Moja kwa moja, Jeshi la Marekani lasema limefanya mashambulizi mapya kusini mwa Iran

Jeshi la Marekani limesema kuwa lililenga vituo vya kurushia makombora kusini mwa Iran pamoja na boti zilizokuwa zikijaribu kutega mabomu ya majini.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Urusi yatishia mashambulizi mapya dhidi ya Kyiv, yawataka raia wa kigeni kuondoka

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Urusi imetishia kuanzisha wimbi jipya la mashambulizi ya “kimfumo” dhidi ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, siku chache baada ya kutekeleza moja ya mashambulizi makubwa zaidi dhidi ya jiji hilo tangu kuanza kwa vita.

    Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ilisema mashambulizi hayo yatalenga “vituo vya kufanya maamuzi” na makao ya uongozi wa kijeshi, pamoja na maeneo ya kutengeneza ndege zisizo na rubani (droni) ndani ya Kyiv.

    Moscow pia imewataka raia wa kigeni na wanadiplomasia kuondoka Kyiv “haraka iwezekanavyo”, huku ikiwatahadharisha watu kuepuka majengo ya utawala na vituo vya kijeshi.

    Kwa upande wake, Ukraine imeelezea vitisho hivyo kuwa “siyo chochote zaidi ya usaliti wa wazi na mbinu za vitisho,” na kuzitaka nchi washirika kuongeza shinikizo dhidi ya Moscow.

    Serikali ya Ukraine ilisema onyo la Urusi kwa raia wa kigeni linaashiria kwamba mashambulizi hayo yanalenga pia kuwatisha wanadiplomasia wa kigeni waliopo nchini humo.

    Ukraine imeongeza kuwa mashambulizi ya Urusi dhidi ya Kyiv hayajawahi kusimama kwa kipindi cha hata wiki moja tangu kuanza kwa vita, huku tishio la usalama kutoka Moscow likiendelea kuwa kubwa kama ilivyokuwa miezi na miaka iliyopita.

    Kwa mujibu wa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, mashambulizi makubwa ya Urusi yaliyofanyika usiku wa Jumamosi yaliua watu wanne na kujeruhi takribani 100 katika Kyiv na maeneo mengine.

    Urusi imesema mashambulizi hayo na vitisho vya mashambulizi zaidi ni jibu la kile inachodai kuwa shambulio la makusudi la Ukraine dhidi ya bweni la wanafunzi katika mji wa Starobilsk siku ya Ijumaa, ambapo maafisa wa Urusi wanasema watu 21 waliuawa.

  2. Qatar yakanusha madai ya kutoa ofa ya dola bilioni 12 kwa Iran ili kufanikisha makubaliano

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imekanusha vikali taarifa zinazodai kuwa Doha imeipa Iran ofa ya dola bilioni 12 kama sehemu ya kuhakikisha kufikiwa kwa makubaliano kati ya pande husika.

    Msemaji wa Wizara hiyo, Majid Mohammed Ansari, aliandika kwenye mtandao wa X kwamba madai hayo “si ya kweli kabisa,” akisisitiza kuwa yameenezwa na vyama vinavyolenga kuhujumu makubaliano na kudhoofisha juhudi za kidiplomasia za kupunguza mvutano na kuimarisha utulivu wa kikanda.

    Ansari aliongeza kuwa jukumu la kidiplomasia la Qatar, kwa ushirikiano na washirika wa kikanda, linajulikana na limerekodiwa wazi, akieleza kuwa madai hayo ni “jaribio la kukata tamaa la kuchafua sifa ya Qatar kama mpatanishi wa kuaminika katika uwanja wa kimataifa.”

    Wakati huohuo, jana Jumatatu, ujumbe wa Iran ulioongozwa na Spika wa Bunge, Mohammad Bagher Ghalibaf, uliwasili Qatar katika ziara isiyotarajiwa, akiwa ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araghchi.

  3. Wakati na mahali pa mazishi ya Ayatollah Ali Khamenei bado haijabainishwa

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mkuu wa Baraza la Uratibu wa Propaganda za Kiislamu katika Mkoa wa Tehran, Mohsen Mahmoudi, amesema kuwa taasisi husika inaendelea kupanga mazishi ya kiongozi wa zamani wa Jamhuri ya Kiislamu, Ayatollah Ali Khamenei, akibainisha kuwa kwa maoni yake, tukio hilo litakuwa “sherehe ya kimataifa itakayorekodiwa katika historia ya ulimwengu wa Kiislamu na Iran.”

    Ameongeza kuwa tayari kuna dalili za mataifa mbalimbali, yakiwemo Iraq, kuonyesha nia ya kushiriki katika tukio hilo, akisema kuwa pia viongozi wa nchi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu pamoja na viongozi wa kile kinachoitwa mistari ya Ustahimilivu watahudhuria mazishi hayo ya kihistoria.

    Hata hivyo, Mahmoudi amesema kuwa taasisi mbalimbali zinaendelea kuratibu maandalizi ya tukio hilo, lakini akasisitiza kuwa “kwa sasa hakuna muda maalum uliopangwa.”

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ali Khamenei aliuawa katika saa za awali za mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel yaliyotokea takribani miezi mitatu iliyopita, wakati wa mashambulizi makali dhidi ya eneo lake la kazi na makazi.

    Soma Zaidi:

  4. DR Congo yasitisha shughuli za uchimbaji madini Jimbo la Kivu Kusini

    H

    Chanzo cha picha, AP

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeweka marufuku ya muda wa miezi mitatu kusitisha shughuli za uchimbaji madini katika baadhi ya maeneo ya Jimbo la Kivu Kusini, kwa mujibu wa waraka wa Wizara ya Madini.

    Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na ongezeko la uchimbaji haramu wa madini na itahusisha wilaya za Mwenga na Shabunda, kulingana na waraka uliotolewa Mei 22 na kutiwa saini na Waziri wa Madini, Louis Watum Kabamba.

    Katika kipindi hicho cha marufuku, timu maalum ya ukaguzi inayoongozwa na Ukaguzi Mkuu wa Madini itafanya tathmini ili kubaini uhalali wa shughuli za uchimbaji katika maeneo husika.

    Serikali ya Kongo inalenga kupunguza udanganyifu katika sekta ya madini pamoja na uendelezaji haramu wa rasilimali za madini katika jimbo hilo.

    Madini ya dhahabu, kasiteriti (bati) pamoja na koltani, ambayo hutumika katika teknolojia ya kisasa na hupatikana zaidi katika Jimbo la Kivu Kusini mashariki mwa nchi hiyo, huchimbwa zaidi na wachimbaji wadogo wadogo wa jadi.

    Mwaka jana, Kongo ilipiga marufuku biashara ya madini kutoka maeneo kadhaa ya uchimbaji wa jadi katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini yaliyoathiriwa na migogoro, kutokana na tuhuma kuwa madini hayo yalikuwa yakitumika kufadhili makundi yenye silaha mashariki mwa nchi.

    Kongo pia ni miongoni mwa nchi zenye hifadhi kubwa zaidi duniani za kobalt, shaba na lithiamu.

    Soma zaidi:

  5. Papa Leo XIV aomba msamaha wa kihistoria kuhusu nafasi ya Vatican katika utumwa

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Papa Pope Leo XIV ameomba msamaha wa kihistoria akikiri jukumu la Holy See katika kuhalalisha utumwa na kushindwa kuupinga kwa karne nyingi, akielezea rekodi hiyo ya Kanisa kama “jeraha katika kumbukumbu ya Kikristo.”

    Kauli hiyo inachukuliwa kuwa moja ya hatua kali zaidi zilizowahi kuchukuliwa na Papa kuhusu kukiri moja kwa moja kuhusika kwa mamlaka za zamani za Vatican katika kuruhusu na kuendeleza utumwa wa watu wasio Wakristo katika enzi ya ukoloni.

    “Kwa hili, kwa niaba ya Kanisa, naomba msamaha kwa dhati,” ameandika katika waraka wake mpana, akieleza “huzuni kubwa” kutokana na mateso yaliyowakumba watu waliokuwa watumwa.

    Pia alikiri kwamba kabla ya kipindi hicho, katika Zama za Kati, taasisi za kanisa nazo zilikuwa na watumwa wake wenyewe.

    Alisema Kanisa lilifikia tu “hukumu rasmi, ya moja kwa moja na ya kimataifa” dhidi ya utumwa katika karne ya 19 chini ya Papa Leo XIII, baada ya kile Papa wa sasa alichokieleza kuwa kipindi kirefu cha ukinzani katika mafundisho na utekelezaji wake.

    Soma zaidi:

  6. Mama mzazi wa aliyekuwa Rais wa Tanzania John Magufuli afariki dunia

    H

    Chanzo cha picha, Jesca Magufuli/ IG

    Mama mzazi wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli, Bi Suzana Magufuli, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Mei 25, 2026, katika kijiji cha Chato, mkoani Geita baada ya kuugua kwa muda mrefu.

    Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na mwanafamilia, Jesca Magufuli, ambaye amesema kuwa Bi Suzana amefariki majira ya saa moja usiku nyumbani kwake Chato.

    “Bibi yetu Suzana Mussa amefariki saa moja usiku nyumbani kwake Chato baada ya kuugua kwa muda mrefu. Taratibu za msiba tutawajulisha baadaye. Bwana ametoa na Bwana ametwaa,” amesema Jesca Magufuli.

    Soma zaidi:

  7. Marekani yasitisha mauzo ya silaha za dola bilioni 14 kwa Taiwan kutokana na vita vya Iran

    Hong Kao ameteuliwa kuwa kaimu katibu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani tangu Aprili.

    Chanzo cha picha, CQ-Roll Call, Inc. via Getty Images

    Maelezo ya picha, Hong Kao ameteuliwa kuwa kaimu katibu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani tangu Aprili.

    Marekani imesema imesitisha kwa muda mauzo ya silaha yenye thamani ya dola bilioni 14 kwa Taiwan ili kuhakikisha ina akiba ya kutosha ya silaha na risasi kwa ajili ya uwezekano wa vita dhidi ya Iran.

    Kaimu Katibu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, Hong Kao, amethibitisha hatua hiyo wakati wa kikao cha Kamati ya Seneti kilichofanyika jana.

    Hatua hiyo imekuja licha ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutotoa msimamo wa wazi kuhusu mauzo hayo siku chache zilizopita, akisema angejadili suala hilo na Rais wa Taiwan.

    Ofisi ya Rais wa Taiwan imesema Ijumaa kwamba haijapokea taarifa yoyote kuhusu kile ilichokiita “mabadiliko katika mchakato wa mauzo ya silaha wa Marekani”.

    Kwa muda mrefu, mauzo ya silaha za Marekani kwa Taiwan yamekuwa chanzo cha mvutano kati ya Washington na Beijing. China inaichukulia Taiwan kuwa sehemu ya eneo lake na haitambui utawala wake wa kujitegemea, huku ikiwa haijaondoa uwezekano wa kutumia nguvu kuirejesha chini ya udhibiti wake.

    “Tumesitisha mauzo haya kwa sasa ili kuhakikisha tuna risasi na vifaa vya kutosha kwa ajili ya Operesheni Epic Fury dhidi ya Iran, na bila shaka kuhakikisha tuna akiba ya kutosha,” Hong Kao aliiambia Seneti.

    Alipoulizwa kuhusu msimamo wa Taiwan kufuatia uamuzi huo wa Marekani, alisema bado hajazungumza na maafisa wa Taiwan.

    “Tunachofanya ni kuhakikisha tuna kila kitu tunachohitaji. Serikali itakapoona inafaa, mauzo ya silaha kwa mataifa ya kigeni yataendelea tena,” alisema.

    Soma zaidi:

  8. Netanyahu: Israel itaongeza mashambulizi dhidi ya Hezbollah

    g

    Chanzo cha picha, ge

    Jeshi la Israel limesema limeanzisha wimbi jipya la mashambulizi kote nchini Lebanon, baada ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kutangaza kuwa nchi yake itaongeza mashambulizi dhidi ya kundi la Hezbollah.

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema limetekeleza mashambulizi dhidi ya malengo ya Hezbollah katika Bonde la Bekaa mashariki mwa Lebanon pamoja na maeneo mengine ya nchi hiyo.

    Kwa upande wake, Hezbollah imesema imejibu mashambulizi hayo kwa kutekeleza mashambulizi 22 kwa kutumia droni na makombora, ikidai kulenga wanajeshi wa Israel, vifaru, kambi za kijeshi na majengo mbalimbali.

    Mapema mwezi huu, Lebanon na Israel zilikubaliana kuongeza muda wa usitishaji mapigano kwa siku 45, ingawa mapigano katika baadhi ya maeneo yameendelea kuripotiwa.

    Katika ujumbe wa video alioutoa Jumatatu jioni, Netanyahu amesema Israel “iko vitani na Hezbollah” na kwamba jeshi limeagizwa “kulipiga kundi hilo pigo kubwa na la kuangamiza.”

    Alisema operesheni za kijeshi za Israel dhidi ya Hezbollah tayari “zimewaondoa zaidi ya magaidi 600,” lakini akasisitiza kuwa hatua inayofuata ni kuongeza kasi na ukubwa wa mashambulizi.

    “Lakini kile kinachohitajika sasa ni kuongeza mashambulizi na kuongeza nguvu ya operesheni hizi,” amesema Netanyahu.

    Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich, na Waziri wa Usalama wa Taifa, Itamar Ben-Gvir, ambao wote wanatoka mrengo mkali wa kulia, wameitaka serikali kupanua operesheni za kijeshi, ikiwemo kuzifikisha hadi mji mkuu wa Lebanon, Beirut.

    Wakati huo huo, Israel imeendelea kutoa maonyo ya karibu kila siku kwa wakazi wa maeneo mapya kusini mwa Lebanon kuondoka makwao, hali iliyochangia kuongezeka kwa idadi ya watu waliokimbia makazi yao hadi zaidi ya milioni moja.

    Lebanon iliingia katika awamu hii ya mzozo baada ya Marekani na Israel kuanzisha vita dhidi ya Iran mnamo Februari 28. Hezbollah, mshirika wa karibu wa Iran, ilirusha makombora kuelekea Israel kujibu shambulio la Israel lililomuua Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.

    Israel ilijibu kwa mashambulizi ya anga kote Lebanon na baadaye kuanzisha operesheni za ardhini. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Lebanon, zaidi ya watu 3,000 wameuawa katika mashambulizi ya Israel tangu kuanza kwa mapigano hayo.

    Serikali ya Lebanon imekuwa ikifanya juhudi za kulivua Hezbollah silaha, lakini imesema kuwa utekelezaji wa mpango huo unategemea kuwepo kwa usitishaji mapigano wa kudumu kutokana na ugumu wa mchakato huo.

    Soma zaidi:

  9. Rais wa Iran aagiza kurejeshwa kwa huduma za intaneti nchini humo

    f

    Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images

    Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ameagiza Wizara ya Mawasiliano kurejesha huduma za intaneti nchini katika hali iliyokuwapo kabla ya Desemba 2025.

    Naibu Waziri wa Mawasiliano amethibitisha kupokea agizo hilo, akisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kurejesha haki za wananchi na kuimarisha imani ya umma kwa serikali.

    Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimeripoti kuwa katika kikao kilichoongozwa na Makamu wa Rais, Mohammad Reza Aref, maamuzi muhimu kuhusu hali ya intaneti nchini yaliidhinishwa.

    Taarifa hiyo ilieleza kuwa baada ya idhini ya mwisho kutoka kwa Rais Pezeshkian, maagizo rasmi yatatolewa kwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ili kuyatekeleza.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, pendekezo la kurejesha huduma za intaneti liliidhinishwa kwa kura tisa za kuunga mkono na baadaye kuwasilishwa katika ofisi ya rais kwa ajili ya idhini ya mwisho.

    Huduma za intaneti nchini Iran zilisitishwa wakati wa operesheni za kukabiliana na maandamano yaliyotokea Desemba mwaka jana.

    Baadaye, zilipunguzwa tena kufuatia mashambulizi yaliyotekelezwa na Israel na Marekani dhidi ya Iran. Hatua ya sasa inaashiria uwezekano wa kurejea kwa huduma za mawasiliano kwa kiwango kikubwa baada ya miezi kadhaa ya vikwazo.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Trump: Urani iliyorutubishwa itakabidhiwa Marekani au kuharibiwa kwa ushirikiano na Iran

    g

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa urani iliyorutubishwa nchini Iran itakabidhiwa mara moja kwa Marekani ili isafirishwe na kuharibiwa, au itaharibiwa katika eneo jingine litakalokubaliwa kwa ushirikiano kati ya Marekani na Iran.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump amesema mchakato huo utafanyika chini ya uangalizi wa mamlaka husika za nishati ya atomiki au taasisi nyingine inayolingana na jukumu hilo.

    Katika ujumbe mwingine kwenye mtandao huo, Trump amechapisha michoro miwili inayolinganisha sera za Marekani dhidi ya Iran.

    Mchoro wa kwanza ulionyesha rundo la fedha ukiwa na maelezo: “Sera ya Iran ya Obama”, akimrejelea rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama.

    Mchoro wa pili umeonyesha meli ya kivita ya Marekani ikishambuliwa kwa mabomu ukiwa na maelezo: “Sera ya Iran ya Trump.”

    Kauli za Trump zimekuja wakati jeshi la Marekani likiwa limetekeleza mashambulizi mapya kusini mwa Iran, hatua inayoongeza mvutano licha ya mazungumzo yanayoendelea kati ya Washington na Tehran.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Jeshi la Marekani lasema limefanya mashambulizi mapya kusini mwa Iran

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jeshi la Marekani limesema limefanya mashambulizi mapya kusini mwa Iran, likilenga maeneo ya makombora ya Iran pamoja na boti zilizokuwa zikijaribu kuweka mabomu ya majini.

    Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) imesema katika taarifa kwamba mashambulizi hayo yalifanywa kwa lengo la kujilinda na yalikusudiwa “kulinda wanajeshi wetu dhidi ya vitisho vinavyotokana na vikosi vya Iran.”

    Msemaji wa CENTCOM, Kapteni Tim Hawkins, alisema jeshi la Marekani linaendelea kulinda vikosi vyake huku likionyesha kujizuia wakati wa kipindi cha usitishaji mapigano kinachoendelea.

    Mashambulizi hayo yamefanyika wakati msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, akisema kuwa kuna maendeleo fulani yaliyopatikana katika mazungumzo na Marekani, lakini akasisitiza kuwa makubaliano ya kumaliza mzozo huo “hayako karibu kufikiwa.”

    Kwa mujibu wa Kapteni Hawkins, mashambulizi hayo yalilenga eneo karibu na Bandar Abbas, mji wa bandari ulioko kusini mwa Iran na makao ya kambi ya jeshi la wanamaji la Iran katika Mlango Bahari wa Hormuz.

    Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilikuwa vimeripoti awali kuwa maafisa wa eneo hilo walikuwa wakichunguza chanzo cha milipuko iliyosikika katika Bandar Abbas.

    Hadi sasa, Iran haijatoa tamko rasmi kuhusu mashambulizi hayo ya karibuni ya Marekani. Pia haijafahamika ni athari gani mashambulizi hayo yanaweza kuwa nayo kwa juhudi za kufikia makubaliano ya amani kati ya Washington na Tehran.

    Mwishoni mwa wiki, Rais wa Marekani, Donald Trump, alikuwa ameashiria kuwa pande hizo zilikuwa karibu kufikia makubaliano, lakini baadaye alisema amewaagiza wapatanishi wa Marekani kutoharakisha mchakato huo.

    Marekani na Iran zimekuwa zikiheshimu usitishaji mapigano tangu Aprili 8. Hata hivyo, Iran imeendelea kudhibiti usafiri wa majini katika Ghuba kupitia Mlango Bahari wa Hormuz, huku Jeshi la Wanamaji la Marekani likijaribu kuzuia shughuli za bandari za Iran.

    Mzozo huo ulianza Februari 28 baada ya Marekani na Israel kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya Iran.

    Tehran ilijibu kwa kushambulia Israel na baadhi ya mataifa washirika wa Marekani katika Ghuba, pamoja na kuzuia kwa kiasi kikubwa usafiri wa majini katika Mlango Bahari wa Hormuz, hatua iliyochangia kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya Jumanne tarehe 26 Mei 2026.