Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Picha 10 za kuvutia zaidi za bahari mwaka 2026
Sili (seal), baba wa samaki aina ya mbuzi-bahari (seahorse) na viumbe wa bahari kuu ambao huonekana mara chache ni miongoni mwa picha zenye kuvutia zaidi katika mashindano ya Ocean Photographer of the Year 2026.
Onyo: Makala haya yana picha ambazo baadhi ya wasomaji wanaweza kuziona kama za kushtua ama kuogofya.
Kila mwaka, mashindano ya Ocean Photographer of the Year huwaalika wapiga picha kuwasilisha picha zao zinazovutia zaidi za bahari mbalimbali.
Katika picha hapo juu, mpiga picha Matthew Smith alimnasa mtoto wa sili (seal) aina ya southern elephant seal akiwa katika udadisi huku akifanya safari yake ya kwanza baharini, katika mabwawa ya maji ya kina kifupi yaliyopo kwenye miamba ya Sea Lion Island, Visiwa vya Falkland.
Tizama chini kuona picha nyingine tisa za kipekee zinazoonyesha uzuri wa bahari za dunia, pamoja na changamoto zinazozikabili.
Baba anayejali
Picha iliyoshinda tuzo ya jumla, iliyopigwa na Julien Anton, inamuonyesha seahorse dume akiwa na mtoto mdogo anayemkabili. Kwa aina nyingi za seahorse, madume ndiyo hubeba mimba, huzaa na kulea watoto. Picha hiyo ilipigwa katika maji ya kina kifupi ya Moorea, French Polynesia.
Jicho la karibu
Viumbe wadogo aina ya copepods, ambao ni crustaceans wanaoishi kwa kujishikiza kwa viumbe wengine, wanaonekana kwenye jicho la giant black sea bass katika picha iliyopigwa na Stephen Lopez karibu na Kisiwa cha Santa Catalina, nje ya pwani ya Kusini mwa California, Marekani.
Takribani miaka 50 iliyopita, samaki huyu alikuwa karibu kutoweka katika eneo hilo, lakini sasa idadi yake inaongezeka tena.
Mshambulizi wa kujificha
Samaki aina ya red scorpionfish anaonekana akimng'ata lizardfish katika picha hii ya Andrea Michelutti, iliyopigwa nchini Philippines.
Tukio hilo la kuvutia linaonyesha uwezo wa scorpionfish kuwinda kwa kujificha - na mapambano ya kila mara ya kuishi katika miamba ya matumbawe.
Njemba mwenye upole
Wakati wa msimu wa kukusanyika kwa dagaa (sardine) nchini Mexico mwaka 2025, mpiga picha Anita Verde alimnasa mgeni huyu asiyetarajiwa - samaki mkubwa aina ya giant oceanic sunfish, mwenye ukubwa unaokaribia gari dogo.
"Alipokuwa akielekea kwetu kupitia maji ya buluu, alionekana kama anang'aa," aliiambia BBC, "kama mwezi mkubwa unaochomoza chini ya maji. Huwezi kujizuia kumtazama samaki huyu machoni. Ana uzuri wa ajabu sana."
Mgeni kutoka kina kirefu
Mitsuna Kawai alipiga picha hii wakati wa majira ya baridi katika zoezi la kupiga mbizi kwenye maji meusi (black-water dive) karibu na pwani ya Osezaki, Japan.
Samaki wachanga aina ya ribbonfish huonekana mara chache wakiwa hai kwa sababu wanaishi katika kina cha hadi mita 900. Samaki mchanga kama huyu anaweza kuwa na urefu wa sentimita chache tu, lakini akiwa mkubwa anaweza kufikia urefu wa mita 1.8.
Katika mpangilio
John Kowitz alipiga picha hii ya kisanaa ya miale mitano aina ya spotted eagle rays ikielea juu ya sakafu ya bahari yenye mchanga huko Hawaii, Marekani.
Miale hii mara nyingi husafiri pamoja kutafuta chakula, ikitumia vipokezi vya umeme kutambua moluska na crustaceans waliofichika chini ya mchanga.
Kulea kwakutumia mdomo
Picha hii ya karibu iliyopigwa na Suliman Alatiqi huko Mawali, Indonesia, inamuonyesha samaki dume aina ya Banggai cardinalfish akiwahifadhi watoto wake walioanguliwa hivi karibuni ndani ya mdomo wake kwa siku 10 bila kula.
Mbinu hii maalumu ya kulea watoto ndani ya mdomo huwasaidia kuwalinda dhidi ya wanyama wanaowawinda hadi watakapokuwa na uwezo zaidi wa kujitegemea.
Kundi la kamba wadogo
Maelfu ya kamba wadogo na dhaifu kama huyu aliyepigwa picha na Francesca Page, hulelewa katika National Lobster Hatchery huko Padstow, Uingereza, kila mwaka.
Porini, ni mmoja tu kati ya kamba 20,000 anayefikia utu uzima. Kamba wachanga wanaolelewa katika vituo maalumu vya uzalishaji wana uwezekano wa kuishi hadi kufikia umri wa kuzaliana mara 1,000 zaidi.
Katika Visiwa vya Faroe, eneo linalojitawala ndani ya Ufalme wa Denmark, nyangumi aina ya pilot whale anauawa na mwindaji katika picha iliyopigwa na Karsten Michels.
Kama sehemu ya desturi ya jadi ya grindadráp, makundi ya nyangumi hao huongozwa kuelekea ufukweni ambako huchinjwa.
Hata uwindaji wa nyangumi kwa kiwango kidogo unaweza kuacha athari kubwa katika mazingira ya bahari kuu.