Jeshi la Israel limesema limeanzisha wimbi jipya la mashambulizi kote nchini Lebanon, baada ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kutangaza kuwa nchi yake itaongeza mashambulizi dhidi ya kundi la Hezbollah.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema limetekeleza mashambulizi dhidi ya malengo ya Hezbollah katika Bonde la Bekaa mashariki mwa Lebanon pamoja na maeneo mengine ya nchi hiyo.
Kwa upande wake, Hezbollah imesema imejibu mashambulizi hayo kwa kutekeleza mashambulizi 22 kwa kutumia droni na makombora, ikidai kulenga wanajeshi wa Israel, vifaru, kambi za kijeshi na majengo mbalimbali.
Mapema mwezi huu, Lebanon na Israel zilikubaliana kuongeza muda wa usitishaji mapigano kwa siku 45, ingawa mapigano katika baadhi ya maeneo yameendelea kuripotiwa.
Katika ujumbe wa video alioutoa Jumatatu jioni, Netanyahu amesema Israel “iko vitani na Hezbollah” na kwamba jeshi limeagizwa “kulipiga kundi hilo pigo kubwa na la kuangamiza.”
Alisema operesheni za kijeshi za Israel dhidi ya Hezbollah tayari “zimewaondoa zaidi ya magaidi 600,” lakini akasisitiza kuwa hatua inayofuata ni kuongeza kasi na ukubwa wa mashambulizi.
“Lakini kile kinachohitajika sasa ni kuongeza mashambulizi na kuongeza nguvu ya operesheni hizi,” amesema Netanyahu.
Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich, na Waziri wa Usalama wa Taifa, Itamar Ben-Gvir, ambao wote wanatoka mrengo mkali wa kulia, wameitaka serikali kupanua operesheni za kijeshi, ikiwemo kuzifikisha hadi mji mkuu wa Lebanon, Beirut.
Wakati huo huo, Israel imeendelea kutoa maonyo ya karibu kila siku kwa wakazi wa maeneo mapya kusini mwa Lebanon kuondoka makwao, hali iliyochangia kuongezeka kwa idadi ya watu waliokimbia makazi yao hadi zaidi ya milioni moja.
Lebanon iliingia katika awamu hii ya mzozo baada ya Marekani na Israel kuanzisha vita dhidi ya Iran mnamo Februari 28. Hezbollah, mshirika wa karibu wa Iran, ilirusha makombora kuelekea Israel kujibu shambulio la Israel lililomuua Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.
Israel ilijibu kwa mashambulizi ya anga kote Lebanon na baadaye kuanzisha operesheni za ardhini. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Lebanon, zaidi ya watu 3,000 wameuawa katika mashambulizi ya Israel tangu kuanza kwa mapigano hayo.
Serikali ya Lebanon imekuwa ikifanya juhudi za kulivua Hezbollah silaha, lakini imesema kuwa utekelezaji wa mpango huo unategemea kuwepo kwa usitishaji mapigano wa kudumu kutokana na ugumu wa mchakato huo.