Mambo 6 ambayo dunia imejifunza kutoka kwa Iran

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Mzozo kati ya Iran na mataifa ya magharibi haswa Marekani umedumu kwa miongo kadhaa, ila hawakuanza kushambuliana moja kwa moja.

Marekani ilikuwa haijawahi kutuma wanajeshi wake nchini Iran au hata katika mataifa ambayo Iran imekuwa na mzozo nao awali kama Iraq, Afghanistan, Yemen na Libya.

Ingawa Marekani imekuwa na vituo vya kijeshi katika eneo la Ghuba, Iran imeonekana kuwa tishio kutokana na mpango wake wa nyuklia.

Ila mwezi Oktoba mwaka wa 2025, Israel ilipoishambulia Iran na baadaye Marekani ikajiunga katika vita hivyo, macho ya dunia nzima yote yaligeukia Iran.

Ingawa vita hivyo vilidumu kwa siku 12, miezi kadhaa baadaye, Israel pamoja na Marekani waliishambulia Iran tena.

Iran imeonyesha kuwa kuna uwezekano wa kuzuia vita dhidi ya Marekani

Iran imeonyesha ustahimilivu wake wa kupigana dhidi ya mataifa mawili, Marekani na Israel.

Mataifa yote yamekuwa yakitumia teknolojia ya hali ya juu katika vita hivyo. Katika vita vya siku 12, Israel iliishambulia Iran na makombora ya kisasa huku Marekani ikilenga vituo vya kutengeneza nyuklia na mabomu.

Wakati huo wengi walihofia kuwa Iran haingeweza kustahimili vita hivyo, ila waliweza kustahimili, licha ya kupoteza wanajeshi wengi.

Baadaye vita hivyo vilikwisha baada ya mazungumzo na Rais Trump kutangaza kuwa wameweza kuharibu uwezo wa kinyuklia wa Iran.

Ila miezi kadhaa baadaye Marekani ilianzisha vita na Iran kuhusu mpango wao wa nyuklia.

Vita hivyo vilivyoanza tarehe 28 mwezi Februari mwaka huu, Marekani na Israel waliishambulia Iran, kwa makombora, mabomu, ndege zisizo na rubani na ndege za kivita

Iran ilijibu kwa makombora na ndege zisizo na rubani kwa kulenga mataifa Jirani.

Marekani inasema imetumia zaidi ya dola billioni 25 katika vita hivyo.

Licha ya Israel na Marekani kudhoofisha Iran, taifa hilo limeonyesha ubabe wake kwa kuweza kustahimili vita kwa muda mrefu.

Kutoka kutishiana hadi kushambuliana

Marekani na Israel wamekuwa wakilaumu Iran kwa kuunga mkono makundi yaliyojihami Mashariki ya Kati, kwa kuwapa fedha, silaha na mafunzo ya kijeshi.

Makundi ha yani Hezbollah, Wahouthi kutoka Yemen na Hamas.

Iran na Israeli wamekuwa vitani kuanzia kitambo ila si kwa njia ya moja kwa moja.

Iran imeonyesha uwezo wake wa kujilinda kutokana na silaha za kisasa haswa ndege zisizo na rubani kutoka Israel, na hata kuweza kulenga Israel katika mashambulizi.

Kufiki sasa hakuna taifa ambalo limeweza kushambulia anga za Israel kama Iran.

Teknoljia katika silaha za kijeshi

Iran inajulikana kutengeneza silaha zenye teknoljia ya kisasa kama makombora yenye masafa marefu, mafupi na silaha za nyuklia.

Marekani imekuwa ikiishinikiza Iran kusitisha mpango wake wa nyuklia suala ambalo limeleta mvutano.

Iran pia imeweza kutengeneza makombora yake na ndege zisizo na rubani za bei nafuu za Shahed 136, ambazo hulenga shambaha na zinaweza kusafiriki umbali wa kilomita 2500.

Ingawa droni hizo hazina kasi sana, haziwezi kutambulika kwa haraka kwasababu hazipai juu sana angani.

Mashambulizi katika mataifa ya Ghuba

Kabla ya vita kuanza, Iran ilikuwa imeonya kuwa ikiwa itashambuliwa italenga mataifa mengine Mashariki ya Kati.

Iran ilianza kwa kulenga vituo vya kijeshi vya Marekani zilizoko katika mataifa ya Ghuba ikiwemo Qatar, Falme za kiarabu, Saudi Arabia, Iraq, Jordan na Kuwait.

Ila mashambulizi hayo yalilenga uwanja wa ndege, kampuni za nishati na mahoteli eneo hilo.

Kulikuwa na hofu ya vita vya kikanda kuzuka, iwapo mataifa hayo yangejibu na kujiingiza katika vita hivyo.

Iran inasisitiza kuwa kambi za kijeshi za Marekani zinafaa kuondolewa eneo hilo

Nguvu ya kijeshi ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran

Vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vilipoanza mwezi Februari, lengo kuu ilikuwa kukandamiza utawala wa taifa hilo na kuwalazimisha kujisalimisha, haswa baada ya kuuawa kwa kiongozi mkuu wa taifa hilo Ayatollah Khamenei na viongozi wengine wakuu walioonekana kuwa na ushawishi.

Ila taifa hilo limeonesha uwezo wa kustahimili vita hivyo, na kuwateua viongozi wengine kwa haraka bila kuruhusu kuwepo kwa mgogoro wa uongozi.

Taifa hilo pia limesema litaendelea kujilinda kwa njia ya kijeshi dhidi ya adui.

Sera ya Marekani katika vita hivyo vya kudhoofisha uongozi wa taifa hilo, haukufaulu na kuwalazimu kutumia njia ya mazungumzo na diplomasia.

Udhibiti wa mlango bahari wa Hormuz

Kabla ya vita kuanza, ni watu wachache sana walikuwa wanafahamu kuhusu mlango bahari wa Hormuz, na umuhimu wake katika biashara za kimataifa.

Ila Iran ilipotishia kufunga eneo hilo la bahari na kuzuia gesi na mafuta kupita, eneo hilo lilipata umaarufu baada ya bei ya nishati kupanda.

Asilimia 20 ya mafuta yote duniani hupitia eneo hili Pamoja na theluji moja ya mbolea.

Bidhaa muhimu kama dawa, chakula na mavazi pia hupitia eneo hili.

Iran imesema itaendelea kudhibiti eneo hili, n ani sehemu ya taifa hilo.

Trump alitishia kuishambulia Iran iwapo haitafungua mlango huo wa bahari.

Baada ya Pakistan kupatanisha mataifa hayo mawili, walikubaliana kusitisha mashambulizi na kufungua mlango huo wa bahari. Ingawa Iran ilifungua mlango huo wa bahari, Marekani ilianza kuzuia meli za mafuta za Iran.

Diplomasia na mbinu zinazotumika katika mazungumzo

Jeshi la Iran limeonyesha ubabe wake katika kufanya mazungumzo na kulinda maslahi ya taifa hilo.

Marekani na Israel wanataka Iran kuwacha kudhibiti mlango bahari wa Hormuz na mpango wake nyuklia.

Iran ilijibu kwa kusema hawatasitisha uzalishaji wa makombora, ila masuala mengine yanaweza kuzingatiwa.

Serikali ya Trump haijapata mafanikio yoyote katika mazungumzo yanayoongozwa na mpatanishi Pakistan, huku taifa hilo likiendelea kujaribu kuwapatanisha mataifa hayo yanayozozana.