Zuio la mikutano ya kisiasa Tanzania ni mtihani kwa taasisi za dola au vyama vya siasa?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Tangazo la Serikali ya Tanzania la kusitisha kwa muda mikutano yote ya hadhara ya vyama vya siasa limeibua mjadala mpana unaozidi mipaka ya siasa za vyama.

Serikali inasema hatua hiyo inalenga kulinda usalama wa taifa katika kipindi ambacho kuna viashiria vya maandamano na vitendo vya uhalifu, huku vyama vya upinzani na jumuiya ya wanasheria wakisema agizo hilo linagusa haki za msingi zinazolindwa na Katiba.

Mjadala huo unakuja wakati mitandaoni kukiwa na miito ya maandamano yanayotarajiwa kufanyika Julai 7, 2026, siku ya kilele cha Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Baadhi ya wanaohamasisha maandamano hayo wanasema lengo ni kushinikiza mabadiliko ya mfumo wa uongozi na kupatikana kwa Katiba mpya.

Hoja hiyo iliibuliwa pia bungeni na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Paschal Inyasi Chinyele, aliyesema kumekuwa na taharuki kuhusu taarifa za maandamano zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, alisema Serikali imebaini kuwepo kwa miito hiyo ya maandamano na kutangaza kusitishwa kwa muda kwa mikutano yote ya hadhara ya vyama vya siasa nchini kama hatua za kiusalama.

Lakini je, hatua hiyo ni mtihani kwa vyama vya siasa pekee, au ni kipimo cha namna taasisi za dola zitakavyotafsiri mipaka ya mamlaka ya Serikali na ulinzi wa haki za kikatiba?

Serikali: Usalama wa taifa ni wajibu wa kwanza wa dola

Miito ya maandamano ya Julai 7 imeibuka ikiwa bado haijapita hata mwaka mmoja tangu maandamano ya Oktoba 29, 2025, yaliyogeuka kuwa miongoni mwa matukio mabaya zaidi ya kisiasa kuwahi kushuhudiwa nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Tume ya Jaji Mohammed Chande iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchunguza matukio hayo, watu 518 walipoteza maisha huku maelfu wengine wakijeruhiwa.

Baada ya tukio hilo, Serikali ilisisitiza mara kadhaa kuwa haitaruhusu tena amani na usalama wa nchi kuhatarishwa. Msimamo huo ulirudiwa na Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, ambaye akizungumza bungeni hivi karibuni alisema Serikali haitaruhusu mtu yeyote kuvuruga utulivu na umoja wa taifa.

"Kwa namna yoyote Serikali haitaruhusu utulivu, amani na utaifa wetu uharibiwe na yeyote yule. Wala tusidanganyane, hatutaruhusu yachezewe."

Aliongeza kuwa usalama wa taifa haupaswi kuwa jambo la mjadala. "Suala la usalama, amani na umoja wa nchi yetu wala si mambo ya kujadiliwa. Tusidanganyane, hatutaruhusu viharibiwe."

Aidha, aliwataka wanaohamasisha maandamano kupitia mitandao ya kijamii kujitokeza wao wenyewe.

"Kwa wale wanaoelekeza kwenye magroup ya WhatsApp waje wenyewe. Wasitumie watoto wa Kitanzania kama chambo, wasitumie mitandao kuchochea vurugu kwenye nchi yetu."

Na katika muktadha huo ndipo Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, alipotangaza kuwa amemuelekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi kutotoa vibali vya mikutano ya hadhara ya kisiasa hadi pale Serikali itakapotoa maelekezo mengine.

"Hatua hii inalenga kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi katika mazingira ya amani na utulivu, huku vyombo vya dola vikifanya kazi ya kuwabaini wahalifu bila changamoto zinazoweza kusababishwa na mikusanyiko mikubwa ya watu," alisema Katambi.

Lakini wanaokosoa wanahoji Je, Waziri huyo ana mamlaka ya kufanya hivyo?

Kwa nini huu ni mtihani kwa taasisi za dola?

Pamoja na mjadala wa kisiasa, hoja kubwa sasa imehamia kwenye tafsiri ya sheria na mipaka ya mamlaka ya Serikali katika kusimamia haki za kikatiba.

Kwa mara nyingine, mjadala wa mikutano ya kisiasa unafufua historia ya maamuzi ya awali, ikiwemo kipindi cha baada ya uchaguzi mkuu wa 2015 ambapo mikutano ya vyama vya siasa ilizuiwa kwa zaidi ya miaka sita, ukiacha vipindi vifupi vya uchaguzi wa 2020 na uchaguzi wa serikali za mitaa. Katika kipindi hicho, taasisi nyingi zilionekana kutochukua hatua za wazi kupinga au kufafanua msingi wa kisheria wa uamuzi huo.

Ibara ya 20 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatamka kuwa kila mtu ana uhuru wa kukutana na kushirikiana na wengine kwa amani. Ukicha sheria ya vyama vya siasa, ibara hii mara nyingi hutajwa katika mijadala ya aina hii, ikitumika kama msingi wa hoja za wanaotetea uhuru wa mikutano ya hadhara.

Hata hivyo, Patrobas Katambi si mwanasiasa pekee; pia ni mwanasheria. Alipotangaza uamuzi huo bungeni akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, alifanya hivyo akiamini kuwa Serikali ina mamlaka ya kuchukua hatua hizo kwa misingi ya kulinda usalama wa taifa.

Lakini tafsiri hiyo imepingwa na wanasheria wengine pamoja na jumuiya ya mawakili. Mawakili akiwemo Peter Madeleka, Jebra Kambole na Peter Kibatala wamehoji uhalali wa agizo hilo, wakisema mamlaka ya Waziri hayawezi kuzidi masharti ya Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Chama cha ACT Wazalendo kimetangaza kuwa kitaenda Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo, kikisisitiza kuwa mikutano ya hadhara ni haki ya kikatiba na si hisani ya mamlaka ya Serikali.

"Mikutano ya hadhara ni takwa la kikatiba na sheria na si hisani ya Waziri na vyombo vya dola," ilisema taarifa ya chama hicho.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, amesema chama hicho pia kitachukua hatua za kisheria kupinga agizo hilo.

"Waziri wa Mambo ya Ndani hana mamlaka yoyote ya kuzuia mikutano inayoruhusiwa na Katiba na sheria. TLS itachukua hatua za kisheria dhidi ya utekelezaji wa agizo hili."

Kwa upande mwingine, kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Thom Mkondya, anasema mjadala haupaswi kuwa kama Serikali ina mamlaka ya kuzuia mikutano au la, bali kama sababu zilizotolewa zinakidhi masharti ya Katiba na sheria.

"Dola inaweza kuahirisha au kuzuia mikutano ikiwa kuna sababu halali na za kisheria kama vile kulinda usalama wa taifa, amani ya umma, afya ya umma au haki za wengine. Mjadala sahihi si kama dola ina mamlaka ya kuzuia au la, bali ni kama sababu zilizotolewa zinakidhi matakwa ya Katiba na sheria."

Kwa upande wake, Serikali inaendelea kuonyesha msimamo kuwa hatua iliyochukuliwa inazingatia mazingira ya sasa ya kiusalama na wajibu wake wa kulinda utulivu wa nchi.

Ikiwa Waziri ambaye ni mwanasheria anaamini kuwa sheria inampa mamlaka ya kuchukua hatua hiyo, lakini wanasheria wengine pamoja na TLS wanapinga tafsiri hiyo, ni ipi tafsiri sahihi ya kisheria?

Jibu la swali hilo haliwezi kupatikana katika majukwaa ya kisiasa pekee. Ikiwa ACT Wazalendo na TLS, pamoja na wadau wengine, watafikisha shauri hilo mahakamani kama walivyotangaza, basi Mahakama ndiyo itakayokuwa na jukumu la kutoa tafsiri ya mwisho ya Katiba na sheria.

Hapo ndipo mtihani wa taasisi za dola unapoanzia.

Usalama wa taifa dhidi ya haki za kisiasa

Mjadala huu umefufua hoja ambayo imekuwa ikiibuka katika demokrasia nyingi duniani. Usalama wa taifa unaweza kwenda umbali gani bila kugusa haki za msingi za wananchi?

Kwa upande wa Serikali, hoja ni kwamba bila amani na usalama hakuna mazingira ya wananchi kutumia haki nyingine. Kauli ya Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba inaakisi msimamo huo. "Suala la usalama, amani na umoja wa nchi yetu wala si mambo ya kujadiliwa. Tusidanganyane, hatutaruhusu viharibiwe."

Kwa upande mwingine, vyama vya upinzani na jumuiya ya wanasheria hawapingi wajibu wa Serikali kulinda usalama wa taifa, bali wanahoji iwapo hatua zilizochukuliwa zimefuata utaratibu unaotakiwa na Katiba.

Kwa mfano kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, anasema: "Mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ni haki ya msingi inayolindwa na Katiba na sheria za nchi. Waziri wa Mambo ya Ndani hana mamlaka yoyote ya kuvunja Katiba."

Huku Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, akisisitiza: "Mikutano sio fujo, mikutano ni elimu."

Kwa sasa, majibu ya hoja hizo zote hayaonekani kupatikana kupitia majukwaa ya kisiasa pekee, au mitandao ya kijamii. Badala yake, yatahitaji tafsiri ya taasisi zinazosimamia sheria.

Kwa mantiki hiyo zuio la mikutano ya kisiasa ya hadhara limekuwa zaidi ya mjadala kati ya Serikali na upinzani. Limegeuka kuwa mtihani wa namna taasisi za Tanzania, kuanzia Mahakama, Jeshi la Polisi, Bunge hadi vyombo vya habari, zitakavyoweka usawa wa kulinda usalama wa taifa na wajibu wa kuheshimu Katiba na haki za msingi za wananchi.