'Utekelezaji wa hukumu ya kifo ya Christa Pike uliotibuka: Nini nilitokea na nini kinafuata?"

    • Author, James FitzGerald
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Muuaji Mmarekani aliyepatikana na hatia, Christa Pike, amelazwa hospitalini na anapatiwa matibabu ya uangalizi maalumu baada ya jaribio la kumuua kwa sindano yenye sumu lililofanywa na mamlaka za Tennessee kushindikana.

Kesi ya Pike, ambaye jaribio lake la kunyongwa lilikuwa tayari limeibua mzozo mkubwa wa kisheria, imezua maswali kadhaa.

Maswali hayo ni pamoja na nini kilikwenda vibaya, nini kitafuata, na kwa wapinzani wa hukumu ya kifo – wasiwasi mpya kuhusu mateso anayoweza kuyapata mfungwa pale utekelezaji wa hukumu ya kifo unaposhindikana.

Nini kilitokea?

Pike, mwenye umri wa miaka 50, alihukumiwa kifo mwaka 1996 kwa kumuua Colleen Slemmer, mwenye umri wa miaka 19. Mauaji hayo yalifanywa pamoja na mpenzi wake wa wakati huo, Tadaryl Shipp.

Utekelezaji wa hukumu yake ya kifo ulipangwa kufanyika Jumatano jioni, kwa saa za eneo hilo. Sindano hizo ziliidhinishwa na Mahakama ya Juu ya Marekani dakika za mwisho, baada ya mvutano mkali wa kisheria.

Pike alidungwa sindano mbili za pentobarbital, lakini mawakili wake walisema sindano hizo zilishindwa kusimamisha mapigo ya moyo wake na bado aliweza kusikika akikoroma.

Idara ya Magereza ya Tennessee ilitetea utaratibu huo na kusema: "Itifaki haitoi utaratibu mwingine wowote wa ziada zaidi ya ule uliotekelezwa jioni hii."

Itifaki ya serikali haielezi kwa uwazi nini kinapaswa kufanyika iwapo mfungwa ataendelea kuwa hai baada ya kupewa dozi ya pili, kwa mujibu wa shirika la habari la AP.

Mamlaka bado hazijatoa maelezo kuhusu kwa nini dozi aliyopewa Pike haikusababisha kifo, ingawa wataalamu wa tiba wametoa nadharia zao.

Dkt. Joel Zivot, profesa katika shule ya tiba ya Chuo Kikuu cha Emory, ambaye aliiambia BBC kwamba aliajiriwa na timu ya mawakili wa Pike kama mtaalamu wa tiba, alisema huenda kiwango cha pentobarbital katika damu yake hakikufikia kiwango cha kutosha kusababisha kushindwa kupumua na moyo kusimama.

Mauaji ya kikatili

Pike alikuwa na umri wa miaka 18 mwaka 1995 alipompiga na kumtesa hadi kumuua Colleen Slemmer, mwenye umri wa miaka 19, pamoja na mpenzi wake wa wakati huo, Tadaryl Shipp. Walikutana katika kambi ya mafunzo ya kazi kwa vijana waliokuwa na changamoto za kitabia.

Mauaji hayo yalisababisha taharuki kubwa kwenye vyombo vya habari mjini Knoxville, Tennessee, baada ya Colleen kupatikana ameuawa huku alama ya pentagramu — ishara inayohusishwa na ibada za kishetani — ikiwa imechongwa kifuani mwake.

Pike alimtuhumu Colleen kwa kumtukana na kujaribu kumpora mpenzi wake. Wakazi wengine wawili wa kambi hiyo baadaye walitoa ushahidi kwamba Pike alikuwa amejigamba kuhusu mauaji hayo kabla na baada ya kutokea, na kwamba aliwaonyesha kipande cha fuvu la Colleen.

Mwaka mmoja baadaye, Pike alihukumiwa kifo, huku Shipp, ambaye alikuwa na umri wa miaka 17 wakati wa mauaji hayo, akihukumiwa kifungo cha maisha jela akiwa na uwezekano wa kuomba kuachiwa kwa msamaha.

Baada ya miaka kadhaa ya rufaa zilizoshindikana, tarehe ya kutekelezwa kwa hukumu ya kifo ya Pike iliwekwa kuwa Jumatano wiki hii.

Iwapo angekufa baada ya kudungwa sindano hizo, angekuwa mwanamke wa kwanza kuuawa kwa hukumu ya kifo katika Tennessee katika kipindi cha zaidi ya miaka 200. Tangu miaka ya 1970, ni wanawake 18 pekee waliotekelezewa hukumu ya kifo nchini Marekani, ikilinganishwa na wanaume 1,663.

Mama wa Colleen alisema alitaka Pike auawe ili binti yake aweze "kupumzika kwa amani hatimaye."

Kabla ya Mahakama ya Juu ya Marekani kutoa idhini yake ya mwisho, mahakama ya rufaa ilisimamisha utekelezaji wa hukumu hiyo. Katika kikao kilichopelekea uamuzi huo, mawakili wa Pike walidai kwamba kwa miaka kadhaa, jimbo la Tennessee lilikuwa limeeleza mahakamani kwamba Pike alikuwa amelidanganya kuhusu madai ya kunyanyaswa kingono alipokuwa mtoto.

Hata hivyo, katika kikao cha hivi karibuni kuhusu njia ya kutekeleza hukumu hiyo, wawakilishi wa serikali walisema hawakupinga ukweli kwamba Pike alikuwa amenyanyaswa kingono na kubakwa.

Kutokana na hilo, timu ya mawakili wa Pike iliomba mahakama ya rufaa iirudishe kesi yake katika mahakama ya wilaya, wakidai kwamba iwapo mahakama za shirikisho zilitumia madai kwamba alikuwa anadanganya kama msingi wa uamuzi wao, basi mchakato wa mapitio ya kesi yake katika mahakama za shirikisho ungekuwa umeathiriwa.

Nini kitafuata?

Idara ya Magereza ya Tennessee ilisema Pike amepelekwa katika kituo cha matibabu cha nje.

Mmoja wa mawakili wake alisema anapatiwa matibabu ya kuokoa maisha hospitalini.

Hali yake ya kiafya bado haikujulikana kwa uhakika kufikia Alhamisi asubuhi.

Katika maoni aliyotuma kwa barua pepe kwa BBC, Dk Zivot alisema: "Kuna uwezekano mkubwa kwamba kutokana na kuchelewa kuanza kumsaidia kurejesha hali ya kawaida ya mwili, amepata madhara kwenye ubongo."

Gavana wa Tennessee, Bill Lee, aliamuru uchunguzi ufanywe na taasisi huru na pia akasema utekelezaji wa mwisho wa hukumu ya kifo uliopangwa kufanyika mwaka huu hautafanyika kama ilivyopangwa.

May Martinez, mama wa Colleen Slemmer ambaye alikuwa akifanya kampeni ya kutaka Pike auawe, aliiambia NBC News kwamba yaliyotokea yalikuwa "vurugu kabisa."

Wapinzani wa hukumu ya kifo nao walitoa maoni yao haraka.

Maya Foa, mkurugenzi mtendaji wa shirika la kimataifa la kisheria Reprieve, alisema: "Hatuwezi kujua kwa uhakika kilichokwenda vibaya, kwa sababu mambo mengi yalitokea bila kujulikana hadharani – sindano ya sumu hutegemea usiri katika kila hatua, ili kuficha ukatili wa serikali unaochukua maisha ya binadamu."

Mamlaka bado hazijaeleza iwapo zitajaribu tena kumuua Pike. Kuna historia ya mamlaka kutekeleza mara ya pili hukumu ya kifo kwa mfungwa wa hukumu ya kifo.

Shipp, ambaye alikuwa mpenzi wa Pike na mshtakiwa mwenza katika kesi hiyo, bado yuko gerezani baada ya kuokolewa dhidi ya hukumu ya kifo chini ya sheria za jimbo hilo. Alikuwa na umri wa miaka 17 wakati Slemmer alipouawa.

Pentobarbital ni nini?

Pentobarbital ni dawa kali ya kutuliza ambayo hupunguza shughuli za mwili, hasa mfumo wa neva. Madaktari wakati mwingine huitumia kutibu baadhi ya hali za kiafya, lakini kwa kiwango kikubwa inaweza pia kutumika kusababisha kifo kupitia sindano yenye sumu.

Matumizi yake katika utekelezaji wa hukumu za kifo yaliangaziwa zaidi mwaka jana baada ya utafiti wa serikali ya Marekani – uliofanywa wakati wa utawala wa Rais Joe Biden – kuibua wasiwasi kuhusu uwezekano wa dawa hiyo kusababisha "maumivu na mateso yasiyo ya lazima."

Serikali yake ilipiga marufuku matumizi ya dawa hiyo katika utekelezaji wa hukumu za kifo za serikali ya shirikisho, lakini marufuku hiyo haikuzifunga majimbo binafsi kama Tennessee, ambayo yanaweza kuchagua njia zao za utekelezaji.

Katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya majimbo yamekabiliwa na ugumu unaoongezeka wa kupata dawa zinazohitajika kwa ajili ya sindano za kutekeleza hukumu za kifo, baada ya kampuni za dawa kupinga matumizi ya bidhaa zao kwa madhumuni hayo.

Idara ya Magereza ya Tennessee haikujibu moja kwa moja madai ya timu ya mawakili wa Pike kwamba pentobarbital iliyotumika ilikuwa "imeharibika." Dawa zinaweza kuharibika kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kupita muda wake wa matumizi na hivyo kupoteza ufanisi.

Idara hiyo ilitoa utetezi mpana wa utaratibu wake na kusema: "Kemikali inayotumika kwa sindano ya sumu katika itifaki hiyo imethibitisha mara kwa mara kuwa inafanya kazi kwa ufanisi."

Je, hili limewahi kutokea?

Jaribio la kumuua Pike halikuwa la kwanza kwenda kombo huko Tennessee.

Utekelezaji wa hukumu ya kifo ya Tony Carruthers, aliyepatikana na hatia ya kuwateka nyara na kuwaua watu watatu mwaka 1994, uliahirishwa mwezi Mei baada ya wahudumu wa afya kushindwa kupata mshipa wa kumpa sindano yenye sumu. Alipewa muda wa mwaka mmoja wa kusitishiwa utekelezaji huo na Gavana Bill Lee.

Kwa upana zaidi nchini Marekani, suala la utekelezaji wa hukumu za kifo unaokwenda kombo linaendelea kuzua wasiwasi.

Mwaka 2022, zaidi ya theluthi moja ya utekelezaji wa hukumu za kifo nchini Marekani ulikuwa na hitilafu au ulikumbwa na matatizo makubwa, kwa mujibu wa Death Penalty Information Center (DPI) – shirika linalotoa takwimu na tafiti kuhusu hukumu ya kifo lakini halichukui msimamo wa kimaadili kuhusu suala hilo.

DPI inasema sindano yenye sumu ndiyo njia ya utekelezaji wa hukumu ya kifo yenye kiwango cha juu zaidi cha kushindikana.

Tukio lililotokea Oklahoma mwaka 2014 limepewa uzito mkubwa. Utekelezaji wa hukumu ya kifo wa Clayton Lockett ulisitishwa baada ya dakika 20 kufuatia kushindwa kufanya kazi ipasavyo kwa sindano iliyokuwa na dawa tatu: mmoja wa mishipa yake ulipasuka na alianza kujikunyata na kutetemeka bila kudhibitiwa.

Nchini Marekani, majimbo 27 kati ya 50 yana hukumu ya kifo kama adhabu inayoruhusiwa kisheria. Serikali ya shirikisho pia inaweza kutekeleza hukumu za kifo baada ya Rais Donald Trump, ambaye anaunga mkono hukumu ya kifo, kuondoa kusitishwa kwa utekelezaji huo mwaka jana. Hata hivyo, hakuna utekelezaji wa hukumu ya kifo uliofanyika tangu wakati huo.

Imetafsiriwa na Faidha Ngaga