Tanzania yazindua rasmi bwawa la umeme

Chanzo cha picha, Mwananchi
Na Florian Kaijage
Bwawa kubwa zaidi Afrika Mashariki la kufua umeme wa nguvu za maji unazinduliwa leo nchini Tanzania.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ndiye mgeni rasmi katika uzinduzi huo. Waziri Mkuu wa Misri, Mostafa Madbouly anamwakilisha Rais, Abdel Fattah el Sisi wa Misri, anakotokea mkandarasi mkuu wa mradi huo, kampuni ya Arab Contractors.
Bwawa hilo lililopewa jina la Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, lina uwezo wa kuzalisha megawatt 2115 za umeme, hivyo kuwa moja ya mabwawa makubwa ya kufua umeme barani Afrika.
Mradi huo ulianza kutekelezwa Juni, 2019 baada ya mkataba kusainiwa mwaka 2018 wakati wa uongozi wa Rais John Magufuli aliyehuisha wazo na usanifu wa bwawa hilo la mwanzoni mwa miaka ya 1970, lakini utekelezaji wake ulishindikana kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa fedha na pingamizi kutoka kwa watetezi wa hifadhi ya mazingira, waliopinga ukataji wa miti kupisha ujenzi huo
Bwawa la Mwalimu Nyerere lipo ndani ya iliyokuwa mbuga ya wanyama ya Selous, iliyopo kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa dunia chini ya Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO).
Ujenzi wake pamoja na mitambo ya kufua umeme umegharimu dola za Marekani bilioni 2.9. Lipo pembezoni mwa mto Rufiji.
Soma pia:






