasa za dunia.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi