Waliokuwa watawala wa Misri warejea kwa ‘gwaride la maiti’
Tukio hilo la kipekee lililogharimu mamilioni ya madola lilishuhudia maiti za kale 22 - wafalme 18 na malkia 4 wakisafirishwa kutoka makumbusho waliokuwa wamehifadhiwa hadi eneo jipya litakalokuwa nyumba yao ya milele umbali wa kilomita 5.
Usalama ukiwa umeimarishwa na msafara uliokuwa wa hadhi ya kifalme na hazina ya kitaifa, maiti hizo zilikuwa zinahamishwa hadi makumbusho mapya ya taifa katika kile ambacho kimeitwa 'Gwaride ya watawala ya kipekee'.
Maiti hizo zilisafirishwa kama tukio la kipekee na zilipitishwa kulingana na muda wa utawala wao kuanzia karne ya nasaba ya watawala katika karne ya 17, Seqenenre Taa II, hadi Ramses IX, aliyetawala karne ya 12.

Chanzo cha picha, Reuters
Moja ya kilichovutia wengi katika tukio hilo la Jumamosi ni maiti ya Mfalme Ramses II, mtawala maarufu wa Ufalme mpya, ambaye alitawala kwa miaka 67 na pia anakumbukwa kwa kusaini mkataba wa kwanza wa amani.
Mwingine ni malkia Hatshepsut, ambaye anachukuliwa kuwa miongoni mwa wanawake watakatifu. Alikuwa mtawala hata kama kulingana na utamaduni na desturi wakati wake, wanawake hawakuruhusiwa kuwa watawala.
Kila maiti ilikuwa imebebwa kwa gari lililopambwa vizuri na kuwekwa vihimili mshtuko na kuzungukwa na msafara wa magari ikiwemo magari ya kivita yaliyokuwa yakisukumwa na farasi.
Maiti hizo zilizokuwa zimehifadhiwa kwa mbinu za kale kwa ajili ya watawala tu, ili kuhamishwa ziliwekwa katika makasha maalum yenye nitrojeni kusaidia kuwalinda dhidi ya hali ya hewa ya nje.
Pia barabara zilizokuwa zinaelekea kwenye msafara huo zilifungwa ili kuhakikisha safari hiyo inakuwa shwari.

Chanzo cha picha, EPA
Maiti hizo za kale ziligunduliwa mwaka 1881 na mwaka 1898 katika hifadhi ya mabaki ya Thebes, uliokuwa mji mkuu wa Misri- ambao sasa hivi unafahamika kama Luxor upande wa juu wa Misri.
"Tayari maiti hizo zimehamishwa mara kadhaa mjini Cairo na kabla ya hapo zilikuwa Thebes, ambako zilikuwa zimetolewa kutoka kwenye makaburi yao hadi maziara mengine kwasababu za kiusalama," Dkt. Ikram, profesa wa historia ya Misri amesema.
Wakati mabaki ya watawala wengi wa Misri yalichukuliwa kutoka Luxor hadi Cairo kwa njia ya boti kupitia mto Nile, maiti kidogo zilisafirishwa kwa treni.
Pia zilikuwa zinahifadhiwa katika makumbusho muhimu na kutembelewa na watalii kutoka kila pembe ya dunia katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Bonde la Wafalme
Mamlaka ya Misri ina imani kuwa makumbusho mapya ambayo itafunguliwa rasmi mwezi huu itasaidia kufufua sekta ya utalii ambayo imeathirika na janga corona.

Chanzo cha picha, Reuters
Msafara wa kuhamishwa kwa maiti za kale Jumamosi ulipeperushwa moja kwa moja mtandaoni kutoa fursa kwa wote waliotaka kufuatilia tukio hilo.
Maiti hizo sasa zitahifadhiwa katika ukumbi wa maiti wa Kifalme na utafunguliwa kwa umma kuanzia Aprili 18.
Ukumbi huo umetengenezwa kiasi kwamba watakaotembelea eneo hilo watakuwa wanafikiria wako kwenye Bonde la Wafalme la Luxor.
'Laana ya Watawala'
Wakati tukio hilo linaonekana kama na kihistoria - maiti za kale za Misri zimekuwa zikihusishwa na ushirikina na ubashiri wa mambo mabaya.
Hivi karibuni, Misri imekumbwa na mfululizo wa majanga.
Wiki iliyopita peke yake, makumi ya watu waliuawa katika ajali ya treni huko Sohag, kaskazini mwa Misri, na pia watu karibu 18 walifariki dunia baada ya jengo kuporomoka.

Chanzo cha picha, Reuters
Pia, wakati matayarisho ya kuhamisha maiti hizo za kale yamekamilika, mfereji wa Suez ulizibwa na meli ya kubeba mizigo kwa karibu wiki moja.
Watumiaji wa mitandao ya kijamii wakawa wanauliza je matukio hayo yana uhusiano wowote na "laana za watawala"
Suala la kuonesha maiti za kale limekuwa gumzo kwa miaka mingi tu.
Wasomi wengi wa Kiislamu wanaamini kuwa waliofariki dunia wanastahili kupewa heshima na sio kuoneshwa kama kioja.
Mnamo mwaka 1980, Rais Anwar Sadat aliagiza chumba cha maiti cha kifalme kifungwe, akisema kuwaonesha ni kudhalilisha maiti.
Rais huyo aliamini kuwa maiti za kale zinastahili kuzikwa tena ingawa matakwa yake hayakutimia.

Chanzo cha picha, EPA
































