Moja kwa moja, Trump asema usitishaji mapigano kati ya Marekani na Iran uko katika 'hali mahututi'
Kufuatia matamshi ya Trump, Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Ghalibaf, aliandika kwenye mtandao wa X kwamba majeshi ya Iran yako “tayari kujibu na kutoa funzo kwa uchokozi wowote”.
Muhtasari
Trump asema usitishaji mapigano kati ya Marekani na Iran uko katika 'hali mahututi'
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid
Iran yasema hakuna mbadala wa kukubali masharti yake ya kusitisha vita na Marekani
Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Glalibaf ni kiongozi wa Iran aliye na ushawishi mkubwa nchini humo.
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, amesema hakuna njia nyingine isipokuwa kukubali haki za wananchi wa Iran kama zilivyoainishwa katika pendekezo la vipengele 14 lililowasilishwa na Tehran.
Kauli hiyo ilichapishwa Jumatatu jioni kupitia akaunti yake kwenye mtandao wa X kwa lugha ya Kiingereza, ambapo alisema: “Njia nyingine yoyote haitakuwa na matokeo na italeta kushindwa mfululizo pekee. Kadri wanavyoendelea kuchelewesha, ndivyo walipa kodi wa Marekani watakavyoendelea kubeba gharama kubwa zaidi.”
Awali, Ghalibaf alikuwa amesema katika ujumbe mwingine kuwa Iran iko tayari kwa hali yoyote itakayojitokeza.
Matamshi hayo yanaonekana kuwa majibu kwa kauli za Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye alionyesha kutoridhishwa kwake na majibu ya Iran kuhusu mapendekezo ya Marekani ya kumaliza mzozo huo.
Trump alisema Jumatatu kuwa usitishaji mapigano kati ya Marekani na Iran uko katika hali ya “kutegemea mashine ya kupumulia”, akimaanisha kuwa makubaliano hayo yako katika hali dhaifu kutokana na kutoridhishwa kwake na msimamo wa Tehran.
UAE yahusishwa na mashambulizi ya siri dhidi ya Iran - Jarida la Wall Street
Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Gazeti la The Wall Street Journal limeripoti kuwa U.A.E imekuwa ikihusika kwa siri katika mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran, kwa mujibu wa vyanzo vilivyoelezwa kuwa na taarifa kuhusu suala hilo.
Iwapo taarifa hiyo itathibitishwa rasmi, inaweza kuifanya UAE kuwa miongoni mwa mataifa yanayoshiriki moja kwa moja katika mzozo unaoendelea dhidi ya Iran.
Chanzo kimoja kilichozungumza na Wall Street Journal kilisema mashambulizi hayo, ambayo UAE haijayathibitisha rasmi, yalihusisha shambulizi dhidi ya kiwanda cha kusafisha mafuta kwenye kisiwa cha Labuan katika Ghuba ya Uajemi.
Mapema mwezi Aprili, wakati ambapo Rais wa Marekani, Donald Trump, alikuwa akitangaza usitishaji mapigano, mashambulizi ya anga pia yaliripotiwa kulenga miundombinu ya mafuta ya Iran kwenye visiwa na maeneo ya baharini yanayomilikiwa na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Iran.
Mashambulizi hayo yalisababisha moto mkubwa na kuharibu sehemu kubwa ya mtambo wa Lavan, hali iliyotarajiwa kuathiri shughuli zake kwa miezi kadhaa.
Baadaye Iran ilisema mtambo huo ulikuwa umelengwa na “shambulizi la adui”, kabla ya kujibu kwa kurusha makombora na ndege zisizo na rubani kuelekea UAE na Kuwait.
Ripoti hiyo pia ilisema kuwa Marekani haikuonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulizi hayo, kwa kuwa usitishaji mapigano ulikuwa bado haujatekelezwa kikamilifu.
Wall Street Journal iliongeza kuwa Washington “iliupokea vyema ushiriki wa UAE” katika operesheni hizo.
Marekani yafanya mazungumzo ya siri kufungua kambi mpya za kijeshi Greenland
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Makamu wa Rais JD Vance alitembelea kambi pekee ya jeshi la Marekani kwenye eneo hilo mapema mwaka huu.
Marekani imekuwa ikifanya mazungumzo ya siri na Denmark kuhusu kupanua uwepo wake wa kijeshi nchini Greenland, kwa mujibu wa maafisa kadhaa wanaofahamu majadiliano hayo, huku mazungumzo kati ya pande hizo yakiripotiwa kupata mafanikio katika miezi ya hivi karibuni.
Maafisa wa Marekani wanataka kufungua kambi tatu mpya za kijeshi kusini mwa Greenland, eneo lenye mamlaka ya kujitawala chini ya Denmark, wakati wakijaribu kutuliza mvutano wa kidiplomasia uliosababishwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, baada ya kutishia kuichukua Greenland kwa nguvu.
Kambi hizo zinatarajiwa kujengwa kusini mwa Greenland na zitajikita zaidi katika ufuatiliaji wa shughuli za majini zinazoweza kufanywa na Urusi na China katika eneo la Atlantiki ya Kaskazini kati ya Greenland, Iceland na Uingereza, eneo linalojulikana kama GIUK Gap.
Ikulu ya White House imethibitisha kuwa serikali ya Marekani inaendelea na mazungumzo ya ngazi ya juu na Greenland pamoja na Denmark, lakini imekataa kutoa maelezo zaidi kuhusu majadiliano hayo.
Denmark hapo awali ilionyesha utayari wa kujadili uwezekano wa kuongezwa kwa kambi za kijeshi za Marekani nchini Greenland, huku Wizara yake ya Mambo ya Nje ikithibitisha kuwa mazungumzo hayo yanaendelea.
“Kuna mazungumzo ya kidiplomasia yanayoendelea na Marekani. Wizara ya Mambo ya Nje haitatoa maelezo zaidi kwa sasa,” msemaji wa wizara hiyo alisema.
Vyanzo hivyo vimesema bado hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa na idadi ya mwisho ya kambi inaweza kubadilika. Moja ya kambi hizo huenda ikajengwa Narsarsuaq katika eneo la zamani lililokuwa na kambi ya kijeshi ya Marekani pamoja na uwanja mdogo wa ndege.
Hata hivyo, maafisa wa Marekani hawajazungumzia uwezekano wa kuichukua Greenland kwa nguvu wakati wa mazungumzo hayo, jambo ambalo Denmark na muungano wa kijeshi wa NATO wamekuwa wakilipinga hadharani.
Kwa sasa, Marekani ina kambi moja pekee ya kijeshi Greenland, tofauti na takriban vituo 17 vya kijeshi vilivyokuwepo wakati wa Vita Baridi. Kambi hiyo ya Pituffik Space Base iliyopo kaskazini magharibi mwa Greenland hutumika kufuatilia makombora kwa ajili ya NORAD, lakini haijajengwa kwa ajili ya ufuatiliaji wa shughuli za majini.
Baadhi ya maafisa wa sasa na wa zamani pamoja na wataalamu wa usalama wa eneo la Arctic wameiambia BBC kuwa Washington ingeweza kusukuma maslahi yake Greenland bila kutoa vitisho vikali dhidi ya mshirika wake wa NATO.
“Kwanini umtishie mshirika kwa operesheni ya kijeshi au uvamizi wakati kile unachotaka kinaweza kujadiliwa kwa urahisi?” alisema afisa mmoja wa zamani mwandamizi wa ulinzi wa Marekani.
Trump alionesha nia ya kuipa Marekani ushawishi mkubwa Greenland tangu muhula wake wa kwanza madarakani, lakini kauli zake za hivi karibuni zimezua mvutano wa kidiplomasia na kuangazia tofauti ndani ya NATO kuhusu msimamo wa serikali yake.
Trump asema usitishaji mapigano kati ya Marekani na Iran uko katika 'hali mahututi'
Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema usitishaji mapigano wa mwezi mmoja kati ya Marekani na Iran uko katika “hali mahututi sana”.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Oval Jumatatu, Trump amesema ingawa usitishaji huo bado upo, umeendelea kuwa “dhaifu kupita kiasi”.
“Ningesema usitishaji mapigano uko katika hali mahututi sana. Ni kama daktari anapoingia na kusema mgonjwa ana nafasi ya asilimia moja pekee ya kuendelea kuishi,” amesema.
Trump pia amewashutumu viongozi wa Iran kwa kuwa “wasiokuwa waaminifu”, akisema wamebadilisha msimamo mara kadhaa katika mazungumzo.
“Huo upuuzi waliotutumia hata sikuumaliza kuusoma,” alisema.
Aidha, Trump ameishutumu Iran kwa kuvunja makubaliano ya kuruhusu Marekani kuondoa akiba yake ya urani iliyorutubishwa, huku akisisitiza kuwa Iran “haitawahi kuwa na silaha za nyuklia”.
Kauli hiyo imekuja baada ya Iran kuwasilisha mapendekezo yake ya kumaliza vita na kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz kupitia ofa mbadala iliyotumwa kwa Marekani Jumapili. Trump aliyakataa mapendekezo hayo, akiyataja kuwa “hayakubaliki kabisa” na “upuuzi mtupu”.
Kufuatia matamshi ya Trump, Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Ghalibaf, aliandika kwenye mtandao wa X kwamba majeshi ya Iran yako “tayari kujibu na kutoa funzo kwa uchokozi wowote”.
Kwa upande wake, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, alisema mapendekezo ya Tehran yalikuwa ya “uwajibikaji” na “ukarimu”.
Baadaye, Ghalibaf alisema katika ujumbe mwingine kuwa “hakuna njia nyingine isipokuwa kukubali haki za wananchi wa Iran kama zilivyoainishwa katika pendekezo la vipengele 14”.
“Kadri wanavyoendelea kuchelewesha, ndivyo walipa kodi wa Marekani watakavyozidi kulipa gharama kubwa,” alisema.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim la Iran, pendekezo la Tehran linajumuisha kusitishwa mara moja kwa vita katika maeneo yote ya mapigano, hatua inayorejelea mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon, kuondolewa kwa mzingiro wa majini wa Marekani dhidi ya bandari za Iran pamoja na dhamana ya kutofanyika tena kwa mashambulizi dhidi ya Iran.
Trump aliikosoa vikali ofa hiyo kupitia mtandao wake wa Truth Social akisema: “Nimesoma majibu kutoka kwa wanaojiita ‘wawakilishi’ wa Iran. Siyapendi kabisa, hayakubaliki kabisa.”