Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Urusi na Ukraine zakubaliana kusitisha mashambulizi ya nishati - Trump

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump amesema makubaliano hayo yanaanza kutekelezwa mara moja, akizitaka pande zote mbili kuyaheshimu na kutoyakiuka.

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu

  1. Trump: Urusi na Ukraine zakubaliana kusitisha mashambulizi ya nishati

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Urusi na Ukraine zimekubaliana kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati, lakini Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema tangazo hilo limekuwa jipya kwake.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump amesema makubaliano hayo yanaanza kutekelezwa mara moja, akizitaka pande zote mbili kuyaheshimu na kutoyakiuka. Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi kuhusu jinsi makubaliano hayo yalivyofikiwa.

    Urusi ilikuwa bado haijatoa tamko kuhusu tangazo hilo, huku Zelensky akiripotiwa kuliambia shirika la habari la Marekani, Axios, kuwa ni kitu kipya kwake, hakijui. Awali, kiongozi huyo wa Ukraine alisema nchi yake ilikuwa tayari kusitisha mashambulizi dhidi ya viwanda vya kusafisha mafuta nchini Urusi iwapo Moscow nayo itasitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine.

    Tangazo hilo linakuja baada ya mvutano kuongezeka kati ya Trump na Zelensky, ambapo siku ya Jumamosi rais wa Marekani aliitaka Ukraine kusitisha mashambulizi dhidi ya viwanda vya mafuta vya Urusi. Trump pia alipendekeza kuwa Ukraine inapaswa kuwa na rais mwingine anayeweza kufikia makubaliano ya kumaliza vita.

    Urusi na Ukraine zimekuwa zikiongeza mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati katika miezi ya hivi karibuni, wakati vita vinavyoendelea tangu uvamizi mkubwa wa Urusi nchini Ukraine mwaka 2022 vikiingia mwaka wake wa tano. Ikiwa itatekelezwa na kuheshimiwa na pande zote mbili, hatua hiyo inaweza kupunguza uharibifu wa miundombinu muhimu ya nishati.

  2. Mabango yatawala Anfield Man City ikizodolewa na mashabiki

    Mechi ya Liverpool vs Manchester City ikienda kuanza, uwanja wa Anfield umetawaliwa na mabango kuelezea kilichofanywa na City kuhusu ukiukwaji wa kanuni za kifedha kama mamlaka za soka England zilivyothibitisha.

    Mabango mengi ni kuisema Klabu hiyo kwu danganyifu. Sakata la Man City kukutwa na hatia ya kukiuka kanuni za kifedha za Ligi Kuu England kunazidisha mvutano kati ya klabu hizo.

  3. Kipchoge, 41, aweka rekodi mpya ya mbio za Melbourne

    Bingwa mara mbili wa Olimpiki, Eliud Kipchoge wa Kenya, ameweka rekodi mpya ya muda katika mbio za marathon za Melbourne, Australia, baada ya kushinda mbio hizo akiwa na umri wa miaka 41. Kipchoge amemaliza mbio hizo kwa saa 2, dakika 9 na sekunde 10.

    Ushindi huo ni wa 17 katika mbio za marathon kwa mwanariadha huyo na wa kwanza tangu aliposhinda marathon ya Berlin mwaka 2023. Kipchoge amesema bado ana uwezo wa kushindana na wanariadha wa kizazi kipya licha ya umri wake kumtupa mkono.

    “Ninaamini mwili wangu bado uko vizuri na nina uwezo wa kushindana na kizazi kijacho,” amesema Kipchoge, akiongeza kuwa anafurahia kushindana na wanariadha vijana.

    Mbio hizo zilipita sehemu ya uwanja wa mashindano ya magari ya Formula One, Albert Park, kabla ya kumalizikia katika uwanja maarufu wa Melbourne Cricket Ground (MCG). Kipchoge amesema alifurahia kuona mashabiki wakimshangilia na kutaja uzoefu huo kuwa wa kipekee.

    Mwanariadha wa Australia, Thomas do Canto, alimaliza katika nafasi ya pili kwa muda wa saa 2, dakika 10 na sekunde 35, huku mwenzake Reece Edwards akishika nafasi ya tatu. Kwa upande wa wanawake, Camille French wa New Zealand alishinda baada ya kutumia saa 2, dakika 28 na sekunde 25.

    Ushindi huo ni sehemu ya ziara ya Kipchoge inayolenga kukimbia mbio ndefu (marathon) katika mabara yote saba ya dunia, likiwemo Antaktika, ndani ya miaka miwili. Fedha zitakazopatikana zitaelekezwa katika taasisi yake inayojihusisha na elimu, utunzaji wa mazingira na afya. Kipchoge ni miongoni mwa wanariadha bora wa mbio ndefu duniani, akiwa na medali mbili za dhahabu za Olimpiki katika marathon na rekodi nyingi katika mchezo huo.

  4. Baada ya kukutwa na hatia ukiukaji wa fedha, Man City kumalizia hasira zake Anfield?

    Manchester City inatarajiwa kukabiliwa na mapokezi ya hasira na makali kutoka kwa mashabiki wa Liverpool itakapokutana na wapinzani wake hao kwenye uwanja wa Anfield jioni hii.

    Sakata la Man City kukutwa na hatia ya kukiuka kanuni za kifedha za Ligi Kuu England kunazidisha mvutano kati ya klabu hizo. Mechi hiyo itaanza saa 12:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki (6:30pm).

    Mvutano huo unatokana na ushindani wa muda mrefu kati ya klabu hizo, hasa baada ya Liverpool kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Manchester City katika misimu ya 2013-14, 2018-19 na 2021-22. Katika misimu miwili ya mwisho ya ushindani wao, Liverpool ilipoteza ubingwa kwa tofauti ya alama moja, hali iliyozidisha hisia za mashabiki wake kuwa klabu yao ilinyimwa nafasi ya kutwaa mataji hayo.

    Manchester City imekutwa na hatia ya kukiuka kanuni za kifedha katika kipindi cha mwaka 2009 hadi 2018, lakini klabu hiyo imekata rufaa dhidi ya uamuzi huo na inaendelea kusisitiza kuwa haina hatia. Wakati huo huo, mustakabali wake unasubiriwa huku uwezekano wa adhabu kubwa, ikiwemo kukatwa alama au kushushwa daraja, ukitajwa.

    Hali hiyo imezua maswali kuhusu uhalali wa matokeo ya msimu huu, hasa kwa kuwa City inaongoza msimamo wa ligi. Adhabu itakayotolewa inaweza kuwa na athari kubwa kwa mbio za ubingwa na historia ya mashindano hayo, ingawa bado hakuna uamuzi wa mwisho kuhusu aina ya adhabu itakayotekelezwa.

    Kocha wa Manchester City, Enzo Maresca, amesema ana imani na uongozi wa klabu hiyo na anataka wachezaji wake waelekeze nguvu zao kwenye mchezo. Hata hivyo, aliyekuwa mshambuliaji wa England, Alan Shearer, amesema kuchelewa kutolewa kwa uamuzi kuhusu adhabu kunaharibu taswira ya ligi na kuongeza kuwa suala hilo ni miongoni mwa matukio makubwa zaidi katika historia ya mashindano hayo.

  5. Watu 109 wafariki dunia boti ikizama pwani ya Djibouti

    Wahamiaji wasiopungua 109, wakiwemo watoto 15, wamefariki dunia huku wengine 116 wakiripotiwa kupotea baada ya boti iliyokuwa imebeba watu 350 kuzama katika pwani ya Djibouti wakielekea Yemen, Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limesema.

    Tukio hilo lilitokea usiku wa Oktoba 8 hadi 9 kaskazini mwa mji wa Obock, Djibouti, baada ya boti hiyo kupinduka ikiwa njiani kuvuka Mlango-Bahari wa Bab el-Mandeb kuelekea Yemen.

    Kwa mujibu wa taarifa ya IOM iliyotolewa Jumapili, Oktoba 11, zaidi ya watu 80 walinusurika katika ajali hiyo. Wote walionusurika ni raia wa Ethiopia, ambao walikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakisafiri kwa boti hiyo.

    Miongoni mwa miili 109 iliyopatikana ni ya wanaume 52, wanawake 42 na watoto 15, wakiwemo wasichana tisa na wavulana sita. Timu za IOM zinafanya kazi pamoja na mamlaka za Djibouti kutoa msaada wa dharura kwa manusura.

    Mkuu wa IOM nchini Djibouti, Alexandre Coissac, amesema tukio hilo ni pigo kubwa na kueleza kuwa shirika hilo linawapa pole manusura pamoja na familia zilizopoteza wapendwa wao au ambazo bado hazijapata taarifa za ndugu zao.

    IOM imesema umaskini, ukosefu wa usalama na athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa sababu zinazowasukuma wahamiaji kuhatarisha maisha yao katika safari hiyo, wakitafuta fursa za kiuchumi katika nchi za Ghuba kupitia Yemen, licha ya kuongezeka kwa machafuko huko Mashariki ya Kati.

  6. Mfungwa aliyenusurika majaribio mawili ya kutekeleza hukumu ya kifo atoka hospitalini

    Christa Pike, raia wa Marekani aliyenusurika jaribio la kunyongwa kwa sindano ya sumu, ameruhusiwa kutoka hospitalini na kurejeshwa gerezani siku 10 baada ya zoezi hilo lililofeli, kwa mujibu wa taarifa ya mawakili wake.

    Pike, mwenye umri wa miaka 50, alidungwa sindano ya dawa ya pentobarbital mara mbili Septemba 30, katika jaribio la kutekeleza hukumu yake ya kifo katika jimbo la Tennessee. Zoezi hilo lilimuacha katika hali mahututi.

    Mawakili wake wamesema Pike amerejea katika gereza alilokuwa akishikiliwa kwa takribani miaka 30 na ataendelea kupata huduma za matibabu. Hata hivyo, haijafahamika ni matibabu gani anayoendelea kupatiwa gerezani.

    Pike alipata fahamu Jumanne na kuanza kuzungumza tena, jambo lililowashangaza wataalamu wa afya na mawakili wake. Wakili wake, Randy Spivey, amesema maneno yake ya kwanza yalikuwa, “Niko wapi?” na “Wewe ni nani?”

    Kwa mujibu wa mawakili wake, Pike alikuwa na matatizo ya kiafya yaliyohusisha nimonia na kuvimba kwa mikono. Pia alisema alikuwa na hasira na kuchanganyikiwa, huku athari za muda mrefu za tukio hilo zikiwa bado hazijafahamika.

    Pike alihukumiwa kifo kwa kushiriki katika mateso na mauaji ya Colleen Slemmer, mwenye umri wa miaka 19, mwaka 1995, akiwa na aliyekuwa mpenzi wake, Tadaryl Shipp. Mawakili wake sasa wanataka hukumu hiyo ibadilishwe kuwa kifungo cha maisha. Hadi sasa, mamlaka za Tennessee hazijaeleza kwa nini jaribio la kutekeleza hukumu hiyo lilishindwa na kama zitajaribu tena kumnyonga.

  7. Jumuia za kimataifa zalaani shambulio la Houthi katika uwanja wa ndege Riyadh

    Nchi mbalimbali pamoja na Umoja wa Mataifa zimelaani shambulizi la waasi wa Houthi nchini Yemen katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Riyadh, Saudi Arabia, lililosababisha vifo vya watu wasiopungua 12 na kujeruhi zaidi ya 300.

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amelitaja shambulizi hilo kuwa baya sana, akisema nchi yake inatathmini uwezekano wa kujiunga na Saudi Arabia katika operesheni za kijeshi dhidi ya waasi hao. Trump pia amesema anatarajia kuzungumza na kiongozi mkuu wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman.

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amelilaani shambulizi hilo na kusema mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia yanakiuka sheria za kimataifa na yanapaswa kusitishwa mara moja.

    Nchi nyingine zilizolaani shambulizi hilo ni pamoja na Misri, Qatar, Pakistan, Jordan, Oman, Palestina na Syria, huku zikionya kuwa mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu muhimu yanatishia amani na usalama wa eneo hilo.

    Ni shambulio la tatu kufanywa katika Uwanja huo ndani ya wiki moja.

  8. Waasi wa Houthi waonya matumizi ya viwanja vya ndege Saudi Arabia

    Msemaji wa waasi wa Houthi nchini Yemen, Yahya Saree, amezionya kampuni za usafirishaji wa mizigo baharini, mashirika ya ndege, wafanyakazi na wasafiri dhidi ya kutumia viwanja vya ndege na anga la Saudi Arabia, akisema maeneo hayo yako katika hatari ya kushambuliwa.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Saree amesema viwanja hivyo vya ndege viko katika maeneo yanayoweza kulengwa na mashambulizi ya vikosi vyao.

    Hata hivyo, amesema viwanja vya ndege vya Macca na Madina havitalengwa na mashambulizi hayo.

    Kauli hiyo inakuja wakati mvutano na mashambulizi kati ya waasi wa Houthi na Saudi Arabia yakiongezeka, hali inayozua wasiwasi kuhusu usalama wa safari za ndege na usafiri wa kimataifa katika eneo hilo.

    Watu 12 wameuawa na wengine zaidi ya 300 kujeruhiwa katika shambulio lilifanyika jana Jumamosi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa King Khalid, mjini Riyadh.

  9. Tetesi za soka Ulaya: Liverpool yamtaka Kounde, Chelsea yamfuatilia Camara

    Liverpool inatajwa kuwa na nia ya kumsajili beki wa Barcelona na timu ya taifa ya Ufaransa, Jules Kounde, huku klabu hiyo ya Hispania ikiripotiwa kuwa tayari kupokea ofa ya pauni milioni 60 kwa mchezaji huyo. (Fichajes - kwa Kihispania)

    Chelsea bado inamtaka kiungo wa Monaco na timu ya taifa ya Senegal, Lamine Camara, mwenye umri wa miaka 22, baada ya kushindwa kumsajili katika dirisha la majira ya kiangazi. Hata hivyo, Chelsea haiko tayari kulipa euro milioni 70 (pauni milioni 59) zinazotakiwa na Monaco kwa ajili ya mchezaji huyo. (Goal)

    Liverpool pia inatajwa kuwa na nia ya kumsajili mshambuliaji wa Brazil, William Gomes, mwenye umri wa miaka 20, anayekipiga Porto. Klabu hiyo ya Ureno imeongeza kipengele cha kuvunja mkataba wa mchezaji huyo hadi euro milioni 100 (pauni milioni 85), huku Liverpool ikionyesha nia ya kumsajili. (A Bola - kwa Kireno)

    AC Milan bado inamfuatilia kiungo wa Bournemouth, Alex Scott, mwenye umri wa miaka 23, licha ya thamani yake kuongezeka. Scott, ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya England, anaendelea kuvutia klabu hiyo ya Italia. (Tuttomercatoweb - kwa Kiitaliano)

    Bayern Munich imefanya mazungumzo mapya kuhusu uwezekano wa kumsajili kiungo mshambuliaji wa Manchester United, JJ Gabriel, mwenye umri wa miaka 16, lakini bado haijatoa ofa. Hata hivyo, Barcelona na Real Madrid zinaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kumsajili kijana huyo, ambaye anadaiwa kuvutiwa zaidi na uwezekano wa kuhamia Hispania. (Sky Sports Germany)

    Manchester City ilifanya mawasiliano na Borussia Dortmund katika dirisha la majira ya kiangazi kuhusu uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Marekani, Mathis Albert, mwenye umri wa miaka 17. (Goal)

  10. Trump: Tutafanya uamuzi haraka kuhusu kuishambulia Yemen

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema anafikiria uwezekano wa nchi yake kujiunga na Saudi Arabia katika mashambulizi dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen, baada ya shambulizi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa King Khalid, mjini Riyadh, kuua watu wasiopungua 12 na kujeruhi wengine 309.

    Trump amesema Marekani itafanya uamuzi huo haraka, akieleza kuwa utawala wake ulikuwa umepata taarifa kuhusu shambulizi hilo muda mfupi kabla ya kutoa kauli hiyo. Miongoni mwa waliouawa ni raia mmoja wa Marekani.

    Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Saudi Arabia imesema waliouawa pia ni pamoja na raia wanne wa Saudi Arabia, Wabangladeshi wawili na raia mmoja mmoja wa Misri, Jordan, Syria, Palestina na Sudan. Baadhi ya waliojeruhiwa wako katika hali mbaya.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imelaani shambulizi hilo, ikiwatuhumu waasi wa Houthi kuishambulia Saudi Arabia. Hata hivyo, waasi hao hawajathibitisha kuhusika na shambulizi la Jumamosi, licha ya kudai kuhusika na mashambulizi mengine ya awali dhidi ya uwanja huo.

    Shambulizi hilo limefanyika wakati mapigano kati ya waasi wa Houthi na vikosi vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia nchini Yemen yakizidi kushika kasi. Mamlaka za Saudi Arabia zimesimamisha shughuli za uwanja huo wa ndege, huku mamia ya safari za ndege zikifutwa au kuelekezwa kwenye viwanja vingine.