Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tunachojua kuhusu uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano kati ya Iran na Marekani
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio anasema taarifa ambayo itamaliza rasmi vita vya Mashariki ya Kati inaweza kutolewa ndani ya muda wa saa chache zijazo baada ya Rais Donald Trump kusema kuwa mazungumzo kati ya Marekani na Iran yako katika hatua za mwisho.
Rubio alisema katika mkutano na waandishi wa habari nchini India, bila kutoa maelezo zaidi, kwamba makubaliano yanayotarajiwa "kwa kiasi kikubwa" yatashughulikia wasiwasi wa Marekani kuhusu Mlango wa Bahari wa Hormuz na kuzuia Iran kupata silaha za nyuklia.
Maafisa wa Iran bado hawajazungumza kuhusu uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano: lakini Rais wa Iran Masoud Peshkeskian amesema leo: "Hakuna uamuzi utakaofanywa nje ya mfumo wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na bila ya uratibu na ruhusa ya Kiongozi MKuu.
Huku hayo yakijiri, ripoti zisizo rasmi na ambazo hazijathibitishwa zinazoelezea uwezekano wa makubaliano kati ya Tehran na Washington kufikiwa.
Axios iliripoti, ikimnukuu afisa wa Marekani, kwamba Tehran na Washington zinakaribia kutia saini makubaliano ambayo yataongeza muda wa usitishaji mapigano kwa siku 60, kufungua mlango wa bahari wa Hormuz, kuruhusu Iran kuuza mafuta, kufanya mazungumzo juu ya kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran, na kumaliza vita nchini Lebanon.
Licha ya maafisa wa Iran kusalia kimya, mashirika ya habari ya Tasnim na Fars, ambayo yako karibu na jeshi na taasisi za usalama za nchi hiyo, yameripoti taarifa zao zisizo rasmi zikielezea uwezekano wa makubaliano kufikiwa, ambayo muhtasari wake kwa jumla unashabihiana na ripoti ya Axios.
Uwezekano wa makubaliano ya Iran na Marekani, kulingana na Axios
Afisa mmoja wa Marekani aliiambia shirika la habari la Axios kwamba mkataba wa maelewano uliotiwa saini na Iran na Marekani ni halali kwa siku 60 na huenda ukaongezwa kwa makubaliano kati ya pande hizo mbili.
Ndani ya siku 60 baada ya makubaliano hayo, Mlango-Bahari wa Hormuz utafunguliwa, na Iran kuondoa udhibiti weka kwenye njia hiyo muhimu ya bahari kuwezesha meli kupita bila kulipa ada yoyote.
Kwa upande wake, Marekani itajindoa vizuizi vyamajini dhidi ya bandari za Iran na kuiruhusu kuuza mafuta katika kipindi hiki, na kuondolewa vikwazo.
Kulingana na Axios, Iran itajitolea "kutouunda silaha ya nyuklia" na kujadili kusimamishwa kwa mpango wake wa urutubishaji na kuondolewa kwa hazina yake ya urani iliyorutubishwa.
Vyanzo viwili vinavyofahamu suala hilo viliiambia Axios kwamba Iran imesema kwa maneno kupitia wapatanishi kiwango cha makubaliano ambayo iko tayari kufanya kuhusu kusimamishwa kwa urutubishaji na kusalimisha akiba ya nyenzo za nyuklia.
Kwa mujibu wa Axios, Marekani imekubali kufanya mazungumzo ya kuondolewa kwa vikwazo na kuachiliwa kwa mali za Iran zilizofungiwa katika kipindi cha siku 60 za usitishaji mapigano, ingawa haya yatatekelezwa kama sehemu ya makubaliano ya mwisho ambayo yanaweza kuthibitishwa wakati wa utekelezaji.
Kwa mujibu wa afisa wa Marekani aliyezungumza na Axios, Iran inataka kuondolewa kwa vikwazo vya kudumu na kuachiliwa mara moja kwa mali yake, lakini Marekani imesema hilo litawezekana tu ikiwa Iran itakubali kufikia "makubaliano ya wazi."
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vikosi vya Marekani vilivyotumwa katika eneo hilo katika miezi ya hivi karibuni vitasalia kwa muda wa siku 60 na vitaondoka mara tu makubaliano hayo yatakapokamilika.
Kwa mujibu wa Axios, rasimu ya hati hiyo pia inaeleza kuwa vita kati ya Israel na Hezbollah nchini Lebanon vitamalizika.
Israel bado haijatoa tamko rasmi kuhusu ripoti hizo, lakini Axios iliripoti, ikimnukuu afisa wa Israel, kwamba Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alionyesha wasiwasi wake katika mazungumzo ya simu na Donald Trump kuhusu kjumuishwa kwa Lebanon katika mkataba wa maelewano kati ya Marekani na Iran.
Afisa huyo wa Marekani pia aliiambia Axios kwamba Bw. Netanyahu alikuwa na wasiwasi kuhusu vipengele vingine vya mpango huo lakini ametoa maoni yake "kwa heshima."
Hapo awali, Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa alizungumza na Benjamin Netanyahu kuhusu Iran na kuongeza kwamba mazungumzo hayoa yalikuwa "mazuri sana."
"Bibi (Netanyahu) ana mambo yake ya ndani (Israel), lakini Trump anapaswa kufikiria juu ya masilahi ya Marekani na uchumi wa kimataifa," afisa wa Marekani aliyezungumza na Axios alisema.
Afisa huyo wa Marekani pia alisisitiza kuwa usitishaji vita nchini Lebanon "hautakuwa wa upande mmoja" na kwamba Israel itaruhusiwa kujibu iwapo Hezbollah itachukua hatua za kushaimbulia.
Vyombo vya habari vya Iran vinasemaje?
Ingawa maafisa wa Iran hawajatoa tamko rasmi kuhusu maelezo ya uwezekano wa makubaliano hayo, mashirika ya habari yaliyo karibu na taasisi za usalama na kijeshi, kama vile Tasnim na Fars, yameangazia suala hilo.
Mashirika hayo ya habari yamechapisha maelezo ambayo yanaendana na masimulizi ya Axios, lakini ripoti zanatilia shaka utashi wa Wamarekani kufikia makubaliano hayo kikamilifu.
Shirika la Habari la Fars liliandika: "Wakati mazungumzo yanaelekea kwenye makubaliano ya awali, vyanzo vya habari vinaripoti uwezekano wa Marekani kurejelea mwenendo wake wa awali na kukiuka mojawapo ya vipengee vya makubaliano ya awali. Hii ni mara ya pili kwa Washington kuchukua hatua kinyume na makubaliano ya awali."
Shirika hilo la habari limewanukuu wajumbe wa timu ya mazungumzo ya Iran wakisema, "Hatuna imani na Marekani, na hali hii ya kutoaminiana iko katika hali mbaya zaidi."
Wakati huo huo, Shirika la Habari la Tasnim pia liliandika kuhusu wasiwasi wa Iran kuhusu Marekani kutotekeleza ahadi zake kuhusu kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya mali yake:
"Mazungumzo yanaonyesha kuwa katika wiki za hivi karibuni Marekani imekuwa ikijaribu kuhusisha kuachiliwa kwa mali hizi na makubaliano ya mwisho yanayoweza kufikiwa kuhusu suala la nyuklia, lakini Iran imesisitiza kwamba sehemu ya mali yake yake lazima iachiwe kabla ya tangazo la maelewano kutolewa. Aidha, utaratibu wa kuachilia sehemu iliyosalia pia lazima iwe wazi wakati wa mazungumzo, na ikiwa Wamarekani watazuia tena mashauriano hayo katika siku zijazo."
Shirika hilo la habari pia limeandika: "Kutokubaliana kati ya Iran na Marekani kuhusu kipengele kimoja au viwili vya uwezekano wa makubaliano ya maelewano kunaendelea, na kutokana na vikwazo vya Marekani, suala hilo bado halijakamilika."
Kwa mujibu wa Tasnim, mpatanishi huyo wa Pakistan amefahamishwa kuwa hakuna makubaliano yatakayofikiwa masuala haya hayasitatatuliwa, ikiwa ni pamoja na kuachiwa kwa mali inayoshikiliwa.
Suala jingine ambalo limetiliwa mkazo na vyombo vya habari vya Iran ni kuahirishwa kwa mazungumzo ya nyuklia hadi baada ya makubaliano ya awali.
Shirika la Habari la Fars liliandika:
"Vyanzo vinavyofahamu mazungumzo hayo vimesisitiza kuwa rasimu ya uwezekano wa makubaliano kati ya Iran na Marekani haijumuishi kifungu chochote kuhusu ahadi za nyuklia za Iran, na masuala yote yanayohusiana na mpango wa nyuklia yameahirishwa kwa mazungumzo siku 60 baada ya makubaliano hayo kutiwa kusaini.
Ikipinga ripoti kuhusu ahadi za nyuklia za Iran, Fars iliandika: "Hakuna ahadi ya kukabidhi akiba ya nyuklia, kuondoa vifaa, kufunga viwanda, au hata ahadi ya kutotengeneza bomu la nyuklia."
Tasnim iliandika kwamba Iran inasisitiza juu ya kutumia mamlaka yake dhidi ya Mlango-Bahari wa Hormuz, na kwamba makubaliano ya kuongeza idadi ya meli zinazopita katika mkondo huo hadi kiwango cha kabla ya vita haimaanishi kuwa hadhi ya njia hii ya maji itarejea katika hali yake ya awali.
Shirika hilo la habari pia limeandika kuwa licha ya kuwepo kwa dalili za uwezekano wa kutiwa saini mkataba huo, Iran iko tayari kwa mazungumzo hayo kufeli, na kunukuu chanzo cha kijeshi kikisema kwamba "Wamarekani kwa mara nyingine wakitekeleza hatua dhidi ya Iran, watakabiliwa na 'toleo la tatu la mapambano ya Iran' ambayo yatatofautiana na vita viwili vya awali katika mkakati na malengo na zana.
Matukio muhimu zaidi katika mazungumzo ya Iran na Marekani
Tathmini ya mazungumzo ya Iran na Marekani chini ya upatanishi wa Pakistan katika wiki za hivi karibuni:
- April 8: Pakistan ilitangaza usitishaji vita wa wiki mbili kati ya Marekani na Iran, ambao ulitarajiwa kukamilika Aprili 22. Donald Trump alisema makubaliano hayo yalikuwa na masharti ya kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz. Pakistan ilisema Lebanon pia ilijumuishwa katika mpango huo, lakini Marekani na Israel zilikanusha hilo.
- Aprili 11: Maafisa wakuu wa Marekani na Iran, akiwemo Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance, Spika wa Bunge Mohammad Baqer Qalibaf, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi, walikutana nchini Pakistan. Baada ya saa 21 ya mazungumzo ya kidiplomasia, tofauti kubwa kati ya Washington na Tehran katika masuala muhimu zilisalia bila kutatuliwa.
- Aprili 12: Maada ya mazungumzo Islamabad kutibuka, Trump alitangaza kuwa ataweka kizuizi cha kijeshi cha majini dhidi ya Iran.
- Aprili 13: CENTCOM ilitangaza kuanza kwa vikwazo vya majini vya Iran, huku Iran ikiendelea kufunga Mlango-Bahari wa Hormuz.
- Aprili 21: Bw. Trump alirefusha kipindi cha usitishaji mapigano kwa muda usiojulikana ili kuruhusu mazungumzo kuendelea.
- Mei 5: Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alitangaza kumalizika kwa "Operesheni ya Epic Fury" .
- Mei 8: Donald Trump alisema kuwa usitishaji mapigano kati ya Marekani na Iran upo, ingawa kumekuwa na mapigano kati ya Iran na Jeshi la Wanamaji la Marekani katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.
- Mei 10: Iran iliikabidhi Marekani mpango ambao ulijumuisha kusitishwa mara moja kwa vita pande zote na kuondoa kizuizi cha majini dhidi ya bandari za Iran. Donald Trump alisema hilo "haliwezekani kabisa."
- Mei 15: Rais wa Marekani alisema atakubali kusitishwa kwa miaka 20 kwa mpango wa nyuklia wa Iran.
- Mei 18: Donald Trump alitangaza kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social kwamba amesimamisha shambulio jipya dhidi ya Iran kwa ombi la nchi za Ghuba ya , lakini ikiwa hakuna makubaliano yatafikiwa, Marekani iko tayari kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya Iran "wakati wowote."
- Mei 23: Bw. Trump alisema makubaliano na Iran "yamekamilishwa kwa kiasi kikubwa" na yatajumuisha kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran amesema tofauti zimepungua lakini akasisitiza kuwa baadhi ya masuala bado hayajatatuliwa.
- Mei 24: Marco Rubio alisema katika mkutano na waandishi wa habari huko New Delhi kwamba "hatua kubwa" imepigwa na kwamba taarifa zaidi zinaweza kutolewa leo.