Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Njia 6 za kutisha ambazo wanaanga wanaweza kufia Mwezini
Mwezi unaficha hatari nyingi kwa binadamu. Bila shaka, mazingira yake makali yanaweza kuhatarisha maisha ya mtu yeyote atakayethubutu kutembea juu ya uso wake.
Wakati wanaanga wa mpango wa Apollo waliposafiri mwezini miaka zaidi ya 50 iliyopita, waliweza kufanya hivyo kwa msaada wa teknolojia ya hali ya juu, vifaa maalumu vya kujikinga na mfumo mkubwa wa usaidizi uliokuwa ukidhibitiwa kutoka duniani.
Kutoka kwa mionzi mikali ya anga za juu hadi joto kali na baridi kali kupita kiasi, mazingira ya Mwezi yalikuwa tishio la kudumu kwa usalama wao. Bila mavazi yao maalumu na msaada wa karibu kutoka kwa kituo cha udhibiti duniani, kuishi huko kungekuwa jambo lisilowezekana.
Hata hivyo, zaidi ya nusu karne baadaye, binadamu anajiandaa kurejea mwezini. Safari hizi mpya hazilengi tena kutua kwa muda mfupi na kuondoka, bali zina lengo kubwa zaidi la kuanzisha uwepo wa kudumu wa binadamu.
Mipango hiyo inalenga kujenga makazi, miundombinu na mifumo ya kusaidia maisha ambayo itawezesha wanaanga kuishi na kufanya kazi kwa muda mrefu kwenye uso wa Mwezi, hatua inayochukuliwa kuwa muhimu katika maandalizi ya safari za baadaye kuelekea sayari ya Mars.
Machi 2026, shirika la anga za juu la Marekani, NASA, lilitangaza mipango ya kujenga kituo cha thamani ya dola bilioni 20 karibu na ncha ya kusini ya Mwezi, ambacho kinatarajiwa kuwa makazi ya kwanza ya kudumu ya binadamu nje ya Dunia.
Makazi hayo yanaweza baadaye kuenea katika eneo kubwa la mamia ya maili za mraba. Awali yataendeshwa kwa kutumia vyanzo vya nishati vinavyotokana na isotopu za mionzi, kabla ya kuhamia kwenye kinu cha nyuklia kitakachosaidia kuyahimili mazingira magumu ya usiku wa Mwezi ambao hudumu kwa wiki kadhaa.
Hata hivyo, kujenga kituo hicho ni sehemu tu ya changamoto. Kazi ngumu zaidi inaweza kuwa kuhakikisha wakazi wake wanaendelea kuishi salama. Ingawa zaidi ya miaka 20 ya maisha ndani ya Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu (ISS) imetoa maarifa muhimu kuhusu kuishi angani, Mwezi unakuja na mazingira na hatari tofauti kabisa.
Zifuatazo ni changamoto sita kati kubwa zaidi zinazoweza kuhatarisha maisha ya wanaanga katika makazi ya kudumu ya mwezini.
1. Kupoteza shinikizo na kukosa hewa
Mojawapo ya hatari kubwa zaidi kwa wanaanga wanaoishi Mwezini ni ukosefu wa wa angahewa. Tofauti na Dunia, Mwezi hauna hewa ya kutosha kusaidia maisha ya binadamu.
Endapo makazi ya wanaanga au vazi la anga (spacesuit) yatatoboka au kuvuja, mwanadamu atakabiliwa na mazingira hatari ya anga. Katika hali hiyo, atakuwa na fahamu kwa sekunde 10 hadi 15 pekee kabla yakuzimia kutokana na ukosefu wa oksijeni. Na bila kurejeshewa shinikizo la hewa, madhara ya kudumu au kifo vingetokea ndani ya takriban sekunde 90.
Kwa sababu hiyo, mifumo ya hewa, milango ya usalama na mavazi ya wanaanga vitakuwa miongoni mwa vifaa muhimu zaidi katika makazi yoyote ya kudumu ya binadamu Mwezini.
Mavazi ya angani ni ngao kuu yanayowalinda wanaanga dhidi ya mazingira hatari ya Mwezini. Kimsingi, suti hizo huwaweka mwanaanga hai kwa kumzunguka ndani ya tabaka nyembamba la hewa yenye shinikizo linalomwezesha kupumua na kudumisha hali ya kawaida ya mwili.
Hata hivyo, mfumo huo ni dhaifu kwa namna moja muhimu sana: kutoboka mara moja tu kunaweza kusababisha mfumo wa usaidizi wa maisha kuanza kushindwa kufanya kazi. Kasi ya hatari hiyo hutegemea ukubwa wa uvujaji. Tundu dogo sana, sawa na lile linaloweza kusababishwa na pini, linaweza kuruhusu hewa kutoka taratibu na kumpa mwanaanga muda wa kuchukua hatua za dharura. Lakini tundu kubwa zaidi linaweza kusababisha suti kupoteza shinikizo lake ndani ya sekunde chache.
Oksijeni inapopungua haraka, ubongo huanza kukosa gesi muhimu inayouhitaji ili kufanya kazi. Ndani ya muda mfupi, mwanaanga anaweza kupoteza uwezo wa kufikiri vizuri na hatimaye kupoteza fahamu.
Wakati huohuo, kushuka kwa ghafla kwa shinikizo kunasababisha athari nyingine hatari. Maji yaliyomo kwenye tishu za mwili huanza kuchemka kwa sababu ya mazingira yenye shinikizo la chini, hali inayoweza kusababisha mwili kuvimba kwa kiasi kikubwa. Ingawa ngozi na mishipa ya mwili huzuia mwili "kulipuka" kama inavyoonyeshwa mara nyingi katika filamu za kisayansi, athari zake bado zinaweza kuwa mbaya na kuhatarisha maisha.
Hatari kama hizi zinaonyesha kwa nini safari za baadaye za muda mrefu Mwezini zitahitaji suti za angani zilizo imara zaidi na mifumo ya usalama inayoweza kukabiliana haraka na hitilafu zozote. Kwa wanaanga watakaotarajiwa kuishi na kufanya kazi kwenye Mwezini kwa wiki, miezi au hata miaka, uadilifu wa suti zao unaweza kuwa tofauti kati ya maisha na kifo.
2. Viwango vya joto vilivyokithiri
Mazingira ya mwezini yana viwango vya joto visivyo na kifani. Kutokana na ukosefu wa angahewa ya kuhifadhi na kusambaza joto, halijoto kwenye uso wake hubadilika kwa kiwango kikubwa sana kati ya mchana na usiku.
Wakati wa mchana wa Mwezini, joto linaweza kuzidi nyuzi joto 120, huku wakati wa usiku likishuka hadi karibu nyuzi -130. Katika baadhi ya mashimo makubwa yaliyo kwenye kivuli cha kudumu, ambako mwanga wa jua haujawahi kufika kwa mabilioni ya miaka, halijoto inaweza kushuka hadi karibu nyuzi -240.
Katika mazingira hayo, mwanaanga asiye na kinga maalum hawezi kuishi kwa muda mrefu. Ndiyo sababu mavazi ya anga za juu yameundwa kwa mifumo ya hali ya juu ya kudhibiti joto ili kulinda mwili dhidi ya kuganda kwa baridi kali au kuathiriwa na joto kubwa la jua.
Mavazi hayo yana tabaka kadhaa za nyenzo imara kama Mylar, Kevlar na vifaa vingine vya kuhifadhi joto na kuzuia uharibifu. Pia yana mfumo wa kupoza mwili unaozungusha maji maalum kuzunguka mwili wa mwanaanga, kusaidia kuondoa joto la ziada na kudumisha kiwango salama cha joto.
Kwa makazi ya kudumu ya binadamu Mwezini, kudhibiti halijoto kutakuwa mojawapo ya mambo muhimu zaidi ya kuhakikisha usalama na uhai wa wanaanga.
3. Kugongwa na vipande vidogo vya mawe ya angani
Hatari nyingine kubwa kwa wanaanga Mwezini ni kugongwa na vipande vidogo vya mawe ya angani vinavyojulikana kama micrometeoroids. Angani, vitu husafiri kwa kasi kubwa sana, kiasi kwamba hata chembe ndogo inaweza kusababisha uharibifu mkubwa inapogonga kitu.
Kwa kasi hiyo, chembe ndogo ya vumbi la angani inaweza kuvunja kioo cha kofia ya suti ya mwanaanga au kutoboa suti yenyewe. Tofauti na Dunia, Mwezi hauna angahewa ya kuunguza au kupunguza kasi ya mabaki haya kabla hayajafika ardhini.
Iwapo suti ya mwanaanga ingetobolewa na kipande hicho, kupotea kwa shinikizo la hewa kungetokea kwa haraka sana, na hali hiyo inaweza kusababisha kuzirai ndani ya sekunde chache na hatimaye kifo ikiwa msaada wa dharura usingepatikana.
Ndiyo sababu makazi ya Mwezini pamoja na suti za wanaanga zinapaswa kujengwa kwa nyenzo imara zinazoweza kustahimili migongano ya chembe ndogo za angani zinazoruka kwa kasi kubwa mno.
4. Mionzi hatari kutoka kwa jua na anga za mbali
Tofauti na Dunia, Mwezi hauna angahewa wala uga wa sumaku unaosaidia kulinda viumbe hai dhidi ya mionzi hatari kutoka Jua na anga za mbali. Hivyo, wanaanga watakaoishi huko watakuwa katika mazingira yenye kiwango kikubwa zaidi cha mionzi.
Wataalamu wanakadiria kuwa wanaanga waliopo kwenye uso wa Mwezi wanaweza kukabiliwa na viwango vya mionzi vinavyozidi kwa kiasi kikubwa vile vinavyopatikana Duniani. Kadri muda wa kuishi Mwezini unavyoongezeka, ndivyo kiwango cha mionzi kinachopokelewa mwilini kinavyoongezeka pia.
Mfiduo wa muda mrefu wa mionzi unaweza kuharibu seli na DNA, jambo linaloongeza hatari ya saratani na magonjwa mengine makubwa. Katika viwango vya juu zaidi, mionzi inaweza kusababisha ugonjwa mkali wa mionzi na kuathiri viungo vya mwili.
Japo mavazi maalumu ya wanaanga yameundwa kutoa kinga dhidi ya sehemu ya mionzi hiyo, tishio kubwa zaidi hutokana na dhoruba za Jua. Hizi hutokea wakati Jua linapotoa kwa ghafla mawimbi makubwa ya chembe zenye nishati nyingi zinazosafiri kwa kasi kuelekea anga za mbali.
Hata wanaanga walioko ndani ya Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu hulazimika wakati mwingine kujikinga katika maeneo maalumu yanayotoa ulinzi zaidi hadi dhoruba hizo zipite. Kwa upande wa Mwezi, ambako hakuna kinga ya asili kutoka angahewa au uga wa sumaku, athari za dhoruba za Jua zinaweza kuwa kubwa zaidi.
Kwa sababu hiyo, makazi ya kudumu ya binadamu Mwezini yatahitaji kujengwa chini ya tabaka nene za udongo wa Mwezi au kutumia ngao maalumu za kinga ili kupunguza kiwango cha mionzi kinachowafikia wanaanga.
5. Sumu ya Carbon dioxide(CO₂)
Kila pumzi anayovuta mwanaanga hutoa Carbon dioxide. Ndani ya vifungo vilivyofungwa vya suti ya angani, gesi hiyo inaweza kujikusanya haraka hadi viwango hatari ikiwa mfumo wa kuchuja wa mkoba utagoma kufanya kazi.
Ndani ya suti ya anga, hitilafu ya mfumo wa kuchuja hewa inaweza kusababisha CO₂ kujikusanya haraka na kufikia viwango hatari. Kadri kiwango hicho kinavyoongezeka, damu huanza kuwa na asidi zaidi, hali inayoweza kusababisha maumivu ya kichwa, kizunguzungu na matatizo ya kuona.
Viwango vya juu zaidi vya CO₂ vinaweza kuathiri uwezo wa mwanaanga wa kufikiri na kufanya maamuzi sahihi. Hali hiyo inaweza kusababisha kuchanganyikiwa, kupungua kwa umakini na hatimaye kupoteza fahamu. Katika mazingira hatari ya Mwezini, kosa dogo la maamuzi linaweza kuwa na matokeo mabaya sawa na hatari yenyewe.
Tatizo linaweza kutokea hata kama mfumo wa kuchuja hewa bado unafanya kazi. Ikiwa feni za kusambaza hewa ndani ya suti zitaharibika, gesi ya CO₂ inayotolewa inaweza kujikusanya karibu na uso wa mwanaanga badala ya kuondolewa. Hii inaweza kumfanya aendelee kuvuta hewa ile ile yenye kiwango kikubwa cha CO₂, na kuongeza hatari ya sumu ya gesi hiyo.
Kwa sababu hiyo, mifumo ya kusafisha na kusambaza hewa itakuwa miongoni mwa teknolojia muhimu zaidi kwa usalama wa wanaanga katika makazi ya kudumu ya Mwezini.
6. Vumbi la Mwezini
Ingawa kwa mbali huonekana kama unga laini wa kijivu, vumbi la Mwezini ni mojawapo ya hatari kubwa zaidi zinazowakabili wanaanga. Vumbi hilo limetokana na mabilioni ya miaka ya migongano ya vimondo iliyosaga miamba ya uso wa Mwezi na kuigeuza kuwa chembechembe ndogo sana zenye ncha kali.
Tofauti na vumbi la kawaida duniani, chembe za vumbi la Mwezini zinafanana zaidi na vipande vidogo vya kioo kilichovunjika. Kwa sababu Mwezi hauna upepo wala maji ya kulainisha chembe hizo, hubaki na ukali wake na uwezo wa kukwaruza au kuharibu vifaa mbalimbali.
Mtaalamu Bailey anasema vumbi la Mwezini ni miongoni mwa hatari ambazo mara nyingi hupuuzwa.
"Wanaanga wa misheni za Apollo walilielezea kama unga laini wenye ncha kali na chaji ya umeme tuli unaonata kwenye kila kitu. Linaweza kuingia kwenye mitambo, kuharibu suti za anga na pia kuwa tishio kwa macho na mapafu."
Tatizo kubwa zaidi ni kwamba chembe hizi ni ndogo mno kiasi cha kuvutwa hadi ndani ya mapafu. Zikiingia mwilini, zinaweza kusababisha madhara ya kiafya na hata kupenya kwenye mfumo wa damu.
Mbali na kuhatarisha afya ya wanaanga, vumbi hilo linaweza pia kuharibu vifaa muhimu vya kambi ya Mwezi, likikwama kwenye viungio vya mitambo, paneli za sola na mifumo mingine inayohitajika kwa maisha ya kila siku.
Kwa sababu hiyo, kudhibiti na kuzuia vumbi la Mwezini kuingia ndani ya makazi kutakuwa mojawapo ya changamoto muhimu zaidi kwa makazi ya kudumu ya binadamu kwenye Mwezi.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi