'Tunafikiri bunduki ndiyo inaweza kulinda amani' – Warioba

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Joseph Warioba, amesema matumizi ya nguvu yanaweza kuleta utulivu lakini hayawezi kujenga amani ya kudumu, akitaka nchi hiyo irejee kwenye misingi ya usawa, uadilifu, uwajibikaji na uzalendo.

Warioba ameyasema hayo katika mkutano wa siku mbili ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), unaojadili hali ya kisiasa nchini Tanzania baada ya matukio ya kabla, siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29 yaliyosababisha vifo vya watu 518 na hatua zinazoweza kuchukuliwa kuelekea mageuzi.

Warioba amesema Tanzania bado iko katika hali ya wasiwasi na ina majeraha yanayohitaji kushughulikiwa.

"Nchi yetu bado iko katika hali ya wasiwasi, bado tunaomboleza, bado tuna vidonda. Itabidi tujitatijie turudi kwenye Tanzania ile yenye usawa, amani, uzalendo, uadilifu, uwajibikaji, ukweli."

Warioba ametaja siasa za kibaguzi, ukabila, mpasuko wa kidini na ukanda miongoni mwa mambo anayoyaona yakigawa jamii.

Amesema pia mjadala kuhusu utambulisho wa Tanganyika na Zanzibar umeanza kuwa chanzo kingine cha mgawanyiko.

Kwa upande wa siasa, Warioba amezitaka taasisi na vyama vya siasa kutafuta njia za kuwaunganisha wananchi, akisema matumizi ya nguvu hayawezi kuwa msingi wa amani ya kudumu.

"Kwa sasa tunafikiri bunduki ndiyo inaweza kulinda amani. Inaweza kuleta utulivu lakini hailindi amani."

Amesema vyama vya siasa vina wajibu wa kuhakikisha ushindani wa kisiasa haugeuki kuwa chanzo cha kuwagawa Watanzania.

"Vyama vya siasa lazima vitafute njia ya kuwaunganisha wananchi badala ya kuwagawa. Tukiendelea hivi kuwagawa wananchi, hata utumie risasi ngapi, hutarudisha amani."

Mkutano huo umehudhuriwa na vyama vya siasa kikiwemo Chama tawala cha Mapinduzi, Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mtungi, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Juma Ali Khatib, makundi ya uwakilishi wa vijana, wafanyabiashara pamoja na mabalozi kutoka nchi mbalimbali.

Kwa upande wake Jaji Mtungi amesema ushiriki wa wadau hao unaonyesha dhamira ya kutafuta muafaka kwa maslahi mapana ya taifa, huku kwa upande wake Khatib akisemma: "Yaliyotokea yametokea sote tumeyaona, sote ni watu wazima, hayakutufurahisha, ni wakati wa kukaa Pamoja kama watanzania kujadili namna bora ili yaliyotokea yasitokee tena".

Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Nicola Brennan, amesema uzoefu wa nchi mbalimbali unaonyesha kuwa imani inaweza kujengwa upya na taasisi za kidemokrasia kuimarishwa kupitia mazungumzo na mageuzi.

"Uzoefu kutoka nchi mbalimbali, ikiwemo Ireland, unaonyesha kuwa imani inaweza kujengwa upya na taasisi za kidemokrasia kuimarishwa pale kunapokuwa na dhamira ya kweli ya mazungumzo na mageuzi" anmesema Brennan.

Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Nicole Providoli, yeye amesisitiza mshikamano wa kitaifa kwamba unajengwa pale mitazamo tofauti ndani ya jamii inaposikilizwa na kuzingatiwa.

Kwa mujibu wa waandaaji, TCD imesema mkutano huo ni jukwaa la kutoa mapendekezo kuhusu mabadiliko ya kikatiba, kisheria na kitaasisi.