Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema usitishaji mapigano wa mwezi mmoja kati ya Marekani na Iran uko katika “hali mahututi sana”.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Oval Jumatatu, Trump amesema ingawa usitishaji huo bado upo, umeendelea kuwa “dhaifu kupita kiasi”.
“Ningesema usitishaji mapigano uko katika hali mahututi sana. Ni kama daktari anapoingia na kusema mgonjwa ana nafasi ya asilimia moja pekee ya kuendelea kuishi,” amesema.
Trump pia amewashutumu viongozi wa Iran kwa kuwa “wasiokuwa waaminifu”, akisema wamebadilisha msimamo mara kadhaa katika mazungumzo.
“Huo upuuzi waliotutumia hata sikuumaliza kuusoma,” alisema.
Aidha, Trump ameishutumu Iran kwa kuvunja makubaliano ya kuruhusu Marekani kuondoa akiba yake ya urani iliyorutubishwa, huku akisisitiza kuwa Iran “haitawahi kuwa na silaha za nyuklia”.
Kauli hiyo imekuja baada ya Iran kuwasilisha mapendekezo yake ya kumaliza vita na kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz kupitia ofa mbadala iliyotumwa kwa Marekani Jumapili. Trump aliyakataa mapendekezo hayo, akiyataja kuwa “hayakubaliki kabisa” na “upuuzi mtupu”.
Kufuatia matamshi ya Trump, Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Ghalibaf, aliandika kwenye mtandao wa X kwamba majeshi ya Iran yako “tayari kujibu na kutoa funzo kwa uchokozi wowote”.
Kwa upande wake, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, alisema mapendekezo ya Tehran yalikuwa ya “uwajibikaji” na “ukarimu”.
Baadaye, Ghalibaf alisema katika ujumbe mwingine kuwa “hakuna njia nyingine isipokuwa kukubali haki za wananchi wa Iran kama zilivyoainishwa katika pendekezo la vipengele 14”.
“Kadri wanavyoendelea kuchelewesha, ndivyo walipa kodi wa Marekani watakavyozidi kulipa gharama kubwa,” alisema.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim la Iran, pendekezo la Tehran linajumuisha kusitishwa mara moja kwa vita katika maeneo yote ya mapigano, hatua inayorejelea mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon, kuondolewa kwa mzingiro wa majini wa Marekani dhidi ya bandari za Iran pamoja na dhamana ya kutofanyika tena kwa mashambulizi dhidi ya Iran.
Trump aliikosoa vikali ofa hiyo kupitia mtandao wake wa Truth Social akisema: “Nimesoma majibu kutoka kwa wanaojiita ‘wawakilishi’ wa Iran. Siyapendi kabisa, hayakubaliki kabisa.”
Akijibu kauli hizo, Baghaei alisema Iran itachukua hatua “kwa njia yoyote itakayohitajika kulinda maslahi yake”.