Trump: Urusi na Ukraine zakubaliana kusitisha mashambulizi ya nishati

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Urusi na Ukraine zimekubaliana kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati, lakini Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema tangazo hilo limekuwa jipya kwake.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump amesema makubaliano hayo yanaanza kutekelezwa mara moja, akizitaka pande zote mbili kuyaheshimu na kutoyakiuka. Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi kuhusu jinsi makubaliano hayo yalivyofikiwa.
Urusi ilikuwa bado haijatoa tamko kuhusu tangazo hilo, huku Zelensky akiripotiwa kuliambia shirika la habari la Marekani, Axios, kuwa ni kitu kipya kwake, hakijui. Awali, kiongozi huyo wa Ukraine alisema nchi yake ilikuwa tayari kusitisha mashambulizi dhidi ya viwanda vya kusafisha mafuta nchini Urusi iwapo Moscow nayo itasitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine.
Tangazo hilo linakuja baada ya mvutano kuongezeka kati ya Trump na Zelensky, ambapo siku ya Jumamosi rais wa Marekani aliitaka Ukraine kusitisha mashambulizi dhidi ya viwanda vya mafuta vya Urusi. Trump pia alipendekeza kuwa Ukraine inapaswa kuwa na rais mwingine anayeweza kufikia makubaliano ya kumaliza vita.
Urusi na Ukraine zimekuwa zikiongeza mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati katika miezi ya hivi karibuni, wakati vita vinavyoendelea tangu uvamizi mkubwa wa Urusi nchini Ukraine mwaka 2022 vikiingia mwaka wake wa tano. Ikiwa itatekelezwa na kuheshimiwa na pande zote mbili, hatua hiyo inaweza kupunguza uharibifu wa miundombinu muhimu ya nishati.











