Serikali yapiga marufuku tena mikutano ya kisiasa Tanzania

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Serikali ya Tanzania imetangaza kusitisha kwa muda mikutano yote ya hadhara ya vyama vya siasa nchini, bila kujali chama husika, ikieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama wa wananchi katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na taarifa za viashiria vya maandamano na vitendo vya uhalifu.

Akizungumza bungeni mjini Dodoma leo Ijumaa, Juni 26, 2026, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, alisema amemuelekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillus Wambura, kutotoa vibali vya mikutano ya hadhara ya kisiasa hadi pale serikali itakapotoa maelekezo mengine.

Katambi alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya serikali kubaini kuwa baadhi ya mvutano wa kisiasa umechangia hali ya taharuki, huku kukiwa na taarifa za miito ya maandamano kuelekea kilele cha Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

"Hatua hii inalenga kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi katika mazingira ya amani na utulivu, huku vyombo vya dola vikifanya kazi ya kuwabaini wahalifu bila changamoto zinazoweza kusababishwa na mikusanyiko mikubwa ya watu," alisema Waziri Katambi.

Hata hivyo wanasiasa wa upinzani wamekosoa hatua hiyo. Mwanasiasa mkongwe, Joseph Selasini kutoka CHADEMA ameandika kwenye mtandao wake wa twitter: "Ni aibu kubwa kwa chama kinachojinasibu kuwa kikongwe na chenye wanasiasa wakongwe kushindwa kujibu hoja. Tunajua kitakachofuata ni kukamata na kuhoji viongozi", anasema Selasini bila kufafanua ni viongozi gani hao na kwanini wakamatwe.

Chama cha ACT Wazalendo nacho kimepinga vikali agizo hilo la zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, ikisema ni maelekezo haramu yanayovunja katiba ibara ya 20 (i) na sheria ya vyama vya siasa, zinazotoa uhuru wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu kufanya mikutano ya kisiasa.

Aidha, aliagiza Jeshi la Polisi kuendelea kufuatilia maeneo yote yanayotiliwa shaka na kuchukua hatua za kisheria, ikiwemo kuyafungia kwa muda endapo kutabainika kuwa yanatumika kwa shughuli zinazohatarisha usalama.

Tangazo hilo limekuja ikiwa ni takribani miaka mitatu tangu Januari 2023, wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipofungua tena mikutano ya vyama vya siasa iliyokuwa imepigwa marufuku kwa zaidi ya miaka sita wakati wa utawala wa hayati John Magufuli. Wakati huo, viongozi wa vyama vya upinzani walipokea uamuzi huo kwa tahadhari, wakieleza hofu kuwa marufuku hiyo ingeweza kurejeshwa wakati wowote.

Kwa sasa, serikali inaeleza kuwa uamuzi wa kusitisha mikutano ya kisiasa unatokana na sababu za kiusalama na juhudi za kuzuia vitendo vya uhalifu vinavyoweza kujitokeza. Wakati huo huo, mitandaoni kumekuwa na miito ya kuitisha maandamano yanayotarajiwa kufanyika Julai 7, 2026.

Oktoba 29, 2025, Tanzania ilishuhudia maandamano yaliyoambatana na vurugu na ghasia katika maeneo mbalimbali, ambapo watu 518 waliripotiwa kupoteza maisha huku maelfu wengine wakijeruhiwa, tukio lililoacha athari kubwa kwa usalama na shughuli za kijamii na kiuchumi nchini.