Mfumo wa mahakama wa Iran unasema umetaifisha mali za watu 249 kwa tuhuma za 'kushirikiana na Israel'
Mfumo wa mahakama wa Iran ulitangaza kuwa umetaifisha mali za watu 249 kwa tuhuma za "kufanya ujasusi na kushirikiana na Israel pamoja na nchi zenye uadui."
Shirika la Habari la Mizan, chombo cha habari cha taasisi hiyo, liliandika kuwa katika miezi ya hivi karibuni, "mali za watu wengi walioisaliti nchi na wananchi wake zimetaifishwa kwa amri ya mahakama."
Watu hao wameelezwa kuwa ni "watu wenye uhusiano" na Israel pamoja na nchi zenye uadui.
Mfumo wa mahakama wa Iran umesema kuwa mali na rasilimali 143 zinazomilikiwa na watu waliofanya "kampeni za propaganda au vitendo dhidi ya nchi na kwa maslahi ya serikali zenye uadui" zimetaifishwa mjini Tehran.
Kwa mujibu wa taasisi hiyo, visa vingi vya kutaifisha mali na kufungia akaunti za benki pia vimefanyika kote nchini Iran: "Kwa jumla, mali za watu 240 walioisaliti nchi zimetaifishwa kwa amri ya mahakama kupitia hatua za kisheria."