Kwa nini Marekani inaanza tena kutekeleza hukumu za kifo hadharani?

    • Author, Sheila Flynn
    • Nafasi, Mwandishi Mwandamizi wa Marekani
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Maelfu ya watu walifurika kutoka sehemu mbalimbali kushuhudia tukio hilo. Wanaume, wanawake na watoto walikusanyika kandokando ya mto mjini Owensboro, katika jimbo la Kentucky, kuhudhuria kunyongwa hadharani kwa mwanamume mweusi aliyepatikana na hatia ya kumbaka na kumuua mjane wa Kizungu mwenye umri wa miaka 70.

Ilikuwa Agosti 14, 1936, siku ya Ijumaa yenye joto kali wakati Marekani ikikabiliwa na moja ya mawimbi mabaya zaidi ya joto katika historia yake. Baadhi ya watu walikesha karibu na jukwaa la kunyongwa ili kupata nafasi nzuri ya kushuhudia tukio hilo, huku wengine wakifanya sherehe usiku uliotangulia. Wakati huohuo, vijana walizunguka wakiuza bisi na vinywaji kwa umati wa watazamaji.

Ilipofika saa 11 alfajiri, muda uliopangwa wa utekelezaji wa hukumu hiyo, idadi ya watu waliokusanyika ilikuwa imeongezeka na kufikia takribani 20,000.

Ndipo Rainey Bethea, kijana yatima mwenye umri wa miaka zaidi ya 20, alipandishwa kwenye jukwaa la kunyongwa. Alikuwa amehukumiwa adhabu ya kifo baada ya kukiri, kwa mujibu wa mamlaka, kuhusika katika wizi, ubakaji na mauaji ya Lischia Edwards, mjane mwenye umri wa miaka 70.

Mchana wa siku iliyotangulia kunyongwa kwake, Bethea alipewa mlo wake wa mwisho uliokuwa na kuku wa kukaanga, vipande vya nyama ya nguruwe, viazi vilivyopondwa, matango ya siki, mkate wa mahindi, pai ya limau na aiskrimu.

Wengi wa waliohudhuria, wakiwemo waandishi wa habari kutoka miji ya mbali kama Chicago na New York, walifika kushuhudia kile kilichokuwa kikitajwa kuwa tukio la kwanza la "mwanamke kusimamia utekelezaji wa hukumu ya kifo". Miezi minne kabla ya tukio hilo, sheriff wa eneo hilo alikuwa amefariki dunia, na mjane wake akachukua nafasi yake kwa muda.

Hata hivyo, licha ya matarajio ya wengi, mjane huyo alikataa kuvuta kifaa kilichotekeleza hukumu hiyo, na jukumu hilo likafanywa na watekelezaji wa adhabu ya kifo walioajiriwa rasmi.

Tukio hilo la kunyongwa kwa Bethea lilihitimisha enzi ya adhabu za kifo hadharani zilizovutia umati mkubwa nchini Marekani. Maonesho na shamrashamra zilizolizunguka tukio hilo ziliwafanya wengi nchini Kentucky kuliona kama fedheha, na miezi 18 baadaye gavana wa jimbo hilo alipiga marufuku utekelezaji wa hukumu za kifo hadharani.

Kufikia wakati huo, majimbo mengi ya Marekani yalikuwa tayari yameondoa utekelezaji wa adhabu ya kifo hadharani, huku mitazamo ya jamii ikibadilika na kuelekea mbinu zilizochukuliwa kuwa za staha zaidi na zinazotekelezwa faraghani.

Japo kulikuwa na tukio jingine la kunyongwa lililoshuhudiwa na mamia ya watu katika jimbo la Missouri mwaka 1937, halikupata umaarufu mkubwa. Hilo ndilo lililokuwa utekelezaji wa mwisho wa hukumu ya kifo hadharani nchini Marekani, hadi sasa ambapo mjadala kuhusu kurejeshwa kwake umeibuka upya.

Zaidi ya miaka 90 baada ya kunyongwa kwa Rainey Bethea, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, alitangaza kuwa jeshi la Marekani litatekeleza hadharani hukumu ya kifo dhidi ya Nidal Hasan, mwanajeshi wa zamani aliyewaua wanajeshi 13 wasio na silaha katika kambi ya kijeshi ya Fort Hood, Texas, mwaka 2009.

Baadaye, Pentagon ilifafanua kuwa hukumu hiyo itatekelezwa kwa mhukumiwa kumiminiwa risasi na itatiririshwa mubashara mtandaoni.

"Watu wanapaswa kuelewa kwamba vitendo vya aina hii vina madhara makubwa," alisema Hegseth.

Tangazo hilo limezua mjadala mkubwa na kuwashangaza wataalamu wa masuala ya adhabu ya kifo. Profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Colorado, Michael Radelet, ambaye amefanya tafiti kuhusu adhabu ya kifo kwa miongo kadhaa, alisema hajawahi kufikiria kuwa Marekani ingerudia utekelezaji wa hukumu ya kifo hadharani.

Alisema uungwaji mkono wa adhabu ya kifo nchini Marekani umekuwa ukipungua kwa miaka mingi. Kiwango hicho kilikuwa asilimia 80 mwaka 1994, lakini sasa kimeshuka hadi asilimia 52, hasa wananchi wanapopewa mbadala wa kifungo cha maisha bila uwezekano wa kuachiliwa huru.

Ingawa bado ni mapema kuelewa kikamilifu mtazamo wa Wamarekani kuhusu kurushwa mubashara kwa utekelezaji wa hukumu za kifo, kuna uwezekano mkubwa kwamba mamilioni ya watu watafuatilia tukio hilo.

Akikosoa hatua hiyo, Radelet alisema kuwa inaweza kuigeuza adhabu ya kifo kutoka chombo cha utoaji haki na kuwa tamasha la umma.

"Adhabu ya kifo inageuzwa kuwa tamasha la burudani. Chukueni vitafunwa vyenu na waalikeni marafiki zenu," alisema.

Mwandishi Sonya Lea, ambaye mwaka jana alichapisha kitabu kuhusu kunyongwa kwa Rainey Bethea, alisema alishtushwa na tangazo la kurushwa mubashara kwa utekelezaji wa hukumu ya kifo dhidi ya Nidal Hasan.

"Mwaka 1936, tukio hilo liligeuzwa tamasha la ukatili. Leo, teknolojia inaweza kulifikisha kwa mamilioni ya watu, jambo linalolifanya kuwa la kutisha zaidi," alisema Lea.

Lea alisema babu na bibi yake walikuwa miongoni mwa maelfu ya watu waliohudhuria kunyongwa kwa Bethea mwaka 1936. Alibaini hilo baada ya kifo cha bibi yake mwaka 2002, aliposoma simulizi aliloacha likieleza kwamba walikuwa karibu kiasi cha kusikia sauti ya shingo ya Bethea ilipovunjika.

Baada ya kufanya utafiti kwa miaka kadhaa, Lea alisema wengi wa wakazi wa Kentucky waliendelea kuathiriwa na kumbukumbu za tukio hilo hata miaka mingi baadaye.

"Niliamini tulikuwa tumeifunga kabisa sura hii ya ukatili. Inatisha kuona Marekani ikirejea mjadala wa aina hii," alisema.

Kwa upande wake, Profesa wa Saikolojia ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Ohio State, Kurt Gray, alisema hali ya mgawanyiko wa kisiasa nchini Marekani huenda imechangia mazingira yaliyowezesha tangazo hilo kutolewa.

"Huenda baadhi ya Wamarekani wanaunga mkono hatua kama hizi, lakini wengi hawafanyi hivyo. Wengine wamezoea kiasi kwamba mambo haya hayawashtui tena," alisema.

Gray aliongeza kwamba badala ya kushangilia utekelezaji wa hukumu za kifo hadharani, baadhi ya wananchi wanaonekana kuupokea kama jambo la kawaida.

"Si kwamba wanaushangilia, bali wengi wanahisi ni hali mpya ya kawaida," alisema.

Utafiti mwingine unaonyesha kuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, na utawala wa Rais Donald Trump huenda hauwakilishi mtazamo wa Wamarekani wengi kuhusu kurejeshwa kwa utekelezaji wa hukumu ya kifo hadharani.

Garen Wintemute, mkurugenzi wa Mpango wa Utafiti wa Kuzuia Vurugu katika Chuo Kikuu cha California, Berkeley, alisema kura za maoni zinaonyesha kuwa uungwaji mkono wa matumizi ya nguvu na adhabu kali umekuwa ukipungua nchini humo.

"Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki la Marekani ametaja hatua hii kuwa ya kinyama. Naamini kauli hiyo inawakilisha hisia za Wamarekani wengi," alisema Wintemute.

Kulingana na yeye, kurejea kwa utekelezaji wa hukumu ya kifo hadharani kunakinzana na maadili na mwelekeo ambao Marekani imekuwa ikiujenga kwa miongo kadhaa.

"Utekelezaji wa hukumu ya kifo hadharani si sehemu ya utambulisho wetu," alisema.

Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, ambaye ni Mkatoliki, amesema hatafuatilia matangazo ya moja kwa moja ya utekelezaji wa hukumu hiyo.

Kwa upande wake, Rais Donald Trump alikwepa kujibu ikiwa atafuatilia utekelezaji huo, lakini alithibitisha kwamba ameidhinisha uamuzi wa kuurusha mubashara.

"Sijali namna hukumu hiyo itakavyotekelezwa, mradi tu itekelezwe. Ninaamini adhabu ya kifo ndiyo adhabu anayostahili," alisema Trump.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi