Taarifa za maelfu ya maafisa wa uhamiaji Marekani zavujishwa baada ya udukuzi

Chanzo cha picha, Reuters
Taarifa za zaidi ya wafanyakazi 41,000 wa Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani (DHS), wakiwemo maelfu ya maafisa wanaotekeleza sheria za uhamiaji, zimevujishwa na kuwekwa hadharani baada ya udukuzi mkubwa.
Taarifa hizo zinajumuisha majina, anwani za kazini na nambari za simu za wafanyakazi wa wizara hiyo, wakiwemo maafisa wa Idara ya Uhamiaji na Forodha (ICE) na Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka (CBP). Pia zinaeleza majukumu yao katika idara husika.
Taarifa hizo zilivujishwa Jumatano, ikiwa ni mara ya tatu katika wiki za hivi karibuni kwa taasisi ya serikali ya Marekani kukumbwa na uvujaji wa taarifa au udukuzi.
Msemaji wa DHS amesema wizara hiyo inafahamu kuhusu uwezekano wa ukiukaji wa usalama wa taarifa na inachukua hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo.
“Tunachukulia kwa uzito vitisho vyote vya usalama vinavyolenga wafanyakazi na maafisa wetu, na tutahakikisha wanalindwa ipasavyo,” alisema msemaji huyo, akiongeza kuwa umma utaarifiwa zaidi taarifa zitakapopatikana.
Uvujaji huo ulitangazwa kupitia mtandao baada ya kundi linalojiita Department of Peace kupata taarifa hizo kutoka kwa DHS.
Mtafiti wa usalama wa mtandao na mwanahabari Maia Crimew, kwa kushirikiana na tovuti ya Distributed Denial of Secrets, waliweka taarifa hizo hadharani.
Taarifa hizo ziliwekwa katika hifadhidata iliyopewa jina la Icepick.























