Nchi 7 duniani ambazo mvua ni 'dhahabu'

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kwa sasa maeneo mengi ya Afrika Mashariki yanaendelea kushuhudia mvua kubwa zilizoanza tangu mwezi Machi mwaka huu, hali iliyosababisha mafuriko, uharibifu wa miundombinu pamoja na maelfu ya watu kuathirika katika baadhi ya nchi. Barabara zimekatika, makazi yakisombwa huku shughuli za kijamii na kiuchumi zikivurugika kutokana na mvua hizo kubwa.

Lakini wakati baadhi ya maeneo duniani yakikabiliwa na mvua nyingi kupita kiasi, kuna sehemu nyingine ambazo changamoto yake kubwa ni ukosefu wa mvua kabisa. Katika maeneo hayo, mvua inaweza kunyesha mara moja tu baada ya miaka kadhaa, na wakati mwingine baadhi ya watu hukua bila kushuhudia mvua kubwa maishani mwao.

Kwa nchi hizo, maji ni rasilimali ya thamani kubwa kuliko kawaida. Serikali hulazimika kutumia teknolojia za kisasa kuzalisha maji safi, kuchakata maji yaliyotumika au hata kujaribu kutengeneza mvua bandia ili kukabiliana na ukame mkali.

Wataalamu wa hali ya hewa wanaeleza kuwa sehemu kubwa ya nchi hizi zipo karibu na majangwa makubwa duniani, hasa Jangwa la Sahara na majangwa ya Mashariki ya Kati. Hali ya hewa ya maeneo hayo husababisha mawingu kushindwa kutengeneza mvua za kutosha mwaka mzima.

Hizi ni nchi saba zinazotajwa kuwa kame zaidi duniani kutokana na kiwango kidogo sana cha mvua wanachopokea kila mwaka. Orodha hii imezingatia wastani wa mvua za mwaka pamoja na mazingira ya hali ya hewa ya muda mrefu.

7. Jordan

Jordan ni moja ya nchi zinazokabiliwa na uhaba mkubwa wa mvua na maji kwa ujumla duniani. Kwa wastani, nchi hiyo hupokea takribani milimita 111 za mvua kwa mwaka, kiwango ambacho ni kidogo sana ukilinganisha na wastani wa duniaa

Sehemu kubwa ya Jordan ina hali ya jangwa, huku maeneo mengi yakishuhudia joto kali na vipindi virefu vya ukame. Mvua nyingi hunyesha kwa muda mfupi wakati wa majira ya baridi pekee.

Tatizo la mvua limeifanya Jordan kuwa miongoni mwa nchi zenye upungufu mkubwa wa maji kwa kila mtu duniani. Ukuaji wa idadi ya watu pamoja na ongezeko la wakimbizi kutoka nchi jirani umeongeza matatizo makubwa ya maji.

Kutokana na hali hiyo, serikali imewekeza mamilioni ya dola katika miradi ya kuhifadhi maji, matumizi ya maji yaliyosafishwa pamoja na teknolojia za kisasa za umwagiliaji ili kupunguza athari za ukame.

6. Namibia

Namibia ni moja ya nchi kame zaidi barani Afrika. Wastani wa mvua nchini humo ni karibu milimita 85 kwa mwaka katika baadhi ya maeneo ya jangwa.

Nchi hiyo ndiyo makazi ya Jangwa la Namib, ambalo linatajwa kuwa moja ya majangwa ya kale zaidi duniani. Kuna maeneo ambayo yanaweza kupita miaka kadhaa bila mvua kubwa kunyesha.

Licha ya ukame huo, Namibia imefanikiwa kuendeleza sekta ya utalii kutokana na mandhari yake ya kipekee ya majangwa na wanyamapori. Hata hivyo, upatikanaji wa maji bado ni changamoto kubwa kwa jamii nyingi vijijini.

Mabadiliko ya tabianchi pia yanaendelea kuongeza hofu ya kuongezeka kwa vipindi vya ukame, jambo linaloathiri kilimo na mifugo ambayo ni tegemeo muhimu kwa wananchi wengi.

5. Qatar

Qatar ni moja ya nchi ndogo lakini kame zaidi duniani. Taifa hilo hupokea wastani wa karibu milimita 74 za mvua kwa mwaka.

Mvua nyingi nchini humo hunyesha kwa vipindi vifupi sana, hasa kati ya miezi ya baridi. Katika majira ya joto, hali ya hewa huwa ya joto kali sana huku kiwango cha unyevunyevu kikiongezeka.

Kutokana na ukosefu wa mito na maziwa ya kudumu, Qatar hutegemea zaidi teknolojia ya kuondoa chumvi kwenye maji ya bahari ili kupata maji safi ya matumizi ya binadamu.

Ukuaji mkubwa wa miji na ongezeko la matumizi ya maji vimeifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa mataifa yanayotumia teknolojia kubwa zaidi kuhakikisha upatikanaji wa maji.

4. Saudi Arabia

Saudi Arabia ni moja ya nchi zinazojulikana zaidi kwa hali ya ukame duniani. Wastani wa mvua kwa mwaka ni karibu milimita 59 pekee katika maeneo mengi ya nchi hiyo.

Sehemu kubwa ya Saudi Arabia imefunikwa na majangwa makubwa, likiwemo Jangwa la Rub' al Khali ambalo ni moja ya majangwa makubwa ya mchanga duniani.

Kutokana na ukosefu wa mito ya kudumu, nchi hiyo hutegemea sana maji ya chini ya ardhi pamoja na mitambo ya kuchakata maji ya bahari. Serikali pia imewekeza mabilioni ya dola katika teknolojia za maji.

Pamoja na hali hiyo, Saudi Arabia imeendelea kukuza miji mikubwa na shughuli za viwanda katika mazingira ambayo kwa kawaida si rahisi kwa maisha ya binadamu.

3. Algeria

Algeria ni nchi kubwa zaidi barani Afrika kwa eneo, lakini sehemu kubwa ya ardhi yake imefunikwa na Jangwa la Sahara. Wastani wa mvua katika maeneo mengi ya nchi hiyo ni karibu milimita 89 kwa mwaka.

Katika maeneo ya kusini mwa Algeria, mvua inaweza kutonyesha kwa miezi mingi au hata miaka kadhaa. Hali hiyo imefanya baadhi ya maeneo kuwa na idadi ndogo sana ya watu.

Ukame umeendelea kuwa changamoto kwa sekta ya kilimo, hasa kutokana na kupungua kwa vyanzo vya maji na kuongezeka kwa joto duniani.

Licha ya changamoto hizo, Algeria inaendelea kutegemea rasilimali za mafuta na gesi kama uti wa mgongo wa uchumi wake.

2. Libya

Libya ni moja ya nchi zinazopokea mvua chache zaidi duniani. Kwa wastani, nchi hiyo hupokea takribani milimita 56 za mvua kwa mwaka.

Zaidi ya asilimia 90 ya ardhi ya Libya ni sehemu ya Jangwa la Sahara. Katika baadhi ya maeneo ya ndani kabisa ya jangwa hilo, mvua inaweza kutonyesha mara moja tu baada ya miaka mingi.

Uhaba wa maji nchini humo umeifanya Libya kutegemea miradi mikubwa ya kusafirisha maji kutoka chini ya ardhi kwenda mijini. Mradi maarufu wa "Great Man-Made River" ni moja ya miradi mikubwa zaidi ya maji duniani.

Wataalamu wanaonya kuwa ongezeko la joto duniani linaweza kuongeza zaidi uhaba wa maji katika eneo hilo la Afrika Kaskazini.

1. Misri

Misri inatajwa kuwa moja ya nchi kame zaidi duniani na ina wastani wa karibu milimita 18 za mvua kwa mwaka, kiwango kinachotajwa kuwa miongoni mwa viwango vya chini zaidi duniani.

Sehemu kubwa ya nchi hiyo ni jangwa, huku maisha mengi yakijikita kandokando ya Mto Nile ambao ndiyo chanzo kikuu cha maji kwa zaidi ya watu milioni 100 wa taifa hilo.

Katika miji mingi ya Misri, mvua ni jambo la nadra sana. Baadhi ya maeneo hupokea mvua kidogo sana kiasi kwamba miundombinu mingi haikujengwa kwa ajili ya kukabiliana na mvua kubwa. Unaweza kukuta barabara nzuri mijini hazina mifereji.

Kutokana na utegemezi mkubwa wa Mto Nile, changamoto yoyote inayohusiana na upatikanaji wa maji katika mto huo huwa suala nyeti kwa uchumi na maisha ya wananchi wa Misri.

Wataalamu wa mazingira wanaonya kuwa ongezeko la watu pamoja na mabadiliko ya tabianchi vinaweza kuongeza hatari ya uhaba wa maji nchini humo katika miaka ijayo.

Makala hii ni kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vikiwemo: NASA, World Bank Climate Data, National Geographic, Britannica na World Atlas.